Kwani, watu wa mitandaoni siyo Watanzania? Rais Samia amejiongoza vibaya!

Apr 24, 2011
29
542
Kwani, watu wa mitandaoni siyo watanzania? Rais Samia amejiongoza vibaya!

Nani anamdanganya Rais wetu Samia? Kama Rais wetu hajadanganywa, kwanini ameamua kujiongoza mwenyewe vibaya katika hili la uhitaji wa katiba?

Nimemsikiliza vyema sana na kurudia mara kadhaa akimueleza mwandishi wa habari, Salim Kikeke wa BBC katika mahojiano maalum kwamba suala la katiba mpya linapigiwa kelele na watu waliopo mitandaoni na siyo watanzania.

Kauli ya Rais Samia naibeba kama taswira halisi ya CCM. Hawataki wimbo katiba mpya kabisa. Wanaamini ni njia ya kuwaondoa madarakani.

Ni kweli wataondoka tu. Hakuna chama cha kudumu madarakani milele. Lakini, katiba mpya itazungumza masuala mengi, haki, uhuru, usawa, utawala bora, afya, elimu, demokrasia. Wananchi, tuwalizimishe, tusiwabembeleze!

Nani alimueleza mpendwa Rais Samia kwamba watu waliopo mitandaoni siyo watanzania? TCRA wanaeleza mwaka 2014 watumiaji wa intaneti walikuwa 14.21M.

Kufikia mwaka 2016 idadi ya watu wenye kutumia simu za mkononi ilifikia watu 39.81M. Hii ni 69% ya watanzania wote. Kufikia mwaka 2016 wanaotumia intaneti walifika 19.86M. Ni kweli, TUNATAKA KATIBA MPYA!

Takwimu za TCRA (mamlaka ya serikali inayohusika na Mawasiliano) imetueleza hadi 2016 ni watanzania 39.81M walikuwa wanatumia simu za mikononi na watumiaji intaneti walikuwa 19.86M, vipi sasa takwimu za miaka 6 baadae, 2022? Ni wazi watumiaji wa intaneti wameongezeka. Ndivyo!

Dunia ipo kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda ambapo shughuli nyingi zinafanyika kwa kutegemea TEHAMA ikiwemo kilimo, uvuvi, ufugaji, viwanda, uchimbaji madini, biashara, utoaji wa huduma kama vile afya, elimu. Watanzania pia ni sehemu ya Dunia, wanatumia mitandao kwa shughuli zao.

Oktoba 14, 2021 katika kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wiki ya vijana na kilele cha mbio za mwenge wa uhuru zilizofanyika katika Wilaya ya Chato mkoani Geita, Kwa kutambua umuhimu wa Tehama, Rais SSH alisema Serikali imeondoa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye simu janja, vishikwambi na modemu ili kuwajengea vijana mazingira ya kujiajiri kwa maendeleo yao.

Siyo uongo, TEHAMA imewezesha shughuli nyingi kurahisishwa katika upatikanaji wake. Huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kama vile Ufugaji, Kilimo, Uvuvi, Afya, huduma za kibenki, uchimbaji madini, ulipaji wa bili za maji na nishati ya umeme kwa njia ya mtandao, ulipaji wa kodi na mapato ya Serikali,

Pia, urahisashaji wa upatikanaji wa huduma za afya na tiba, elimu, huduma za Vipimo, masoko, biashara, taarifa za hali ya hewa na upatikanaji wa taarifa mbalimbali na kupunguza upotevu wa mdana na gharama za kusafiri kutoka eneo moja kwenda eneo jingine kwa ajili ya kupata huduma na mahitaji mbalimbali. Maana yake, watanzania wapo mitandaoni wengi tu

Rais wetu, Samia amejiongoza vibaya katika hilo. Anasema watanzania wanataka maji, barabara, shule, hospitali, miundombinu, umeme na uchumi ulioharibika.

Nani aliharibu uchumi? Ninyi wenyewe mlitupa hadithi za uchumi wa kati wa viwanda na ukuaji wake wa kasi ya 7.3%. Nani kaharibu uchumi wenu imara usiotegemea mabeberu.

Hao wanaosema wanataka maji, barabara, shule, hospitali, miundombinu,umeme na uchumi ulioharibika wapewe, ni haki yao.

Wanalipa kodi, siyo hisani, ni haki yao kurejeshewa huduma stahiki za kijamii. Hao wanaotaka katiba nao ni haki yao. Katiba yetu imepitwa na wakati na haina misingi simamizi ya kujisimamia. Wapewe!

Hao waliopo mitandaoni ndiyo hao wapo mtaani. Mfano, mimi, MMM, nipo mtandaoni, lakini pia ninaishi mtaani, ninayo familia. Mke na watoto.

Tafsiri ya Rais ya kwamba waliopo mitandaoni siyo sahihi. Yeye pia yupo mitandaoni, ana akaunti Twitter na inaongoza kutoa salamu za vifo. Hivyo naye tumhesabu kama mmoja kati ya waliopo mitandaoni au wale waliopo ardhini, Magogoni na hawataki katiba?

