Kwanini sitotii Kifungu cha 5 cha sheria ya Usalma wa Taifa

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,991
Utangulizi

Kuna wakati ambapo, raia au binadamu yeyote yule anatakiwa achukue msimamo. Kuna baadhi ya matukio ambayo yanatukia katika maisha na mazingira yetu ambayo yanatulazimisha kufanya uchaguzi. Mazingira au matukio hayo mara nyingi ni yale ambayo yako nje ya uwezo wetu, na ambayo hatuna uwezo wa moja kwa moja kuyazuia kutokea. Hata hivyo pindi yanapotokea, basi tunajikuta tunawekwa katika mahali ambapo kutochagua siyo sehemu ya uchaguzi. Ni lazima tuchague, ni lazima tuamue. Wakati kama huo kwa wananchi wa Tanzania umefika.

Sheria ya Usalama wa Taifa ya 1970

Tarehe 30 mwezi Machi 1970, Rais wa Muungano Mwalimu J. K. Nyerere alitia sahihi sheria mpya ya Usalama wa Taifa ambayo inajulikana kama "Sheria ya Usalama wa Taifa ya 1970". Sheria hiyo ambao imedumu kwa miaka zaidi ya thelathini na tano sasa, imekuwa ni sababu ya hofu na woga wa wananchi kwa nchi yao au vyombo vyao vya usalama. Pamoja na sheria hiyo zipo sheria nyingine nyingi ambazo kutumika kwake nchini kumekuwa kama leseni kwa vyombo vya usalama kufanya watakalo. Miongoni mwa sheria hizo ni ile ya "Kuzuia na Kuweka Kizuizini".

Hata hivyo kati ya sheria ambazo zilitumiwa vibaya huko nyuma na siku za hivi karibuni kuanza kutajwa tajwa ili kuzuia kusambaa huru kwa habari ni hiyo ya Usalama wa Taifa. Kipengele kikubwa kinachotumiwa kutishia wale walioupata mkataba wa Buzwagi ni kipengele cha tano cha sheria hiyo kinachosema: (msisitizo wangu)

5.-(1) Any person who communicates any classified matter to any
person other than a person to whom he is authorized to communicate
it or to whom it is m the interests of the United Republic his duty to
communicate it shall be guilty of an offence and liable on conviction to
imprisonment for a term not exceeding twenty years.
(2) In a prosecution for a contravention of subsection (1) it shall be
no defence for the accused person to prove that when he communicated
the matter he did not know and could not reasonably have known that
it was classified matter..


Katika kuelewa uzito wa kipengele hicho ni lazima tuelewe "classified matter" ni nini? Yaani "Suala Nyeti" Kwa mujibu wa sheria hiyo Classified matter ni:

"classified matter'' means any information or thing declared to be
classified by an authorized officer;


Ina maana Mkataba wa Buzwagi, kalamu ya Karamagi, na chumba walichosainia mkataba vyote vyaweza kuwa "classified"! Lakini maana hiyo inatuleta kwenye jambo jingine ni nani huyo ambaye "Authorized officer"? mwenye madaraka ya kuamua jambo fulani ni "Siri"?

Kwa mujibu wa sheria hiyo hiyo:

"authorized officer'' in relation to any provision of this Act means a
person authorized by the Minister to exercise the powers or perform
the duties conferred or imposed by such provision;


Na mwisho tunajiuliza ni Waziri gani mwenye mamlaka hayo? kwa mujibu wa sheria hiyo Waziri anayezungumzia ni:

''Minister'' means the Minister for the time being responsible for
national security;


Sasa, utaona kuwa sheria hii jinsi ilivyo licha ya kutoa maelekezo ya nini kifanyike inatoa pia upana mkubwa wa maana ya "national security" na pia inaweka vitu vingi mikononi mwa waziri huyo na hatari yake ni kuwa Waziri anaweza kutaja kitu chochote na jambo lolote kuwa ni la usalama wa Taifa na hivyo kutangaza habari zake kuwa ni kosa linaloweza kusababisha mtu kufungwa miaka 20!

Ni kwa sababu hiyo basi, wanapoanza kuzungumzia kuwa kuvujisha mkataba huu ni kosa na serikali inafikiria hatua za kuchukua basi wanajua wana msingi mzuri wa kesi hiyo. Kwa vile sheria hiyo haiwalazimishi serikali kwenda mahakamani kuthibitisha kuwa jambo fulani linatishia usalama wa Taifa basi ni rahisi sana kwa wao kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote anayeonekana kutishia usalama wa Taifa.

