Kwanini hutakiwi kucheza ndani ya majengo ya ibada?

Jackwillpower

JF-Expert Member
Oct 4, 2017
2,299
3,411
Habari wapendwa katika Kristo!!!!

Suala la kucheza katika majengo ya ibada limekuwa ni changamoto katika madhehebu mengi ya Kikristo, na kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele hali ya kucheza inazidi kuvuka mipaka na kufanana na Ulimwengu, yaani imefikia wakati sasa imekuwa ni vigumu kutofautisha muimbaji wa nyimbo za injili na muimbaji wa nyimbo za Kidunia na imekuwa vigumu kutofautisha wimbo wa kumtukuza Mungu na wimbo wa Kidunia, kwa sababu Wakristo tumeacha kufanya HUDUMA na tumeingia kufanya BIASHARA, MASHINDANO NA MAONYESHO kupitia kivuli cha Injili.

#Warumi 12:2 Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.

Kwa hiyo zipo nyimbo za kumtukuza Mungu na Nyimbo za kidunia ambao zinamtukuza shetani, vilevile zipo style za kucheza za kumtukuza Mungu na kuna style za kidunia zinazo mtukuza shetani, kwa hiyo ni vizuri kukaa na kutafakari je hiyo style ya kucheza mnayoitumia Kanisani kwenye Ibada ni ya kidunia au ni ya kumtukuza Mungu!!

Fikiria kwanza Kanisani unacheza Kiduku na kwenye madisko na kumbi za starehe wanacheza viduku, Kanisani unengue na kukata viuno na kwenye Sengeli wanengue na kukata viuno.

1 #Wakorintho 10:31 Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.

Sasa katika Biblia tunaona kuna baadhi ya watu walicheza katika matukio mbalimbali, na kupitia mifano hiyo basi watu tumechukua kama kielelezo cha kuhalalalisha uchezaji ovyo ndani ya makanisa na hadi sasa Makanisa yamegeuka kuwa sawa na madangulo. Tunapozugumzia Kuheza kuna mapana yake, na kuna mipaka yake, kwa kuzingatia mazingira pia.

#Mfano: Wanajeshi wanapofanya MATCHING tunasema #wanacheza Gwaride, wanacheza kwa stape na pia wakiwa katika mistari, na hili hufanyika katika tukio maalumu. Lakini Wanajeshi hawahawa wakitoka vitani na wameshinda vita uchezaji wao ni tofauti na ule wa Gwaride kila mtu atacheza kivyake na kwa style yake kutokana na furaha aliyo nayo moyoni.

#Mfano: Mtoto anapoenda kwa baba yake kuomba fedha ya Ada huenda kwa unyenyekevu na kicho mbele za baba yake, lakini mtoto huyuhuyu anapoenda kwa baba yake kumpa matokeo ya kufaulu kwake mtihani, huwa anakuwa na furaha hata kumpelekea kurukaruka na kucheza kwa sababu amefaulu.

Kwa hiyo hata katika Biblia kuna aina mbalimbali za Uchezaji kulingana na matukio:

#Mfano:Isaka alicheza na mke wake:

#Mwanzo 26:8 Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe.

Wana wa Israel walipovushwa bahari ya Shamu walicheza #NOTE hawakucheza Hekaluni.

#Kutoka 15:20-21 Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza.Miriamu akawaitikia,Mwimbieni Bwana ,kwa maana ametukuka sana;Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.

Lakini tunaona uchezaji waliocheza wana wa Israel ukiongozwa na Miriamu ulikuwa ni uchezaji wa stapu, style ya Matching kwa sababu biblia inasema Walimfuata nyuma yake na Miriamu akiwa ametangulia akiwaitikia ina maana walikuwa wanacheza style ya kuzunguka Duara na sio kunengua na kukatika viuno.

Baada ya Daud kumuua Goliati watu waliimba na kucheza., bali walicheza kama matokeo ya furaha baada ya ushindi wa vita, na wala hawakucheza wakiwa kwenye hema Takatifu.

1 #Samweli 18:6-7 Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake.

Daudi baada ya kufanikiwa kulirudisha Sanduku la Bwana mahali pake, tunaona anacheza, #NOTE: Hakucheza Hekaluni na wala alipokuwa mbele ya Sanduku hakucheza ovyo bali alirukaruka tu kwa shangwe ;

Ni kweli alicheza lakini alicheza kistaarabu na wala hapa hakujifunua nguo, Bali alikoenda kucheza hadi akajifunua nguo ni nyumbani kwake Na wala sio mbele za Sanduku la Bwana. Kwa hiyo kuna aina za uchezaji alizocheza Daudi

1. Aina ya uchezaji Mbele ya sanduku la BWANA: Daudi alipokuwa mbele za uwepo wa Mungu alicheza, lakini hakujifunua nguo yoyote, ina maana alicheza kwa Adabu na staha mbele za Mungu.

