Kwaheri ya kuonana wapiganaji wetu

PJ

JF-Expert Member
Oct 10, 2007
297
32
Kwaheri ya Kuonana Wapiganaji Wetu

MWENYEZI Mungu ni mmoja. Yeye ndiye huwajalia waja wake ufahamu na utambuzi. Huyu kamjalia busara na hekima na mwingine kajaliwa maisha ya ujanjaujanja tu. Shetani ni mwovu naye ana waovu wake. Unafiki kama ulivyo usaliti ndiyo kazi ya shetani.

Wasaliti wa wananchi sasa Mungu anawaanika hadharani. Waumini wa kweli hujiepusha na shetani na wote wafanyao kazi yake nao humsujudia Mwenyezi Mungu Subhaanah wa taaala.
Wiki chache zilizopita Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipompata Spika mpya bila kusita alisema moja kwa moja kuwa hajui kama kuna mafisadi maana fisadi ni mtu anayetongoza wake za watu.

Kwa mtazamo wake ni kwamba hata kama watu wanaotongoza wake za watu wapo, hili si suala la kujadiliwa bungeni. Nadhani ni kweli hili si suala la kitaifa. Bungeni iende mijadala ya kitaifa. Mtu akikutongozea mkeo kuna taratibu za kufuata. Unaweza ukaanzia hata kwa mwenyekiti wako wa mtaa kuna ubaya gani? Sema tatizo linakuwa pale mkeo naye anaporidhia.

Swali la kujiuliza hapa ni je mafisadi wapo au hawapo? Kwa mtazamo wa mama Spika mafisadi hawapo. Kama anasimamia maana halisi ya neno fisadi kama lilivyotafsiriwa katika kamusi ya Kiswahili sanifu ya Oxford toleo la pili yuko sahihi.

Akibaki na uelewa huu maana yake mijadala ya ufisadi na mafisadi bungeni katika kipindi chake ni marufuku. Sijui kama hawa wenzetu walielewa kuwa ule ulikuwa mwanzo wa sinema.
Waswahili nao wana msemo wao usemao, lisemwalo lipo, kama halipo linakuja. Kama kweli jambo halipo utalisemaje? Kwanza utalijuaje mpaka uliseme? Hata hivyo nao hawakuwa wajinga.
Ndugu yetu Reginald Mengi aliwahi kulitangazia taifa kupitia televisheni yake kuwa mafisadi papa wapo na akawataja kwa majina. Alikuwa anakiri hadharani kuwa ufisadi kwa maana tofauti na ile iliyoko katika kamusi upo.

Ndugu yetu Rostam Aziz naye alilitangazia taifa kupitia Televisheni ya Taifa kuwa kuna mtu hapa nchini ambaye ni fisadi nyangumi. Naye akamtaja nyangumi wake kwa jina. Vile vile na yeye alikuwa anakiri hadharani kuwa ufisadi kwa maana tofauti na ile iliyoko katika kamusi upo.

Siko hapa kuhubiri dini lakini nilitangulia kusema kuwa Mungu ni mmoja. Binti yangu bado yuko shule, kweli Mungu yupo. Ninapoandika (nilipokuwa naandika} makala hii binti yangu anaingia na ripoti ya shule ya kufunga muhula. “Baba, baba nimekuwa wa kwanza”. Akaniambia.

Mara chache sana anakuwa wa tatu lakini mara nyingi anakuwa wa pili. Sasa wa kwanza, sikuona sababu ya kuzuia machozi ya furaha. Kweli Mungu hamtupi mja wake.

Mungu wetu kwa huruma yake hiyohiyo kwetu Watanzania, Rais wetu Jakaya Mrisho Kikwete ametutangazia baraza lake la mawaziri. Wengine tunawajua, wengine hatuwajui. Ni jema ni baya tutapata muda mwingine wa kulijadili, leo tuuone upendo wa Mungu kwetu kutokana na baraza hili.
Ameturejeshea mwana mwema John Pombe Magufuli katika ujenzi wa barabara za nchi yetu. Tunamshukuru kwa maana aliyekuwako kabla angekuwa hakuwapo ingekuwa bora zaidi kwetu na kwa nchi yetu. Alikuwa mtu wa kuthibitisha ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma kwa kujenga barabara ambazo kwa kweli hazikuwa barabara.

