Leo ndio ilizaliwa Tanzania

Mtu wa Pwani

JF-Expert Member
Dec 26, 2006
4,184
671
Leo ni Muungano
2008-04-26 09:18:54
Na Mhariri.


Leo ni Kumbukumbu ya Siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutimiza miaka 44 ambapo sherehe hizo kitaifa, zinafanyika katika Uwanja wa zamani wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo zitakazohudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa kitaifa na wananchi ambapo pamoja na mambo mengine, atakagua gwaride lililoandaliwa na vikosi mbalimbali vya Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Mhariri na timu yake yote ya gazeti hili, inawatakia sikukuu njema Watanzania wote katika maadhimisho hayo muhimu ya kitaifa.



SOURCE: Nipashe
 
44 years lakini bado viongozi wetu wanadai Tanzania ni nchi changa!
Hivi tunapata faida gani kwenye huu muungano? Somebody pse help!
 
kule kwetu tunasema muunganu udumu

maana si haba akina woowoowoo wanatufikia kwa wingi
 
Mpaka leo hii kero za muungano zinakwepwa kujadiliwa kwa mapana na marefu....kwani kuna siri gani kati hapo???suala la muungano pia lijadiliwe kwa kura ya maoni litafanikiwa sana sana ni maoni yangu tu
 
zijadiliwe vipi?

kuna kamati ya pamoja baina ya zanziba na bara

kule waziri kiongozi na huku waziri mkuu.

pia kuna wizara ya mambo ya muungano
 
Wazanzibari wameonekana na mabango wakidai kura ya Maoni kuhusu muungano ambao umijaa kero zisizotibika,wanaziita AIDS.
 
Nisaidieni Kujua Jinsi Ya Kuanzisha New Thread


Ukiingia kwenye jukwaa la siasa juu kushoto Utaona maandishi New Thread bonyeza hapo na utapelekwa kwenye ukurasa mpya ambao utaweza kuanzisha new thread.
 
Huu Muungano bado ni wa upande mmoja. Kuna kasoro nyingi sana, lakini zile ambazo ni wazi ni kama vile Zanzibar kuwa na Serikali yake (SMZ), kuwa na wabunge wake (wawakilishi kwa upande wa Zanzibar, na wabunge wa muungano).

Kasoro nyingine ni pale ambapo TRA wanadai kodi upya kwa Watanzania wanaoamua kwenda Unguja kununua vitu mbali mbali, hususan magari. Unaweza kutozwa kuanzia laki 3 hadi 9, kama "tofauti" ya kodi, yaani, tofauti ya kodi inayotozwa Unguja na ile inayotozwa Bara. Kwa nini kuwe na tofauti? Yaani, watu wa Unguja wana unafuu katika kulipa kodi?

Tujadili kuhusu huu Muungano, tuone kama bado una faida kwetu sote. Nani haswa anayefaidika? Kama kweli ungekuwa Muungano halali, basi, hakungekuwa na Rais wa Zanzibar, bali, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini hata hivyo hapo kuna utata... kwani, huyo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano angetawala Zanzibar peke yake?

Hili suala ni gumu kuliko tunavyolifikiria. Tatizo ni kwamba, waasisi wa Muungano huu leo hawapo, na sisi hata pale ambapo walipokuwa hai hatukuwa na "ubavu" na kuwaambia, Mwalimu Nyerere hapa umekosea, au Sheikh Karume, hapa si sawa.

Mjadala uendelee.

./Mwana wa Haki
 
Wana JF

Ni furaha ilioje kuwa sasa muungano wetu umetimiza miaka 44. Ni muungano pekee wa nchi mbili za Afrika ambao umedumu muda wote huu licha ya misukosuko kadhaa. Yale yanaitwa kero za muungano ni mengi kweli kweli na kila siku yanaongezeka. Mafuta yatakapoanza kuchimbwa/kupatikana huko Pemba, Muungano utakuwa katika jaribio kubwa sana.

Nadhani ni wakati sasa wa kujadili Muungano wetu kwa lengo la kupitia upya na ikibidi kufanya mabadiliko makubwa ili tudumu miaka 44 mingine.

Prof. Isa Gulamhussein Shivji amezindua Kitabu juzi kinaitwa 'Pan-Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika-Zanzibar Union.'

Ni kitabu kilichofanyiwa utafiti mzuri na kimetoa picha nzima ya Muungano, ulivyotokea, yaliyompata Aboud Jumbe kwa kutaka Muungano urekebishwe mwaka 1983 - 1984 na hali ya sasa. Ni kitabu cha kusoma hasa.

