Zitto Kabwe: Baadhi ya Vitabu nilivyosoma mwaka 2019

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Mar 2, 2007
1,562
10,880
Baadhi ya Vitabu nilivyosoma mwaka 2019 – Zitto Kabwe

Mwaka 2019 nimejaaliwa kusoma vitabu 34 (2018:49 na 2017:36+3). Ni sahihi kuwa idadi imepungua sana, hii ni kwa sababu shughuli nazo zimekuwa nyingi, haswa masuala ya ujenzi wa chama na kuhami demokrasia. Mwaka 2019 ndio mwaka nimekanyaga mahakamani mara nyingi zaidi kuliko wakati wowote wa maisha yangu. Majukumu yanapozidi, muda wa kujisomea unapungua. Hata hivyo nashukuru sana nimejikongoja mpaka kufikia vitabu 34.

Ingizo jipya ni riwaya za mwandishi wa Kituruki Orhan Pamuk ambaye nimesoma vitabu vyake 4 mwaka huu. Amenifanya kupenda kusoma kazi za waandishi wengine kutoka Uturuki kutokana na riwaya zake zenye mchanyato wa masuala ya Siasa za Uturuki, utamaduni, mapenzi na maisha ya watu kiujumla. A Strangeness in Mind ndio ilinivutia kuliko zote katika Riwaya za Pamuk nilizoorodhesha hapa. Hii ni riwaya inayoeleza maisha ya kijana Mevlut aliyetoka shamba na kuhamia mjini na namna maisha yalivyobadilika kwa kasi. Ni hadithi inayoonyesha tamaduni za kituruki kuhusu ndoa na mahusiano ya ndugu na familia. Kitabu hiki kitakufanya uione Uturuki na mapinduzi ya kijeshi yalivyoigubika mwaka hadi mwaka, pamoja na mtanziko wa Siasa zenye kuheshimu misingi ya Dini au kufuata umagharibi. Riwaya za Pamuk nilizosoma ni pamoja na;

1. Orhan Pamuk - Snow

2. Orhan Pamuk - Silent House

3. Orhan Pamuk - A Strangeness in Mind

4. Orhan Pamuk - Instanbull

Nilisoma pia Riwaya nyengine kadhaa zikiwemo kazi za watunzi mliozoea kuwaona kama Jefrey Archer na John Grisham katika orodha zangu za miaka ya hivi karibuni. Pia nilimsoma Mzee Makaidi, kazi yake aliyoandika mingi nyuma. Mwaka huu nimevutiwa sana na kazi za mtunzi wa kitanzania anayechipukia Bwana Lello Mmasy. Riwaya na Mimi na Rais ilinikosesha usingizi kwani sikutamani kuacha kuisoma. Ni Riwaya iliyosadifiwa vizuri na kwa ubunifu mkubwa huku ikichora picha halisi yenye kuvutia msomaji.

Riwaya hii naifananisha na ile ya A Man of The People ya Chinua Achebe (kwa ubunifu na labda utabiri). Nchi ya Stanza na Rais wake Bwana Costa aliyekuwa anaharibu Uchumi wa Taifa lake, katika riwaya hii, inaweza kuwa ni nchi yeyote ya Afrika katika hali ya sasa.

Nilifurahi pia kusoma kazi ya Mama Fatma Jinja iitwayo The Shirazi Enigma kwani ni hadithi yenye historia kubwa ya Zanzibar. Ukitaka kujua usasa na uchangamano wa watu wa mataifa mengi Zanzibar soma hadithi ya Salwa katika Riwaya hii. Bwana Abdulrazak Gurnah pia anasimulia hadithi katika historia ya Zanzibar pia. Kazi yake niliyoorodhesha hapa ni historia ya Siasa na familia za Zanzibar katika miaka ya Sabini na Themanini. Mtunzi wa Riwaya Helmut Zell kutoka Ujerumani pia alinivutia kazi yake ya Black Money in Dar. Ukisoma Riwaya hiyo unakumbuka mtifuano wa sakata la Escrow mwaka 2014. Kama kwa Mmasy, nilijisoma pia kwa Zell. Riwaya nilizosoma ni pamoja na;

5. Jeffrey Archer - Nothing Ventured

6. Abdulrazak Gurnah - Gravel Heart

7. Fatma Jinja - The Shirazi Enigma

8. E J E Makaidi - The Serpent: Hearted Politician

9. Helmut Zell - Black Money in Dar es Salaam

10. Lello Mmassy - Mimi na Rais

11. Jeniffer M Makumbi - Kintu

12. John Grisham - The Guardians

Kama kawaida, napenda historia. Hivyo mwaka huu nilisoma vitabu vya historia kadhaa ili kupata maarifa ya tulipotoka ili niweze kutafakari huko tunakokwenda. Vitabu vya historia nilivyosoma ni pamoja na;

