Kwanini waliowajibika na `waliochoka` wawemo kwenye kamati za Bunge?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,825
287,849
Kwanini waliowajibika na `waliochoka` wawemo kwenye kamati za Bunge?

2008-03-24 10:34:42
Na Hamisi Mzee

Viongozi wa kamati za Bunge na wajumbe wake wametangazwa miongoni mwao wamo baadhi ya vigogo waliowajibika kutokana na kashfa ya Richmond na hata baadhi ya mawaziri walioomba kupumzika kutokana na kuwemo kwenye uongozi kwa muda mrefu.

Katika makala haya, Hamis Mzee anahoji kwanini watu wale wale? Na kama ni taratibu kuwa kila mbunge kuwemo kwenye kamati basi taratibu hiyo iangaliwe upya.

Wakati wa uongozi wa awamu ya kwanza chini ya Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere kulijengeka tabia ya viongozi kubadilishwa kwa kuhamishwa na kupewa nyadhifa zingine za juu katika maeneo mbalimbali ya uongozi.

Tabia hii kwa kiasi kikubwa ilikera lakini hakukuwa na jinsi ya kufanya.

Ilikuwa ni kawaida kabisa kuona kiongozi anakosea hapa anapewa nyadhifa nyingine hali iliyofanya baadhi ya watu kuhisi kwamba ilitokana na huruma ya Baba wa Taifa.

Kwa bahati mbaya tabia hii inaelekea kushika mizizi kwani uongozi unaonekana kama ni sifa ya watu fulani tu `waliobarikiwa` na wanaokubalika na wenye mamlaka.

Hivi karibuni, Bunge lilipocharuka na kuwa mbogo kuhusu kashfa ya mkataba wa Richmond na kupelekea kuanguka kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa mwanzo katika uongozi wa awamu hii ya nne na mawaziri wengine wawili, ilionekana kuwa sasa chombo hicho kinashika hatamu na kuchukua nafasi yake sahihi katika jamii.

Kufuatia hatua ya kung`atuka Waziri Mkuu, Rais wa Jamhuri Jakaya Mrisho Kikwete alilazimika kuvunja baraza la mawaziri na kuunda jipya ambapo alipunguza idadi ya mawaziri na katika mchakato huo pia aliwaacha baadhi ya mawaziri ``waliochoka`` kwa maana ya kuwemo kwenye baraza la mawaziri kwa miaka mingi baadhi yao wakianzia tangu awamu ya kwanza, ya pili , ya tatu na hata ya nne.

Hata wakati Rais alipokuwa akitangaza Baraza lake jipya, wananchi na wachunguzi wa mambo ya kisiasa waliona hatua hiyo kuwa ni ``poa``.

Kwa vigogo waliojiondoa kutokana na kashfa ile ya Richmond iliyohusu mgao wa dharura wa umeme, wananchi waliona ni vizuri wako nje.

Kamati iliyochunguza kashfa hiyo iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe ilionekana imefanya kazi ya kishujaa.

Kashfa iliyowaondoa vigogo hao ni ya ufisadi mkubwa ambapo taifa linapoteza mamilioni ya fedha kila siku kulipia mkataba huo wa mradi wa umeme wa dharura.

Baada ya kung`oka kwa viongozi hao zaidi kutokana na kuwajibika kwa makosa yanayoelekea kufanywa na watendaji wao au maamuzi yao ya kutoishauri serikali vizuri na kutokuwa makini, wananchi katika baadhi ya maeneo waliandamana kuunga mkono taarifa ya kamati teule ya Bunge na kutaka serikali kuwa makini kuhakikisha inaziba mianya yote ya ufisadi.

Miongoni mwa hatua zilizopendekezwa na kamati ya Bunge ni kutaka mikataba iwe inapitiwa Bungeni kuhakikisha mianya yoyote inayoweza kupelekea ufisadi na taifa kuingia hasara inaepukwa.

Kwa bahati mbaya kabla ya wananchi hawajasahau yaliyotokea katika sakata hilo la Richmond, majina ya wale waliong\'oka kwa kuwajibika yamejumiusha kwenye wajumbe wa kamati za Bunge.

Hii bila shaka itawashangaza wananchi. Kwanini wale wale kila mara?

Inawezekana hiyo imetokana na utaratibu wa Bunge lakini kutokana na mambo yaliyotokea ingekuwa vizuri viongozi hao waliowajibika na hata wale waliotaka kupumzika nyadhifa zao za uwaziri kutokana na kukaa kwenye uongozi kwa muda mrefu wangewekwa pembeni.

Na huo ndiyo ungekuwa mwanzo wa mchakato na njia yao ya kutoka kabisa katika siasa.

Kama ni suala la uzoefu, watu wengine wataupata lini?
Kama ni utaratibu wa bunge ni lazima kila mbunge awemo kwenye kamati, ni vizuri uangaliwe upya kwani kamati za Bunge kutokana na mtazamo wa kuzipa nguvu na mamlaka zaidi ikiwemo kuangalia mikataba inayatia shaka kwa watu walioboronga au kuonekana wameboronga kuwemo kwenye kamati hizo.

Hivi wananchi wanatakiwa waelewe vipi? Hakuna wengine ama watu hao watakuwa na mapya?

Kama ilivyojitokeza baadhi ya vigogo wamebwagwa kwenye kuwania uongozi wa kamati za Bunge, ni wazi hata kwenye ujumbe zinahitajika nguvu mpya ili Bunge liweze kwenda na kasi na ari mpya.

SOURCE: Nipashe
 
Mtoa mada mbona hujatuambia hizo kamati na wahusika waliorudishwa ni akina nani?ili tumchambue mzee six
 
Hakika ingefaa zaidi watafutwe watu wengine kuliko hawa waliopitishwa sasa hivi. Wamewahi kuongoza kamati kama hizo lakini hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanywa. Je, tutazamie chochote kipya? Au ni mvinyo ule ule kwenye chupa mpya?
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom