Kwa Waziri wa Mambo ya ndani, RPC & RTO Mwanza: Kwanini vijana wenu (Traffic Police) wanatubambakia faini madereva bila kujua..?

The Palm Tree

JF-Expert Member
Apr 13, 2013
7,951
12,535
Hii siyo haki na kamwe siyo halali hata kidogo.

Sisemi kwamba madereva hawafanyi makosa ya usalama barabarani, yanafanyika lakini hata hivyo siku hizi kwa kiasi kikubwa madereva wengi wanajitahidi kuwa makini. Hili hata mimi nakubali.

Hii haijaja hivihivi bali ni kwa sababu idara ya Polisi - Usalama barabarani wamefanya kazi kubwa kujenga nidhamu kwa watumiaji barabara kuanzia kwa waenda kwa miguu hadi madereva wenyewe. Kwa hili hongereni Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, hii kidogo inaonesha baadhi ya polisi hawapendi hali hii. Wao wanataka waone madereva wanakosea tu ili wawatoze faini, kidogo waingize serikalini na kidogo waibe ziwe zao.

Hii wakati mwingine inafanyika kwa kutafuta makosa ya kulazimisha na wakikosa wanakubambikia faini bila wewe dereva kujua ulitenda kosa gani na wapi.

Kinachotokea ni kuja kushitukia deni lilishajizalisha kwa 100% pale unapokuwa katika safari zako na kusimamishwa na kuambiwa gari yako inadaiwa...!

Huu mchezo mchafu kabisa uko Mwanza.

Kwa uchunguzi wangu naweza kusema bila shaka yoyote kuwa RPC , RTO, OCDs na DTOs wa jiji la Mwanza na wilaya zake wanaujua, na (pengine) wanaushiriki pamoja na vijana wao wanaowapanga barabarani.

Wanao onewa zaidi kwa 95% ni madereva wa magari yanayotoa huduma ya usafiri ndani ya jiji (daladala) Hiace na Coaster.

Kinachofanyika ni hiki: Mmesambaza vijana wenu (Traffic police) kila barabara kuu za mji; inayoingia kutoka Shinyanga/Dar, inayotoka kwenda Musoma/Tarime/Sirari, inayokwenda Airport/Igombe nk.

Police wanawataka madereva hawa (wanaotaka kuwa salama), kila siku watoe kwa police kati ya Tshs. 5,000 hadi 10,000. Wanaita "Uhuru na usalama wako fee". Hii ni ya kwao, haingii kwenye mfuko wa serikali na haikatiwi risiti.

Dereva yeyote akikaidi na akionekana kupingana nao kwa siku kadhaa ama wiki, basi cha mtema kuni atakiona.

Kinachofanyika, kuna polisi wanatembea na Pikipiki SANLG au TOYO ama KINGLION nk zenye namba za kiraia tu (siyo PT) wanasaka kila "daladala" ambayo haijatoa "fee" isiyo rasmi. Wanachukua namba ya usajili ya gari. Unapigwa faini kwa makosa usiyoyajua mawili ama matatu bila wewe kujua.

Utaendelea na kazi yako vizuri. Inafika siku ya siku unasimamishwa na kuambiwa gari yako inadaiwa.

Bahati mbaya unakutwa na hali hiyo zinakuwa zimepita siku ama wiki kadhaa na faini hiyo inakuwa imeshajizalisha (penati) mara mbili.

Mtazozana na askari lakini mwisho wa siku mfumo unasoma na kuonesha unadaiwa na inakulazimu ulipe tu. La hutaki, acha kazi yako siku hiyo, paki gari yako yadi ya polisi mpaka upate fedha uje ulipe deni lako.

Hii siyo nzuri na siyo fair. Huu ni uonevu na ni wizi wa mchana kweupe unaofanywa na askari wenu.

Uchunguzi wangu umebaini pia kuwa, hiki kinachofanyika viongozi wa jeshi la polisi ngazi ya mkoa na wilaya wanakijua na hivyo ni wazi kuwa kina baraka zao.

Na hii maana yake kila kinachopatikana huko barabarani kinagawanywa sawia kuanzia chini hadi kwa kwa maafisa wa polisi walio ofisini...!!

Tunaomba hii tabia iachwe mara moja.

Jeshi la polisi kitengo cha Usalama Barabarani wafanye kazi yao fairly kwa mujibu wa sheria na utaratibu.

Tozeni faini madereva wazembe na wasiojali sheria za usalama barabarani kwa uwazi na ukweli huku dereva naye akiwa atambua kuwa amefanya kosa na anastahili kuadhibiwa.

Aidha nitoe rai pia, kuwa, jamani wakati mwingine siyo kila kosa ni faini. Hekima na busara itawale tafadhali. Makosa mengine ni ya kuelimishana kwa kutoa maelekezo tu. Siyo kila kosa ni faini wakati huo huo labda ikitokea ulimpa maelekezo na muda wa kuerekebisha dosari fulani na asifanye hivyo.

Nasema hivi kwa sababu kuna askari mwingine akikusimamisha ni kama amekula ndimu, amekunja uso hasikilizi wala haelewi.

Yeye akiona mpasuko mdogo tu wa kioo usiozidi 2cm, au huna fire extinguisher au pengine leseni ime - expire siku mbili au tatu zilizopita, yeye haelewi wala hasikilizi badala yake ni kufoka kwa karaha mwanzo mwisho na mwisho anakulamba na faini juu.

Let's be fair ndugu zangu. Hali yenyewe ya uchumi ndiyo hii. Pesa imeminywa. Imo mikononi mwa wachache tu.

Ila Muhimu ni hili. Traffic police acheni kuvizia na kubambikia makosa...!!

Msitumie machine zenu hizo za risiti vibaya eti tu kwa sababu una ugomvi binafsi na mwenye gari namba fulani...!

Nawatakia kazi njema polisi wema na wenye maadili wote.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom