Kwa nini usomi wetu ugeuke kuwa laana kwa Watanzania?


L

lugamba2001

Member
Joined
Aug 18, 2009
Messages
12
Likes
0
Points
0
L

lugamba2001

Member
Joined Aug 18, 2009
12 0 0Ukifanikiwa kuongea na wanafunzi wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne au hata cha kidato cha sita, wengi wao kama si wote, wana ndoto za kuendelea kusoma, hadi vyuo vikuu na ikiwezekana nje ya nchi. Hili la kujivunia kama nchi, ni swala linalotufananisha na wengine wote waishio ulimwenguni hapa, wanaohangaika usiku na mchana kuyaboresha maisha yao.

Kutokana na maendeleo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi katika nchi nyingi, elimu imeoneka ndiyo chanzo cha maisha bora na mafanikio. Ingawa uhalisia wake unaweza kuthibitika kuwa tofauti toka mtu hadi mtu au nchi moja hadi nyingine. Linalonisumbua mimi, labda na baadhi ya watu wenye akili ya kwaida, ni matokeo ya elimu hiyo. Kwamba, mchango wa elimu hiyo kwa maendeleo ya nchi yetu, ndiyo huo tulioutarajia? Wengi wanavyozidi kusoma zaidi na zaidi, vivyo hivyo nchi inazidi kugubikwa na ujinga na utumwa wa kifikra. Ina tofauti gani na ‘mkorogo’ unaopakwa na dada zetu wakawa wazungu angalau usoni, wakati mwili wote ukibakia wa kiafrika. Je, si chanzo cha taabu na laana kwa Watanzania? Walioikosa wakinyanyapaliwa na walioipata, wakieendelea kuwa watumwa wa elimu yenyewe au wa kule waliokoipata. Tuijadili hoja.

Baada ya madarasa, na kusafiri sana, katika nchi mbalimbali, mtu aliyetegemewa kuwa mkombozi wa wale wasiofika alikofika, wakayajua anayoyajua yeye. Akitegemewa kuja na hoja za kuikomboa jamii, kama tulivyokuwa tukiambiwa zamani kuwa elimu ni mwanga, na ni silaha, badala yake sasa elimu ni giza totoro. Siyo silaha ya ukombozi tena, bali ya ukandamizaji. Ndugu, jirani na wajuani wake wanageuka kuwa wahanga wa kwanza wa elimu ya mjoli wao.

Kama wao, msomi wetu naye hazijui tena shida zetu, kwa kuwa kule alikotoka au vilipoandikwa vitabu alivyosoma kuna internet, magari ya kisasa, treni za umeme na madege makubwa makubwa, basi hata sisi shinda zetu ni hizohizo! Jamani, jongoo aulizwaje rangi wakati hana macho? Si umpe macho kwanza? nitakuwaje na shinda ya internet, wakati huo umeme wenyewe siuju? Ya nini mimi hiyo mitandao? Tukiangalia mifano hai, ukweli uko wazi, ukitaka utakubali au wala sikulazimishi ukikataa. Niweke wazi kabla ya mjadala, mimi si mwanasiasa, nazungumzia hoja wala si watu.

Ukitafakari mwelekeo ya nchi yetu, hasa baada ya kustawi kwa yule dhalimu aitwaye ‘globalization’ au utandawazi kama si wizi. Wasomi wetu, wanajifikiria au kufikiria kuwa na wao wamebadilika, na kwa maana hiyo hawawezi tena kufikiria huko walikozaliwa, au vilipozikwa vitovu vyao, huzifikiria Ulaya na Asia. Kwa kujua au kutojua, wanafikiria kwa niaba ya wale matajiri wezi, au wamejiruhusu wenye elimu yao wafikirie kwa niaba yao. Ubaya wa bahati yetu ni imani kubwa tuliyowapa wasomi wetu hawa.
Hushangai kumkuta msomi akitetea kwa nguvu zote, ndugu zake wafukiwe aridhini au wakafie baharini huko, ili Asia na Ulaya au America wakapatiwe ajira. Ati ulimwengu wa sasa ni mitandao bwana! Haioni kabisa nafasi ya kuishi bila internet wakati ameishaitumia au hata kaisoma kwenye vitabu! kumbe kabla hajaiona aliishije.

