Kwaheri kaka yangu, mzungumzaji wangu Jimmy Mdoe

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,857
30,205
KWAHERI KAKA YANGU BURIANI MZUNGUMZAJI WANGU JIMMY MDOE

Nilikuwa nakaribia kufunga ofisi yangu ujumbe ukaingia kunipa kifo cha Jimmy Mdoe.

Nilifahamiana na Jimmy Mdoe kwa karibu katika miaka ya 1980.

Nilikuwa ndiyo kitabu changu cha maisha ya Abdul Sykes kimetoka na yeye naamini ni katika watu wa mwanzo kukisoma.

Siku moja akaniita akaniambia kaona makosa kadhaa katika kitabu changu pale nilipotaja magazeti na wamiliki wake wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.

Akanieleza kuwa alikuwa akinitafuta anieleze historia ya gazeti la Mwafrika ambalo sikulieleza ipasavyo.

Nilivuna elimu ya bure siku ile kutoka kwa Jimmy Mdoe ambae kwa umri mimi ni bwana mdogo kwake.

Alifurahi sana jinsi nilivyowaeleza wajomba zake wawili katika harakati za kuikomboa Tanganyika - Steven Mhando na Peter Mhando.

Alinieleza kuwa jinsi nilivyomweleza mjomba wake Steven Mhando na msimamo wake mkali dhidi ya ukoloni ndivyo alivyokuwa katika maisha yake hadi uhuru ulipopatikana.

Siku moja Jimmy Mdoe katika mazungumzo akaniongezea kitu ambacho sikuwa nakijua.

"Unajua Steven Mhando ndiyo alikuwa Mwingereza wao? Steven Mhando alikuwa na kipaji kikubwa sana cha uandishi wa lugha ya Kiingereza katika kundi lao lote lile la Julius Nyerere, Hamza Mwapachu, Abdul Sykes wote wale hakuna aliyemfikia Steven Mhando kwa kuandika Kiingereza. Barua akiandika Steven Mhando Nyerere alikuwa hathubutu hata kubadili nukta wala koma. Hii ndiyo sababu ya kumwita Mwingereza wao."

Hakika hili sikuwa nalijua. Iko siku niko Tanga miaka mingi sana imepita nilikutana na Mwalimu Steven Mhando barabarani, Mkwakwani Road.

Alikuwa mtu mzima kavaa kofia ya pama kichwani anatembea kwa hatua ndefu ndefu kama mtu mwenye haraka kichwa kainamisha chini.

Nilikuwa nimeongozana na Sharif Mohamed Yahya na yeye kwa kujua mapenzi yangu katika historia akanionyesha Steven Mhando aliyekuwa anakuja akielekea tulikokuwa tunatoka sisi.

Jimmy Mdoe alikuwa na hazina ya "anecdotes," akiniambia kuwa Mwalimu Nyerere akipenda kumwita yeye, "Mhando" jina la mjomba wake badala ya jina la baba yake, Mdoe.

Jimmy Mdoe alipata kunihadithia kisa kimoja alipokuwa BBC katika miaka ya 1960 Nyerere alipofanyiwa mahojiano na mtangazaji mmoja wa BBC World Service aliyekuwa na sifa ya kuwahenyesha marais kutoka nchi za Kiafrika kwa maswali yake ya uchokozi, kuudhi na kebehi.

Jimmy anasema vijana wengi kutoka Afrika waliokuwa watangazaji walikuwapo pale studio kusikiliza mahojiano yale.

Mahojiano yalikwenda vyema kwa pande zote mbili zikirushiana makombora.

Lakini huyu mtangazaji Mwingereza alikuwa mjanja alikuwa na swali lake kaliweka akingojea zibakie dakika chache kipindi kumalizika ndiyo amvurumishie Mwalimu na wakati Mwalimu anahangaika kutafuta majibu yeye atamaliza kipindi.

Hii ndiyo ilikuwa kawaida yake kuwafedhehesha viongozi kutoka Afrika.

Waingereza wana msemo, "Caught with pants down."

Huyu Mwingereza alitaka kumweka Mwalimu katika hali kama hiyo ya kuvukwa na nguo ili kumfedhehesha mbele ya ulimwengu kwa kushindwa kutoa majibu ya maana kwa swali aliloulizwa.

Bado kama dakika tatu kipindi kumalizika yule Mwingereza akamtoa nyoka wake kikapuni. Akamwomba Mwalimu aeleze kuhusu machafuko yaliyoko Afrika yanayosababisha vifo vingi.

Mwalimu hata bila ya kufikiri kwa robo sekunde akasema, "Basi kuhusu machafuko na vifo tuanze na machafuko na mauaji yaliyoko Northern Ireland."

Studio upande ule walikokuwa akina Jimmy Mdoe ililipuka kwa vifijo.

Kidagaa kilimuozea Mwingereza. Kipindi kilikuwa kinamalizika na dakika zinayoyoma na Mzungu kakaukwa na koo.

Mwalimu kama kawaida yake katumbua macho anamungunya midomo yake anamwangalia yule mtangazaji.
Mwingereza alitoka studio kichwa kakiinamisha.

Nilikuwa sichoki kumsikiliza Jimmy Mdoe.

Kwaheri kaka yangu kwaheri mzungumzaji wangu Jimmy Mdoe.

May be an image of 1 person and text
 
Leo bro umeleta habari za Jimmy huyu huenda ni James wale wanaokunanga na dini zao hawana la kusema.keep it up we we ni hazina ya thamani sana.
 
Nilisoma kitabu cha hadithi za watoto, utotoni mwangu, mwandishi Fred Jim Mdoe; kama sikosei, kitabu ni Jua na Upepo. Sijui ndio huyu mwandishi mwenyewe?

Pumzika kwa Amani
 
Mohamed Said,

Mimi namkumbuka Fred Jim Mdoe kutokana na jarida lake la Fahari miaka ile ya enzi za Uhuru na Mzalendo.

Pia alikuwa anazungumza Kiingereza kilichonyooka kwelikweli, na alikuwa mtu very smart mtanashati.

Rest in Peace Fred Jim Mdoe.
 
Back
Top Bottom