Rais Samia anajua, labda kama amekubali kudanganywa au ameruhusu madaraka yamzidi nguvu. Samia alikuwa makamu mwenyekiti wa bunge maalum la katiba (BMK) mwaka 2014.

Bunge hilo lilifanya kazi ya maoni ya wananchi, kupitia tume ya Jaji Warioba, walitoa maoni yao nchi nzima, wanataka katiba mpya. SSH hajui alikuwa alifanyia kazi maoni ya wananchi na siyo CCM?

Wakati wa kukusanya maoni ya tume ya mabadiliko ya katiba, uliwekwa utaratibu kwa wananchi kutoa maoni kwa ambao watakuwa mbali na hawawezi kufika mbele ya tume.

Iliwekwa namba ya simu, unaandika ujumbe wako humo. Pia kulikuwa na ukurasa wa Facebook. Sasa hivi Kuna Clubhouse, Instagram, Facebook, Twitter etc, ndiyo SSH ashangae watu wa mitandaoni kutaka katiba mpya?

Rais Samia asikwepe jukumu na wajibu wake. Katiba hii haikumpa madaraka awe mfalme au Sultan, hapana. Ni LAZIMA atusikilize SISI waajiri wake.

Tunataka katiba mpya. Kama anadhani sauti haitoshi, anaweza kuunda kamati au tume maalum kukusanya maoni ya umma au kura za maoni. Athibitishe!

Hii haitakuwa mara ya kwanza kuunda tume. Harakati za kudai kurejeshwa mfumo wa vyama vingi zilipokolea nchi nzima mwaka 1991, Rais Ali Hassan Mwinyi aliteua Tume iliyoongozwa na Jaji Mkuu, Francis Nyalali kukusanya maoni ya wananchi na kutoa mapendekezo kujua kama taifa lilihitaji mfumo wa vyama vingi au kuendelea na mfumo wa chama kimoja.

Harakati hizo zilisababisha kubadilishwa kwa Katiba ili kurejesha mfumo huo ambao ulikuwa umefutwa Januari 14, 1963 kwa Azimio la Halmashauri Kuu ya Tanu.

Kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi kulisababisha kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1992, mbali na kusajili vyama anapaswa kuhakikisha sheria hiyo inafuatwa na vyama vya siasa.

Rais SSH anapaswa kutambua kwamba katiba mpya tunayohubiri kila uchwao, itaweka misingi ya kiuchumi imara ambayo itapambana na ufisadi mkubwa na ubadhirifu wa mali za umma unaofanywa na watawala na watumishi wa umma. Hatutataka tena kuwaona mafisadi wa ESCROW, EPA, RICHMOND, wakitamba mtaani. Katiba iwashughulikie.

Uchumi imara lazima uwekewe misingi. Lazima ziwepo itikadi na falsafa za kiuchumi ambazo tunatakiwa kuzifuata katika uchumi wa Dunia.

Je, katiba yetu imeweka misingi hiyo? Nchi yetu haina 'blueprint' ya kiuchumi. Tutaiweka vizuri katika katiba mpya. Itawajibika kutuongoza, tusiyumbishwe na upepo.

Serikali inayokusanya kodi kwa wananchi, haipaswi kufanya huduma za kijamii kama ni hisani. Ni wajibu wa serikali kutoa huduma za kijamii na hazipaswi kuzuia mambo mengine muhimu kufanyika. Tunaweza kupata fedha za kutengeneza katiba yetu (hata kwa kuchangishana) kama kilio chenu ni fedha.

Kama mnaweza kupata Shs. 11 bilioni za kutengeneza filamu yenu ya 'Royal Tour' ambayo hatujui kesho inaweza ikafanikiwa au isifanikiwe kutuletea neema, na mmetumia Shs. 7 bilioni, sioni sababu ya ninyi kusema fedha za kutengeneza muundo upatikanaji katiba mpya ni tatizo. Tunazo fedha. Fedha zipo. Umma tunazo. Tuwape?

Mwl, Nyerere alifuta mfumo wa siasa wa vyama vingi mwaka 1965 baada ya safari ya China. Tanzania ilirejea katika mfumo wa vyama vingi vya siasa Julai 1992.

Kilikuwa kipindi muhimu na cha mafanikio kwa wanaharakati wa mageuzi kama Mabere Marando, James Mapalala, Bob Makani na Edwin Mtei na wengine ambao waliongoza harakati hizo za kupigania mfumo huo.

Hata huu muundo wa siasa za vyama vingi vya kisiasa, CCM na wengine wengi (80%) hawakuupenda. Waliukata. Ni 20% tu walisema twende nao.

CCM Waliendesha kampeni nzito hadi kwenye taasisi za umma na vyombo vya kijeshi, wakatae. Na kweli waliukataa. Wachache walisema tunataka mfumo huo. Na busara 'za watu timamu' zikasema twende na wachache.

Chama cha siasa kinatakiwa kufanya siasa bila kujali vikwazo na changamoto zilizopo, kuepuka vyama shikizi vinaibuka nyakati za uchaguzi. Lakini mazingira ya kufanya siasa kwa uhuru yamekuwa na wakati mgumu, hasa baada ya Serikali kupiga marufuku shughuli za vyama vya siasa.

Sasa mmepiga marufuku mikutano ya hadhara, Maandamano ya vyama vya siasa ambayo yameruhusiwa na Sheria ya vyama vya siasa.

Ni Kwa namna gani vyama vya siasa, vitawafikia wananchi wao, kuwapa elimu ya uraia na kuwauliza kuhusu uhitaji wa katiba mpya? Acheni uoga. Tuwasikilize watu

Msijitazame tu kama CCM. Tokeni nje ya sanduku hilo, muone Tanzania yote. Mnaweza kuwa mnasikilizana wana CCM pekee, nje hamsikii, na ukizingatia mmewapa hofu wananchi, hawawezi kuandamana kuonyesha hisia zao na vyama vya siasa vipo kifungoni, hamsikii sauti za katiba mpya.

Uhuru wa kiraia na kisiasa si wa kudumu na unabanwa na sheria na kanuni nyingi sana nchini Tanzania. Uhuru huo unadhibitiwa na dola kupitia Jeshi la Polisi na vyombo vingine.

Chaguzi zilizopita hazikuwa huru na za haki. Rais Samia anapaswa kulitibu hilo kwa kutuacha na katiba mpya ambayo itaweka uwanja sawa wa kufanya siasa za vyama vingi bila dola kupora mchakato wa uchaguzi.

Dunia inabadilika, inastaarabika, inalinda misingi ya utawala bora ndani ya mipaka yao kupitia katiba, sisi tunabaki na kuganda hapo hapo tulipokuwa mwaka 1977.

Tutakuwa na aakili kweli? Bila shaka tunapaswa kustaarabika, Dunia inabadilika na sisi tunapaswa kubadilika pamoja na Dunia.

Nanukuu kauli ya Freeman Mbowe ameitoa Machame, Hai, Kilimanjaro, 20/3/2022 wakati akitoa shukrani kwa Kanisa la KKKT, Usharika wa Nshala Machame - Hai, kumshukuru Mungu na kanisa kwa kumuombea kwa kuwekwa gerezani kwa siku 227 tangu alipokamatwa July 2021, Mwanza katika kongamano la katiba mpya

“Huwa najiuliza, katika suala la katiba hivi tunagombania wapi, na kwanini tugombane. Hawa wanasema wanataka katiba na hawa wanasema wanataka shule, kwani aliyesema anataka shule wapi alisema hataki katiba bora?. Tukae tuzungumze tofauti zetu ziko wapi.” - Freeman Aikaeli Mbowe

Wananchi ndio jeshi la mstari wa mbele la ulinzi wa Katiba ya nchi yoyote Duniani. Tusimame kukataa kurudishwa kwenye mfumo wa chama kimoja.

Umoja wa ulinzi wa demokrasia (Democratic Front ) Ni muhimu zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote katika miaka 30 ya uwepo wa demokrasia yetu. MSIOGOPE!

Muda wa katiba mpya ni sasa, siyo jana, siyo kesho, siyo vinginevyo. Saa ya ukombozi ni sasa!

#MMM, Martin Maranja Masese
 
Watanzania wa kawaida hatuitaki katiba mpya ya serikali 3 itatuongezea mzigo wa Kofi

Kama CDM mpo tayari kudai katiba mpya yenye serikali 2 semeni tuwaunge mkono
 
Kauli ya Rais SSH naibeba kama taswira halisi ya CCM. Hawataki wimbo katiba mpya kabisa. Wanaamini ni njia ya kuwaondoa madarakani. Ni kweli wataondoka tu. Hakuna chama cha kudumu madarakani milele. Lakini, katiba mpya itazungumza masuala mengi, haki, uhuru, usawa, utawala bora, afya, elimu, demokrasia. Wananchi, tuwalizimishe, tusiwabembeleze!
Wao katiba mpya wanawaz tu kuwatoa madarakani.

Hawafikirii faida nyingi na pana za katiba mpya.
 
Martin Maranje Masese:

Andiko ni zuri lakini nini hasa dhumuni lako mkuu? Tunamlenga mtanzani gani wa jukwaa la social network/ vijijini ambao network mpk kupanda juu ya mti au anayesubiri barabara na maji yamfikie?
Ili kujua watu wa vijijini wnaataka katiba mpya au hawataki acha wafanyiwe makongamano na elimy ya kutosha.

Maana wao hawana mabando na smartphone. Wape uhuru wa kukusanyika uone mtiti wake.
 
Hata huu muundo wa siasa za vyama vingi vya kisiasa, CCM na wengine wengi (80%) hawakuupenda. Waliukata. Ni 20% tu walisema twende nao. CCM Waliendesha kampeni nzito hadi kwenye taasisi za umma na vyombo vya kijeshi, wakatae. Na kweli waliukataa. Wachache walisema tunataka mfumo huo. Na busara 'za watu timamu' zikasema twende na wachache.
Vyombo vinasikia. Wakati ni sasa.
 
Back
Top Bottom