Ni rahisi tu kuona, ni kama hivi: ‘Lazima tuweke mfumo wa kisassa wa mabilioni, ili kwa huo, watu waombe udahili katika vyuo vikuu’. Maskini! Ni wangapi kati ya hawa wanaoomba kudahiliwa kupitia huo mtandao wanajua kuutumia? Wamejulia wapi? Kwa taarifa tu, kuna shule zisizozidi 50 kati ya shule zaidi ya 1300 katika Tanzania, zinafundisha computer. Hata hizo, zinazofundisha si za wale wanaohitaji sana hiyo huduma kwani, wengi wao utawakuta vyuo vikuu vya nje baada ya hapo!

Sina nia kubeza jitihada hizo tukufu, za waheshimiwa wala kuwadhalilisha Watanzania, kwamba hawajui kutumia mtandao, lakini ukweli unabaki palepale. Mradi huo, hauna mwonjo wa kuendeleza taifa ni mradi wa kutoa ajira kwa walio ubuni mfumo huo ambao bila shaka ni walewale. Si watakuja kuukarabati ukiharibika, kuuboresha ukichakaa na mambo mengine yanayofanana na hayo? Kwa nini kisingewekwa kipambele kuhakikisha kwamba, angalau kila anaye maliza kidato cha sita anajua kutumia computer kama kweli wazo letu ni teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa taifa? Unafikiria pesa hizo zingenunua computer ngapi za kawaida kwa ajili ya shule zetu? Shida kubwa ni kuwa hatuifikirii nchi yetu! Kwa nini kuwekeza mabilioni hayo ya wakata mkaa wa kule kijijini Simbo kuwapa ulaji Wamarekani au Wazungu wasio na shida hiyo?

Ni kweli leo kazi hiyo haiwezekani tena kwa njia ya kawaida? Ni ‘mkorogo’ tu huo! Tutang’aa usoni, mwili utabakia mweusi tu! Sijapata kuamini hata siku moja kuwa kuna maendeleo katika taifa lisilo na vipaumpele. Na pale unapotumia mabilioni ya walima mahindi wa kule Msagali kujenga jumba la mabilioni ili mtu mmoja akae, ili tu afanane na wenzie wa huko alikosoma au kutembelea. Je ndiyo vipaumbele vya hao wenye mali? Ninaogopa kufikiria, itakuwaje, wanaozaliwa na kukulia kwenye huo ukwasi wa kimagharibi watakaposhika hizo ofisi, kama wazazi wao waliozaliwa vijijini, hawakufikirii tena, wale wafikao vijijini, kama ‘study tour’ je? si watatugeuza nyani kabisa ili watalii waje kututazama?

Yapo mengi katika vyuo vikuu vya kwetu, nikiyaona napata mtikisiko wa akili. Chuo kinawekeza kwenye teknolojia ya ‘smart card’, ni kwa ajili ya kujifunza au utafiti? Kama jibu ni ndiyo nitawaunga mkono,vinginevyo huo ni ‘mkorogo’ tu! Na kwa nini wavuti (website) za vyuo vyetu zisiwe ‘Demo’ tu, Ni watanzania wangapi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo au waliovyuoni wanaotumia internet kila siku? Au tuwekeze sana kwenye Website na mitandao ili tukasifiwe huko Ulaya? Kwa nini kipaumbele kisiwe kuineza hiyo tekinolojia kwanza. Nilitarajia msomi afikirie mbali zaidi ya kutumia tu kazi ya mwenzie.

Kwamba watu, wanawekeza kununua magari ya kifahari (Shangingi), kwa nini usitembelee hata punda ikiwezekana ili ujenge barabara kwanza? Kwa nini uwafikirie Wajapani na viwanda vyao kama kwamba wanakutegemea wewe ndiyo waishi? Hakika kuna tatizo! viwekwe kwanza vipaumbele kwenye mambo ya msingi yatakayo fanya uchumi wetu ikaimarika, kama vile barabara, kilimo, elimu, afya na nishati hayo mengine yatafuata tu. kama vile ambavyo mtu hatafuti majani wakati wa masika ndivyo ilivyo starehe katika nchi yenye misingi bora ya kiuchumi.

Ukiwasikiliza walio nje ni kizunguzungu kitupu, wanalaumu na kulaani Tanzania!!, Wanajisemea, ukifika uwanja wa ndege bongo, mahotelini, aah, bandari! ni wizi mtupu! Hata walio na mamlaka ya kufanya kitu nao kwa kuwa wamefika Ulaya na Marekani wanalaani tu. Wala hauoni chochote kinacho onyesha kuwa, kweli hali ile inawakera. Ukifatilia kwa makini utagundua la kukushtusha, wizi na uzembe huo unaouona au kuusikia kwenye vyombo vya habari ni michezo ya kitoto tu, ni kuigiza kile kinachofanywa wa wazazi! Hao ndiyo wasomi wetu, wala hawapati taabu kusema huku wakijua kuwa ni uwongo! Je ndiyo mwanga huo? mbona mwajifunza uovu zaidi? Mbona hao wenzenu hawatendi hayo kwao?

Mtu akienda nje mara tatu, anaongeza ujinga mara tatu na akiisha kukaa huko ndiyo hafai kabisa! Afadhari uongee na mwanakijiji ana wazo la kujenga nchi, kuliko huyo aliyepata kukaa marekani au Ulaya. Anawafikiria Wamarekani tu, hatufikirii tena tunaoishi katika vijiji vya Nondwa Dodoma, Nyarubanda kule Kigoma wala Londo kule Lindi. Tuseme basi, anafikiria Kimarekani, lakini mbona wao wanaziendeleza nchi zao?

Napendekeza mojawapo ya vigezo vya mtu kuwa Rais wa nchi, asiwe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje au Kufanya kazi nje hasa Ulaya, Marekani au Asia. Maana yeye ataka, Dar ikeuka mara moja kuwa Washington na Manzese igeke siku moja kuwa Manhattan, badala kuangalia misingi ya kiuchumi yeye anangalia, kule nje wana hiki na kile basi watuletee tu, hatuna sababu ya kuhangaika kujua jinsi ya kujenga ‘flyover’ wakati pale Washington lipo au wewe haujaliona nini? Tutahangaikia marubani? wakati pale China wamejaa? Au walimu vyuoni wakati ‘graduate’ kibao kule India? “They have 300 Univerisities!” waweza fikiria wao waliamka tu wakakuta vimejaa! Nani aliyeturoga Watanzania?
.
Dawa ya jipu ni kulipasua, tena bila ganzi! 
patriot1

patriot1

Member
Joined
Nov 3, 2009
Messages
14
Likes
18
Points
5
patriot1

patriot1

Member
Joined Nov 3, 2009
14 18 5
shida kubwa twapenda kuiga iga sana,madhara yake ni hadi kiama kama hatutabadilika.Ni wataalam wa kudurufu kila kitachopendeza machoni petu.
 
L

lugamba2001

Member
Joined
Aug 18, 2009
Messages
12
Likes
0
Points
0
L

lugamba2001

Member
Joined Aug 18, 2009
12 0 0
kwa hakika yapo mengi ayafanyayo, mwandamu lakini, kuiga kuna madhara makubwa zaidi! Mara zote tuwahusisha wasanii na mambo ya kuiga, lakini ukweli twawaonea tu, uigaji mbaya zaidi ni ule wa kukopi kitu cha kitaaluma na kuhamisha kitu kama kilivyo bila kujali mazingira na wakati!
 

Forum statistics

Threads 1,236,789
Members 475,220
Posts 29,268,246