Bila ajizi, Shivji, katika moja ya sentensi zake za hitimisho anasema, 'constitutionalism and Democracy were least respected both in the formation of the Union and its continued existence. Political pragmatism and expediency governed the relationship (between Tanganyika and Zanzibar)'

Kama muungano wetu utaendelea kuwapo kwa sababu tu ya ridhaa ya chama kinachotawala na mfumo wa muungano ukawa ni zao la sera ya chama fulani cha siasa, muungano hautadumu. Ni vema muungano ujengwe katika misingi imara ya katiba na kukubalika na pande zote mbili.

Ni wakati wa kuangalia mfumo wa muungano ambao utakuwa thabiti bila kupoka utaifa wa nchi zinazoungana. Huu ni wakati wa kufanyia mabadiliko muungano wetu ili kuuimarisha.

Kuna majibu rahisi sana hutolewa katika suala la mfumo wa muungano. Vyama vyetu ya siasa vinasema ama tuwe na serikali mbili (CCM) au serikali tatu (CHADEMA, CUF, NCCR-M etc). Mpaka sasa hakuna chama cha siasa kinachosema wazi kinataka serikali moja (ofcourse, kuogopa backlash from Zanzibar). Kwa mfumo wowote tutakaoutaka katika muungano lazima kutambua kuwa mataifa haya yalipoungana yalikuwa ni mataifa mawili tofauti. Jamhuri mbili zilizozaa dola moja. Hivi sasa vijana wengi tunajua Tanzania tu. Wengine ukituambia turudi kuitwa raia wa Tanganyika tutakataa kata kata. Mimi nitakataa. Lakini Wazanzibari wengi wanegependa kuitwa raia wa Zanzibar. Ni vema tulijadili hili kwa mapana. Tuone kama tunaweza kuwa na mfumo mzuri wenye kutoa uhuru wa ndani kwa mataifa yaliyoungana lakini kubakia na muungano wenye nguvu sana.

Tume ya Nyalali ilipendekeza kuwe na serikali tatu na Marais watatu (Comoro style). Mwalimu alikataa. Nakubaliana nae katika hili kwani mfumo ule ungevunja muungano mara moja. Lakini haituzuii kufikiri. Hivi mfano tukiwa na Rais mmoja wa muungano mwenye nguvu, jeshi, polisi, uhamiaji, fedha za muungano, mambo ya nje,Biashara ya nje na mambo yote yale 11 ya awali kabisa ya muungano, na tukawa na Mawaziri Wakuu kwa Tanganyika na Zanzibar wanaotokana na chama chenye wajumbe wengi katika mabunge yao, itakuwaje? si tutakuwa tumepata serikali 3 zenye ufanisi na mgawanyo wa madaraka ulio wa wazi na bado kubaki na dola moja?

Mimi nadhani tufikiri, kujadili na kuamua kuhusu muungano. Hatuwezi kuwa na sababu zilezile za 1960s kutetea muungano. Hautadumu. Tuweke mfumo utakaodumisha muungano na hata kuvutia nchi nyingine kuingia katika muungano maana watakachopata ni ulinzi wa dola lakini mamlaka ya ndani yataendelea kuwapo. Burundi waweza jiunga, Rwanda pia na hata Comoro.....!!!!! kwa sababu watabaki na Mawaziri wakuu watendaji watakaopatikana kutoka na uchaguzi na kuthibishwa na mabunge yao na kuwa na uhuru kabisa na mambo ya ndani ya nchi zao.

Tutafakari muungano wetu!
 
Muungano uliozaliwa na nchi mbili Tanganyika na Zanzibar. Swali, kwa nini Zanzibar bado iko hai wakati Tanaganyika ililazimishwa kuuwawa? Je, tunaweza kuifufua Tanganyika?
 
Salim Said Salim
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania iliyounganisha Bara (Tanganyika) na Visiwa vya Unguja na Pemba (Zanzibar) leo imetimiza miaka 44 tokea kuundwa kwake.


Muungano huu ulikuja kwa kushitukizia. Wananchi hawakuutarajia kwa vile hapakuwepo fununu wala minong’ono juu ya kuundwa kwake.

