Laiti Watanzania wangetambua nguvu ya kisiasa waliyonayo!

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,045
Posted Date::12/11/2007
Laiti Watanzania wangetambua nguvu ya kisiasa waliyonayo!

Na Tonny Adamms

wananchi

MIAKA 46 ya watu wa taifa kujitawala wao wenyewe siyo mchezo wala kitu cha mzaha. Kipindi hicho kirefu kinapaswa kuwa kielelezo cha ukomavu wa kifikra, wa kubuni mambo na mikakati, ukomavu wa kudadisi na kuhoji, ukomavu wa kukataa kuendelea kunyanyaswa au kugeuzwa vikaragosi na yeyote yule awaye.

Dhana ya kujiamini kwamba hata sisi Watanzania pia tunaweza ilipaswa kuwa ndiyo salaam yetu ya kila siku kila kuchapo. Lakini ile baridi ya unyonge itokanayo na umaskini ama wa akili au wa kipato bado dhahiri imetanda katika kaya na familia nyingi hapa nchini hususan vijijini wanakoishi Watanzania walio wengi.

Huhitaji shahada ya falsafa kulitambua jambo hili. Panda basi lolote la abiria linaloelekea kokote kule nchini, kutwa nzima ukiwa safarini chunguza,dadisi na fanya tathmini ya hali ya maisha ya Watanzania utakao waona katika upeo wa macho yako.

Kisha jiulize, iweje watu wote wale uliowaona katika vijiji mbalimbali waonekane wakiwa na maisha duni kiasi kile, wawe na makazi duni kiasi kile na wakiishi katika mazingira duni kiasi kile Je, watu wote wale hawana akili ya kuishi? Je, kwani ni wavivu na hawajitumi kiasi cha kutosha? Au akili zao zina mgando au zimedumaa? Tatizo ni nini hasa?

Kipindi hicho cha miaka 46 iliyopita utaweza kukigawa katika makundi makubwa matatu. Kwanza, kipindi cha kujifunza ambacho hakikupaswa kuzidi miaka mitatu. Pili, kipindi cha majaribio? ambacho nacho hakikupaswa kuzidi miaka mitano.

Tatu, kipindi cha kuthubutu kutenda ambacho hakikupaswa kuzidi miaka kumi. Nne, kipindi cha kutathmini matendo ya miaka kumi iliyotangulia ambacho hakikupaswa kuzidi miaka mitatu.

Yote hayo yalipaswa yafanyike ndani ya miaka 18 tu.

Baada ya hapo Watanzania sasa tukiwa wakomavu na tuliojiamini, tulipaswa kuthubutu na kuibuka na mikakati ambayo ingeweza kutuvusha katika hali ya uhakika zaidi kwa kipindi kirefu zaidi cha miaka mingine isiyo pungua hamsini (1981- 2030).

Hebu tuyalinganishe yote yaliyo tokea toka mwaka 1961 tulipopata Uhuru wa kisiasa na hali halisi ya jinsi mambo yalivyotokea au kutendeka katika awamu mbalimbali za uongozi.

Je, hapa tulipo sasa tupo katika mtiririko huo nilioutaja au pembeni yake kidogo au pembeni kabisa?

Katika yote tutakayo yazungumza au kuyadurusu hakuna litakalo kuwa muhimu kupita vyote kama Rasilimali na Watu.

Jitihada kubwa sana zilifanyika hususan wakati wa Uongozi wa Mwalimu Nyerere za kusomesha vijana wetu wenyewe katika fani mbalimbali. Vijana wengi kati ya hao hivi sasa ni watu wazima kupindukia ambao wengi kati yao walipaswa kuwa wamestaafu katika harakati za mikikimikiki ya shughuli za kisiasa. Au hata zile za Uongozi katika ngazi yoyote ile.

Walipaswa hivi sasa wawe washauri tu katika fani na nyanja mbalimbali walizozitumikia kwa kipindi kirefu cha maisha au utumishi wao.

Lakini hali halisi hivi sasa ikoje? Bado wapo wengi kati ya hao waliojisahau na kudhani kwamba wao pia wapaswa kuwa mstari wa mbele kwa sasa, kwani walikuwa wakifikiri nini mpaka wakashindwa kukupasia? kijiti? Uchu na Ubinafsi ama wa kutaka kuabudiwa au wakutaka mwingine asipate au kutokana na umaskini wa roho tu wa kutotosheka na alichokipata bado umewazingira wazee wetu wengi ambao hivi sasa wanasutwa na wakati kuwapiga chenga.

Tujiulize, nini matokeo ya hao wazee ving?ang?anizi katika nafasi za uongozi kwa kipindi kirefu maamuzi mengi yakifanyika wao wakiwa katika nafasi nyeti za kudhibiti mabadiliko, athari zake kwa wanataaluma wetu zimefikia kiwango gani?

Wengi wamekata tamaa kutokana na malipo na mishahara duni na kutokuwepo kwa mipango ya wazi ya kuwaendeleza kitaaluma na kimaslahi.

Wengi wao hivi sasa ni watu wazima ambao nadiriki kusema kwamba walinyimwa fursa ya kuonyesha umahiri wao na kuitumia vilivyo elimu yao kwa faida ya taifa letu. Tuiruhusu hali hii iendelee hadi lini na iendelee kwa faida ya nani?

Rais Jakaya Kikwete aliposhinda katika Uchaguzi Mkuu uliopita kwa asilimia kubwa, wengi walitarajia kwamba baada ya kujifunza na yote haya yaliyopita bila ya wasiwasi wowote angekuja na Baraza jipya kabisa la mawaziri.

Sura zote zingekuwa ngeni na pasingekuwepo hata na sura yoyote iliyokuwapo katika awamu zote zilizopita. Siyo dhambi kuwaacha waliokuwamo katika Mabaraza ya Mawaziri yaliyopita na kuanza na timu mpya. Faida zake ni nyingi mno kuliko hasara.

Siyo kuja na sura mpya tu za Mawaziri bali hata ile idadi ya Mawaziri nayo pia ingeashiria uwezo duni wa kiuchumi unaoikabili nchi yetu kwa sasa. Wengi walitarajia kwamba idadi ya Mawaziri isingezidi 12. Kwani hata sekta zenyewe kuu za uchumi hazizidi kumi na mbili. Na badala yake Idara za Serikali ndizo ambazo zingepaswa ziimarishwe zaidi. Na katika utawala mikoani, Wilaya ndizo ambazo zingepaswa ziimarishwe zaidi kiutendaji, kifedha na kiutawala kuliko ilivyo hivi sasa.

Mipango na Maamuzi mengi yalitarajiwa sasa yangetoka chini kwenda juu na siyo toka juu kwenda chini. Utayarishaji wa Bajeti ya Serikali au Bajeti ya Maendeleo na Upangaji wa rasilimali adimu zilizopo nchini kwa ajili ya mahitaji ya kimaendeleo mengi ya kitaifa unaendeshwa au kutekelezwa kinadharia zaidi kuliko kihalisia. Na yote hayo yanafanyika kwa kufuata zaidi miongozo ya Benki ya Dunia na Taasisi ya Fedha ya Kimataifa.

Wote tukiwa na shauku kubwa ya maendeleo na hali bora zaidi ya maisha, ni vema basi wale tuliowachagua wawe viongozi wetu wa muda husika (na siyo viongozi wetu milele).

Taasisi zetu za Kitaifa ziakisi uhalisia wa Watanzania kimapato, kielimu na kitamaduni na zisijigeuze mbuni aliyefutika kichwa chake mchangani. Watanzania watakapotoa kilio chao kuhusu adha ya maisha wanayoipata kutokana na maamuzi yasiyo sahihi ya kisiasa ni vema taasisi zetu husika ziwajibike ipasavyo na kuchukua hatua stahili na zisigeuke mbuni.

Watanzania watakapotoa kilio chao kuhusu kuzidi kupanda kwa gharama ya maisha, kupanda kwa bei za vitu na mahitaji mbalimbali na kuzidi kushuka au kudorora kwa thamani ya shilingi ni vema taasisi husika ziwajibike ipasavyo na kuchukua hatua stahili.

Lakini itakapotokea kwamba taasisi zenyewe za kitaifa ndizo chanzo cha tatizo na kisha taasisi hizo zikadiriki kuutetea udhaifu na mapungufu ya kiutendaji yaliyodhihirika basi Watanzania watambue kwamba taasisi hizo ni pandikizi na zipo pale kwa manufaa na maslahi ya watu wachache.

Mambo mengi yatahitaji mabadiliko ili kukidhi mahitaji ya wakati bila ya kupoteza mwelekeo na mshikamano wa kitaifa.

Yule atakayedai kwa mfano suala la Katiba sasa limefungwa na halijadiliki, aulizwe anatamka hivyo kwa maslahi ya nani, ya kwake binafsi au ya kikundi cha watu wachache wanaotaka kubakia katika safu ya Uongozi milele au kwa maslahi dhati ya kitaifa? Katiba ya nchi siyo Biblia wala Msahafu kwamba haujadiliki na hauwezi kutolewa kasoro.

Katiba ya nchi lazima iwe kielelezo cha utamaduni na taratibu za maisha ya kila siku zilizokubalika katika jamii husika. Maendeleo mapya huzaa mahitaji mapya ambayo nayo pia wakati mwingine hulazimisha taratibu za maisha zibadilike na hata dira na mwelekeo nao pia waweza kubadilika. Inapofika hatua hiyo, katiba nayo yapaswa kwenda na wakati kwa sababu huo ndio mwongozo wa taifa husika.

Ukomavu wa kifikra tulioupata katika kipindi hiki cha miaka 46 iliyopita utufikishe mahali ambapo kila Mtanzania atambue kwamba ana haki na dhamana sawa ya kupitisha maamuzi yaliyo sahihi katika kuuelekeza mustakabali wa nchi yetu katika mafanikio makubwa na bora zaidi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Kamwe tukatae kuikabidhi dhamana hiyo kwa wenzetu wachache wanakaopenda kufikiri na kutenda kwa niaba yetu.

Kila Mtanzania ni mdau katika kupitisha maamuzi yote ya mwisho katika jambo lolote lile linalohusu taifa lake. Atakayepitisha maamuzi yoyote yenye taswira ya kitaifa yeye binafsi bila kuwashirikisha Watanzania katika ujumla wao aulizwe kafanya hivyo kwa maslahi ya nani, yake binafsi au ya kikundi cha watu wachache wenye uchu na tamaa ya kutawala?

Laiti Watanzania wangetambua nguvu ya kisiasa waliyonayo mikononi mwao yote haya yasingepata nafasi ya kuotesha mizizi.
 
Mwandishi alikuja vizuri sana na habari hii tokea mwanzo hadi alipofikia sehemu hiihapa chini, ambapo mtiririko na mpangilio vikaanza kuvunjika:

Baada ya hapo waTanzania sasa tukawa wakomavu na tuliojiaini, tulipaswa kuthubutu na kuibua na mikakati ambayo ingeweza kutuvusha katika hali ya uakika zaidi kwa kipindi kirefu zaidi cha miaka mingine isiyopungua hamsini (1981 - 2030"

Ingefaa zaidi atimize ahadi hii aliyoitoa hapa chini katika uchambuzi wake:

"Hebu tuyalinganishe yote yaliyotokea tokea mwaka 1961 tulipopata Uhuru wa kisiasa na hali halisi ya jinsi mambo yalivyotokeaau utendeka katika awamu mbalimbali a uongozi."

Inaonekana baada ya hapa, mwandishi nadhani alianza kuwa na haraka na uandishi wake, na matokeo yakawa kwamba ahadi aliyoitoa hakuitimiza sawasawa.

Litakuwa jambo zuri kama mwandishi atachukua muda kidogo na ayatimize hayo aliyotaka kuyasema katika mpangilio alioahidi kuufuata katika sentensi yake hiyo hapo chini.

Uchambuzi wake utakuwa wa nguvu hasa kama atakubali kufuata na kuitimiza ahadi aliyoitoa. Kama anayo nafasi pana kidogo, hicho kinaweza kuwa itabu cha maana.
 
Ukiona walio wengi wanalalama..... jua hakuna aliye salama......
Indicator za kukua kwa uchumi hazipo upande wetu.....
 
Watanzania sasa tukiwa wakomavu na tuliojiamini, tulipaswa kuthubutu na kuibuka na mikakati ambayo ingeweza kutuvusha katika hali ya uhakika zaidi kwa kipindi kirefu zaidi cha miaka mingine isiyo pungua hamsini (1981- 2030).
 
Back
Top Bottom