Kamanda Asiyechoka
JF-Expert Member
- Sep 13, 2020
- 3,165
- 4,581
View attachment 2036704
Wanabodi,
Hili ni bandiko lililotokana na makala yangu hii, kwenye Safu yangu ya "Kwa Maslahi ya Taifa", kwenye gazeti la Nipashe kila siku za Jumapili. Kila nipatapo muda, huja na hizi makala zangu za "Kwa Maslahi ya Taifa" ambazo huja kwa mtindo wa swali, halafu jibu utatoa wewe msomaji mwenyewe.
Makala ya leo, ni makala ya pongezi kwa Rais Samia, kwa “nonsense” ya sukari, Rais Samia, anastahili pongezi za dhati, swali ni jee tuishie kwenye nonsense ya sukari tuu, au tuangazie na nonsense nyingine zote tuziache tusonge mbele? .
Naomba kuanza mada yangu ya leo, kwa kufundisha lugha kidogo, neno “nonsense” ni neno la kizungu lenye kumaanisha “ujinga”, hivyo uamuzi wowote unaiotwa “nonsense” ni “uamuzi wa kijinga”, Baba wa Taifa, alilitumia sana neno hili “nonsense”, ila yeye Baba wa Taifa, haikuishia tuu kwenye kulaumu maamuzi ya kijinga, “nonsense”, bali pia aliwaita watoa maamuzi hayo “wajinga”, ninanayo mifano mingi ya Mwalimu Nyerere kutumia neno “nonsense”
Mfano mzuri kabisa ni wakati Mwalimu Nyerere anaaga na kungatuka kwenye urais, alikiri serikali yake imefanya makosa mengi tuu , akakiri kuna baadhi ya maamuzi yalikuwa ni “nonsense”, makosa, lakini pia akasema “kufanya kosa sii kosa, kosa kurudia kosa”.
Wakati tukijiandaa kwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, ile 1995, Mwalimu alizungumza na sisi waandishi wa habari, kwenye ukumbi wa Hoteli ya Kilimanjaro, na mimi nilikuwepo, akizungungumzia ubinafsishaji wa benki ya NBC, Mwalimu akaishangaa serikali kukubali masherti ya nchi mabeberu, kuwa NBC ni li benki likubwa sana, lenye nguvu sana, lazima livunjwe, ndipo turuhusu ushindani wa mabenki, Mwalimu akauli NBC ina ukubwa gani?, “a mere NBC?!, this is “nonsense”.
Hata hapa, kwenye video hii
kwa hisani ya Dada yangu, Maria Sarungi, Baba wa Taifa alitumia neno nonsense.
Mtu kuambiwa mjinga, ni kweli umetukanwa lakini ujinga sio tusi, ni kutojua tuu, mtu mjinga akiisha elimishwa, ujinga unamtoka, anakuwa mwerevu. Mtu mjinga akiisha elimishwa, ujinga usipomtoka, huyo sasa sio mjinga, huyo ni mpumbavu!.
Rais Mkapa wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, aliwaita watu fulani “malofa na wapumbavu”,
na haikuwa habari kubwa.
Rais Magufuli, aliwahi kumuita mawaziri fulani “mpumbavu” na haikuwa habari kubwa.
Juzi kati katika ziara za Rais Yoweri Museveni nchini Tanzania, katika kuzungumzia hoja ya sukari, Rais Samia pia alitumia neno “nonsense”.
Baada ya kutumika kwa neno hilo, huku kwenye mitandao ya kijamii kukalipuka “Rais Samia Katukana”, aliyetoa msimamo kuwa Tanzania hatutanunua sukari ya Uganda ni Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda. Baadhi ya mitandao ya kijamii ikamchagiza Prof. Mkenda kuwa asikubali kutukanwa hadharani, bora ajiuzulu kutunza heshima yake na asipojiuzulu atatumbuliwa!.
Sio mara moja nimeongea katika makala zangu, kuwa media ya Tanzania, hatuna watu wazuri wa kufanya uchambuzi wa habari, “news analysis”, Rais Samia alipotumia neno “Nonsense”, hakumtukana Waziri Prof. Mkenda ni “nonsense”, ameishangaa uamuzi ule wa kugomea sukari ya Uganda kwa kisingizio cha kulinda viwanda vya ndani, hivyo lile neno “nonsense” ni neno kwa ajili ya uamuzi ule na sio kwa ajili ya kumlenga mtu Prof. Mkenda.
