Uchaguzi 2020 Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM: Dkt. Hussein Ally Mwinyi achaguliwa Kugombea Urais Zanzibar kupitia CCM. Membe afukuzwa rasmi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,789
11,930
UPDATES 13:15hrs: Matokeo ya Kura za ya wanachama watatu waliokuwa wakiomba ridhaa ya kuwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM.

1. Dkt Hussein Ali Hassan Mwinyi -kura 129 (78.65%)

2. Dkt Khalid Salim Mohamed -kura 19 (11.58%)

3. Shamsi Vuai Nahodha -kura 16 (9.75%).
Zanzibar 2020 - Wasifu: Dr. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Rais ajaye wa Zanzibar



Leo Halmashauri Kuu ya CCM inapokea mapendekezo ya Kamati Kuu kuhusiana na waliopendekezwa kugombea Urais wa JMT na ule wa Zanzibar.

Kadhalika itapokelewa ripoti ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa miaka 5 iliyopita na kupitishwa ilani ya miaka 5 ijayo.
Mkutano uko mubashara TBC na Channel ten, ITV, Star tv na Upendo tv

=======

UPDATES:

=========

Wajumbe wameshaketi ukumbini wakimsubiri mwenyekiti ambaye ataingia wakati wowote kuanzia sasa. Rais Magufuli ameingia ukumbini na wajumbe wote wanamshangilia kwa shangwe na vigelegele.

Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM amefungua kikao hiki na kutoa rai kuwa ianzwe ajeda kubwa ya Uchaguzi wa Mgombea Urais Zanzibar

Rais Magufuli pamoja na Wajumbe wa kikao wamekubaliana kuanza na ajenda ya Wagombea Urais Zanzibar. Mpaka sasa kuna jumla ya majina matano ya Ugombea Urais Zanzibar.

Dr Bashiru amewataka Wagombea watano waliopitishwa na kamati maalumu ya halmashauri kuu kuja mbele ili kusalimia alafu baada ya mchakato huo Mwenyekiti atataja majina matatu yaliyopita.

Rais Magufuli (Mwenyekiti wa CCM) ametoa idhini ya majina matatu yaliyopendekezwa kusomwa na katibu Mkuu wa chama Dkt. Bashiru ambaye amesema kuwa Wagombea watatu waliopita ni:

1. Dkt. Khalid Salum Mohamed.
2. Dkt. Hussein Ally Hassan Mwinyi.
3. Shamsi Vuai Nahodha.
1594377643167.png


Rais Magufuli amewakaribisha Wagombea ambao hawakupita ili kutoa neno la shukrani.

Prof. Mbalawa pamoja na Mh. Hamis Mussa Omari wamekuja mbele ya wajumbe wa mkutano huu na kurumshukuru Mungu pamoja na Wajumbe kwa hatua waliyofikia pamoja na kumshukuru Rais Magufuli katika masuala mbalimbali. Sambamba na hilo, Prof Mbalawa na Mh. Hamisi Mussa wameahidi kumuunga mkono Mgombea atakayefanikiwa kupita kugombea Urais ili CCM ishinde.

Baada ya Wajumbe ambao hawakupita kutoa shukrani Rais Magufuli amewakaribisha Wagombea waliopita kutoa neno lao kwa ufupi

Hussein Ali Hassan Mwinyi
(Salamu)

Nimesimaama mbele zenu kuomba kura zenu, mnichague kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi ujao katika nafasi ya Urais wa Zanzibar.

Elimu yangu ni shahada ya Uzamili katika fani ya Udaktari wa Binadamu. Uzoefu wangu katika serikali ni wa miaka 20. Nimeingia serikalini mwaka 2000 na nipo hadi sasa.

Naibu Waziri wa Afya tangu mwaka 2020-2005. Baada ya hapo nimekuwa waziri kamili kwa miaka 15 kwa miaka mbalimbali ikiwemo ya Afya, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano; na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, nafasi ambayo nimeishika kwa miaka 11 hadi hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu kwenye chama nimekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama chetu; nimechaguliwa mara mbili. Nimekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa vipindi vitatu. Na nimekuwa kwa nafasi yangu ya Ubunge, Mjumbe wa Halmashauri Kuu za mkoa, wilaya na jimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi yangu kwenu endapo mtanichagua basi nitayaenzi Mapinduzi ya mwaka 1964 ya Zanzibar na nitadumisha Muungano wetu.

Lakini pia, nitayaendeleza yote yaliyofanya na awamu zilizotangulia, hususan awamu ya saba (7)chini ya Dkt. Ali Mohammed Shein.

Vilevile niwaahidi kwamba nitatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi yam waka 2020/25 itakayotolewa kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima na kwa unyenyekevu mkubwa, naomba mnipigie kura za NDIYO mimi Hussein Ali Hassan Mwinyi.
(Maagano)

Shamsi Vuai Nahodha
(Salamu na Shukrani kwa Mwenyezi Mungu na Chama)

Mimi Shamsi Vuai Nahodha ambaye nagombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi niliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu kwa muda wa miaka 17 na ni miongoni mwa watu wachache sana waliopata bahati ya kuitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama mtekelezaji mkuu wa Ilani kwa muda wa miaka 10 mfululizo. Nadhani rekodi hiyo inashikiliwa na mzee wangu Seif Ali Idd na mimi ninayefuata.

Nimetafakari sana wakati nimataka kugombea nafasi hii adhimu kwa taifa letu. Na nikafikia mahali nikadhani kuna jambo mimi kwa kushirikana na wenzangu ninaweza kulifanya. Kwanini nadahani naweza kuifanya kazi hii kwa ufanisi sana? Nimejifunza mengi kutoka kwa viongozi wetu wa chama na kitaifa – Dkt. Magufuli na Mzee wangu Dkt. Shein. Katika kipindi chote hiki nimejifunza karama ya uongozi. Namna kiongozi anavyotakiwa awe, tabia za kiongozi.

Dkt. Shein ametuonesha sisi vijana namna kiongozi wa kiataifa anatakiwa awe. Ni mnyenyekevu na mpole sana.

Mwaka 2010 nilisimama hapa kushindana naye. Baada ya hapo hakuonesha nongwa. Alinisikiliza kwa umakini sana. Amenitendea zaidi ya ninavyostahiki.

Watu wengi wanaofanya kazi na Shein wanaweza wanamuona wa kawaida sana kwasababu ya unyenyekevu lakini ana moyo mpana sana.

Kama nitapata nafasi ya kuchaguliwa kuwa mgombea na hatimaye Rais wa Zanzibar, nitafanya kila niwezalo kusimamia Muungano, Mapinduzi na rasilimali za Taifa letu kwa ujasiri wa juu sana.

Dkt. Khalid Salum Mohamed
(Salamu)

….Kufikia nafasi hii ni ndoto.

Nilisoma Donge, skuli ya Msingi. Elimu ya Sekondari nilisoma Fidel Castro, Pemba. Na baadaye nilienda kusoma mafunzo ya Kilimo (certificate) katika Chuo cha Kilimo Naliendele, Mtwara.

Baada ya hapo nilipata mafunzo tena Uyole, Mbeya. Nilifanya mafunzo ya Diploma Mlingano, Tanga. Na baadaye kufanya digrii ya kwanza Sokoine. Digrii ya pili ya Agricultural Economics nilifanyia Chuo Kikuu cha Reading cha UK. Nilirudi nikafanya tena digrii ya uzamivu katika chuo cha Sokoine.

Niliajiriwa toka mwaka 1980 katika Wizara ya Kilimo. Nilifanya kazi kama Afisa Kilimo wa Wilaya na Mkoa. Baadaye nikawa Mkurugenzi wa Mipango na Sera katika Katika Wizara ya Kilimo, Zanzibar. Na baadaye nikawa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto.