Tangazo la kuundwa kwake, lilitokana na mkutano uliofanyika Dar es Salaam kati ya aliyekuwa Rais wa Tanganyika (enzi hizo), Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Wolfango Dourado, amesema mara kwa mara hakushauriwa na hakuwa na habari ya mazungumzo ya kuundwa kwa Muungano. Hata baadhi ya mawaziri katika Serikali ya Rais Karume, akiwemo marehemu Abdulrahman Babu, walisema hawakushauriwa juu ya kuundwa kwake.

Wakati ule nikiwa kijana wa karibu miaka 18, nilisikia kwa mara ya kwanza kuundwa kwa Muungano kupitia taarifa ya habari iliyosema Mwalimu Nyerere na Karume wametia saini mkataba wa Muungano.

Mambo yaliotajwa kuwa ya Muungano yalikuwa 11, ikiwa ni pamoja na mambo ya ndani, mambo ya nje na ulinzi.

Katika makubaliano yale, Zanzibar ilikuwa na mamlaka kwa mambo mengi kama fedha, biashara, ushirikiano wa kimataifa, elimu, kilimo na afya.

Siku hizi baadhi ya mambo haya yamekuwa ya Muungano, huku zikisikika kelele kwamba yameingizwa katika orodha hiyo kiujanja ujanja.

Hivi leo, idadi hasa ya mambo ya Muungano haijulikani kwa uwazi. Huyu anasema hili na yule anasema lile. Wapo wanaosema ni 29, wapo wanaoeleza kuwa ni zaidi ya 35 na wapo wanaosema hawajui.

Ukitaka kujua hali halisi, jaribu kufanya utafiti mdogo kwa wabunge au wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wakiwamo mawaziri, kuwataka wakwambie mambo gani ni ya Muungano na yepi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina mamlaka nayo.

Kama utawauliza watu 20, wakitokea wawili ambao orodha zao zitafanana itakuwa ni miujiza. Si ajabu hata orodha ya Rais wa Muungano, Jakaya Kikwete na ya Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume nazo zisifanane.

Licha ya kupambana na misukosuko ya kila aina, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wabunge wa Bara kudai kufufuliwa Jamhuri ya Tanganyika na wengine wa Visiwani kutaka mahakama itamke Muungano si halali, Muungano huu umedumu muda mrefu kuliko wowote ule uliofanyika barani Afrika.

Baadhi ya miungano iliyoundwa na baadaye kuvunjika ni kama ule wa Guinea iliyounda muungano wa kisiasa na Ghana mwaka 1958 na Mali ilijiunga 1961, lakini ilipofika 1963 kila nchi ilichukua njia yake.

Rwanda na Burundi, zilikuwa nchi moja mwanzoni mwa karne ya 20 na kujulikana kama Rwanda-Urundi, lakini mwaka 1962 kila upande ukawa nchi.

Senegal na Gambia ziliungana na baada ya muda zikavunja muungano na kugawana mbao. Eritrea ilikuwa sehemu ya Ethiopia, lakini leo ni nchi mbili hasimu.

Guinea Bissau ilikuwa sehemu ya visiwa vya Cape Verde, lakini leo kila moja ni taifa huru. Somalia ni nchi iliyogawanyika vipande na orodha ya majina yake hata wenyewe Wasomali hawaijui.

Mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1960 wakati wa kugombea uhuru, lilikuwepo Shirikisho la Nyasaland lililokuwa la nchi tatu ambazo leo ni Malawi, Zimbabwe na Zambia.

Kudumu kwa miaka 44 kwa Muungano wa Tanzania, ni jambo la kupigiwa mfano, lakini ukweli ni kwamba Muungano wa Tanzania una matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Kinachosikitisha ni kuona matatizo haya yanafumbiwa macho kama vile hayapo na hayaonekani.

Hivi sasa wapo wanaosema mfumo wa serikali mbili ndio mzuri, lakini wapo wanaotaka uwe wa serikali tatu na wapo waliosema serikali moja ndiyo safi na hata kuwahi kuelezwa na kiongozi wa juu wa CCM kwamba sera ya CCM ilikuwa serikali mbili kuelekea moja. Ziliposikika kelele za kukataa serikali moja kutoka Visiwani, tamko lile likamwagiwa maji ya moto.

Baadhi ya wanasiasa Visiwani na raia wa kawaida wanalalamika hadharani na vibarazani kuwa kila siku zikienda mbele Zanzibar inamezwa ndani ya Muungano na kukandamizwa hasa katika mambo ya uchumi na biashara.

Wengine wanadai Wazanzibari hawana haki ya kuamua mambo yao na lile wanalolitaka wao hupinduliwa linapojadiliwa Bara. Mfano unaotolewa ni katika kura za maoni ndani ya CCM wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi.

Katika Baraza la Wawakilishi suala la uchimbaji wa mafuta kuwa la Muungano lilizusha balaa na viongozi wa Serikali ya Zanzibar kusema mafuta yameingizwa katika orodha ya mambo ya Muungano kupitia mlango wa nyuma.

Viongozi hawa walitaka dhahabu na almasi ziingizwe katika kikapu cha Muungano na si Bara iendelee kufaidika peke yake na madini hayo.

Kwa upande wa Bara wapo wanaoona Zanzibar inafaidika zaidi na kusema Serikali ya Muungano inaidekeza sana.

Wapo wanaoshangaa kusikia baadhi ya wakati Hazina ya Muungano imetoa fedha kulipa mishahara ya watumishi wa Serikali ya Zanzibar.

Mara kadhaa wapo walioshauri kufanyika kura ya maoni juu ya Muungano, lakini wapo waliohisi baada ya miaka 44 hapana haja ya kufanya hivyo.

Sababu wanayoitoa ni kuwa, zaidi ya theluthi mbili ya Watanzania wa leo hawajui habari za Tanganyika wala Zanzibar kama dola tofauti.

Badala yake panasikika ushauri wa kura ya maoni juu ya kuundwa serikali ya mseto Zanzibar na mambo ya Muungano.

Lakini masuala ya kuondolewa dhamana ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Muungano kama ilivyokubaliwa awali katika mkataba wa Muungano na kuondolewa hati za usafiri kati ya Bara na Visiwani hayasikiki kuzungumziwa kura ya maoni. Kwa kifupi kilichopo ni vurugu tupu.

Mwanasiasa maarufu, Rashidi Kawawa, ambaye alikuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere na Mzee Karume, alisema mwaka juzi kuwa ni dhambi kuhoji uhalali wa Muungano. Hakueleza kwa nini ni dhambi kuhoji Muungano na isiwe dhambi kutaka kura ya maoni kwa suala la serikali ya mseto.

Wapi duniani dhana ya serikali ya umoja wa kitaifa imeonekana kutotakiwa na watu wake, kama watu hao si wachawi? Watanzania tunasema umoja ni nguvu, sasa hivyo umoja huo utajengwa kwa kukataa serikali ya umoja wa kitaifa?

Ukweli ni kwamba Muungano una matatizo, isipokuwa pakitokea mvutano na hata kusikika lugha za hasira kutoka kwa viongozi wa Bara na Visiwani, juhudi za haraka haraka hufanywa kuziba viraka kwa kutumia chandarua.

Hapo utaona panatumika zaidi siasa kupooza tatizo na si kuiangalia hali halisi kwa undani na kupata ufumbuzi wa kudumu.

Kwa ujumla, viongozi kutoka Bara na Visiwani wanapata shida juu ya Muungano. Anavyoona huyu ndivyo mwingine anaona sivyo. Matokeo yake ni kuwababaisha wananchi.

Utasikia huyu anasema suala fulani ni la Muungano na mwingine wa upande wa pili anasema jambo hilo lipo katika mamlaka ya Zanzibar.

Mifano ni suala la Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (IOC) na kujitoa baada ya vuta nikuvute iliyokaribia kupeleka kamba ya Muungano kukatika.

Zanzibar ililazimishwa kujitoa ili Serikali ya Muungano ijiunge, lakini sasa ni zaidi ya miaka 10 na suala hilo haliguswi, huku Wazanzibar wakilalamika.

Zanzibar iliwapeleka mahakamani watu 18 kwa shutuma za kutaka kuipindua serikali na kumuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour miaka minane iliyopita.

Kinachoonekana hapa ni sawa na kusema mjukuu ni wangu, lakini mama yake au baba yake sikumzaa.

Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambayo ni ya Muungano ilisema Zanzibar si dola na kwahivyo uhaini hauwezi kufanyika.

Alipouawa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume mwaka 1972, zaidi ya watu 50 walifunguliwa kesi ya uhaini Zanzibar.

Wakati ule hoja ya kusema uhaini hauwezi kufanyika Visiwani kwa kuwa Zanzibar si dola haikujitokeza. Wakati ule Muungano ulikuwa na miaka minane.

