Kwanini twashindwa kuwapandisha wakubwa kizimbani? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kwanini twashindwa kuwapandisha wakubwa kizimbani?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Kakke, Dec 23, 2011.

 1. Kakke

  Kakke JF-Expert Member

  #1
  Dec 23, 2011
  Joined: Dec 4, 2010
  Messages: 1,797
  Likes Received: 389
  Trophy Points: 180
  [​IMG]

  Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa ni miongoni mwa marais wa kiafrika ambao katika utawala wao yametokezea maafa na vifo vya raia kadhaa huko Zanzibar hivyo ni miongoni mwa marais ambao wanapaswa kufikishwa katika mahakama za kimataifa kutokana na vifo vilivyotokea chini ya uongozi wake ambapo yeye alikuwa amiri jeshi mkuu


  Na Ahmed Rajab

  UKWELI, ingawa ni adhimu, una tabia mbaya. Una tabia ya kuudhi na hata ya kuuma. Ndiyo maana haishangazi tunapojikuta tunaukwepa.

  Alhamisi iliyopita nilikuwa Bush House, jijini London, kwenye studio za BBC Focus on Africa, kusajili kipindi cha mwisho wa mwaka niliposikia kwamba mahakama moja nchini Ufaransa imemhukumu rais wa zamani wa nchi hiyo Jacques Chirac, baada ya kumpata na hatia ya ufisadi. Nilishtuka nilipojisikia nikijiambia: ‘Ndiyo maana wazungu wanatushinda.'

  Halafu mbiombio nikajilaumu kwa dhana potovu kwamba kila cha mzungu ni chema. Nilichelea yasije mawazo yangu yakateleza mithili ya yale ya mshairi maarufu wa lugha ya Kifaransa, Léopold Sédar Senghor. Senghor aliyezaliwa Senegal na aliyekuwa mmoja wa wahubiri wakuu wa falsafa ya négritude (uweusi) aliwahi safari moja kuhoji kwamba wazungu ndio wenye kutumia akili na watu weusi tumejaa jazba tu. Hatuna letu ila mihemko, mahamasa na hisia nzitonzito. Kinyume na wazungu, alisema, sisi hatuyapimi mambo na kuyachanganua.

  Wengi walimlaumu Senghor kwa dhana hiyo. Pamoja na kuwa mshairi na msomi mkubwa, Senghor alikuwa mwanasiasa mahiri. Alikuwa rais wa mwanzo wa Senegal kwa muda wa miaka 21 na anaheshimika kwa kuwa wa kwanza barani Afrika kuuacha urais kwa hiyari yake alipomkabidhi wadhifa huo waziri mkuu Abdou Diouf tarehe mosi Januari mwaka 1981.

  Senghor alikosea pakubwa alipohoji kwamba ni wazungu peke yao wenye uwezo wa kuchambua mambo kwa kutumia akili. Hata hivyo, sidhani kama ninakosea nisemapo kwamba wazungu wametushinda na wangali wanatushinda kwa mengi. Bila ya shaka si yao yote yaliyo mema au yanayopaswa kupigiwa mfano. Lakini ukweli, na ukweli unauma, ni kwamba, kwa jumla, wanatushinda.

  Wanatushinda, kwa mfano, katika kuziheshimu sheria. Ushahidi ni kama huo uamuzi wa mahakama iliyokuwa ikiyasikiliza mashtaka dhidi ya Chirac. Juu ya kuwa baadhi ya wakuu Wakifaransa walijaribu kuzuia Chirac asishtakiwe, hakimu alikataa. Hatimaye haki ilitendeka, ilionekana ikitendeka na Chirac akapata alichostahiki: hukumu ya kifungo cha nje cha miaka miwili.

  Hukumu hiyo imethibitisha jinsi demokrasia nchini humo ilivyopevuka. Kuna mengi yasiyo sawa katika demokrasia hiyo lakini kwa hatua iliyochukuliwa dhidi ya Chirac, Ufaransa ina haki ya kujigamba kwamba imeonyesha mfano mwema.

  Kwa wasiomjua, Chirac ni kipenzi cha wengi na mkakamavu katika siasa za Ufaransa. Ni mwanasiasa aliyekuwa na ustadi wa kuyapangua makundi ya mahasimu zake ndani ya kambi yake na hata kuyagonganisha vichwa. Wengi wakimuona kuwa ni kiongozi wa siasa za ‘shujaa wa Ufaransa', rais wa zamani Jenerali Charles de Gaulle.