Mwaka 2005 nilibahatika kuwa Program Analyst katika Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na baadaye kurudi serikalini na kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo. Nilikuwa Mwenyekiti wa ZSSF, mfuko wa hifadhi ya Jamii kwa miaka 6.

Dk. Shein alinichagua kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Pale nilijifunza mambo mengi kuhusu Muungano. Nilisimamia masuala wanayoyaita “Kero za Muungano”.

Niliingia kwenye siasa mwaka 2016 baada ya uchaguzi wa marudio. Na nilichaguliwa tena na Dk. Shein kuwa Waziri wa Fedha kwa miaka mitatu hadi Machi 2019.

Uzoefu wangu wa Kisiasa. Nimejiunga na CCM tangu mwaka 1980.

Ali Mohammed Shein
…Walijitokeza wanaCCM 32 mmoja akaona mbavu zake nyembamba akawapisha wengine wakabaki 31. Tulifanya kazi nzuri sana ya kuwapima na kuwachuja. Tulifanya tukiwa na akili njema na tulifanya kazi nzuri. Tumeona wana uwezo mkubwa kwa namna walivyojieleza.

Naamini chama chetu kitashinda uchaguzi huu.

Kila mwanachama wa chama hiki ana haki yake na uhuru wake kugombea ndani ya CCM. Yasistangazwe yasiyokuwepo. Sijambeba mgombea wala sitombeba mgombea.

Mheshimiwa mwenyekiti umenitaka niseme hilo. Nimelisema waziwazi.

Rais Magufuli
Mheshimiwa Dkt Shein amefanya makubwa sana. Amenunua meli, zao la krafuu sasa hivi magendo yameisha, aejenga bvituo vya afya, hospitali nauchumi umekua kwa asilimia 7. Mzee Shein anaheshimu demokrasia na Katiba ya Chama cha Mapinduzi ndiyo maana kama watangulizi wake umefika wakati anasema “muda wangu umeisha”

Sasa kikao hiki kikayatambue haya. Kwamba tunayemchagua atakwenda kuyaendeleza na mengine makubwa zaidi.

Katika hizi kampeni kila mtu atapewa mtu wake, utasikia huyu wa fulani huyu wa fulani

Hawa wote watatu hapa wanafaa ndiyo maana Kamati Kuu ya Halmashauri ikawaleta hapa. Ila yupo anayefaa sana

Tusimame vizuri, maneno mengine yanaletwa na Upinzani na sisi tunayabeba tu

Tuchague vizuri ili mtu akatuongoze vizuri. Na mimi nina imani atakayeshinda hapa atakuwa Rais wa Zanzibar. Tuanze kupiga kura

Rais Magufuli amsamehe Abdulrahman Kinana
Ilikuwa mwezi wa wa pili Central Committee ilaamua kutoa adhabu kwa baadhi ya wanachama wetu ambao walikiuka maadili na misingi ya chama chetu.

Kikao kile kilitoa mapendekezo ya adhabu kwa baadhi ya wanachama wetu kutokana na misingi na Katinba halali ya chama chetu. Lakini ni hivi karibuni baada ya miezi kama mnne au mitano, mwenzetu mmoja ambaye ni Former Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi alijitokeza hadharani kule Arusha, na nafikiri shahidi ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha – akaomba radhi., akautia kwa kitendo alichokifanya. Na kikubwa zaidi, ndugu yetu huyu aliomba radhi hadharani.

Ni kitendo kigumu sana kwa mtu kukifanya. Kinahitaji nguvu ya Mwenyezi Mungu tu kutubu hadharani. Mimi alinigusa sana. Nina uhakika hata ninyi wajumbe muliguswa sana. Alikuwa amepewa adhabu ya miezi 18. Hakukataa kutumikia adhabu ile.

Sasa niliona Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama tawala, chama chenye huruma. Chama chenye mapenzi mema. Chama dume. Niwaombe kwa huruma yenu kama itawezekana, huyu ndugu yetu ambaye amekubali mpaka sasa kutumikia adhhabu miezi mine, tumsamehe.

Kupitia kikao hiki napenda kusema Abdulrahman Omari Kinana amesamehewa rasmi. Niwashukuru wajumbe wa kikao hiki kwa huruma ya upendo

Yule mwingine ambaye hata jina lake sitaki kulitaja yeye ameshaondoka moja kwa moja. Adhabu yake si mnaikubali?

.....Wajumbe wamshukuru na “kumpashia’” Mwenyekiti kwa kulifikisha taifa Uchumi wa Kati....

Ujumbe toka Songwe kuhusu wanasiasa wa vyama pinzania kupewa nafasi za uongozi CCM
Kuna malalamiko ya Wanasongwe kwamba wanacham,a wa vyama vya upinzani wanavyotoka kule kuja kwetu, kwetu ni neema. Na kama Katiba ya CCM inavyosema kuwa kila binadamu ni sawa, , ni kweli tunawapokea; lakini wananchi wamekuwa wakivunjika sana mioyo wanapopewa nafasi za uongozi katika chama chetu na kuwaacha wanachama wa CCM ambao walipigana kufa na kupona 2010 hadi 2015.

Wanavunjika mioyo kuona wanapita bila mbadala, na viongozi wa CCM walio sehemu husika wakiwa wanawasapoti kwa asilimia nyingi. Kwahiyo Mwenyekiti, hilo ni la Wanasongwe siyo langu, hasa kwa jimbo letu la Tunduma na Momba, hali ya kisiasa siyo nzuri nimeona niliweke vizuri.

Majibu ya Mwenyekiti Magufuli:
Nimekusikia. Nilifikiri hilo ungelizungumzia kwenye kamati yako ya siasa ya wilaya na ya mkoa kwamba wanaokuja huwahitaji. Lakini chama hiki ni chama cha watu wote; kina misingi yake, kinameza watu wote kwahiyo kama hilo suala kama lipo kule mulitafutie ufumbuzi. Makongoro alikuwa NCCR lakini sasa hivi ni CCM damu damu. Mzee Wasirra alwahi kwa NCCR. Wakati mwingine tuwe na mioyo ya Kumtanguliza Mungu.

Tatizo moja la siasa zetu tutanajiwekea vizingiti kwamba huyu akija atatushinda lakini mukiachiwa hamushindi.

MATOKEO YA UTEUZI
Job Ndugai:
Kwa niaba ya timu ya wasimamizi naomba nisome matokeo kama ifuatavyo:

Ndug. Shamshi Vuai Nahoda amepata asilimia 9.75 ya kura, ambazo ni kura 16

Dkt. Khalid Salum amepata asilimia 11.58, ambazo ni kura 19

Na Dkt. Hussein Mwinyi amepata kura 129, ambazo ni asilimia 78.65

Naomba kuwasilisha

Mwenyekiti Magufuli atangaza rasmi uteuzi wa Dkt. Mwinyi
Kwahiyo ndugu zangu wajumbe, kwa matokeo haya ambayo ninyi mumeamua kwa hiari yenu, bila kulazimishwa na mtu, bila kushurutishwa na mtu, kwa upendo wenu moyoni, kwa kumtanguliza Mungu wenu na kwamba aliyechaguliwa mutakwenda kumtetea kwa nguvu zote kwa ajili ya CCM na maslahi ya CCM. Dkt. Hussein Mwinyi ndiye atakuwa mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar.

Neno la Shukrani toka kwa Dkt. Mwinyi
Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu aaliyetujalia kukamilisha shughuli hii kwa salama na Amani.

Wagombea tulikuwa wengi, na hatimaye leo nimepatikana kuipeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar. Ni heshima kubwa sana. Kura nilizopata hapa ni nyingi sana. Hii inaonesha Imani yenu juu yangu. Nitalitumikia taifa kwa uwezo wangu wote.

