Licha ya mabadiliko ya uongozi vitambulisho NIDA bado ni tatizo

101 East

JF-Expert Member
Feb 25, 2015
1,040
2,119
Licha ya mabadiliko ya kiutawala na kiutendaji yaliyofanywa katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kipindi cha miaka minne mfululizo, bado utoaji wa vitambulisho kwa wananchi umekuwa wa kusuasua.

Foleni katika ofisi za NIDA zimetamalaki wananchi wanaohitaji huduma hiyo ili kuwawezesha kupata vitambulisho watakavyovitumia kwa shughuli mbalimbali ikiwamo usajili wa laini za simu kwa alama za vidole.

Kutokana na mahitaji kuwa makubwa ya wananchi kuhitaji vitambulisho hivyo na muda wa usajili uliokuwa umepangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni Desemba 31, juzi Rais John Magufuli aliongeza muda wa kusajili hadi Januari 20 mwakani baada ya hapo laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa zizimwe.

Nida iliyoanzishwa mwaka 2008 inapitia kipindi hicho ikiwa imeshapitia mabadiliko makubwa ya uongozi tangu mwaka 2016 mpaka sasa.

Mwaka 2015, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu na watumishi wengine wanne walisimamishwa kupisha uchunguzi wa matumizi ya Sh179.6 bilioni zilizotumika katika mradi wa vitambulisho vya taifa.

Baada ya kuondolewa kwa Maimu, Rais Magufuli alimteua Dk Modestus Kipilimba ambaye alikaimu nafasi hiyo kwa miezi minane kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Kwa sasa Kipilimba ni Balozi Mteule.

Baada ya Dk. Kipilimba kuondoka NIDA, nafasi yake ilikaimiwa na Andrew Massawe aliyekaa kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kuondolewa na kuwekwa Dk. Arnold Mathias Kihaule Oktoba 3, 2018, nafasi anayoendelea nayo hadi sasa.

Mbali na mabadiliko ya uongozi, wakati Dk. Kipilimba akiongoza NIDA alitangaza kusitisha mikataba ya wafanyakazi 597 wa mamlaka hiyo akisema ni kutokana na ufinyu wa bajeti.

Wafanyakazi hao waliondolewa huku ikielezwa vitambulisho vya Taifa vilivyotumia kiasi kikubwa cha fedha za umma havikuwa na ubora unaotakiwa ikiwa ni pamoja na kukosa saini ya mmiliki na ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo.

Dk. Kipilimba pia alitaja sababu ya kubadilika kwa mpangokazi wa mamlaka hiyo kuwa ni pamoja na eneo la majukumu yake kwa kuwa hatua zote za usajili zilitakiwa kufanyika katika ngazi ya wilaya na watumishi wachache watekeleza kazi hiyo kwa kushirikiana na watendaji katika ngazi za mitaa na vijiji.

Huku kitambulisho hicho kikiongezeka umuhimu wake kutokana na kuhitajiwa katika shughuli tofauti na zoezi la sajili wa laini za simu ukihitaji nyaraka hiyo kwa wakati mmoja, mabadiliko hayo yaliyolenga kupunguza gharama za uendeshaji yanaonekana kulemewa na mahitaji makubwa yaliyopo.

Takwimu za TCRA zinaonyesha kuwa hadi Desemba 25 laini zilizokuwa zimesajiliwa kwa alama za vidole ni milioni 22.40 kati ya laini milioni 47 milioni zilizo sokoni. Moja ya nyaraka muhimu katika usajili wa laini kwa alama za vidole ni kitambulisho hicho.

Huku TCRA ikiwa imeweka Desemba 31 kuwa siku ya mwisho ya kusajili laini kwa mfumo huo, na upatikanaji wa kitambulisho kutokuwa na kasi nzuri, ofisi za Nida katika maeneo yote zimekuwa zikifurika watu kuanzia alfajiri kila siku.

Wakati kazi hiyo ikianza, ilichukua takriban wiki mbili kwa mhitaji kutumiwa ujumbe unaompa namba yake na baadaye kumjulisha kuwa kitambulisho chake kiko tayari.

Lakini wananchi wengi walioongea na Mwananchi katika siku za karibuni wameeleza kufuatilia kwa muda mrefu bila ya kupata namba au kujulishwa kinachoendelea.

“Hii ni kutokana na wahudumu kuwa wachache, hapa ndipo tunapoweza kusema Serikali imefeli,” alisema Godfrey Mshana alipozungumza na Mwananchi juzi jijini Arusha.

