Leo ni siku ya wakimbizi duniani, serikali kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa wakimbizi nchini

real G

JF-Expert Member
Feb 7, 2013
5,245
2,000
Serikali kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) inakusudia kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa wakimbizi wanaozaliwa nchini katika kambi za wakimbizi. Lengo la mpango huo ni kuwafanya watoto hao kuwa na hati zinazotambulika kisheria na zenye kubainisha waziwazi uraia wao wa asili.

upload_2017-6-20_11-15-46.jpeg


Taarifahiyo ilitolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Balozi Hassan Yahya kuhusu Siku ya Wakimbizi Duniani inayofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mpango huo unatarajia kuanza kwa vyeti vya kuzaliwa kutolewa kabla ya mwisho wa mwaka huu na utakuwa ni utaratibu wa kudumu.

“Ni vema ikafahamika kuwa hati hizo ni muhimu hata baada ya maisha ya ukimbizi. Uamuzi huu unafuatia makubaliano kati ya serikali na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na wakimbizi (UNHCR).

“UNHCR watasaidia nyenzo muhimu zinazohitajika katika zoezi hilo,” alisema Balozi Yahya na kuongeza:

“Nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wakimbizi wanapata hati zote muhimu zinazohitajika kama cheti cha kuzaliwa, kitambulisho kwa mujibu wa mikataba ya Kimataifa ambayo nchi imeiridhia.”

Mbali na mkakati huo, Balozi Yahya alisema Serikali itaendelea kuchukua hatua muhimu za kuboresha huduma kwao katika sekta za elimu, afya, makazi na kuihuisha Sera ya Wakimbizi ili ieandane na changamoto za wakati huu.

Kwa upande wa elimu, alisema Serikali inatambua tatizo la upungufu wa madarasa katika kambi za wakimbizi akisema linatokana na upungufu wa fedha zinazotolewa na wahisani kufadhili mradi mzima wa kuhifadhi maelfu ya wakimbizi toka nchi za jirani na kwingineko.

“Pamoja na hayo, nchi yetu kwa kushirikiana na UNHCR na wadau wengine itafanya jitihada za kujenga madarasa na miundombinu mingine muhimu kuhakikisha kuwa watoto wote wa wakimbizi wanapata elimu bora na ujuzi utakaowanufaisha wao na jamii zao,” alisema.

Alitaja eneo lingine litakalopewa kipaumbele kwa lengo la kuboresha huduma kwa wakimbizi kuwa ni mradi wa kuhuishwa Sera ya Wakimbizi na Sheria pamoja na mambo mengine.

Alisema sera mpya na sheria zitakazotungwa zitakusudia kupanua wigo wa wakimbizi wenye ujuzi na sifa za kupata ajira kama wataalamu katika sekta mbalimbali na pia kupata fursa za kujiari wenyewe nje ya kambi.

Akizungumzia maadhimisho hayo yanayofanyika Dar es Salaam leo yakiwa na kauli mbiu ya mwaka huu ya ‘Tuko Pamoja na Wakimbizi’, alisema Serikali inakumbusha jukumu la kila mmoja kutafuta ufumbuzi wa matatizo ambayo yamesababisha wao kujikuta katika hali hiyo.

Alisema mpaka sasa Tanzania ina jumla ya wakimbizi 345,000. Hata hivyo alisema Tanzania inaendelea kuhifadhi wakimbizi hao toka nchi za Maziwa Makuu za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Pembe ya Afrika kama Somalia na wachache toka nchi mbalimbali.

Aliongeza kuwa wakimbizi hao wanahifadhiwa katika kambi zilizoko Kigoma za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli na wengine wachache waliosalia baada ya wenzao wengi kupata uraia ambao wapo Katavi na Tabora.

“Kwa vipindi mbalimbali wamekuwepo wakimbizi tofauti tofauti kama vile wakati wa harakati za kupigania uhuru Kusini ya Afrika ambapo kulikuwa na wakimbizi toka Afrika Kusini, Namibia, Msumbiji, Angola na Zimbabwe ambao walirudi katika nchi zao baada ya ukombozi kupatikana.”

Aliitaka Jumuia ya Kimataifa kuongeza ufadhili kuzisaidia nchi changa, kama Tanzania, kutekeleza jukumu la kuhifadhi wakimbizi.

“Misaada wanayotoa inasaidia katika kupatikana bidhaa mbalimbali ambazo zitatumiwa na wakimbizi na huduma nyingine wanazohitaji. Ni vema ikaeleweka pia kuwa Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu wa kuzisaidia jamii ambazo zinaathirika na uwepo wa wakimbizi wengi kama Kagera, Kigoma, Katavi na Kigoma,” alisema Balozi Yahaya.

Awali siku hiyo ilikuwa inaadhimishwa Barani Afrika peke yake ikiitwa Siku ya Wakimbizi Barani Afrika na kuanzia mwaka 2001 Maadhimisho hayo yalianza kufanyika Duniani kote baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuelekeza hivyo katika kuadhimisha miaka 50 ya Sheria ya Kimataifa ya Wakimbizi.

Kihistoria siku hii ilikuja baada ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 2000 kukubaliana kuanzia Juni 20, 2001 na kila ikifika tarehe hiyo kila mwaka itakuwa ikiadhimishwa.

Kwa mujibu wa UNHCR, watu milioni 65.6 wamekimbia makazi yao ambapo kati yao watu milioni 22.5 ni wakimbizi na nusu yao ni watoto chini ya miaka 18.

Katika takwimu hiyo ambayo ni kubwa tangu Shirika lianzishwe, kati yao milioni 10 wamekosa uraia na huduma muhimu katika nchi walizokimbilia kama afya, elimu, na kuajiriwa.

Kwa Afrika nchi ambayo imetoa wakimbizi wengi ni Sudan Kusini (Milioni 1.4) ambayo inaungana na nchi za Afghanistan (Miloni 2.5) na Syria (Milioni 5.5) kwa pamoja zimetoa asilimia 55 ya wakimbizi Duniani.

Hali hiyo imepelekea UNHCR kuajiri wafanyakazi 10,900 kuanzia Mei 2017 ambao asilimia 87 wanafanya kazi katika makambi mbalimbali katika nchi 130 Duniani wakishughulikia masuala mbalimbali ikiwemo ulinzi wa wakimbizi.

Nchi za Kiarabu na Ulaya karibuni zimekuwa katika kiwango cha juu kuwa na wakimbizi wengi kuzidi zile zilizopo chini ya Jangwa la Sahara.

Hadi mwaka 2015 kwa mujibu wa UNHCR, watu milioni 16 Afrika walikimbia makazi yao na kuhama nchi zao ambapo katika takwimu hiyo, watu milioni 10.7 ndiyo walikimbia makazi na milioni 5.2 walikimbia nchi zao.

Nchi ambazo zimepokea wakimbizi wengi barani Afrika hadi 201 ni Kenya na Ethiopia ambazo zinapokea wakimbizi kutoka nchi za Somalia, Sudan na Sudan Kusini.

Chanzo:Mwananchi
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom