Kwa sifa hizi wanasiasa wetu wamestahili kupewa digrii za heshima? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kwa sifa hizi wanasiasa wetu wamestahili kupewa digrii za heshima?

Discussion in 'Jukwaa la Elimu (Education Forum)' started by AHAKU, Jan 5, 2011.

 1. A

  AHAKU Member

  #1
  Jan 5, 2011
  Joined: Jan 28, 2010
  Messages: 26
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Salamu wakubwa nimeinyaka taarifa hii kutoka mtandao wa gazeti la Mwananchi

  Monday, 03 January 2011 19:43


  Nani wanastahili kupewa shahada za heshima?

  Na Florence Majani
  AGOSTI mwaka jana, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Mayunga Nkunya alizungumza na waandishi wa habari na kutoa tahadhari ya kuwepo kwa vyuo vikuu visivyotambulika vinavyotoa shahada za heshima hususan kwa wanasiasa.

  Anasema aghlabu shahada hizo hutolewa kwa wahusika baada ya kutoa fedha kwa nia ya kujipa hadhi kwa wanajamii ili kutimiza malengo yao binafsi. “Hali hii pia inaongezeka kwa kasi nchini, na inashangaza kuona kwamba katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, watu maarufu wanatunukiwa digrii za aina hii kutoka katika taasisi ambazo kutambuliwa kwake kunatia shaka siyo Tanzania pekee bali hata katika nchi zilizomo taasisi hizo,” alinukuliwa akisema.
  Ukimtoa Profesa Mayunga, mjadala wa watu hasa viongozi wa siasa kutunukiwa shahada za heshima umekuwa ukiibuka mara kwa mara nchini.

  Mapema mwaka jana, mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Kainerugaba Msemakweli akafikia hatua ya kuchapisha kitabu kinachotaja majina ya wanasiasa aliowatuhumu kuwa na sifa feki za kisomi. Nini maana ya shahada ya heshima na nani anastahili kupata hadhi hiyo? Makala haya yanafafanua.

  Historia ya shahada za heshima
  Kumbukumbu za kimtandao zinaonyesha kuwa shahada ya heshima ya awali ilitolewa nchini Uingereza na Chuo Kikuu cha Oxford miaka ya 1470. Aliyetunukiwa alikuwa Lionel Woodville ambaye baadaye alikuwa Askofu wa Salisbury.
  Kwa Tanzania, shahada hizi zilianza kutolewa mwaka 1985, na mtu wa kwanza kupewa alikuwa mwalimu Julius Nyerere ambaye kumbukumbu zinamwonyesha kuwa aliwahi pia kutunukiwa shahada za aina hiyo zaidi ya 23 kutoka vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi.

  Nani anastahili Shahada ya Heshima?
  Kwa mujibu wa Naibu Makamu Mkuu (Taaluma) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Makenya Maboko, shahada ya heshima ni ile itolewayo kwa mtu mwenye vigezo stahiki na aliyetoa mchango mkubwa wa maarifa, elimu au ujuzi katika eneo fulani la kitaaluma.

  “Kwa kawaida shahada hizi hutolewa kama njia ya kuheshimu na kutambua michango ya watu hao katika maarifa, ujuzi au eneo la kitaaluma kwa mfano, afya, uchumi, mazingira, sayansi au fasihi,’’anafafanua.
  Nao mtandao wa Wikipedia unaielezea shahada hii ambayo aghlabu huwa ni ya digrii ya Udaktari ama Uzamili kuwa inatolewa kwa kujali mchango wa mhusika katika eneo la kitaaluma na jamii kwa jumla.
  Aidha, taarifa za mtandao huo zinaongeza kusema, mtunukiwa wa shahada hiyo hapasi kuwa na uhusiano wa awali na taasisi inayompa heshima hiyo.

  Mara nyingi mchakato wa kutoa shahada hii huambatana na sherehe ambayo mtunukiwa hutakiwa kutoa hotuba ambayo ni sehemu muhimu ya tukio hilo.