Wakati kitambulisho ni nyaraka muhimu katika kusajili laini, simu zimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku, zikitumika katika malipo, kuhamisha fedha, kuhifadhi nyaraka, mawasiliasno na kuperuzi habari mbalimbali duniani.

Takwimu za miezi sita iliyopita za TCRA zinaonyesha kuwa miamala ya thamani ya Sh16 trilioni ilifanyika katika kipindi hicho, fedha ambazo ni takriban nusu ya bajeti ya nchi.

Mbali na umuhimu huo katika sekta ya fedha, simu zimetengeneza ajira kadhaa kwa wauzaji wa muda wa maongezi, wahamishaji fedha, watiaji muziki huku baadhi ya wasanii wakinufaika na milio inayotumia nyimbo zao, bila ya kusahau matangazo ya kibiashara.

Pia upatikanaji wa ajira serikalini nao unahitaji vitambulisho hivyo. Sekretarieti ya Ajira imetangaza kuwa hadi mwisho wa Septemba 2019, watu wote wanaoomba ajira serikalini lazima wawe na vitambulisho hivyo.

Rais Magufuli juzi alitangaza ahueni kwa wamiliki wa simu alipoongeza siku 20 kuanzia Januari mosi za kusajili laini, lakini umati wa watu wanaokusanyika ofisi mbalimbali za NIDA unadokeza kuwa kasi ya utoaji vitambulisho haitawezesha wamiliki wa simu kukamilisha usajili ndani ya muda huo.

Wananchi waendelea kusota

Ikiwa ni siku moja baada ya Rais Magufuli kuongeza siku 20 za upatikanaji wa vitambulisho hivyo, wananchi wameendelea kutoa malalamiko ya usumbufu wa kuvipata.

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya wananchi jijini Dodoma walisema utaratibu wa NIDA unawataka wakapige picha ukumbi wa vijana wa Mambo Poa uliopo mtaa wa Uhuru na kwenda kuchukua namba ya kitambulisho ofisi za NIDA zilizopo Jengo la Bima, umbali wa takriban kilomita moja.

Utaratibu wa kupiga picha eneo tofauti na wanalochukua namba unawapa usumbufu na kutumia muda mrefu kuzunguka sehemu hizo mbili.

Fred Kano alisema alikwenda kupiga picha kituo cha Mambo Poa na kutakiwa kuchukua namba ya utambulisho katika jengo la Bima zilipo ofisi za NIDA, lakini alipopewa namba hiyo ili akasajili laini zake aliambiwa namba hiyo imekosewa.

Jijini Dar es Salaam, licha ya kumshukuru kwa kuongezwa siku 20, wametaka muda huo uongezwe hadi miezi miwili.

Mwandishi wa Mwananchi aliyefika kituo cha Nida kilichopo eneo la Mombasa Ukonga alishuhudia wananchi wakiwahi kuandika majina yao kwenye kitabu na kupata namba zinazowawezesha kupata huduma mapema alfajiri ya saa 11.

Katika kituo hicho kila aliyewahi kufika alikwenda getini alipo mlinzi na kuandika jina lake kwenye kitabu na muda aliofika kisha anapewa namba na kukaa pembeni kusubiri muda wa ofisi kufunguliwa saa 1:30 asubuhi.

Baadhi ya wananchi katika wilaya ya Temeke, Dar es Salaam waliiomba NIDA kupunguza kuomba baadhi ya nyaraka ambazo upatikanaji wake ni mgumu ili kuondoa usumbufu.

Mwananchi ilifika ofisi za NIDA zilizopo Chang’ombe na kukuta idadi ya watu ikiwa ndogo jambo ambalo lilitajwa kuchangiwa na dalili za mvua na manyunyu yaliyokuwa yameanza.

Fatma Issa alisema licha ya kuwa jana aliombwa cheti cha kuhitimu darasa la saba na baadaye akaombwa cheti, “cha mama wakati amefariki, mimi nikiwa mdogo nakitoa wapi.”

Mjini Moshi, imeelezwa tangazo la Rais kuongeza siku limeonekana kuwachanganya wananchi kufuatia tamko lililowahi kutolewa na serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, kuwa hakuna laini itakayozimwa huku pia wakilalamikia changamoto ya kukosekana kwa mtandao.

Nyongeza na Rachel Chibwete (Dodoma), Tausi Ally, Aurea Semtowe (Dar es Salaam), Florah Temba na Janeth Joseph (Moshi)

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom