Mtoto wa Mkulima
JF-Expert Member
- Apr 12, 2007
- 683
- 122
Hii dhana ya kuwa kila kitu kifanyike dar bila kuangalia strategic location nadhani ni matatizo ya kimaamuzi. Serikali inampango wa kujenga chuo kipya na cha kisasa cha utalii Dar. Mimi kwa moani yangu ningependekeza hiki chuo kijengwa Arusha ambako ndio kuna mandhari ya kitalii au badi Bagamoyo. Hii nadhani ninjia moja wapo ya kupunguza idadi ya watu Dar na kujenga ajira nnje ya Dar. Sio lazima kijengwe Arusha tuu lakini nasugest kisijengwe Dar.
Chuo cha kisasa cha utalii kujengwa Dar
2007-12-17 08:22:59
Na Futuna Seleman
Serikali inatarajia kujenga chuo kipya cha kisasa cha utalii, kitakachotoa mafunzo ya ngazi ya juu ili kuepusha Watanzania wengi kukimbilia nje ya nchi na kulipia gharama kubwa.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe, katika sherehe za mahafali ya tano ya Chuo cha Taifa cha Utalii.
Profesa Maghembe alisema kuwa, wizara kwa kushirikiana na serikali ya Ufaransa, tayari imefikia makubaliano ya kujenga chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Alisema taratibu za kumpata mkandarasi zipo katika hatua za mwisho na wakati wowote kuanzia sasa ujenzi utaanza.
Waziri Maghembe alisema kuwa, inakadiriwa kuwa asilimia 7.4 ya ajira zote nchini ni za sekta ya utalii na katika kila ajira 13 moja ni ya sekta ya utalii hivyo ni changamoto kubwa ya kuhakikisha kuwa kunakuwepo na wataalamu wa kutosha na wenye sifa zinazotakiwa kutoka hapa nchini.
``Sambamba na ujenzi wa chuo kipya, wizara ina mikakati ya kuinua viwango vya mafunzo yanayotolewa na vyuo vingine vya hoteli na utalii ili viweze kutoa mafunzo bora yenye kukidhi mahitaji ya soko,`` alisema Waziri Maghembe.
Alisema kuwa, katika miaka ya hivi karibuni sekta ya utalii katika pato la Taifa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo katika miaka ya 80 ilikuwa inachangia asilimia moja ya pato la Taifa ambapo hadi kufikia mwaka 2006 imeongezeka hadi kufikia asilimia 17.
Aidha, alisema idadi ya watalii wanaotembelea nchini imeongezeka kutoka wastani wa watalii 525,121 mwaka 2001 hadi kufikiwa watalii 644,124 kwa mwaka 2006.
Alifafanua kuwa katika kipindi hicho mapato yanayotokana na utaliii yaliongezeka kutoka dola za kimarekani milioni 725 hadi kufikia milioni 862 ambapo aliongeza kuwa sekta ya utalii ni ya pili katika kuchagia pato la taifa ikitanguliwa na sekta ya kilimo.
Aidha, alisema wizara inaandaa mitaala ya kitaifa ya mafunzo ya hoteli na utalii itakayotumiwa na vyuo vyote nchini kazi ambayo itafanywa na NACTE ambao wanajukumu la kudhibiti ubora wa mafunzo.
Kadhalika alisema, utafiti umebaini kuwa nafasi nyingi za uongozi wa juu katika sekta ya hoteli na utalii ziko mikononi mwa wageni hali inayotokana na chuo kutoa mafunzo katika ngazi ya cheti tu kwa muda mrefu tangu kianzishwe.
Alisema kwa mara ya kwanza chuo hicho kimewatunuku wahitimu wa stashahada ya usafirishaji na utalii ambayo imehakikiwa na NACTE hivyo itasaidia wahitimu hao kuwa washindani katika soko la ajira na kuwa na uwezo wa kujiajiri.
``Chuo kimeanzisha programu hiyo, nataka muendelee kuanzisha programu nyingine za uongozi katika fani ya hoteli mara ya ujenzi wa chuo kipya utakapokamilika kwani kutakuwa na vifaa vya kisasa na vya kutosha,`` alisema Professa.
Aliwataka Watanzania kuwa wa kwanza kujiandikisha na kufaidi matunda ya chuo kitakachojengwa kwa kujiendeleza zaidi.
``Ni vyema tukatumia vyuo vyetu hapa nchini badala ya kukimbilia nje ya nchi ambapo huenda gharama zake zikawa ni za juu zaidi,`` alisema
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi ya ushauri wa wizara hiyo Bi Blandina Nyoni aliwaasa wahitimu hao kuwa, wawakilishi wazuri mahali popote watakapokwenda kwa kufanya kwa uadilifu na uaminifu kwa kuzingatia utoaji huduma wa kiwango cha juu na cha kitaalamu.
Pamoja na mambo mengine alisema kuwa, nchi ina vivutio vya utalii maarufu na vyenye hadhi na ubora wa hali ya juu lakini ili inufaike hakuna budi kuwekeza katika rasilimali watu ili kiwango cha huduma zinazotolewa kwa watalii na wageni ziendane na ubora wa vivutio vilivyopo nchini.
SOURCE: Nipashe