Mwaka jana, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alisema madai ya ukiukwaji haki za binadamu Zanzibar yaliyotolewa bungeni, Dodoma, yangelishughulikiwa na Tume ya Haki za Binadamu ya Muungano.

Serikali ya Zanzibar ikaja juu na kusema tume, ijapokuwa ilikuwa na wajumbe kutoka Visiwani, haikuwa na mamlaka ya kufanya kazi Zanzibar. Sasa Zanzibar imelegeza kamba na tume inatarajiwa kufanya kazi Visiwani, lakini kwa kiasi gani itaweza kutanua mbawa zake Zanzibar haijulikani.

Zipo wizara ambazo si za Muungano ambazo zimekuwa zikiongozwa na Wazanzibari na hili limekuwa likilalamikiwa na kuulizwa kwa nini watu kutoka Bara hawachaguliwi kuwa mawaziri katika Serikali ya Zanzibar? Vile vile wapo Wazanzibari waliogombea ubunge Bara, lakini watu wa Bara ni mwiko kugombea uwakilisha au udiwani Visiwani.

Hii ni hoja ya msingi, lakini hili linafumbiwa macho kwa sababu za kisiasa.

Serikali ya Zanzibar iliikataa Tume ya Kupambana na Rushwa na Ufisadi ya Muungano kufanya kazi Visiwani kwa vile rushwa na ufisadi si mambo ya Muungano.

Rais Kikwete ameonekana kutaka kujaribu kupata ufumbuzi kwa hayo mambo yanayoitwa kero za Muungano kwa kufanyika mazungumzo ya mara kwa mara ya pande mbili.

Mpango huu ni mzuri, lakini suala ni je, nia ya kweli ipo kumaliza hizo kero za Muungano?

Wapo wanaouliza kwa nini watu hawa wachache wawe na kibali cha kuamua hatima ya nchi hii na Rais Kikwete asilione hili jambo muhimu kama suala la serikali ya mseto, na kwa hivyo bora kupata ridhaa ya wananchi kwa kutumia kura ya maoni ili sauti za wananchi zisikike?

Jambo muhimu ni kwa viongozi kuelewa huu ni Muungano wa watu na si wa viongozi pekee au watu wa chama fulani.

Wakati viongozi wanabadilishana mawazo juu ya Muungano na raia nao wapewe nafasi ya kufanya hivyo.

Muungano una matatizo mengi. Faraja iliopo ni kwamba, wachache ndio wanaosema hawautaki, isipokuwa wanatofautiana juu ya mfumo na namna unavyoendeshwa.

Wapo viongozi, hasa wa Zanzibar, ambao huutumia Muungano kama karata yao ya mwisho pale wanapotaka jambo lao na wenzao wa Bara kuona walitakalo wenzao si jambo jema. Hapo ndio utawasikia watu hawa wakisema: “Tuachieni na Zanzibar yetu na nyie mkae na Tanganyika yenu.” Huu ndio ukweli na inafahamika.

Hawa ni watu hatari kwa Muungano ambao umewaleta pamoja watu wa Bara na Visiwani licha ya kuwepo matatizo.

Wapi Muungano umetokea inaeleweka, ijapokuwa hakuna ajuaye hiyo nakala ya mkataba asilia wa Muuungano ipo wapi na unasema nini ili utumike kama hadidu rejea tunapozungumzia kero za Muungano.

Hata hivyo, safari ya Muungano ya siku zijazo ni tabu kutabiri kama ulivyo upepo wa Bahari ya Hindi. Vile vile haieleweki kama nahodha wa hiki chombo kilichokuwepo safarini yupo mbele kama ilivyo safari ya meli au yupo nyuma kama ilivyo safari ya ngalawa.

Abiria wanajua wapo kwenye chombo na wapo safarini, lakini wapi wanakwenda hawafahamu!

Ni vizuri matatizo yaliyopo yakapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuimarisha Muungano. Watanzania wamechoshwa na nyimbo ya “tupo mbioni kushughulikia kero za Muungano”. Ni vizuri hizo mbio sasa zikafika mfundoni au angalau watu wakaelezwa zilianzia wapi, ni za masafa gani, zipo wapi na mwisho wake upo wapi.

Tuadhimishe Muungano kwa kufurahia mafanikio yetu kama taifa la watu wanaoelewana, lakini tusipuuze matatizo tuliokuwa nayo.
 
Mzee Zitto, heshima yako!

