Laiti watu hawa wangeandika kumbukumbu zao

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,910
30,253
LAITI WATU HAWA WANGEANDIKA KUMBUKUMBU ZAO
Wengine tayari wameshatangulia mbele ya haki miaka mingi na wengine hivi karibuni na wengine bado wanaishi na nawaombe dua Allah awape umri mrefu.

Vitabu hivi viwili, ‘’Maisha Yangu Miaka Minane Ndani ya Baraza la Mapinduzi: Khaini au Mhanga wa Mapinduzi?'’ cha Khamis Abdallah Ameir na ‘’My Life, Speeches and Writings,’’ cha Balozi Jua Mwapachu vimenifanya nikae kitako niwaze.

Fikra zangu zimenipeleka nyuma kuwafikiria watu mashuhuri na kila mtu kwa namna yake ya pekee kabisa watu ambao mimi nimejaaliwa kukutana nao.

Katika kusuhubiana na watu hawa nikawajua maisha yao na kutambua kuwa hawa si watu wa kawaida wana historia ambazo lazima waandike ili historia hiyo isije kupotea.

Katika hawa wengine sikupata kuwajua kwa karibu na tukafahamiana kwa undani na katika hawa wako ambao tulifahamiana na tukajenga urafiki mkubwa.

Wengine narudia kusema wa hai na wangine wameshafariki.

Hawa ambao walikuja kuwa rafiki zangu hawa kwa vinywa vyao wenyewe walinieleza historia za maisha yao katika kipindi kirefu cha urafiki wetu nami nilikuwa siku zote nikiwaambia lazima waandike kumbukumbu zao kwani ndani ya maisha yao kuna mengi ya faida na haitapendenze hazina kama hiyo waingie nayo kaburini.

Ajabu kubwa ya watu hawa ni kuwa ni kama vile hawataki kuandika.

Kwangu mimi mwimbo wangu kwao ukawa ni huo huo kila tunapokutana.

Andika bwana acha ajizi, andika, andika, andika.

Na wao wakaendelea kunipuuza nami sikukubali kupuuzwa kirahisi.
Nikaenelea kuimba mwinbo wangu ule ule.

Andika, andika, andika.
Kisha siku moja napokea taarifa rafiki yangu huyu ameaga dunia.

Nini kinachobakia kwangu?

Majonzi na majuto nikimjutia rafiki yangu kwa kuwa mkaidi na kukataa kunisikiliza kuhusu yeye kuandika kumbukumbu zake.

Kila siku namkumbuka baba na rafiki yangu Ahmed Rashad Ali.

Huenda si wengi wanamfahamu mtu huyu mwanaharakati, mtangazaji wa Sauti ya Unguja, mpigania uhuru Afrika na Zanibzr na bingwa wa propaganda.

Gamal Abdel Nasser alipata kumwamia Ahmed Rashad Ali, ''Shambulia serikali yote ya Muingereza ila Malkia, huyu muache.''

Ahmed Rashad alizaliwa mwaka wa 1919 na alikulia na kulelewa katika nyumba ya masultani wa Zanzibar.

Babu yake jina lake Bakashmar alipata kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Sultan katika miaka ya 1800.

Mzee Rashad alikuwa akianzia hapa kunieleza maisha yake.

Akinieleza safari yake ya kwanza kuja Dar es Salaam miaka ya katikati 1930 akifuatana na mjomba wake.

Ilikuwa wakati wa ‘’Sports,’’ na alikuwa yupo na mjomba wake katika jengo la Arab Association, Ring Street (sasa Mtaa wa Jamhuri) ndipo alipokutana na Abdul Sykes na yeye kaongozana na mjomba wake Muarab jina lake Omar Amiran.

Watoto hawa wawili Ahmed Rashad na Abdul Sykes walibakia marafiki maisha yao yote.

Akimaliza hapa Ahmed Rashad atanihadithia maisha yake baada ya kumaliza shule Zanzibar na kupelekwa India kusoma zaidi wakati wenzake wanakwenda Makerere.

Vita Vya Pili Vya Dunia (1939 - 1945) vikamkuta Ahmed Rashad India akiwa mwanafunzi na baada ya vita atakutana na rafiki yake Abdul Sykes na mdogo wake Ally, Kalieni Camp, Bombay.

Abdul na Ally walikuwa wamevaa unifomu za KAR wako katika kambi ya jeshi wakisubiri kurejeshwa Tanganyika baada ya vita kumalizika.

Wote walikuwa vijana.

Akiwa mwanafunzi India, Ahmed Rashad Ali alishuhudia harakati za India za kupigania uhuru wake.

Ahmed Rashad atanieleza misuguano iliyokuwapo kati ya Mohamed Ali Jinah na Nehru katika kuwakabili Waingereza wakidai uhuru wa nchi yao.

Nilikuwa sichoki kumsikiliza Ahmed Rashad Ali.

Siku zote baada ya mazungumzo yetu nilikuwa lazima nitamwambia Mzee Rashad aandike kumbukumbu zake na yeye jibu lake lilikuwa hana historia ya maana ya kuandikwa watu wasome.

Lakini Ahmed Rashad Ali mwaka wa 1952 alishitakiwa mahakamani kwa kosa la uchochezi wa siasa na ikabidi akimbie nchi kwenda Misri kwa msaada wa Gamal Abdel Nasser kwa sababu Zanzibar kwake yeye palikuwa hakukaliki tena.

Alipofika Misri Gamal Abdel Nasser alimfungulia kituo cha radio, ‘’Radio Free Africa,’’ afanye propaganda kusaidia Afrika kupigania uhuru wake.

Hapa kuna mengi sana.
Siwezi kuyaeleza yote.

Ahmed Rashad Ali kafariki bila kuandika kumbukumbu zake.

Nimekutana na watu wengi mfano wa Mzee Ahmed Rashad ambao mimi nilitambua thamani ya kumbukumbu zao kuwa ndani ya kitabu.

Kilani nikikutana na Abdilatif Abdallah humuimbia mwimbo wangu ambao sasa ni maarufu, ''Andika, Andika, Andika.''

Nilipata fursa ya kumtembelea nyumbani kwake Humburg na tukawa na muda mkubwa sana wa mazungumzo na akanieleza mengi katika maisha yake toka akiwa jela hadi anatoka na kuondoka Kenya.

Rafiki yangu Salim Himid.

Nilianza kumwimbia mwimbo wangu huu wa, "Andika, Andika, Andika,'' toka alipokuja Tanga kumtembelea ndugu yake Mohamed Mshangama na ndipo tulipofahamiana.

Nilimshauri aandke kumbukumbu zake baada ya yeye kunieleza historia ya maisha yake vipi alisafiri ''overland,'' kutoka Zanzibar hadi Paris kwenda kutafuta elimu katika miaka ya 1960.

Baada ya kuhitimu akajikuta yuko Comoro kama Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje.

Nilikwenda Paris na nilikutana na Salim Himid.
Sitosahau safari hii.

Asubuhi Salim atanipitia hotelini kwangu twende matembezini.

Ndani ya basi, treni na tukiwa tunatembea kwa miguu nilimshughulisha mwenyeji wangu kuhusu historia ya maisha yake.

Siku tunaagana nilimkumbusha umuhimu wa yeye kuandika kumbukumbu zake.

Salim Himid hakuandika hadi anafariki mwaka juzi.
Ndipo nikasema laiti watu hawa wangeandika kumbukumbu zao.

Unaweza kusoma taazia za hawa wapenzi wangu hapo chini:


 

Similar Discussions

Back
Top Bottom