2 #Samweli 6:16-19 Ikawa, sanduku la Bwana lilipoingia mji wa Daudi Mikali, binti Sauli, akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi akiruka-ruka na kucheza mbele za Bwana; akamdharau moyoni mwake.Wakaliingiza sanduku la Bwana, na kuliweka mahali pake, katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana.Kisha Daudi alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani akawabarikia watu kwa jina la Bwana wa majeshi. Akawagawia watu wote, mkutano wote wa Israeli, wanaume kwa wanawake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu. Basi watu wote wakaenda zao, kila mtu nyumbani kwake.

#NOTE: Program zote za kupokea sanduku zilimalizika salama na Daudi akawabariki watu salama na kila mtu akarudi nyumbani kwake, na wala haioneshi Daudi akijifunua nguo.

2. Aina ya uchezaji wa pili ni ule aliocheza akiwa nyumbani mbele ya wajakazi wake na si mbele za BWANA; Baada ya kumaliza program zote salama ndipo sasa Daudi wakati anarudi nyumbani kwake akaanza kucheza ovyo hadi kujifunua nguo.

2 #Samweli 6:20 Ndipo Daudi akarudi ili awabarikie watu wa nyumbani mwake. Na Mikali, binti Sauli, akatoka nje aende kumlaki Daudi, naye akasema, Mfalme wa Israeli alikuwa mtukufu leo namna gani, akijifunua mwili wake mbele ya vijakazi vya watumishi wake, mfano wa watu baradhuli mmojawapo, ajifunuavyo mwili wake mbele ya watu, asipokuwa na haya!

Uchezaji huu wa DAUD akiwa nyumbani ni tofauti na ule aliocheza mbele za BWANA na ndio maana Mikali akasema Daud anacheza mfano wa watu #BARADHULI,

Ukisoma Biblia yako yenye misamiati mwishoni mwa Biblia inasema #BARADHULI ni Mtu asiyefaa, au ni mtu #Mpumbavu sana. Ina maana kwamba Daudi alivuka mipaka ya uchezaji wa siku zote na ndio maana hata mke wake alishangaa. Kwa hiyo na wale wanaocheza makanisani kwa kumuiga Daudi kwamba alijifunua hadi nguo nao ni MABARADHURI yaani ni #WAPUMBAVU.

Sasa aina hii ya uchezaji wa pili wa Daudi ndio uchezaji unaotumiwa na baadhi ya Wakristo ndani ya majengo ya ibada na ndio mtindo huohuo unaotumiwa na wacheza #Sengeli na #Bongofleva ambao hucheza hadi kujifunua nguo,ndani yake kuna viduku na unenguaji(kukata mauno). Kwa hiyo hata wale ndugu zangu wanaosema wanacheza Makanisani kwa sababu Daudi alicheza hadi kufunua nguo wanakosea;

Daudi alipokuwa mbele za Mungu hakucheza viduku, au kunengua na wala hakujifunua nguo, bali alipokuwa nyumbani ndipo alicheza hadi akajifunua nguo, kwa mantiki hiyo kama unamuiga Daudi kwa kucheza ovyo, basi hivyo viduku kachezee nyumbani sio Kanisani, maana hata Daudi alifanya hivyo pia na wewe jifunue nguo.
Lakini pia kwa wale wanaume mnaosema mnamuiga Daudi kwa kucheza basi nawaombeni mumuige Daudi pia kwa kutembea na wake za watu, maana Daudi alizini na mke wa Uria.

Kwa hiyo si kila jambo ndani ya Biblia linahitaji utekelezaji hapana!! Kuna matukio mengine yaliandikwa ili kutuonya sisi tusiige,

1 #Wakorintho 10:11 Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.

Sasa kinacho sababisha watu kucheza ovyo ni kutokana na uwepo wa mrundikano wa vyombo vingi ambavyo vikipigwa hupelekea midundo yenye msisimuko wa mwili, Na ndipo sasa baada ya tukio hili la Daudi la kucheza ovyo hadi kujifunua nguo Mungu ikabidi atoe onyo juu ya vyombo vya musiki kwa wale wanaomuiga Daudi:

#Amosi 6:5 ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi;

Kwa hiyo kitendo alichokifanya Daud cha kupiga vyombo vingi vya musiki hadi ikampelekea kujifunua nguo Mungu hakukiafiki na ndio maana anaonya.

Licha ya kwamba tunamuona Daudi akicheza kwenye matukio mbalimbali, lakini katika suala la uimbaji ndani ya Ibada Daudi alikuwa makini na alipokea maelekezo kutoka kwa Mungu jinsi ya kuongoza kwaya ya Walawi, na hatuoni waimbaji hawa wakicheza kwenye Hema Takatifu wala Hekaluni, bali walisimama wakiwa na vyombo vyao waliimba kwa utulivu nyimbo za kumtukuza Mungu

2 #Mambo ya Nyakati 29:25 Akawasimamisha Walawi nyumbani mwa Bwana wenye matoazi, wenye vinanda, na wenye vinubi, kama alivyoamuru Daudi, na Gadi mwonaji wa mfalme, na Nathani nabii; kwani Bwana aliamuru hivi kwa manabii wake.

