Kwanini Dk. Mpango ni mpango kamili

Ngaliwe

Senior Member
Dec 30, 2015
161
364
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwashangaza na kuwapa matumiani Watanzania kwa namna alivyoanza utendaji wake wa kazi, taratibu na kwa uhakika anathibitisha kwamba kauli yake kwamba nchi iko kwenye mikono salama na hakuna kitakachoharibika.

Uteuzi wa Dk. Philip Isidori Mpango siyo tu umewaacha wamegwaya wasiolitakia mema taifa hili, lakini pia umeonyesha kuwa Rais Samia siyo tu amekuwa mwanafunzi mzuri wa Hayati Rais John Magufuli, kama ambavyo amekuwa akishuhudia mwenyewe, zaidi sana ameonyesha ni kwa namna gani amedhamiria kuendeleza pale walipoishia yeye na mtangulizi wake katika kuijenga Tanzania mpya.

Wapiga ramli na wale ambao walijifanya mashabiki wa muda wa Rais Samia, walijisadikisha bila kufikiri kwamba huu ni wakati wa kufuta na kuondoa kabisa urithi na fikra (legacy) za Hayati Magufuli, wamebaki wanaaibika. Sasa ujumbe umewafikia bayana kwamba Tanzania inasonga mbele hakuna muda wa kurudi kwenye maisha ya upigaji, rushwa, fitna na ubabaishaji katika utendaji kazi. Huu ni wakati wa kuendelea kulinda rasimali za Taifa kwa nguvu zote.

Uteuzi Dk. Mpango haukuja kwa bahati mbaya, huyu ni Waziri wa Fedha wa pili ambaye amehudumu katika wizara hiyo kwa muda mrefu zaidi, ukiondoa Waziri Amir Jamal aliyekuwa Waziri wa Fedha kuanzia Mwaka 1965 hadi 1972, na badaye kushika wadhifa huo tena mwaka 1975 hadi 1977 katika awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, Dk. Mpango ni waziri wa pili kuongoza wizara hiyo wa muda mrefu zaidi, ameshikilia wizara hiyo tangu mwaka 2015 hadi Machi, 2021 alipiteuliwa na kudhinishwa na Bunge kuwa Makamu wa Rais.

Hii maana yake nini? Ana uwezo mkubwa na anaaminika. Kudumu katika wizara nyeti namna hiyo chini ya uongozi wa Hayati Rais Magufuli halikuwa jambo la lelema, hiki ni kilelezo wazi cha uwezo na umahiri wake katika kuchapa kazi lakini zaidi sana uaminifu na uadilifu wake katika kuchapa kazi za ujenzi wa Taifa.

Dk. Mpango licha ya uadilifu, aliyaelewa vyema maono, malengo na dira za hayati Rais Magufuli na msaidizi wake wakati huo, Mama Samia, ndiyo maana iliwezekana kwake kuongoza wizara hiyo nyeti na kuwezesha ukusanyaji mkubwa wa mapato yaliyowezesha ujenzi wa miundombinu na miradi mikubwa ya kimkakati nchini.

Ukiyataja mafanikio ya Hayati Rais Magufuli katika jambo lolote huwezi kuacha kutambua mchango wa wizara ya fedha katika kuwezesha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Bwawa la Umeme la Nyerere, usambazaji wa umeme vijijini, ujenzi wa daraja la Tanzanite, daraja la Busisi, ununuzi wa ndege, ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati, kuongezeka kwa bajeti ya wizara ya afya na mafanikio mengine mengi.

Makamu wa Rais ni mtendaji zaidi kuliko mwanasiasa, hii ndiyo kusema Rais Samia anataka kujikita zaidi katika utendaji na utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mpainduzi (CCM). Kama ambavyo mwenyewe ameahidi baada ya uteuzi, kazi anayokuwa nayo kubwa itakuwa kwanza ni kuendeleza juhudi za kuyaendeleza yote mazuri yaliyoachwa na Rais Magufuli kwa manufaa ya Mama Tanzania.

Rais Samia anastahili pongezi za dhati na za pekee kwa uteuzi huu kwa sababu, anaonyesha dhamira ya dhati ya kuwatetea watanzania wanyonge katika kupata mahitaji yao ya lazima na muhimu kwa maisha. Dhamira yake ya dhati ya kukamilisha utekelezaji wa ilani kama alivyoshiriki kuinadi inajionyesha wazi, na kutoa matumini kwa watanzania kwamba yajayo yanafurahisha.

Watanzania tunayo kazi moja tu, kumuunga na kumpa ushirikiano wa kutosha Rais Samia na Makamu wake Dk. Mpango, tuwatie nguvu katika kuendeleza mpambano ya vita hivi vya kuchumi, hasa katika ulinzi wa rasimali zetu kama taifa.

Madini yetu lazima yaendelee kulinufaisha taifa, rasilimali za ardhi misitu ni wajibu wetu kuzilinda kwa manufaa yetu, haki kwa wanyonge na hasa wafanyabisahra ndogo ndogo na akina mama vijijini lazima itendeke, hatuna mashaka na uongozi wa Rais Samia katika hili, muhimu ni kuwaombea yeye na msaidizi wake, Mungu awaweke salama awalinde dhidi ya hila za wala rushwa, walafi na wasiolitakia mema taifa hili.

Kwa uteuzi wa Dk. Mpango kuwa Makamu wa Rais, Rais Samia amekamilisha mpango kamili wa kuijenga Tanzania mpya kwa nguvu na kazi ile ile iliyoanza na awamu ya tano, na kwa kweli hii ni namna njema sana ya kumuenzi Hayati Magufuli ambaye Mtanzania yeyote mwenye mapenzi mema, anakili kwamba ameifanyia makubwa nchi hii.
 
Back
Top Bottom