Lissu: Desemba tutaamua kama tunaendelea na mazungumzo na CCM au tunaachana nao

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,371
8,107
Chama cha Demokrasia na Mandeleo (CHADEMA) kimesema kitaamua kama kiendelee mazungumzo na CCM au la ifikapo mwezi Desemba kwa kuwa mambo mengi wanayolalamikia hayatekelezwi.

Kauli ya CHADEMA imekuja wakati mazungumzo hayo yakiwa yametimiza miezi sita, huku kukiwa na usiri mkubwa wa kinachojadiliwa.

Majadiliano ya kwanza yalifanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Mei 20 mwaka huu kwa Rais Samia Suluhu Hassan akiambatana na viongozi waandamizi wa CCM na Serikali, ambao walikutana na ujumbe wa viongozi wa CHADEMA, ulioongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe.

Kikao kingine kilifanyika Novemba 5, 2022 jijini Dar es Salaam na vigogo wa CCM wakiongozwa na makamu mwenyekiti-Bara, Abdulrahman Kinana na upande wa CHADEMA ukiongozwa na Mbowe waliongoza wajumbe kujifungia katika kikao cha siri.

Lakini akizungumza juzi kwa simu kuhusu ziara ya viongozi wa chama hicho Ulaya na Marekani, makamu mwenyekiti wa CHADEMA (Bara), Tundu Lissu alisema kwa miezi sita sasa kati ya mambo wanayolalamikia katika vikao hivyo, lililotekelezwa ni kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa pekee.

“Tuna majadiliano na CCM, lakini hayajazaa matunda kwenye uendeshaji wa siasa na bado tunaendelea kuzungumza.

“Basically, ukiachilia suala la kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa, Rais hajafanya lolote katika madai yetu,” alisema Lissu anayeishi nchini Ubeligiji.

Alisema licha ya kujadili malalamiko yao yakiwemo ya kupatikana kwa Katiba mpya na mikutano ya hadhara; “Hajabadilisha sheria yoyote katika madai yetu.”

Kuhusu madai ya Katiba mpya alisema, “zaidi ya kusema kwenye chama chake kuwa wako tayari, hakuna chochote kilichofanyika, tunaona anaendeleza alichofanya mtangulizi wake (Hayati Rais) John Magufuli.”

Lissu alisema kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa mazungumzo hayo, watafikiria vinginevyo katika kikao wanachotarajia kukutana mwezi ujao (Desemba).

“Baada ya miezi sita ya mazungumzo, hatujaona matunda na mwezi ujao tutakutana tuangalie kama tuendelee au tusiendelee,” alisema.

Lissu anaongoza ujumbe wa viongozi wa chama hicho akiwemo Katibu Mkuu John Mnyika, wakifanya ziara katika nchi za Ujerumani, Ubeligiji na Marekani kuzungumza na vyama vya siasa rafiki kuhusu hali ya siasa nchini.

Viongozi wengine waliomo katika msafara huo ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalim, Mjumbe wa Kamati Kuu Zeudi Mvano na Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, John Pambalu.

Alisema katika mikutano na vyama rafiki, wanawaeleza hali ya kisiasa na kutafuta suluhisho katika ufanyaji wa siasa nchini.

“Kwanza tunajenga urafiki na tunawaeleza hali yetu ya siasa. Tunatarajia watatusaidia kuieleza Serikali kwa njia ya kidiplomasia, kisiasa kwamba mambo tunayodai hayafanyiwi kazi,” alisema Lissu.

Alipotafutwa kwa simu na kuulizwa kuhusu madai ya CHADEMA, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu alisema hawezi kujibu kwa kuwa hajamsikia Lissu.

“Mgoja nitafute muda nisikilize hicho alichozungumza ndipo nipate muda wa kujibu,” alisema Shaka.

Ripoti ya kikosi kazi iliyokabidhiwa kwa Rais Samia Oktoba 21 ilipendekeza, “Mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa iruhusiwe kufanyika kwa mujibu wa Katiba na Sheria.”

Kuhusu Katiba mpya, ripoti hiyo ilipendekeza kukamilishwa kwa mchakato wa kuipata kupitia mjadala wa kitaifa, ili kupata muafaka katika masuala ya msingi.

Pia ripoti hiyo imependekeza kuhuishwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni, kuundwa kwa jopo la wataalamu baada ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhuishwa, kutolewa kwa elimu ya uraia kuhusu Katiba mpya na mwisho kura ya maoni

Hata hivyo, akipokea ripoti hiyo, Rais Samia alisema Serikali inakwenda kuyafanyia kazi, “lakini mapendekezo yao si amri kwa Serikali.”

CHADEMA na Sera ya Majimbo

Katika hatua nyingine, taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na CHADEMA juzi, ilieleza chama hicho kitaendeleza sera yake ya majimbo kama mkakati wa kushusha mamlaka zaidi kwa wananchi na kuharakisha maendeleo.

“Tumekuwa tukiinadi sera ya majimbo tangu 2010 na katika mchakato wa kupatikana Katiba mpya Tanzania tunataka tushawishi wananchi kutuunga mkono na kuingizwa rasmi kwenye Katiba,” alisema katibu mkuu wa CHADEMA, John Mnyika katika taarifa hiyo akiwa ziarani Ulaya ambako walikutana na naibu waziri mkuu wa Serikali ya Jimbo la Brandenburg nchini Ujerumani, Michael Stibgen.

Kwa upande wake, Stubgen alisifu mfumo wa Serikali za majimbo na kuunga mkono haja ya Tanzania kuutumia kutokana na ukubwa wake.

Alisema mfumo huo una changamoto pia kwa kiasi fulani hasa katika eneo la masilahi ya Serikali Kuu na za majimbo, lakini zinatibiwa na uwepo wa Katiba za Serikali Kuu na za majimbo.

“Tuna Katiba ya Serikali Kuu (Federal) na za Serikali za Majimbo (Regional) zinaelekeza masuala mbalimbali ikiwemo ya mapato, namna ya kupitisha sheria na kanuni jambo ambalo linatoa wepesi katika uendeshaji,”alieleza

Kwa upande wake, Lissu aliushukuru uongozi wa Brandenburg kuwapa nafasi ya kukutana nao na kubadilishana uzoefu.

Alimkaribisha Brandenburg nchini Tanzania ambapo babu na wazazi wake waliishi mwanzoni mwa miaka ya 1900.

MWANANCHI
 
Kung'ang'ania kukaa ubeligiji kumekupotezea mvuto kwenye siasa za Tanzania Lissu.

Effect ya Chadema kwa sasa ni ndogo sana.
Kuna madiliko wayafanye kwanza ndani kwao then waje kwetu wapiga kura.
 
Back
Top Bottom