  Akifafanua taratibu za utoaji wa shahada hizo kwa mujibu wa chuo chake, Profesa Maboko anasema shahada hiyo hutolewa katika kipindi maalum kijulikanacho kwa jina la tathlitha (tranium). Hiki ni kipindi cha miaka mitatu ambacho muda wake huanza Julai.
  “Chuo kikuu cha Dar es Salaam hakitoi shahada za heshima zaidi ya tatu katika kipindi hicho cha miaka mitatu yaani tathlitha,” anasema na kuongeza kuwa mchakato wa kumpata mtunukiwa huanza kwa mjumbe wa baraza la chuo kupendekeza jina la mtu anayedhani anastahiki kwa kigezo cha awali cha mhusika kuwa na angalau shahada moja katika eneo la taaluma.

  “Baada ya jina hilo kupendekezwa, fomu iliyojazwa hupelekwa kwa makamu mkuu wa chuo ambaye huipeleka kwenye kamati ya wajumbe ambayo hujumuisha mwakilishi kutoka wizara ya elimu, makamu wa chuo anayeshughulikia taaluma, mtu mwenye taaluma kama ya aliyependekezwa pamoja na wengine” anasema.
  Anasema, baada ya kamati hiyo kufanya majadiliano ya kina, kura za siri hupigwa huku na matokeo kupelekwa kwa mkuu wa chuo ambaye huwa na maamuzi ya mwisho.

  Ili kuilinda hadhi ya shahada hiyo nyeti, Maboko anasema chuo hicho hutoa shahada hizo mara chache na mara ya mwisho watu watatu walitunukiwa nao ni Rais mstaafu Benjamini William Mkapa na Juma Mwapachu ambao walipewa shahada katika fani ya Fasihi na Profesa Jorgen Sen wa Denmark aliyepata heshima katika sayansi
  Anaongeza kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianza kutoa shahada hizo tangu miaka ya 1980.Baadhi ya watunukiwa ni pamoja na Mwalimu Julius Nyerere aliyetunukiwa Shahada ya Heshima ya Diplomasia mwaka 1985. Mwingine ni Profesa Godfred Vogel aliyetunukiwa shahada hiyo upande wa sayansi mwaka 1997.

  Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Profesa Tolly Mbwete anasema chuo chake huanza na pendekezo kutoka kwa mwanafunzi ama mhadhiri.

  “…..anayependekeza ni lazima aainishe ni kwa sababu gani amempendekeza mtu huyo. Baada ya hapo pendekezo hilo huwasilishwa kwa Makamu Mkuu wa chuo na kisha kupelekwa katika baraza kwa majadiliano kabla ya kupigiwa kura za siri,” anaeleza.
  Akitaja sifa za anayestahili kupewa heshima hiyo kwa mujibu wa chuo chake, Profesa Mbwete anasema: “Mtu anayependekezwa kupewa shahada katika chuo chetu ni yule aliyetoa mchango mkubwa kwa umma au kwa taifa na sio lazima mchango katika taaluma bali ni kazi ya ziada yenye manufaa kwa umma nje ya wajibu wake wa kazi.”

  Kwa mujibu wa kumbukumbu za chuo hicho, baadhi ya watu maarufu waliotunukiwa shahada za heshima za chuo hicho ni pamoja na Mwalimu Julius Nyerere, Nelson Mandela, Benjamini Mkapa na Jane Godel.

  Hizi ndizo sifa za nani anapaswa kupewa shahada ya heshima. Hata hivyo, watu wengi katika duru kadhaa za mijadala wanahoji kwa nini shahada hizo sasa zimekuwa zikitolewa kama njugu hasa kwa wanasiasa nchini, na je wanaopewa ni kweli wanastahili?
  Upo wasiwasi kuwa huenda siasa au kujikomba vinatumika kama vigezo vya utoaji shahada hizo. Kwa upande mwingine jamii inaaswa kuwa makini na vinavyoitwa viwanda vya kutengeneza digrii ambavyo nia yao kuu ni kujipatia fedha na umaarufu
   
Loading...