Hawa waimbaji hawakuimba wakiwa wanacheza viduku au kukatika viuno bali waliimba wakiwa wamesimama

2 #Mambo ya Nyakati 35:15 Nao waimbaji, wana wa Asafu #wakasimama mahali pao, kama alivyoamuru Daudi, na Asafu, na Hemani, na Yeduthuni mwonaji wa mfalme; nao mabawabu walikuwa katika kila lango; hawakuhitaji kuondoka katika huduma yao, kwa kuwa ndugu zao Walawi wakawaandalia.

KWANINI HAITAKIWI KUCHEZA NDANI YA MAJENGO YA IBADA?

1. Eneo la ibada sio sehemu ya kurukaruka kama Disko, ni mahali pa unyenyekevu palipotengwa maalumu kwa ajili ya mwanadamu kumuabudu Mungu na ndio maana tunatoka nyumbani kwenda kanisani. Kwa hiyo kinahitajika kicho.
#Waebrania 12:28-29 Basi kwa kuwa tunapokea ufalme usioweza kutetemeshwa, na mwe na neema, ambayo kwa hiyo tumtolee Mungu ibada ya kumpendeza, pamoja na unyenyekevu na kicho;maana Mungu wetu ni moto ulao.
#Habakuki 2:20 Lakini Bwana yumo ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele zake.
2. Malaika wenyewe ambao ni watakatifu wanamuabudu Mungu kwa kuimba kwa unyenyekevu wakiwa wamefunika nyuso zao, na sio kwa kurukaruka:
#Isaya 6:2-3 Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.
3. Ikiwa unapoenda kwa Baba yako mzazi au kwa bosi wako kuomba msaada unaenda kwa unyenyekevu na kicho, inakuwaje kwa Mungu uende kwa kucheza viduku na kunengua, ambaye yeye Mungu ni zaidi ya baba yako,na ni zaidi ya boss wako?
#Malaki 1:6 Mwana humheshimu baba yake, na mtumishi humcha bwana wake; basi, kama mimi ni baba yenu, heshima yangu iko wapi? Na kama mimi ni bwana wenu, kicho changu ki wapi? Bwana wa majeshi awauliza ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau jina langu. Nanyi mwasema, Tumelidharau jina lako kwa jinsi gani?
4. Je kuna mtu ambaye Alisha wahi kwenda kwa mzazi wake au kwa Boss wake kuomba mahitaji Fulani na akaenda kwa kupiga kelele na kwa kuchezcheza viduku?
Kucheza ndiko kunawafanya watu waimbe nyimbo za matusi na za kipuuzi,kwa sababu asiliia kubwa ya nyimbo za siku hizi hazina ujumbe wowote, bali zinapendwa kwa sababu ya style za kucheza na midundo iliyomo, #Zaburi 47:7 Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote, Imbeni kwa akili.


Sasa zipo nyimbo nyingi za injili ambazo ni za kipagani lakini zinapendwa kwa sababu ya midundo na aina ya uchezaji.mfano kuna muimbaji mmoja wa injili aliimba kwamba “SHETANI NA MAMA MKWE WAKE WAMEKALIA MISUMARI” Sasa huu ni upagani na sio fundisho la Biblia kwamba shetani ana mkwe, lakini kwa sababu ya style za kucheza na midundo inayofuika sauti watu tunazifurahia tu kwamba ni nyimbo za injili, wakati ni upagani.

Kwa hiyo hata Daudi anaposema watu tumsifu Mungu kwa kucheza hakuwa ana maanisha kucheza viduku na kukata viuno kwenye ibada maana yeye mwenyewe hajawahi kucheza ibadani viduku wala kukata viuno kama ilivyo katika makanisa ya leo,

#Zaburi 150:3-5 Msifuni kwa mvumo wa baragumu; Msifuni kwa kinanda na kinubi;Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na filimbi; Msifuni kwa matoazi yaliayo; Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.

MUNGU ATUSAIDIE NDUGU ZANGU TUJUE JINSI YA KUTOFAUTISHA KATI YA MAMBO MATAKATIFU NA MAMBO YA KIDUNIA TUSICHANGANYE PAMOJA: #Ezekieli 44:23 Nao watawafundisha watu wangu tofauti iliyopo kati ya vitu vitakatifu na vitu vya sikuzote, na kuwafundisha kupambanua kati ya yaliyo machafu na yaliyo safi.

MUNGU AKUBARIKI
1650061839806.png

1650061852527.png
 
Back
Top Bottom