Kwa ujinga wetu, tunaporwa roho na rasilimali | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kwa ujinga wetu, tunaporwa roho na rasilimali

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by sulphadoxine, Dec 2, 2011.

 1. sulphadoxine

  sulphadoxine JF-Expert Member

  #1
  Dec 2, 2011
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,264
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  MEI 2 5, 1963, mjini Addis Ababa, Viongozi wa nchi 31 za Afrika walioanzisha Umoja wa nchi huru za Afrika [OAU] siku hiyo, walikuwa na kazi ngumu kucha gua kipi kipewe kipaumbele na umoja huo, kati ya vita vya ukombozi wa kisiasa dhidi ya ukoloni mkongwe, na vita vya ukombozi dhidi ya ubeberu wa kiuchumi wa nchi za Magharibi.

  Ni Rais wa kwanza wa Ghana na mwanaharakati wa mapambano barani Afrika, Kwame Nkrumah, aliyetegua kitendawili hiki kwa tamko lake maarufu kwamba, “Utafuteni kwanza ufalme wa kisiasa na mengine yote mtazidishiwa”.

  Kwa kibwagizo hicho, OAU ilianza harakati kwa kujikita zaidi katika vita vya ukombozi wa kisiasa barani Afrika badala ya ukombozi wa kiuchumi. Nkrumah akasema, Ghana iongoze harakati hizo na Makao Makuu ya ukombozi yawe Accra, Ghana; lakini Julius K. Nyerere wa Tanzania akapinga, akasema, Makao Makuu yawe Dar es Salaam, karibu na kichwa cha udhalimu – Afrika Kusini ya Makaburu, ili iwe rahisi kuutokomeza ubaguzi wa rangi. Nyerere akashinda, Makao Makuu ya harakati za kupigania uhuru barani yakawa Dar es Salaam.
  Ile dhana ya Nkrumah kwamba ukijikomboa kisiasa utakuwa pia umejikomboa kiuchumi haikufanya kazi, wala haijafanya kazi hadi leo. Afrika sasa yote ni huru, lakini hakuna hata nchi moja ya Kiafrika iliyo huru kiuchumi; zote ni masikini, zinazidi kuwa masikini kuliko hata kabla ya enzi za uhuru.
  Kati ya nchi 42 masikini sana duniani [LDCs], 28 zinatoka bara la Afrika ambazo zimebebeshwa na nchi tajiri deni la zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 40 ambalo halilipiki. Tanzania pekee ina deni linalozidi dola bilioni nane. Hali hii ya umasikini imezidi kuongezeka kutokana kwamba, viongozi wengi walioongoza harakati za kuleta uhuru hawakufanya hivyo kwa lengo kamili la kuondoa ukoloni na utegemezi; walichotaka ni kuchukua nafasi ya wakoloni na kubakia ndani ya mfumo wa kikoloni.
   
 2. sulphadoxine

  sulphadoxine JF-Expert Member

  #2
  Dec 2, 2011
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,264
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  Afrika inaundwa na nchi 53 zinazojiita mataifa huru. Bara hili limeingia karne ya 21 likiwa mhanga mwenye makovu wa ajali kuu mbili: Kwanza, ni biashara ya utumwa iliyojenga dhana kwa mataifa ya nje kwamba Mwafrika ni mtu wa kutumikishwa daima; hana utamaduni wala asili ya kutamani kwa kuwa utamaduni wa mdogo hauna mvuto kwa mkubwa. Pili, ni ukoloni mkongwe wenye kudhalilisha na kunyanyasa utu na ubinadamu.

  Historia imetuonyesha kwamba, Mkoloni sio tu hukalia na kupora nchi, bali hukalia na kupora kila kitu mpaka roho ya mtawaliwa. Na katika kujaribu kumfanya mtawaliwa huyo kuwa mali yake na mtumwa milele, humjeruhi na kumlemaza roho na mwili kwa kupotosha utamaduni wake, kiasi cha kuuteketeza kumfanya [mtawaliwa] ajione kama mtu asiye na asili wala historia. Ni Viongozi wachache mno wa harakati za mwanzo za huru walioingia uwanjani wakilielewa hili. Wengi hawakuelewa kuwa uhuru maana yake ni kufanya kazi na kujitegemea. Uhuru pia ni njia ya maisha huru ya watu katika juhudi za kuishi, na kuendelea kuishi kama taifa huru lenye mifumo yake huru kisiasa, mila na desturi, dini, mifumo ya imani na mfumo wa utoaji haki. Kwa baadhi ya watu wa nje, Afrika ni bara moja kubwa la wajinga wasiostaarabika, lisiloweza kuendelea wala kuendelezwa [bali kuporwa tu], lenye watu waliochanganyikiwa, wasio na uwezo wa kuweka mambo yao sawa isipokuwa kwa kusaidiwa na mataifa ya Ulaya.

  Chini ya mtizamo huu, Waafrika ni watu wanaotaka misaada kutoka nje daima – chakula, silaha za kivita kumalizana wao kwa wao, misaada ya fedha kuimarisha uchumi na Serikali zao zinazofilisika, vitega uchumi, utaalamu n.k., katikati ya utajiri wa rasilimali zinazosubiri kuvunwa na wageni, huku wananchi wake ni masikini wa kutupa. Wakati Mwafrika akiendeleza harakati za uhuru wa kisiasa, mkoloni aliyekuwa akiondoka alihakikisha anaweka na kuacha mfumo [wa siri] wa kiuchumi tegemezi kwa mtawaliwa usioweza kutikiswa na shamra shamra za uhuru na ngonjera za Umoja wa Afrika, na kwa sababu hiyo, uhuru [wa bendera] hautamsaidia wala kumwongezea Mwafrika chochote. Ndiyo maana, tangu uhuru Afrika imegubikwa na matatizo kibao: udikteta uliokithiri ambapo Viongozi waliovaa viatu vya wakoloni, wanaonekana wakatili kuliko wakoloni wenyewe; rushwa, vita vya wenyewe kwa wenyewe, ufisadi wa wazi wazi, uchumi usiojali, kufifia kwa uzalendo na maadili ya kitaifa. Yote haya yanaifanya Afrika kuwa bara la mabwege, lisiloweza kuzaa watakatifu, na kufanya Viongozi wote kuwa mashetani.
  Na kwa sababu Viongozi wetu wamepozwa kiroho na kimwili, wamejikana utu na uwezo wao mithili ya watumwa wa kale, hivyo Afrika imekosa ubunifu na kujiamini kiasi kwamba mipango yote ya uchumi na maendeleo sasa lazima ibuniwe, kushushwa na kuratibiwa kutoka nje, hata kama inaangamiza uhuru wetu.
   
Loading...