  De Gaulle alijiuzulu tarehe 28 Aprili 1969 baada ya kushindwa kwenye kura ya maoni. Alikwishakusema kwamba atajiuzulu endapo atashindwa kwenye kura hiyo iliyohusu mageuzi aliyotaka kuyafanya katika baraza la senate la bunge na katika mfumo wa serikali za kienyeji.

  De Gaulle alifariki ghafla mwaka 1970. Alipofariki rais aliyemrithi Georges Pompidou alitangaza kuwa ‘Jenerali de Gaulle amefariki. Ufaransa ni kizuka'. Kwa kusema hivyo Pompidou alimaanisha kwamba de Gaulle alikuwa bwana wa Ufaransa.

  Wakati huo Chirac alikuwa waziri na akijulikana kwa lakabu ya ‘buldoza'. Baadaye akachaguliwa Meya wa Paris, wadhifa alioushika kwa muda wa miaka 18. Aliwahi pia kuwa waziri mkuu mara mbili. Mwishowe akawa Rais kuanzia 1995 hadi 2007.

  Kumbe katika muda wote huo ‘buldoza' Chirac alikuwa akijipakaza tope za ufisadi. Miongoni mwa shutuma zilizomuandama ni ile kashfa iliyomhusisha na ulipaji mishahara ya watumishi wa kubuni, yaani ‘wafanya kazi hewa', wakati alipokuwa meya wa Paris na matumizi mabaya ya fedha za umma kwa maslahi yake binafsi.

  Wengine wakaongeza mengine wakisema, kwa mfano, kwamba familia ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon marehemu Rafiq Hariri ilisaidia kulipia jumba la kifahari la Chirac linaloukabili mnara wa Eiffel, jijini Paris.

  Shtuma nyingine ni kuwa marais kadhaa wa Kiafrika walimpa yeye na waziri wake mkuu Dominique de Villepin dola milioni 20 za Marekani ziwasaidie kwenye kampeni za uchaguzi.

  Kwenye kampeni ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2002 inasemekana Chirac alipokea dola za Marekani milioni sita na laki mbili kutoka kwa marais wafuatao: Blaise Compaoré wa Burkina Faso; Abdoulaye Wade wa Senegal; Laurent Gbagbo wa Côte d'Ivoire; Denis Sassou Nguesso wa Congo and marehemu Omar Bongo wa Gabon pamoja na Obiang N'guema wa Equatorial Guinea.

  Ingawa sheria ilimstahi alipokuwa rais baada ya kuacha madaraka ilimuonyesha kwamba hakuna anayeweza kuikwepa.

  Yaliyomfika Chirac ndio yaliyonifanya nitafakari na kujiuliza kwa nini ikawa wazungu wanatushinda. Kwa nini hakuna kampeni Afrika ya kutaka hao marais waliotajwa washughulikiwe kisheria kwa kutumia fedha za umma kumhonga Chirac?

  Bila ya shaka wazungu hawakutushinda katika kila kitu, lakini hatuwezi kukataa kwamba wametupiku kwa kuwafanya viongozi wao wawajibike. Sisemi kama wamekamilika. Wapo wakorofi miongoni mwao wanaozipinda sheria lakini kwa jumla mwelekeo wao ni wa kuheshimu katiba na sheria zao.

  Inasikitisha kuona kwamba nchini Tanzania mtindo wa wakubwa kung'ang'ania madaraka umekuwa sehemu ya utamaduni wa kiutawala. Ni nadra kwa wakubwa kuwajibika na hakuna anayethubutu kuwashurutisha wafanye hivyo.

  Sana sana pakizuka kadhia ya ufisadi bunge ndilo huijadili kadhia hiyo. Mara nyingi huo huwa ndio mwisho wake. Huonekana jambo kubwa pale wakubwa wanapojiuzulu kama walivyofanya mawaziri watatu pamoja na aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa.

  Ikiwa wakubwa wanafikishwa mahakamani kama walivyofikishwa mawaziri wa zamani Basil Mramba na Daniel Yona basi kesi hupigwa danadana. Huendeshwa kivarangevarange wakati umma umekaa macho ukitaka kujuwa iwapo washtakiwa kweli wana hatia au wanasingiziwa.

  Inavyodaiwa ni kwamba Yona, akiwa waziri wa fedha, pamoja na Ben Mkapa, akiwa rais wa awamu ya tatu, walijinunulia mgodi wa makaa wa Kiwira bila ya kufuata taratibu. Kwa hilo, Mkapa naye aliikiuka katiba ya nchi kwa kuigeuza Ikulu kuwa pahali pa kufanyia biashara.

  Msomaji mmoja wa Raia Mwema alinikumbusha hivi karibuni kuwa Mkapa naye anastahiki apelekwe kwenye Korti ya Kimataifa ya Jinai huko Hague kwa mauaji yaliyotokea Visiwani Januari 2001. Raia waliuawa kwa sababu waliandamana na mauaji hayo yaliwapeleka mamia ya wananchi wengine waikimbie nchi yao. Isitoshe Mkapa aliwasifu askari waliohusika na kuwapandisha vyeo.

  Tabu yetu Afrika ni kwamba tumezoea kuiga lakini tunapoiga hatuigi sawasawa. Tunasema tunafuata mfumo wa utawala wa kibunge wa Westminster lakini tunaufuata mfumo huo kijuujuu tu. Hatuviheshimu vyombo vya kisheria wala hatuvipi uhuru na mamlaka kamili. Badala yake tunaligeuza suala zima la demokrasia na utawala bora liwe mazingaombwe.

  Ukweli ni kwamba sheria katika nchi nyingi za Kiafrika zinawalinda viongozi na wapambe wao. Wanapofikishwa mahakamani kesi zao huwa ni za kiini macho. Nchini Zambia, kwa mfano, serikali ya Rais Levy Mwanawasa ilimfungulia mashtaka rais aliyemtangulia Frederick Chiluba kwa makosa 100 ya ufisadi na kuhaulisha fedha za umma na kuziingiza kwenye akaunti zake binafsi katika mabenki ya London.

  Kesi ya Chiluba ilisotasota kwa miaka sita hadi baada ya kufariki Mwanawasa mwaka 2008 na urais kushikwa na Rupiah Banda, aliyekuwa rafiki wa Chiluba. Mwaka 2009 mahakama ya Zambia ikasema Chiluba hana hatia. Wakati kesi ilipokuwa inaendelea nchini Zambia mahakama moja ya London ilimpata Chiluba na hatia ya kuchota takriban dola milioni 58 za Marekani na mahakama ikamtaka azirudishe fedha hizo. Mahakama ya Lusaka ikamlinda. Ilikataa kumpeleka Uingereza ikihoji kwamba ya Uingereza ni ya Uingereza na ya Zambia ni ya Zambia.

  Huo ni mfano mmoja wa namna viongozi Wakiafrika wanavyolindana. Sikusudii kuwa kila kiongozi anayeshtumiwa kwa ufisadi au kwa makosa mengine lazima apatikane na hatia. La hasha. Ninachokusudia ni kwamba lazima mahakama iachiwe ifuate mchakato wake.

  Tukumbuke tu kwamba yaliyomfika Chirac hayana mmoja, yanaweza kuwafika viongozi Wakiafrika na wala wakati haugandi bali unakwenda na kubadilika. Viongozi wetu watakuwa wanajidanganya wakidhania kwamba yaliyomfika Chirac ama Zine El Abidine Ben Ali wa Tunisia ama Hosni Mubarak wa Misri hayatoweza kuwatokea.

  Upepo wa mabadiliko wa miaka ya 1990 haukuzikumba nchi za Kikoministi za Ulaya ya Mashariki tu bali ulivuma barani Afrika pia. Huko ulisaidia kuleta mabadiliko ya kuachana na mfumo wa chama kimoja cha kisiasa. Waliokuwa na dukuduku hawakuwa na hila ila nao waliridhia ingawa kwa shingo upande.

  Mwanzoni mwa mwaka huu pakavuma dhoruba ya mageuzi Afrika ya Kaskazini. Matokeo yake tumeyaona. Na hii hatua ya kuhakikisha kwamba hakuna anayeweza kuuhepa mkono wa kisheria ni upepo utaogeuka kimbuga barani Afrika wakati utapofika. Mwenye macho haambiwi tazama.

  CHANZO:
  RAIA MWEMA
   
 2. bakuza

  bakuza JF-Expert Member

  #2
  Dec 23, 2011
  Joined: Nov 15, 2010
  Messages: 488
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 35
  Walishatuambia tukiwakamata Uchumi wa nchi utayumbaau hukusikia?Maana wametuibia mpaka uchumi wote wa Nchi wameumiliki wao.
   
 3. M

  Malova JF-Expert Member

  #3
  Dec 23, 2011
  Joined: Apr 21, 2011
  Messages: 777
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 45
  tuanze basi, au unaonaje?
   
Loading...