Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,096
- 15,370
Tarehe 22 Mei 2026, Dar es Salaam
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinalaani na kupinga vikali kurejea kwa kasi matukio yenye sura ya utekaji nchini. Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na visa kadhaa ambavyo baadhi ya watu walidaiwa kutekwa na baadaye baada ya mijadala mingi katika mitandao ya kijamii, Jeshi la Polisi limekuwa likiibuka kuthibitisha kuwashikilia wahusika. wanaodaiwa kutekwa.
Hata hivyo vipo visa ambavyo wahanga walidaiwa kutekwa na mpaka leo hawajapatikana. kwa mfano, Katika siku za hivi karibuni miili kadhaa ya watu waliofariki imeokotwa ikiwa inaelea kwenye maji katika maeneo tofauti huku kukiwa hakuna maelezo ya kutosha kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama juu ya vyanzo halisi vya mili hiyo kuonekana ikiwa katika hali hiyo. Sambamba na matukio hayo, mnamo tarehe 20 Mei 2026, kuliibuka taarifa za kutekwa na watu wasiojulikana kwa msaidizi binafsi wa mwenyekiti wa CHADEMA Mhe. Tundu Lissu ndugu David Jumbe katika eneo la Mabwepande jijini Dar es Salaam na baadaye kupatikana akiwa amefungwa pingu.
LHRC inaamini kuwa kuongezeka kwa matukio yanayofanana na utekaji ni ishara ya kuzorota kwa usalama, haki za binadamu na imani ya wananchi kwa vyombo vya dola. Matukio haya yanazua hofu na kutokuaminiana katika jamii. Pia, kukosekana kwa uwajibikaji kunaweza kuendeleza ukiukwaji wa sheria, kudhoofisha utawala wa sheria, haki za raia, mshikamano wa kijamii na taswira ya nchi katika kuheshimu haki za binadamu na demokrasia.
LHRC inatoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi kuzingatia taratibu za ukamataji kama ilivyoanishwa katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20, Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322 na kanuni za kudumu za Jeshi la Polisi(PGO) ili kuondoa taharuki katika jamii kwamba fulani ametekwa kutokana na ukamataji usiofuata sheria. Pia vyombo vya usimamizi wa sheria vinapaswa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kupitia Ibara ya 15(1), ambayo inaeleza kuwa: "Kila mtu ana haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru." Aidha, Ibara ya 15(2) inaendelea kueleza kuwa hakuna mtu anayepaswa kukamatwa, kufungwa, kuzuiliwa au kunyimwa uhuru wake bila kufuata utaratibu uliowekwa na sheria.
Mwisho, LHRC inashauri;
L Vyombo vya ulinzi na usalama, kuhakikisha kuwa taratibu zote za ukamataji zinafuatwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na sheria nyingine za nchi.
ii. Jeshi la Polisi liwasake kwa haraka, liwatambue, liwatie nguvuni na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watu wote wanaohusika na matukio haya ili wawajibishwe kwa mujibu wa sheria na kujibu tuhuma zinazowakabili.
Imetolewa na:
Dkt. Anna Henga
Mkurugenzi Mtendaji- Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)