Kwanini ni muhimu kumsikiliza mwanao?

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
Mara nyingi huwa tunasisitiza umuhimu wa kumsikiliza mtoto. Kwanini tunasisitiza sana suala hili? Taarifa nyingi tunazopokea katika Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto kuhusu ukatili wa kingono huusisha mzazi/mlezi aliepuuza pale mtoto alipojaribu kueleza anachotendewa. Ukimuuliza mtoto ‘Je ulimuambia mtu yeyote?’ Mara nyingi jibu linakua ‘Nilimwambia mama/baba akaniambia “Unanisumbua. Toka hapa!”’ Wazazi hupuuza mashitaka ya watoto hadi wanapogundua watoto wamepata madhara na kujeruhiwa kwa sababu ya ukatili huu.

Watu wengi wamejijengea dhana kuwa watoto ni wasumbufu na wana maswali mengi na stori zisizo na maana. Ni kweli watoto wana maswali mengi kwa kuwa bado wanakua na wanagundua mambo mapya kila siku. Ni kweli pia kuwa kuna baadhi ya stori wanazohadithia watoto ambazo ni za kufikirika na wakati mwingine hutuhadithia stori hizi tukiwa tumechoka. Lakini hii haikunyimi nafasi wewe mzazi/mlezi kumsikiliza mwanao hata kama ni ‘makelele’. Kumbuka kuwa watoto, hasa wadogo, bado hawajajua kujieleza vizuri. Mara kwa mara watoto hutueleza mambo ya maana yanayohitaji umakini au utatuzi wetu kama wazazi/walezi.

Kulea mtoto hasa katika dunia ya sasa kuna changamoto nyingi na watoto wetu wanakabiliwa na mazingira hatarishi kila siku. Mzazi/mlezi unaposhindwa kumsikiliza mtoto na kumjengea dhana kuwa yeye siku zote anakusumbua, mtoto anashindwa kukushirikisha hata pale anapokuwa na shida au anapohitaji utatuzi na ushauri wako wa haraka. Usipomsikiliza wewe, nani wa kumsikiliza?

Wewe kama mtu mzima unapomsemesha mtu mzima mwenzako na haonyeshi kukujali wala kutilia maanani yale unayomwambia unajisikia vibaya na pengine utaacha kumueleza kile ulichokusudia. Vivyo hivyo, watoto hujisikia vibaya pale wazazi wasipowasikiliza mara kwa mara na baada ya muda wanaacha kuwashirikisha wazazi hata pale wanapofanyiwa mambo mabaya na kujikuta katika mazingira hatarishi.

Ukimsikiliza mtoto unampa kujua kuwa yeye ni wa thamani kwako na unamjali na kujali mawazo yake. Wataalamu wanaeleza kuwa mzazi akimsikiliza mtoto hujenga mahusiano ya karibu sana na kumfanya mtoto awe muwazi akiwa mdogo na hata akiwa mtu mzima. Utakuwa na rafiki wa karibu wa kumwamini ambaye ni mwanao hata akiwa mtu mzima. Jenga kumsikiliza hata ikiwa ni makelele. Jali mawazo yake na umjibu sio tu kwa kumfurahisha ila kwa kumaanisha.

Kama siku zote una majukumu mengi, jitahidi kupanga muda wa kuongea na mtoto uwe ni muda wa kuongea nae tu na sio jambo lingine. Msikilize kwa makini pale anapokuwa anaongea na utumie lugha rahisi kumuelewesha kwa ufasaha pale anapozungumza jambo ambalo haliko sahihi. Wataalamu wa makuzi ya watoto hueleza kuwa watoto wanaosikilizwa hujengeka na kuwa watu wazima wanaoheshimu mawazo ya wengine na kutoa mawazo yao kwa kujiamini na kujithamini.

Endapo utajenga tabia ya kumsikiliza mtoto, utamuepusha na mengi katika jamii na kuepuka yale majuto ya ‘Ningejua.’ Wazazi/walezi wengi hushtuka baada ya mtoto kukatiliwa sana kiasi cha kuumizwa vibaya na ndipo neno ‘Ningejua’ huja. Waswahili husema “Majuto ni mjukuu,” ila kwa nini ujute wakati unaweza kumuepusha mtoto wako na mabaya mengi kwa kumsikiliza na kumfanya awe rafiki wako wa karibu? Ukimsikiliza mtoto umemlinda pia.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

 
Mbali na kujua mengi pia tabia hii husaidia kuongeza urafiki na upendo mkubwa mno katika familia.

Wazazi wengi wa kanda ya ziwa hasa wakurya na wajaluo hawana(ga) kabisa muda wa kuwasikiliza watoto sijui kwann?

Wamekaa kikatili katili tuu..aaaagh.
 
"Ukimsikiliza mtoto unampa kujua kuwa yeye ni wa thamani kwako na unamjali na kujali mawazo yake. "- Sema Tanzania
 
Kuongea na kumsikiliza mtoto ni njia nzuri mnoo ya kujua changamoto anazopitia mtoto!
 
Shukrani mkuu kwa mada zako juu ya malezi ya watoto katika familia zetu
Lakini inatupasa tutambue kuwa malezi ni kitu tata sana
Utata ni pale unapokuta familia inayojitahidi kulea watoto kwa upendo, kujali na kumpatia mtoto mahitaji yote muhimu still bado unakuta familia hzo ndio viwanda vya kuzalisha watoto waliopinda.

Pia kuna zile familia tulizolelewa akina sisi yaani naweza sema nature ya mazingira ya kitaa ndio iliyoplay part kubwa zaidi kuliko visheria na controls za Mama na Baba na hivyo tulipata kujifunza mambo mengi kwa vitendo zaidi maana hawakua na overprotection kwa watoto na siku ukizungua unachezea kipigo cha mbwa koko.

"Tupunguze uzungu na kuwadekeza watoto"
 
Sema Tanzania

Kwanza nikushukuru kwa ujumbe huu. Lakini pia nikuombe siku ukipata muda utueleze kwa undani ni jinsi gani unaweza kumsikiliza mwanao akiwa anaongea na jinsi ya kuongea ili mwanao akusikilize kwa makini

usisahau kunitag siku ukitoa hili somo.
 
Wazazi washamba hasa baba akiwa na viseti " anaowa mke mwengine" ukimpa mawazo hataki...akiwa mzee pesa hakuna anakulaumu wewe .....
 
Mbali na kujua mengi pia tabia hii husaidia kuongeza urafiki na upendo mkubwa mno katika familia.

Wazazi wengi wa kanda ya ziwa hasa wakurya na wajaluo hawana(ga) kabisa muda wa kuwasikiliza watoto sijui kwann?

Wamekaa kikatili katili tuu..aaaagh.
MAKABILA YANAYOFUGA NG'OMBE HUWA HAYANA MUDA WA KUSIKILIZA WATOTO...
 
Back
Top Bottom