Hakika umenena. Hata hivyo, kwa maoni yangu, nadhani tatizo la Muungano wetu siyo tofauti na matatizo mengine yanayolisibu Bara letu la Africa. Mosi, katiba za nchi zetu zimewapa madaraka makubwa viongozi wetu, pili, katiba hizo hizo, zimewanyima wananchi mamlaka ya kuamua mustakabari wa nchi zao.

Binafsi nimekuwa nikiwashangaa wanao hoji uhalali wa jinsi Tanzania ilivyoundwa, bila kuhoji uhalali wa jinsi Tanganyika ilivyoundwa. Kwa ufupi, wananchi tulikwisha ungana. Muungano wa wananchi ulikuwapo kabla ya Tanganyika na kabla ya Tanzania. Awali ya yote, sisi wote asili yetu ni moja. Walioleta matatizo ni wakoloni kwa lengo la kututawala. Wanaoleta matatizo sasa hivi ni wanasiasa kwa lengo hilo hilo la kutawala.

Tazama, toka nikiwa mdogo, sikuwahi kujua kama Mpemba alitoka Zanzibar. Dada zangu walinituma mafuta ya kibatari, mkate, maziwa, unga, mchele, nakadhalika. Nimelelewa nikitambua kuwa mahitaji muhimu yalipatikana kwa Mpemba na Mangi. Sikuwahi kuishi Pemba wala Moshi, lakini sikuwahi kuwa allergic na Wachaga au Wapemba. Hii ina maana kwamba, wananchi tulikwisha kuungana na mahusiano yetu (Mhaya, Mpemba, na Mchaga) yalikuwa kama nilivyoyaeleza.

Tanganyika ilipoungana na Zanzibar, ilizaliwa Tanzania, na Tanganyika ikafa. Hivi kuna Mtanganyika yeyote aliyepata ukurutu eti kwa sababu Utaifa wa Tanganyika ulipotea? Sasa inakuwaje Zanzibar wanasema tukiungana ikawa Serikali moja, watapoteza utaifa wao? Lengo la mwanasiasa yeyote ni kupata madaraka. Lengo la chama cha siasa chochote ni kupata madaraka, kwa kisingizio kuwa, eti ili kiweze kutekeleza sera zake.

Suala la hatima ya Muungano wetu haliwezi kuamuliwa na watu ambao lengo lao ni madaraka. Amini usiamini, Maalimu Seifu angependa kuwa na Serikali ya Pemba, Karume angependa kuwa na Serikali ya Unguja, Kikwete angependa kuwa na Serikali ya ukanda wa Pwani, Mbowe angependa kuwa na Serikali ya ukanda wa kaskazini, nakadhalika. Hiyo yote ilimradi kila mtu awe na madaraka. Ndio maana wanasiasa wetu wanataka Serikali mbili, tatu, nne, tano, sita, na kuendelea.

Wazo la Serikali moja haliingii akilini mwa vyama vya siasa na wanasiasa wenyewe, kwa sababu linapunguza madaraka, yaani badala ya Marais wawili, watatu, wanne, au watano, (kama watakavyo wanasiasa weneywe), tutatakiwa kuwa na Rais mmoja. Binafsi, si mwanachama wa chama chochote cha siasa, na wala siyo mwanasiasa. Ukiniambia tuwe na Serikali moja chini ya Rais mmoja, na Waziri Mkuu mmoja, sina matatizo yoyote, kwa sababu sijawahi kutatizwa au kukwazwa na ujirani wa Mpemba.

In fact, ujirani wangu na Mpemba umeninufaisha kwa kunipatia mahitaji muhimu kutoka katika duka lake kwenye kona ya mtaa wetu. Na yeye alinufaika kwa kupata faida ya biashara yake. Ushirikiano, ujirani na kuchanganyikana kwetu, haukufuta utamaduni wa Mpemba, au utamaduni wangu wa Kihaya. Zaidi ya yote, tukiwa na Serikali moja, mimi na mpemba tutapunguziwa msalaba wa kugharamia viyoyozi na mashangingi ya viongozi wa Serikali mbili, tatu, au nne. Jamani! Serikali mbili zinatutoa makamasi na kututia umasikini. Juu ya yote, wanasiasa wanataka kutuongezea Serikali nyingine?

Raia wengi wa Bara na Visiwani siyo wanansiasa na wala siyo wanachama wa vyama vya siasa. Haya mawazo ya Serikali tatu, nne, na kuendelea ni ya wanasiasa na kwa sababu wanaangalia baadae zao na wala sio baadae za wananchi. Nadhani ni makosa kuendelea kuwaachia wanasiasa na vyama vya siasa kuamua mustakabari wa muungano wetu. Raia hawana matatizo, wanachochewa tu na wanasiasa.