Naomba tukubaliane, kama neno “nonsense” ni kwa uamuzi ule wa kugomea kuagiza sukari kutoka nchini Uganda, au auamuzi wa kugomea kuagiza bidhaa zozote kwa nia njema na lengo zuri la kulinda viwanda vya ndani, uamuzi kuhusu sukuri, haukutolewa na Waziri Prof. Mkenda kusema ni uamuzi wake binafsi, pia nilimsikia Waziri Mkuu, Majaliwa Kassin Majaliwa akiuzungumza. Huu ni uamuzi wa Baraza la Mawaziri lililopita, hivyo kauli ya rais Samia haimlengi mtu, inalenga uamuzi wa kugomea kuagiza sukari ya jirani Uganda.
Sasa twende kwenye ukweli wenyewe wa alichokisema Rais Samia uamuzi ule kweli ni “nonsense”. Hii maana yake ni kile niliwahi kukisema katika makala zangu za nyuma, kuwa viongozi wetu sio malaika, ni binaadamu, hivyo wanaweza kabisa kufanya makosa na kutoa muuamuzi “nonsense”, kama bazara la mawaziri limeweza kupitisha uamuzi kama huo, hili la sukari ni uthibitisho tuu wa uwezokano seriali yetu kufanya maamuzi “nonsense”.
Tena nonsense kubwa kuliko ya sukari, sio kwa serikali yetu kugomea kuingiza nchini sukari ya jirani zetu wa Uganda, serikali yetu iligomea kuingiza Tanzania Bara sukari kutoka Zanzibar!. Wakati huku bara tuna uhaba wa sukari, sukari ilipanda bei kutoka shilingi 1,800 kwa kilo, hadi shilingi 2,500 kwa kilo. Kule Zanzibar bei ilibaki 1,500 hadi 2,000.
Kiwanda cha sukari Zanzibar, kilikuwa na sukari ya kutosheleza kabisa kumaliza upungufu wa sukari huku bara, hivyo kikaomba kuleta sukari yake Bara kukabili upungufu, haswa kwa kuzingatia bei ya huku Bara imechangamka kuliko bei ya Zanzibar, ilikataliwa.
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Zanzibar, Amina Salum Ali, akavuka bahari, kuja bara kusemezana na waziri mwenzake…lakini wapi, alikataliwa!. Waziri Amina Salum Ali akaigeukia taasisi ya TradeMark East Afrika inayoshughulika na kuondoa vikwazo vya kibiashara visivyo vywa kikodi (non tariff barriers), na kukiripoti hicho kikwazo cha sukari.
Yaani Tanzania bara inakabiliwa na uhababa wa sukari, Zanzibar inayo sukari ya ziada bwelele, Zanzibar inakataliwa kuingiza sukari yake bara, na badala yake, wenye viwanda ndio wanaoruhusiwa kuagiza sukari ya bei chee kutoka ng’ambo, kufidia huo upungufu!, kwa uamuzi kama huu, ni neno gani zuri zaidi ya kulitumia zaidi ya neno “nonsense?”.
Nampungeza sana rais Samia kwa kukemea na kukomesha hii nonsense ya kwenye sukari, na sasa nitoe wito kwa rais wetu Mama Samia, hizi nonsense za kwenye sukari, zisiishie tuu kwenye sukari, tende na kwenye nonsense nyingine zote za uondoshaji wa vikwazo vya uingizaji nchini bidhaa muhimu ambza viwanda vya ndani vimeshindwa kutosheleza mahitaji ya bidhaa hizo.
Kwa sasa taifa linakabiliwa na upungufu wa sementi, mfuko wa sementi ya Tanzania kwa mikoa ya pembezoni, kama Arusha, na Moshi, imefikia bei ya shilingi 24,000 kwa mfuko. Sementi ya Kenya ni shilingi 12,000 kwa mfuko mpaka inafika dukani Tanzania. Watu wanahitaji sementi haipo, hapo kwa jirani yetu sementi bwelele, bei chee, lakini hairuhusiwi kuingia Tanzania, kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani. Hii pia ni nonsense!. Hivyo baada yah ii nonsense ya sukari, twende kwenye nonse nyingine zote za vikwazo vya uingizaji bidhaa.
Angalizo: Kuunga mkono huu msimamo wa rais Samia kuondoa nonsense ya sukari, na kutaka nonsense nyingine zote ziondoshwe, namaanisha kufungua milango ya soko huria kwa zile bidhaa tuu za muhimu ambazo viwanda vyetu vya ndani, vimeshindwa kuzalisha kukidhi mahitaji ya kutosheleza soko la ndani, na sio soko holela. Viwanda vya ndani vikifanikiwa kuzalisha kutosheleza soko, tuendelee kuvilinda, hata kama ulizi huo utatuumiza sisi wananchi kulazimika kununua bidhaa zate zinazozalishwa nchini kwa bei kubwa, ndioko kujenga nchi kwenyewe na sio kukimbilia cheap imports kwasababu tuu ni cheap!.
Wasalaam.
Paskali.
Mtoa mada huna akili.