Katika kuzingatia hayo, ninajikuta kuwa kwa dhamira safi siwezi kabisa kutii kifungu hicho cha sheria kwani kinagongana moja kwa moja na kifungu cha Katiba yetu cha 18 ambacho kinasema kuwa:

18.-(1) Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru
kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta,
kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo
chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa
mawasiliano yake kutoingiliwa kati.
(2) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu
matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu
kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala
muhimu kwa jamii.


Hivyo basi majaribio ya kuingilia mawasiliano ya watu au kwa namna moja au nyingine kutafuta ni nani aliye na nakala za mkataba huo au mikataba mingine ni kugongana na Katiba. Kwa dhamiri safi siwezi kutii sheria ambayo naamini kuwa si halali na ni kinyume na Katiba. Kwa heshima kubwa na taadhima nimechagua na nimeamua kwa makusudi kabisa kutoitii sheria hiyo kwani kuitii au kujifanya naitii nitakuwa ninaisaliti dhamira yangu.

Ni kweli kuwa sheria hiyo ilitungwa kihalali na chombo halali, lakini athari zake katika maisha ya wananchi na katika utawala wa sheria na ukuu wa Katiba kunaifanya sheria hiyo isiwe yenye kutetea maslahi ya wananchi. Hata kama sheria imetungwa kihalali siyo lazima kuitii hasa kama athari zake ni kinyume na ukweli, usawa, haki, uwazi na uwajibikaji. Sheria ya Ubaguzi ilitungwa na vyombo halali, sheria ya kubagua watu weusi kwenye majimbo kadhaa huko Marekani zilitungwa kihalali n.k Wakati umefika kutotii sheria ambazo zimetungwa kihalali lakini athari zake ni kinyume kabisa usawa mbele ya sheria na Katiba.

Nimechagua, kutotii kipengele hicho cha sheria hiyo na kwa sababu hiyo nitaendelea kutoa nakala na jambo lolote lile ambalo limefanywa kificho na serikali yetu kwa kisingizio cha usalama wa Taifa na ni jukumu lao kuthibitisha mbele ya mahakama kuwa suala hilo ni la usalama wa Taifa!
 
"one has a moral responsibility to disobey unjust laws, and An individual who breaks a law that conscience tells him is unjust and who willingly accepts the penalty of imprisonment in order to arouse the conscience of the community over its injustice, is in reality expressing the highest respect for the law". "-Martin L. King.

"People imprisoned for following their consciences will not be criminals. They will be upholders of a noble tradition of resistance to injustice"-Henry David Thoreau (A US and democrat politician)
 
mkjj sema hayo ukiwa huko huko juu ya matawi ole upotee nje udondoke na usiitii uone tulivyo, utaelewa kwa nn macho yasiwekwe mgongoni
 
Mwanakijiji soma toleo jipya la katiba as ammended in year 2005, hicho kipengele bila ya kuadhiri sheria za nchi kimefutwa hivyo hakuna kipengele kama hicho tena ndio maana hata Buzwagi wameshindwa kumkamata Lissu na wengine kama CHADEMA ambao wanaugawa mkataba huo hadharani tena mchana kweupe ukienda kwenye makao makuu yao utawakuta na tena wanakupigia copy free of charge.
 
Haki Sawa, kipengele hicho cha sheria hakijafutwa na mabadiliko ya Katiba! Kumbuka katika Tanzania, hata mahakama ikitangaza kuwa kipengele fulani au sehemu fulani ya sheria ni kinyume na Katiba haina maana kuwa sheria hiyo imefutwa automatically.
 
Nazungumzia kipengele cha katiba kinachosema bila ya kuadhiri sheria za nchi hakipo tena kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , ibara ya 18.

Tafuta katiba toleo la 2005 ,utaweza kuona haya ninayosema mkuu.
 
Hiyo ni good news, kwamba hiyo sheria kandamizi ya usalama wa taifa sasa haina nafasi tena kwani inakinzana na sheria mama ya katiba ya Tanzania,

Sasa hapa la msingi ni kuomba na kusihi wasamalia wema watusaidie kupata hiyo mikataba mingine ya huko nyuma nayo ichambuliwe kama karanga ili watu tuzidi elewa tulivyo uzwa mchana kweupe, na pengine hii itasaidia kutupa fundisho la kutorudia kosa hapo 2010.
 
Back
Top Bottom