13. W H Ingrams - Zanzibar: Its History and Its People

14. Judith Listowel - The Making of Tanganyika

15. Linda Pappas Funsch - Oman Reborn: Balancing Tradition and Modernisation

16. A Monument to China - Africa Friendship: Firsthand Account of the Building of The TAZARA

17. Amilcar Cabral - Unity and Struggle

18. Paul Kenyon - Dictatorland

19. Yuval Noah Harari - Sapiens: A Brief History of Humankind

Mwaka huu tumebahatika kupata vitabu vya baadhi ya Viongozi wetu nchini. Rais wa Awamu ya Tatu Mzee Benjamin Mkapa ameandika Wasifu wake. Amesimulia maisha yake. Kabla ya hapo Mzee Njelu Kasaka, aliyekuwa Mbunge na Katibu wa Kundi la G55 lililotaka Serikali ya Tanganyika alitoa kitabu chake pia. Vitabu muhimu sana katika kuifahamu Tanzania ilipotoka na ilipo kupitia maisha ya wanasiasa hawa. Nimefurahi sana kusoma vitabu vyao. Pamoja nao pia nilisoma vitabu vya watu wengine kama vile Hashil Seif ambaye alishiriki mapinduzi ya Zanzibar.

Kitabu cha Balozi Wilibrod Slaa kinaeleza maisha yake na pia nini kilitokea katika chama cha CHADEMA mwaka 2015. Sio kitabu cha kupuuza kwani kina mafunzo mengi kwa wanasiasa. Nasikitika kuwa Balozi Slaa alichagua ya kutoandika kwani labda kupitia kwake ningeweza kujua haswa ushiriki wake katika kufukuzwa kwangu kwenye chama ambacho yeye alikuwa Katibu Mkuu. Nilikinunua ili nisome suala hilo, bahati mbaya hakusimulia mkasa ule wa Zitto na Kitila.

A Son of Two Countries cha Casmir Rubagumya ni wasifu wa Mtanzania mwenye asili ya Rwanda ambaye aliishi maisha ya ukimbizi na wazazi wake, kusoma mpaka kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu na hatimaye kustaafu. Alipata uraia wa kuandikisha na kuitumikia Tanzania kwa weledi wake wote. Licha ya kubembelezwa kurudi Rwanda baada ya mauaji ya kimbari, aligoma na kuendelea kuwa Mtanzania tofauti na wenzake wengi wa aina yake ambao waliamua kurudi Rwanda. Ni simulizi ya maisha yenye kusisimua na mafunzo. Ni Kitabu kimojawapo ambacho nilipokishika sikukiacha mpaka namaliza. Wasifu na Tawasifu nilizosoma ni pamoja na;

20. Benjamin W Mkapa - My Life, My Purpose

21. Njelu Kasaka - Maisha, Siasa and Hoja ya Tanganyika: G55

22. Hashil Seif Hashil - Mimi, Umma Party na Mapinduzi ya Zanzibar

23. Willibrod P Slaa - Nyuma ya Pazia: CHADEMA ilivyosalitiwa 2015

24. Casmir M Rubagumya - A Son of Two Countries

25. Sergey Plekhanov - Sultan Qaboos Bin Said A Said: A Reformer on the Throne

26. Ken Saro-Wiwa - A Month and a Day: A Detention Diary

Mchanganyiko wa vitabu mbalimbali kama kawaida. Ni katika kuongeza maarifa au kurutubisha itikadi ya Ujamaa. Pia katika kujifunza makosa ya wengine ili kutorudia makossa hayo. Vitabu mchanganyiko mwaka huu ni pamoja na;

27. James Brent Styan - The Bosasa Billions

28. Christine Berry + Joe Guinan - People Get Ready: Preparing for a Corbyn Government

29. P. Anyang’ Nyong’o - Presidential or Parliamentary Democracy in Kenya?

30. Greg Mills et al - Democracy works

31. Nick Robinson et al - The Power of Journalists

32. Douglas Rogers - Two Weeks in November: The Astonishing Inside Story of the Operation that Toppled Mugabe

33. Nanjala Nyabola - Digital Democracy, Analogue Politics

Zawadi kubwa niliyopata mwaka huu ni kitabu kinachoeleza Aya za Qur’an Tukufu na muktadha wa kila Aya katika kushuka kwake. Ni kitabu kinachokaa pembeni ya Kitanda changu kwa ajili ya marejeo ya mara kwa mara. Wanazuoni wa mirengo yote ya Dini ya Kiislam wameshiriki katika kuandika ‘comentaries’ za kitabu hiki.

34. Sayyed Hossein Nasir - The Study Quran

Mwaka huu ninatangaza kitabu changu cha Mwaka, yaani Kitabu kilichonivutia zaidi kuliko vyote nilivyosoma mwaka huu. Kitabu changu cha Mwaka 2019 ni Two Weeks in November cha Bwana Douglas Rogers. Kitabu hiki kinaeleza namna Watu mbalimbali waliokuwa maadui na marafiki, waliokuwa wakiviziana kuuana na wapinzani wakubwa, walivyoshirikiana kumwondoa madarakani Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe mwezi Novemba mwaka 2017.

Ni kitabu cha matukio ya kweli ambayo huwezi dhania ni kweli, unaweza kudhani ni hadithi tu. Licha ya kwamba kuondolewa kwa Mugabe madarakani hakujaleta ahueni kwa wananchi wa Zimbabwe, mbinu, mikakati na mafunzo ndani ya Kitabu hiki ni somo tosha kwa wapigania demokrasia kote Afrika. Hiki ni kitabu ambacho utakirudia hata mara 10 bila kuchoka.

Kila Rais wa Afrika, kila Mkuu wa Majeshi, kila Kiongozi wa Upinzani na kila mwanasiasa mwenye kujitambua asome kitabu hiki. Akifanye rejea yake ya mara kwa mara. Wiki 2 za Novemba 2017 zaweza kutokea katika nchi yeyote ambayo Viongozi wake hawazingatii demokrasia, utawala wa sheria, Utu na mshikamano katika kuendesha Taifa. Tafuta nakala yako.

Nawatakia kheri katika kumaliza mwaka 2019 na kila la kheri katika mwaka 2020. Nawashawishi kupata muda wa kujisomea japo kitabu kimoja kila mwezi. Kusoma ni kurutubisha ubongo.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Dar es Salaam
Disemba 20, 2019
 
Hongera sana Kaka Zito Kabwe. Vijana wajifunze na kujizoesha kusoma vitabu. Sio kushinda kwenye pooltable na Draft. Mwaka huu nmesoma Vitabu viwili. Hakika kitabu ni mbolea ya Ubongo.

Kikubwa naona jiandae Uandike Kitabu kwa mkono wako. Achana na kile alichoandika Dada Asha kukuhusu. Natamani kusoma kitabu chako. Mungu akufanyie wepesi uweze kuandika
 
mkuu Zitto
kusoma vitabu ni jambo zuri sana, ila kusoma ni jambo moja na kutumia maarifa uliyopata kwenye Maisha halisia ni jambo linguine.

Tumekushauri mara kadha kuitumia ACT kama jukwa la kujengea uwezo wa uongozi watu wengi iwezekanovyo "Capable human resouces" kwa kuamini kwamba kama kila chama kitafanya hivyo, hiyo itakuwa ni njia mojawapo muhimu ya kuifikia Tanzania iliyobora.

Shida huwa inakuwa ni nini mkuu?
 
Vitabu vinafundisha na kukujenga kwa mengi sanaaa. Ukiwa husomi hutojua, Ila siku ukianza ndio utajuta kuchelewa.
Utatamani usome vyote kwa wakati mmojaa,
Lkn tatzo linakuja usomaji wa vitabu unakua mzuri unaposoma ukiwa ume relax.
 
Mheshimiwa Zitto huwa hajibu maswali kwa wakati au kutojibu kabisa, huwa sielewi shida ni nini
mkuu Zitto
kusoma vitabu ni jambo zuri sana, ila kusoma ni jambo moja na kutumia maarifa uliyopata kwenye Maisha halisia ni jambo linguine.

Tumekushauri mara kadha kuitumia ACT kama jukwa la kujengea uwezo wa uongozi watu wengi iwezekanovyo "Capable human resouces" kwa kuamini kwamba kama kila chama kitafanya hivyo, hiyo itakuwa ni njia mojawapo muhimu ya kuifikia Tanzania iliyobora.

Shida huwa inakuwa ni nini mkuu?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Zitto huwa Ana muda mwingi wa kusoma vitabu kuliko kuwa na muda mwingi wa kusikiliza kero za wananchi wa Jimbo lake ndio maana jimbo.lake choka mbaya.
 
kulikuwa na maana gani kuandika (2017: 36+3) badala ya (2017: 39) ?
Kuna maana nilieleza mwaka 2018. Mwaka ulipoisha nilikuwa nina vitabu 3 sijamaliza ( Feast of goat, zeitoun na jumba maro ). Sikutaka kuvihesabu into 2018. Kwa hiyo huwa naandika kuwa nilisoma 36 Lakini nilikuwa bado nasoma 3 wakati naweka list ya 2017.
 
mkuu Zitto
kusoma vitabu ni jambo zuri sana, ila kusoma ni jambo moja na kutumia maarifa uliyopata kwenye Maisha halisia ni jambo linguine.

Tumekushauri mara kadha kuitumia ACT kama jukwa la kujengea uwezo wa uongozi watu wengi iwezekanovyo "Capable human resouces" kwa kuamini kwamba kama kila chama kitafanya hivyo, hiyo itakuwa ni njia mojawapo muhimu ya kuifikia Tanzania iliyobora.

Shida huwa inakuwa ni nini mkuu?
Suala hilo mbona ndio kazi kubwa ya ACT Wazalendo. Ni kazi endelevu
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom