Lipumba: Katiba Mpya 2014 hawezekani

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
[h=1][/h]
Na Aidan Mhando, Mwananchi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba amesema mchakato wa Katiba Mpya una vikwazo vingi na kwamba Katiba haiwezi kupatikana mwaka 2014 kama Rais Kikwete alivyoahidi hivyo, kuna haja ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Bara.
Hii ni mara ya pili kwa Lipumba kutoa kauli hiyo. Mei mwaka huu, alitoa tamko kama hilo alipoonyesha wasiwasi wake kuhusu upatikanaji wa Katiba Mpya akadai ni janja ya CCM kumwongezea muda Rais.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Lipumba alisema kuwa amekuwa akiutafakari kwa kina mchakato wa Katiba Mpya kama unaweza kukamilika mwaka 2014, lakini jibu linalomjia, hakuna.
Alitaja baadhi ya vikwazo ambavyo vinaweza kukwamisha kupatikana kwa Katiba Mpya kuwa ni Daftari la Kudumu la Wapigakura kama halijaboreshwa na kasi ndogo ya utoaji wa vitambulisho vya utaifa ambavyo vitatumika kupigia kura hiyo.
Wakati Profesa Lipumba akisema hayo, tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeeleza kuwa haina mpango kwa sasa wa kuboresha Daftari la Kudumu Wapigakura kwa ajili ya kura za maoni kwa sababu muda uliobaki ni mfupi.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, kuwa itakuwa vigumu kuliboresha daftari hilo kwa ajili ya upigaji wa kura za maoni utakaofanyika mwanzoni mwa mwaka 2014 kwa sababu muda uliobaki ni mfupi na hakuna fedha za kufanya hivyo.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi alipoulizwa bungeni mwisho mwa wiki kuhusiana na kauli ya Jaji Lubuva alisema msimamo uliotolewa na Waziri Mkuu kuhusiana na daftari hilo ndiyo msimamo hasa wa Serikali.
Desemba 5, mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alivihakikishia vyama vya siasa na Watanzania kwamba Daftari la Kudumu la Wapigakura litaboreshwa kabla ya upigaji kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya ya Tanzania.
Waziri Mkuu alisema hayo wakati akihitimisha hotuba yake ya Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013, ambapo suala la Daftari la Wapigakura liliibua mvutano mkali baina ya wabunge na Serikali.
Profesa Lipumba alisema kuwa kutokana na hali ilivyo sasa ni wazi kwamba Katiba Mpya haiwezi kupatikana kabla ya mwaka 2015, hivyo kuna haja ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kushughulikia mchakato wa Katiba na kuimarisha uwajibikaji wa vyombo vya dola.
“Ni wazi kwamba hatuwezi kupata Katiba mpya ifikapo Aprili 26, wakati tunasherehekea miaka 50 ya Muungano, kwani bado mchakato huu ni mrefu na unahitaji muda wa kutosha,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Rasimu ya mwisho ya Tume ya Katiba itapatikana mwezi huu, huku na Rais anawajibika kukamilisha undaji wa Bunge la Katiba kwa kuteuwa wabunge 201 baada ya kupata mapendekezo, hivyo itakuwa bahati Bunge la Katiba kuanza mwisho wa mwezi Januari kitu ambacho kinarefusha mchakato huu.”
Alisema kura ya maoni kuhusu Katiba haiwezi kuendeshwa kwa ufanisi bila kuwa na Daftari la Wapiga kura linalotumika, na kwamba kura hiyo inapaswa kupigwa na wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Aidha, Profesa Lipumba alibainisha kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, inatumia Tume ya Zanzibar kuwa wakala na datfari la Zec kubaini wapigakura wa Zanzibar, jambo ambalo linawanyima haki Wazanzibar kupiga kura kwa madai kuwa hawana vitambulisho vya ukaazi.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alisema mchakato wa Katiba Mpya unapaswa kuwapa wananchi matumaini ya kujenga Tanzania mpya yenye haki sawa kwa wote.
Alisema Tanzania ipo mbioni kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa kikatiba, kwani mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yanakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, lakini hayakinzani na sheria mama.

Chanzo Mwananchi
 
Back
Top Bottom