Leo Kampigie Kura Mtu Huyu Mmoja Na Atayabadili Kabisa Maisha Yako Kwa Miaka Mitano Ijayo

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
“Miaka mitano ijayo utakuwa sawa na ulivyo leo, isipokuwa kwa watu utakaokutana nao na vitabu utakavyosoma.” ― Charlie Tremendous Jones

Rafiki yangu mpendwa,
Leo tarehe 28/10/2020 ni siku ya kipekee kwenye maisha ya kila Mtanzania, kwani tunapata nafasi ya kwenda kushiriki kuamua ni watu gani wa kutuongoza kwa miaka mitano ijayo.

Hili ni tukio ambalo huwa linatokea mara moja kila baada ya miaka mitano na maamuzi tunayofanya tunakaa nayo kwa kipindi hicho cha miaka mitano.

Kwenye ujumbe wa leo nina mambo mawili; jambo la kwanza ni kukusihi ukapige kura leo na jambo la pili ni mtu muhimu unayepaswa kumchagua leo ambaye atayabadili maisha yako kwa uhakika.

Tuanze na umuhimu wa kupiga kura leo.

Kama wewe ni Mtanzania mwenye umri zaidi ya miaka 18 na umejiandikisha kupiga kura, basi leo nenda kapige kura. Huna sababu yoyote kwa nini usipige kura yako siku ya leo.

Hivyo nikuombe sana rafiki yangu, nenda kapige kura, mimi nakwenda kupiga kura mapema na wewe fanya hivyo. Ni haki yetu na ushiriki wetu kwenye kufanya maamuzi ya namna gani taifa letu liongozwe.

Kuna sababu za kijinga nyingi ambazo watu wamekuwa wanazitumia kujihalalishia kutokupiga kura, leo nakwenda kuvunja sababu kubwa tatu zinazotumiwa sana.

Sababu kwa kwanza; sina muda wa kupoteza.

Wapo wanaosema hawana muda wa kupoteza kwenda kupanga foleni kupiga kura, ni bora watumie muda huo kwenda kutafuta pesa au kufanya yao mengine.

Rafiki, hii siyo tu sababu ya kijinga, bali ni ya hovyo mno. Uchaguzi unatokea mara moja ndani ya miaka mitano, hata kama utapoteza simu moja, ni moja kati ya siku 1825. Sasa hebu niambie tangu mwaka 2015 mpaka leo ni siku ngapi umezipoteza bila ya kufanya chochote. Hata huko ni mbali, tuangalie tu mwaka huu 2020, ni siku ngapi umeipoteza kwa mambo yasiyo na msingi? Usitumie sababu hii, nenda kapige kura, hupotezi chochote ambacho hujawahi kupoteza siku za nyuma.

Sababu ya pili; ninayemkubali atashinda hata nisipompigia kura.

Wapo ambao wanaona kwa sababu upande wanaoukubali una nguvu ya kushinda, basi hawana haja ya kupiga kura, kwa sababu hata wasipopiga, upande huo utashinda.

Rafiki, hata kama upande unaoupigia kura unaona utashinda, kura yako bado inatoa ujumbe kwa upande huo, kuonesha kwamba unauunga mkono na hivyo kujua unawakilisha watu sahihi.

Sababu ya tatu; ninayemkubali hawezi kushinda hivyo nikipiga kura ni kuipoteza.

Wapo ambao wanaona upande wanaoukubali hauwezi kushinda, hivyo hata wakienda kupiga kura ni kuipoteza kura hiyo maana haitaleta ushindi.

Rafiki, kura unayopiga siyo kwa sababu ya mtu kushinda au kushindwa, bali ni kuonesha msimamo wako, unasimamia upande upi. Hivyo hata kama upande ulioupigia umeshindwa, upande unaoshinda unakuwa umepata funzo, kwamba kuna wananchi hawakubaliani na kile wanachosimamia. Hiyo inafanya upande huo kutafuta njia za kuwahudumia wananchi wote, hata wale wasiokubaliana nao.

Kama hutaenda kupiga kura kwa sababu upande unaoukubali haushindi, utawaacha wale wanaoukubali upande unaoshinda wapige kura, anayeshinda ataona anakubalika na wote, kumbe kuna ambao hawamkubali. Hivyo kapige kura, kura yako imebeba ujumbe mzito kuliko tu kuamua ushindi.
Kwa hayo machache rafiki yangu, nikusihi sana uende ukapige kura leo, ni tukio ambalo halitatokea tena mpaka miaka mitano ipite, usipoteze nafasi hii ya kushiriki kwenye demokrasia na kutuma ujumbe wako ni wapi unasimama.

Mtu muhimu unayepaswa kumchagua leo kama unataka maisha yako yabadilike.

Rafiki, najua kampeni za kuomba nani achaguliwe zimefungwa jana. Lakini leo nataka nimpigie kampeni mtu mmoja ambaye hayuko kwenye karatasi za kupigia kura unazokwenda kukutana nazo, ila ana nguvu kubwa ya kuyabadili maisha yako.

Huyu ni mgombea ambaye akikupa ahadi zake, una uwezo wa kumfuatilia na akazitekeleza, siyo mwanasiasa wa kukuambia kuna mchakato na upembuzi yakinifu. Una uwezo wa kumkamata wakati wowote na kumhoji ahadi zake na utekelezaji wake.

Kumwona mgombea huyo, nenda mbele ya kioo, kama una kioo kikubwa kasimame mbele ya kioo hicho, kama una kioo kidogo kishike na kukitazama.

Ile sura unayoiona kwenye kioo, ndiye mgombea wa kwanza unayepaswa kumpigia kura leo hii, kabla hujatoka kwenda kuchagua wagombea wengine.

Utaratibu wa kumpigia kura mgombea huyo ni kwa kutumia kauli hii; “Mimi …… (taja jina lako) nimejichagua kuwa kiongozi mkuu wa maisha yangu, maisha yangu ni jukumu langu na nitachukua hatua kuhakikisha yanakuwa bora. Kila siku nitakazana kuwa bora zaidi ya nilivyokuwa jana, kila siku nitajifunza kitu kipya na nitajituma kwa kwenda hatua ya ziada kwenye kila ninachofanya. Kila siku nitakazana kukuza kipato changu zaidi kwa kukazana kutoa thamani kubwa zaidi kwenye kile ninachofanya. Kwa kila kipato ninachoingiza, asilimia 10 nitajilipa mimi mwenyewe kwa kuweka akiba sehemu ambayo siwezi kuitumia na baadaye nitawekeza akiba hiyo ili izalishe zaidi. Kila kinachotokea kwenye maisha yangu nitakitumia kwa manufaa zaidi, sitalalamika wala kumlaumu yeyote, kama kuna kitu sikipendi nitakibadili na kama siwezi kukibadili nitaachana nacho. Haya ndiyo maisha niliyochagua kuyaishi kwa miaka mitano ijayo na kila siku nitajikumbusha hili kabla ya kuanza siku yangu.”

Chapisha kauli hiyo na iwekee sahihi na kuiweka sehemu ambayo kila siku unaweza kuisoma kabla hujaianza siku yako.
 
Imeisha hiyo
20201028_072007.jpg
 
Kwa vijana wa nchi hii wakamchague ambaye hatofungia mitandao kwa uwoga wa kushindwa na kuficha maovu yake yasionekane.
Kama kajaribi wakati wa uchaguzi ataendelea kufunga mitandao ukimpa ridhaa tena.
Hii ni karne ya Vijana wa milliard na keyboard.
Mtoeni jamaa wa Chato Mchague Tundu Lissu
 
Kwa vijana wa nchi hii wakamchague ambaye hatofungia mitandao kwa uwoga wa kushindwa na kuficha maovu yake yasionekane.
Kama kajaribi wakati wa uchaguzi ataendelea kufunga mitandao ukimpa ridhaa tena.
Hii ni karne ya Vijana wa milliard na keyboard.
Mtoeni jamaa wa Chato Mchague Tundu Lissu
Vijana wa keyboard bado mnaendelea kwenye keyboard
vijana wa ukweli tumeshafanys yetu
 
Lakini CDM mjifunze kuhamasisha wapiga kura wenu ambao wengi ni vijana,wiki moja kabla ya uchaguzi muwatembelee kwenye vijiwe vyao muwaelimishe umuhimu wa kura
Kama alivyosema mtoa mada wengi wao ni washabiki Kama timu lakini hawajui umuhimu wa kura kwenye maisha yao tofauti na wamama,wazee na watu wazima wengine wanashabikia ccm
Nimetoka kupiga kura yangu lakini observation yangu kwa mda mfupi niliokaa kituoni vijana ni wachache saaana wengi ni wamama,wazee na watu wa umri wa makamo ambapo automatically unaweza tambua votting patterns
 
Kwa vijana wa nchi hii wakamchague ambaye hatofungia mitandao kwa uwoga wa kushindwa na kuficha maovu yake yasionekane.
Kama kajaribi wakati wa uchaguzi ataendelea kufunga mitandao ukimpa ridhaa tena.
Hii ni karne ya Vijana wa milliard na keyboard.
Mtoeni jamaa wa Chato Mchague Tundu Lissu
Ndo naelekea mkuu, graduate nina jambo langu.
 
Back
Top Bottom