Eti tukiungana na kuwa Serikali moja, Watanganyika na Wazanzibari watapoteza utamaduni wao na mwishowe utaifa wao. Tazama kizazi kipya cha Tanzania sasa hivi! kuna utamaduni gani? Ni saida Karoli peke yake anayeweza kucheza ngoma ya Kihaya. Vijana wa kisasa, siyo tu ngoma za makabila yao, hata lugha za makabila na lugha ya taifa ya Kiswahili inawapiga chenga. Vijana wanavaa suruali utafikiri zimeelemewa na kinyesi. Wanaume wanavaa eleni, wengine wanapeperusha bendera za Marekani, wengine wanaimba utafikiri mtu kameza chura. Je huo ni utamaduni wetu?

Tamaduni nizionazo sasa hivi nchini kwetu ni za ulaya. Je tumeungana na taifa lolote la ulaya? Utaifa wetu? hivi tunavyoweka uchumi wetu mikononi mwa mataifa tajiri mbona hatukumbuki uhuru na utaifa wetu? kwani tumeungana na nchi tajiri mpaka kuuza utaifa na uhuru wetu? Wanasiasa acheni kuwaghilibu watu. Binafsi nadhani tunahitaji Serikali moja, Rais Mmoja, na Waziri Mkuu mmoja. Kama Wazanzibar wanaona hilo haliwezekani, basi hakuna haja ya kuendelea kuwabebesha wananchi msalaba wa Serikali Mbili au zaidi.

Viongozi wanaoshindwa kwa kura lakini hawataki kutoka madarakani. Wanaoingia madarakani kwa kuhonga, tena kutumia fedha ya wananchi (EPA -BOT replica). Waliyotayari kumwaga damu za watu ili waendelee au watwae madaraka. Na wanaowaibia wananchi kila kukicha, hawawezi kuachiwa peke yao kuamua muundo wa Muungano. Wataukataa Muundo wa aina yoyote unaowapunguzia ajira, hata kama utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi. Rai yangu ni wananchi kuendeleza mchakato kama huu wa JF, ili kuhakikisha kuwa maamuzi magumu kama haya yanatolewa mikononi mwa wanasiasa na kurudishwa mikononi mwa wananchi wote.
 
Kwa ufpi Tanganyika haikuondoka au serikali yake haikuzamishwa ipo lakini imekuwa paused.Anytime ikitakiwa inaweza kuwa playing na ndipo itapopatikana au kukubaliwa ile sera ya serikali Tatu.
Maana hakuna historia inayoonyesha kuvunjwa kwa serikali ya Tanganyika.Kama ipo ni lini na wapi ilikubaliwa kuvunjwa kwa serikali ya Tanganyika ,Mtikila anaweza kwenda kuidai serikali ya Tanganyika mahakamani ? Nikitazama kwa mbaali naona huu Muungano ni kivuli kikubwa sana wanachojificha mafisadi katika kuwaangamiza WaTanganyikans na WaZanzibarians .Ndio humo kwenye Muungano waimojificha.
 
Nawapongeza Watanzania wote kwa kuadhimisha miaka 44 ya Muungano... Si haba mafanikio ni mengi kwa kuwa!

1. Utaifa upo... hakuna anayejitambulisha kama mZanzibar au mTanganyika nje ya mipaka yetu. na hata ndani ni kwa nadra.

2. Watu wamechanganyika! Idadi kubwa ya Watanzania hawajui hata Tanganyika ilikuwa je...

3. Ikumbukwe kwamba Tanyanyika huru ilidumu kwa muda mfupi sana... yaani December 1961 hadi April 1964.

Changamoto...

Muungano wetu umekuwa wa kisiasa na Kijamii zaidi...

Kwa sasa tunapenda uwe ujikite kiuchumi...yaani zanzibar ianze kuwa na viwanda vidogo vidogo iachane na kutegemea Utalii tu... kwa kuwa hii ni hatari..
 
