Elections 2010 Lipumba achambua ahadi za JK, Duni akerwa na wizi wa kura

Sokomoko

JF-Expert Member
Mar 29, 2008
1,915
127
Waandishi wetu
MGOMBEA urais kwa tiketi ya CUF, Prof Ibrahim Lipumba jana alitumia muda mwingi kuchambua kwa njia ya kejeli ahadi za mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete akitumia lugha na mifano rahisi, huku mgombea mwenza wa chama hicho akianika mbinu alizodai kuwa zilitumika kuiba kura kwenye chaguzi zilizopita.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha TBC1, Prof Lipumba alisema hajaona utekelezaji wa ahadi hizo za mwaka 2005 na kwamba badala yake mambo yamekuwa mabaya zaidi.

"Ahadi hizi za CCM ni chupa mpya, lakini kilichomo ndani ni kilekile kibovu... ni chupa mpya lakini kilichomo ni gongo ileile," alisema Prof Lipumba ambaye alikuwa akizungumza taratibu na kwa mifano huku maelfu ya watu waliofurika kwenye viwanja vya Jangwani wakimshangilia kwa nguvu.

Prof Lipumba alitumia muda mwingi kuelezea jinsi uwajibikaji ulivyoshuka kwenye serikali ya sasa kiasi cha elimu kushuka sana, huduma za afya kutolewa ovyo huku mgombea huyo wa CCM akisafiri kila mara kwenda nje ya nchi kwa madai kuwa anatafuta misaada.

Alisema huduma za afya zimedorora kwa sababa mgonjwa anapoenda hospitalini anakuta daktari ameshalewa gongo na badala ya kumpima kwa vifaa, hutumia mkono wake kujua joto.
"Kwa kuwa anakuwa ameshakunywa gongo, mwili wake huwa na joto lakini yeye hufikiria joto la mgonjwa liko juu na hivyo kusema ana malaria," alisema Prof Lipumba.

"Anatumia fedha nyingi kwenda San Francisco, Marekani kuomba vyandarua... mimi sitaenda Marekani, nitatumia simu tu," alisema Prof Lipumba.

Aliongeza kuwa nusu ya watoto wanaomaliza elimu ya msingi hawajui kusoma kitabu cha darasa la pili, kutokana na elimu wanayopewa madarasani na walimu wao kutokuwa na ubora.

“Wapo wanaomaliza darasa la saba lakini hawawezi kufanya hesabu za darasa la pili, hata ukimuuliza tisa mara saba anabaki kukushangaa tu... wanaomaliza kidato cha nne wakiulizwa swali kwa Kiingereza, hawawezi kujibu; wanabakia kusema yes, yes,” alisema Lipumba.

“Tanzania ya sasa inatakiwa kumaliza tatizo la elimu kwa shule za msingi mpaka vyuo vikuu."
Prof Lipumba alikejeli kauli mbiu ya "Maisha Bora kwa Kila Mtanzania aliyoitumia Kikwete kwenye uchaguzi wa mwaka 2005, akisema kuwa imekuwa kinyume chake.

"Badala ya maisha bora, yamekuwa maisha bomu," alisema Prof Lipumba huku akishangiliwa na wanachama na wafuasi wa chama hicho.

"Bakora za maisha bora tunachalazwa wote bila ubaguzi... kwa hili tunawasifia CCM kuwa wamelitekeleza kwa kutushirikisha wote kwa kuwa tunaumia sote."

Lipumba, ambaye anagombea kwa mara ya nne sasa, alisema kuwa Kikwete alitoa ahadi nyingi ambazo mpaka sasa bado hajaziteleza, lakini bado anaendelea kumwaga ahadi nyingine.

“Naishangaa CCM imeshindwa kutimiza ahadi zake za mwaka 2005, na mgombea wake anatoa ahadi nyingine bila uwoga huku akidhani wananchi wamelala wamesahau ahadi alizozitoa awali,” alisema Lipumba.

Lipumba alizitaja ahadi hizo kuwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba bora za walimu na wafanyakazi nchi nzima, hospitali bora kwa wilaya tatu za Dar es Salaam, kumaliza tatizo la maji, ujenzi wa barabara za lami kuanzia Dodoma-Iringa hadi Babati.

Nyingine ni pamoja na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Dodoma hadi Iringa na kupeleka umeme mkoa wa Kigoma, maji safi na salama mkoa wa Lindi, kumaliza tatizo la soko ya zao la korosho Lindi na Mtwara, kuupatia mkoa wa Tabora maji safi na salama na treni ya umeme mkoani Tabora.

“Sasa mtu anasema ataweka treni ya umeme wakati reli ya kati tu inasuasua. Hasemi amezitekeleza vipi ahadi zake za 2005 badala yake anazidi kumwaga ahadi mpya, huuu ni kiongozi bora au kiongozi bomu,” alihoji Lipumba.