Sasa hivi hakuna Team Mwinyi, sisi sasa ni Team CCM.

Katika maisha yangu nimefanya mitihani mingi, lakini mkubwa kuliko yote ulikuwa ni huu.

Mkutano huo wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, kwa kauli moja umempitisha John Magufuli kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Hotuba ya Rais Magufuli
Umeusimamia vizuri Muungano. Sikupata shida mzee wangu, kila nilipokuita uliitikia. Tume-solve mambo mengi, umekuwa mkweli mno - Nataka niwaambie ndugu zangu, kuongoza hakuhitaji makeke, matusi. Huyu baba ni mnyeyekevu. Najua huwezi kupendwa na kila mmoja

Uliyatimiza yaliyo mazuri kwa Zanzibar. Ajira, umefanya mengi. najua kesho kwenye Mkutano Mkuu yatazungumzwa - Ninachowaomba ndugu zangu Wazanzibari jengeni umoja wenu. Msisikilize mengi yanayosemwa na Wapinzani mkayabeba

Hata baada ya Uchaguzi huu watazungumza mengi, labda kwa kuwa Uchaguzi huu ulikuwa 'live'. Wanaosema si WanaCCM, maneno ni ya Wapinzani wenu - Bila CCM, Zanzibar hakuna Muungano, hakuna maendeleo. Zanzibar ni nchi tajiri, wanaitamani mabeberu

Kuchaguliwa huku tumtangulize Mungu, alipanga siku moja Mwinyi atashinda. Hata mimi sikujua kama siku moja nitakuwa Rais- Ila kwa mapenzi ya Mungu akasema nitakuwa Rais. Siwezi kuwa na kiburi kwa nafasi hii, hii kazi ni ya utumishi na utumishi una gharama

Nilikuwa nakumbuka Mwanamama Catherine, anafanya kazi kubwa ila alipata misukosuko hadi wengine wakawekwa ndani- Nikazungumza Kiongozi uliyemteua wewe anamuweka ndani kiongozi wa CCM kwa kosa ambalo halipo? Nashukuru ulichukua hatua

Napenda kuwashukuru tena kwa msamaha mlioutoa kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana. Ametubu hadharani na ninyi mmemsamehe hadharani. Asanteni sana- Nimemuagiza Katibu Mkuu amualike Kinana kesho kwenye Mkutano Mkuu pamoja na Wastaafu wengine.
 
Wazanzibari hata siwaelewi; yaani wana jeshi, mahakama, wimbo wa taifa lao, na bunge.

Lakini pamoja na mbwembwe zao zote hizo, Rais wao anachaguliwa Dodoma, Tanzania Bara, sijui wanakwama wapi?!.

Hii ni sawa na baba wa familia kuwa na nyumba yako, unaacha pesa ya matumizi kila siku, lakini chakula kinapikwa kwa jirani, na umeshazoea kwenda kula huko.
 
Kuna kijana amezuiwa kupewa maiti ya mkewe hapo Muhimbili National Hospital mpaka atakapolipa shilingi 1,470,800.

Wasamaria walimsaidia kuchimba kaburi ili amhifadhi marehemu mkewe lakini kutokana na kuwekewa ngumu na serikali ya wanyonge, wamelazimika kufukia kaburi kisha kumchangia fedha za nauli kijana huyo ili arejee kwao Mtwara.

Hivi sasa huyo bwana yuko njiani akielekea makwao akiwa amebeba kichanga cha wiki tatu na maiti ya mkewe ikiendelea kushikiliwa hapo Muhimbili.

Huyu ni mmoja kati ya wapiga kura mnaowategemea. Kwa hakika hakuna chama cha kidhalimu duniani kinachoweza kuishinda CCM.

Kama umeguswa wasiliana na huyu mnyonge anayeteseka kwa kunyimwa mwili wa mpendwa wake kwa namba ya simu 0778 140 361
 
Back
Top Bottom