Mzee Aboud Jumbe Mwinyi alisema kuwa muundo wa sasa wa muungano ulikuwa ni wa muda. Muungano ulikusudiwa kuwa ni wa serikali tatu. Hata hivyo, kama nilivyosema awali, twapaswa kuchukua tahadhari tunaposema serikali tatu. Serikali sio kuwa na Rais na Waziri Mkuu na Mawaziri. Maana hata Halmashauri za Wilaya ni serikali na twaita serikali za Mitaa. Nchi zenye mfumo wa Shirikisho zina serikali za Majimbo. Mfano, Afrika ya Kusini, Marekani, Ujerumani nk. Serikali hizi haziongozwi na Marais. Zinaongozwa na watu wanaopewa majina mbalimbali. Mfano Afrika Kusini na Ujerumani wanaitwa Premiers (Aus deutsch es ist MinisterPreasident). Marekani wanaitwa Magavana etc. Sisi ukitamka serikali tatu, inakuja akilini Marais watatu. Hapana, sio lazima.

Nimesema hapo juu, twaweza kuwa na Rais mmoja wa Muungano mwenye nguvu na Mawaziri Wakuu wenye uhuru katika Tanganyika na Zanzibar. Mara baada ya Uchaguzi Rais anakiomba chama cha siasa chenye Wawakilishi wengi katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kuunda serikali na hivyo Kiongozi wa chama hicho anakuwa Waziri Mkuu. Vile vile Rais anakiomba chama cha siasa chenye wawakilishi wengi katika Baraza la Wawakilishi la Tanganyika kuunda serikali na hivyo kiongozi wa chama hicho anakuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika. Bunge linakuwa ni la Muungano tu na linakuwa kama Upper House au Senate hivi . Makamu wetu wa Rais ambae atakuwa anatoka sehemu ya pili ya Muungano ambapo Rais hatoki, anaweza kupewa kazi ya kuwa Mkuu wa shughuli za Serikali katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mawaziri wa Muungano wasiwe wabunge na mambo kama hayo.

Pia kunakuwa na chombo kinachoitwa Baraza la Muungano linalkutana mara moja kwa mwaka kujadili masuala ya muungano ambapo wajumbe wanakuwa ni Rais wa Muugano, Makamu wa Rais na Mawaziri Wakuu kutoka Zanzibar na Tanganyika. Kila baada ya kikao hicho, Rais wa Muungano anahutubia Bunge la Muungano 'State of the Union Address'. Hii inakuwa kila mwezi Aprili kwa mfano. Haya ni mambo ninayofikiri tunaweza kuyafanya. Sijayafanyia uchambuzi wa kutosha. I am just brainstorming myself!!!

Inawezekana kabisa kuwa na Serikali tatu zenye ufanisi na ambazo hazitapelekea Muungano kuvunjika. Serikali moja ni suala ambalo mimi kwa maoni yangu naona si jema kwani litaweka madaraka makubwa kwa central government kitu ambacho tunaona sio sahihi. Kuna haja ya kushusha madaraka chini. Mfumo wa Serikali wenye Rais Mmoja wa Mungano kama Mkuu wa Nchi na Mkuu wa Serikali ya Muungano na Mawaziri Wakuu watendaji kwa Zanzibar na Tanagnyika unaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa sana matatizo ya Muungano na manunguniko yalipo kutoka pande zote.

Vile vile mfumo huo ushushe madaraka chini katika Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kwa kuwa na Mameya watendaji wenye kuwajibika kwa Baraza la Madiwani na kuondokana kabisa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Chini ya hapo tunakuwa na serikali za Vijiji zilizo imara katika mfumo uliopo sasa.

Imefika wakati Rais Kikwete aamue kupanda juu ya chama chake cha siasa na kuwa 'stateman' kwa kuanzisha mjadala mpana wa kisiasa kuhusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni wakati mwafaka kujitazama na kuangalia upya mfumo wetu wa utawala. Huu ni wakati wa kuweka mfumo utakaofanya muungano wetu udumu na hata kuvutia wengine kuingia katika muungano bila kuogopa kumezwa 'identity' yao. Tunaweza kuwa Taifa kubwa na lenye nguvu sana katika eneo la Maziwa Makuu. Is this not Tanzanian Dream?
 
Mzee Aboud Jumbe Mwinyi alisema kuwa muundo wa sasa wa muungano ulikuwa ni wa muda. Muungano ulikusudiwa kuwa ni wa serikali tatu.

Ndio maana niliwahi kusema huko nyuma kuwa Jumbe anazo akili sana ndio maana alipoona mambo ya kuburuzwa tu akaamua kuweka mguu chini, akaishia kuwekwa pembeni!
 
Back
Top Bottom