Tuliandika kuwa kwa ujenzi wa kifisadi wa barabara uliofanywa katika Barabara ya Kilwa - Bendera Tatu hadi Mbagala Rangi Tatu, jina la John Pombe Magufuli lisingeweza kusahaulika katika kumbukumbu za Watanzania.

Mungu kasikia kilio cha watu wake. Kawarudishia mwana mwema huyu barabarani. Kama ningelikuwa na uwezo wa kumfikia ndugu Magufuli ningemwambia neno moja nalo ndilo hili.
Wakati wenzako watakuwa na kazi moja tu katika muhula huu ya kujitengezea mitandao kwa ajili ya urais wa 2015 wewe mtandao wako uwe ni barabara. Jenga barabara kama huna akili nzuri. Watanzania wa 2015 watakuwa ni watu tofauti na wa leo. Barabara hizi zitakuja kukusemea. Nazo zitakuwa ndiyo mtandao wako.

Rais wangu walau katika nafasi nne ulizocheza umecheza kama Pele. Kumtoa nje ya nchi na kumpeleka Afrika ya Mashariki mbali, Wahehe wanasema ni sawa na kumpa mbwa mfupa akahangaike nao huko, ikiwezekana akafe nao.

Naye kwa kuwa amekubali basi watu watasema amejinyonga mwenyewe kumbe sumu aliyokwisha kuimeza ingemua tu. Huu ndio mwanzo wa mwisho wa mtu huyu.
Kumpeleka mtu akawe chini ya uangalizi wa ndugu John Pombe Magufuli umefunga kazi. Hivi kweli kuna mtu yeyote anaweza kusuka dili au misheni chini ya uangalizi wa Magufuli? Baba kuwachinjia baharini watu hawa Mungu akubariki sana.

Haya hayakutokea kwa bahati mbaya. Hii ndiyo mipango ya Mungu. Walipokubali nyadhifa hizo Mungu alitaka Watanzania wawajue hawa ni watu wa aina gani.
Baba Muadhama aliposema wanaopiga kelele za ufisadi kwa sababu wao wamekosa nafasi ya kufisadi wanyamaze kwa kuwa wanawaongezea wananchi hasira hawakunyamaza. Sasa watanyamaza na amani itapatikana.

Bora ndugu yetu Fred Mpendazoe angalau alitutajia jina moja la fisadi lakini hawa walikuwa wanasema mafisadi, mafisadi tu. Hawakuwahi kututajia hata jina la fisadi mmoja. Nawalilia watu hawa kama Kristo alivyoulilia mji wa Yerusalemu. Laiti wangelijua mateso na machungu ya 2015 wangekomboka sasa.
Wakati huu waliowamezesha ndoana hii wataamua, wawakaange, wawachemshe au wawatupie mbwa. Kwa hakika watakuwa hawafai kuliwa na binadamu.

Unapofungwa ufisadi mmoja unaanzishwa ufisadi mwingine. Sasa ni ufisadi wa udini. Wana wema wa Vox Media waliandaa mdahalo kati ya kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni wa sasa na yule aliyepita. Nawashukuru wana wema hawa kwa jitihada zao za kuwapa fursa Watanzania wenzao kutambua mwenendo wa nchi yao unavyokwenda na kutambua aina ya viongozi walionao.
Wengine tulikwenda tukijua kuwa tunakwenda kupambana kutumia vichwa vyetu ili kufikia muafaka wa kupata Tanzania tunayoitaka.

Kwa bahati mbaya sana wengine walikuja kupambana kwa kutumia vifua vyao na hisia zao. Mapambano ya vichwa hayana uhasama wala jazba, watu mnapambana kwa hoja. Lakini ya hisia na ushabiki tu kama mpirani ni hatari na ni ujinga.

Watu walipoanza kuimba CCM CCM ndani ya mdahalo bila sababu ya kuonekana ndipo likanijia lile wazo la polisi mtu na polisi mbwa. Nikajiuliza, inawezekana CCM wamepata polisi mbwa? Kama ni hivyo taifa linapelekwa kuzimu.

Omba ukamatwe na polisi mtu kuliko kukamatwa na polisi mbwa. Haelewi kitu. Nikajikuta katika mazingira magumu. Sikusema chochote, kuogopa kufanana nao.
Jirani yangu akaniuliza, kwa nini kila anayesema nchini kuna tishio la udini ni Mwislamu? Nikashtuka, ala kumbe. Mheshimiwa alitoa mfano uliotupatia jibu. Alisema kuwa aliambiwa na mtu wa CHADEMA kuwa wao CUF wananuka Uislamu na yeye akamjibu kuwa CHADEMA nao wananuka Ukatoliki.
Mtu mwenye uelewa kama yule kuufananisha Uislamu na Ukatoliki, kitu ambacho ni sawa sawa na kuufananisha Utanzania na Usukuma au Uhaya, kabila mojawapo katika Tanzania hakuwezi kuwa kitu cha burebure tu au bahati mbaya. Kumbe tatizo hapa si udini ni Ukatoliki kwa sababu ingekuwa ni udini angesema Ukristu.

Na ukatoliki unaosemwa hapa siyo ule wa Baba Mtakatifu ni ukatoliki wa Dk. Slaa. Ndiyo kusema tishio kwa watu hawa wanaosema udini siyo udini wala si Ukatoliki ni Willibrod Slaa. Lakini Dk. Willibrod Slaa na nchi, kipi muhimu zaidi jamani?
Ndugu zangu tujifunze kwa yaliyotupata huko nyuma. Manabii wa uongo waliisimamisha nchi kwa miaka mitatu wakituhubiria juu ya vita hewa ya ufisadi. Kumbe haikuwa ufisadi ilikuwa ni Richmond. Kumbe haikuwa vita ya ufisadi wala ya Richmond ilikuwa ni woga wa watu hawa ambao kwao walimwona mtu mmoja tu kuwa mtu tishio kwao.

Wenzetu sasa ni mawaziri. Wanakula na kusaza wao na familia zao. Tuliokuwa tunawashabikia tunaendelea kunuka jasho. Na sasa litatutoka jasho la damu.
Hakuna tishio la udini katika nchi yetu. Ni kikundi na mbinu za watu wachache katika utawala ambao wanamwona ndugu Wilbroad Slaa kuwa mtu tishio katika utawala wao.
Watanzania tujiulize tuko tayari kukaa tena miaka mitatu au zaidi mingine tukiwa kwenye vita hewa ya udini kama tulivyokaa kwa ile vita hewa ya ufisadi? Ni mikosi gani tulizaliwa nayo?
Wale walioimba CCM CCM katika mdahalo watakapowaona viongozi wao wakipewa vyeo wanavyovililia na kuwageuzia mgongo kama vile hawakuwapigania, nina hakika watayakumbuka maneno yangu haya nukta kwa mkato. Wahenga walisema, Wajinga ndio waliwao. Tumeliwa vita hewa ya ufisadi sasa wanatupeleka katika vita nyingine hewa ya udini ili waendelee kutukamua mpaka tone la mwisho. Mwenyezi Mungu atawaamulia WAJA WAKE.

Source: Tanzania Daima (By Pascally Mayega)
 

Nabii X

Member
Oct 24, 2010
7
0
Mimi mwenyewe mara nying najiulza nakuwaza majbu nnayopata ni watanzania 2nafanywa wendawazmu,ila ukwel mabadlko ni lzma bnafs nimechoka uongo
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Top Bottom