Kuhusu serikali yake iwapo atachaguliwa, Prof Lipumba alisema asilimia kubwa ya viwanda vya pamba nchini vimekufa na kwamba CUF itahakikisha kuwa anavifufua viwanda hivyo ili kuongeza uchumi wa Watanzania kwa kuwa vinaajiri watu wengi.

“Naumia sana kuona vijana wengi wanapata taabu ya ajira, badala yake wanakuwa wezi wauza chupa za maji, karanga huku vigogo wakiwaangalia wakiteseka kimaisha wakiwa zao majuu,” alisema Lipumba.

"Kinachodidimiza sekta ya viwanda ni ukosefu wa umeme... kama serikali ingeweza kuzalisha umeme katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji zingepatikana megawati 500.
“Nchi hii imebahatika kuwa na makaa ya mawe ambayo yanaweza kuzalisha megawati 1000, pia kuna gesi sehemu nyingi tu ambazo tukizitumia tunaweza kuzalisha umeme mwingi zaidi wa kuuza hata nje ya nchi.”

Katika hotuba yake ya utangulizi kabla ya Prof Lipumba kuzungumza, mgombea mwenza wa chama hicho, Juma Haji Duni alitoa tuhuma za wizi wa kura ambao ulifanywa na CCM kwenye jimbo la Namtumbo, akisema kuwa alipewa nyaraka za njama hizo na mtu ambaye alieleza amemuhifadhi jina lake kwa ajili ya usalama wake.

Alisoma nakala za barua hizo ambazo zinatoa maelekezo kwa wasimamizi wa uchaguzi na viongozi wa vijiji kuhakikisha CCM inashinda kwenye jimbo hilo kwa kuchelewesha kuanza kwa upigaji kura na mgawanyo wa karatasi za ziada ambazo alisema zilishatiwa alama ya kura na pia kuanika nyaraka aliyodai kuwa ni makubaliano yaliyofikiwa baina ya watu ambao alidai kuwa walikuwa kwenye njama hizo.

Baadaye Haji Duni alitoa vifaa alivyodai vilitumiwa na viongozi hao wa vijiji wakati wa wizi huo na kusababisha watu kuanza kupiga kelele kuilaani CCM.

Duni Haji aliwataka Watanzania kuichagua CUF ili waondokane na umasikini.

Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Hussein Issa, Patricia Kimelemeta, Minael Msuya na Hidaya Omary
Add this page to your favorite Social Bookmarking websites

Comments




+1 #2 SHEMEJI 2010-10-29 08:41 "Kuhusu serikali yake iwapo atachaguliwa, Prof Lipumba alisema asilimia kubwa ya viwanda vya pamba nchini vimekufa na kwamba CUF itahakikisha kuwa anavifufua viwanda hivyo ili kuongeza uchumi wa Watanzania kwa kuwa vinaajiri watu wengi."

NAKUUNGA MKONO KABISAAA PROF. KWA HILI, SIKU HIZI HATA MARAPURAPU YA KUFUTIA MIKONO GARAGE NI YA MITUMBA KUTOKA CANADA SIYO PAMBA YETU TOKA URAFIKI AMA MWATEX TENA, HUU NDIO UONGOZI WA CCM UNAOTUONGOZA,
PAMBA YETU, MIWA YETU, KATANI ZETU, KOROSHO ZETU, MAWESE YETU, VYOTE HIVYO KIKWETE ANAONA HAVINA MAANA BADALA YAKE ANAONA KWENDA KUJIPENDEKEZA MAREKANI NDIYO KUENDESHA NCHI,
NINA MASHAKA NA MASOMO YAKE YA UCHUMI KAMA NI YA KWELI AMA ALIHUDHURIA KWA AJILI YA KUONGEZA IDADI YA WASOMI WASIOJUA KITU?
ZIARA ZA KIKWETE ZIMETUUDHI HATA SISI WANANCHI HATA PICHA NA WACHEZA SINEMA SIJUI ZILIMAANISHA NINI KWA RAISI WETU.

wewe ndiye prof. Bwana hata kama hukuchaguliwa itakuwa ni kwa ajili ya kutojua thamani ya watu kama ambavyo tumezoea kutupa pamba yetu safi na kuagiza mitumba toka ulaya ituambukize maradhi tuongeze gharama za matibabu.
HII NDIYO NHI YA WADANGANYIKA BWANA

MUNGU TUOKOE NA DHAHAMA HII KAMA KUNA DHAMBI TULIFANYA BASI SASA UTUSAMEHE KWA MAANA MATESO HAYA YAMEZIDI.
wenu Mtanganyika
Quote









0 #1 cheka 2010-10-29 08:07 eeeeh kazi kwelli kweli jamani,lakini tutafika tu
Quote







Refresh comments list

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!
 
Hizi njama zinazofanywa na CCM za uwizi kura ni budi lipewe msimamo sio kuachwa katika mikutano ya kampeni
 
Back
Top Bottom