kwa nini Rais kikwete asitumie HEKIMA kama hii ya Mwl. Nyerere

The Seeker

New Member
May 10, 2010
4
0
Oktoba 1966 kundi la wanafunzi kama 400, wengi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, waliandamana hadi Ikulu kwenda kupinga sera mpya ya kuwataka kwenda kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa wakiwa bado chuoni na wakiwa huko watalipwa asilimia 40 ya mshahara ambao wangelipwa kama wangekuwa tayari wamehitimu na wako uraiani.
Baadhi yao wapo kwenye serikali leo hii na wengine wameshika nafasi za juu nchini (sitawaja kwa sasa). Walienda Ikulu wakiwa na lengo la kumlalamikia Makamu wa Rais, Mzee Kawawa ambaye ndiye alikuwa anasimamia JKT; tena wakiwa na mabango ambayo mojawapo lilitoa tusi la wazi kwa serikali kuwa “maisha chini ya ukoloni yalikuwa ni bora”.
Walipofika Ikulu walipokewa siyo na Kawawa tu; bali na Mwalimu Nyerere mwenyewe na viongozi wengine na bila kutumia nguvu ya polisi au jeshi akawaacha watoe ujumbe wao na kuusoma mbele yake. Aliwasikiliza na kuzipima hoja zao.
Wanafunzi wale walimaliza kwa mbwembwe; huku wakishangiliwa wakisema kuwa “mheshimiwa hadi pale madai yetu yatakapotekelezwa na mtazamo wa viongozi wetu dhidi ya wanafunzi utakapobadilika, hatukubali Jeshi la Kujenga Taifa mioyoni mwetu. Miili yetu itakwenda lakini roho zetu zitakuwa nje” na kama vile kutia chumvi kidonda wakatangaza; “mapambano kati ya wanasiasa na wasomi yataendelea, asante”.
Nyerere alikuwa na uwezo wa kuyakataa madai yao na kuwatimua; alikuwa na uwezo wa kuruhusu vikosi vya usalama kuwatia ndani mara moja; lakini hakufanya hivyo. Aliamua kwanza kuwajibu kwa hoja katika mojawapo ya hotuba zake ambazo huwezi kuzipata mahali popote (wachache nadhani tunayo).
Sitaingia ndani ya hiyo hotuba, lakini aliweza kuonyesha kwa nini madai yao hayana msingi na ni madai makubwa, na kuwa yanatokana na imani kuwa wafanyakazi wa wakati ule serikalini walikuwa wanalipwa kiasi kikubwa sana.
Matokeo yake ni kuwa Nyerere pale pale alitangaza kukata mshahara wake kwa asilimia 20 na kukata mishahara ya watumishi wote serikalini! Hakuhitaji kutumia jeshi au polisi kutuma ujumbe huo!
Kikwete angeweza kabisa kuonyesha kuwa anajali maslahi ya wafanyakazi kwa kukata mshahara wake, wa mawaziri na kuhakikisha kuwa mishahara yote ya ngazi za juu inapunguzwa ili kuona ni kiasi gani kingeweza kupatikana, na kiasi hicho kingetumiwa kuongeza kima cha chini.
Nina uhakika kabisa kuwa endapo serikali ingeamua kukata mishahara ya juu na marupurupu kwa asilimia 15 tu, kima cha chini kingeweza kuwa zaidi ya 315,000; lakini tunaambiwa haiwezekani, serikali haina fedha!
Sasa hana hoja. Hakuwa na uwezo wa kujibu hoja hizo za wafanyakazi. Alichobakiwa nacho ni vitisho. Kama nilivyosema wiki iliyopoita, vitisho peke yake havitatui matatizo.
Bado tunapoteza fedha nyingi katika manunuzi ya umma, bado tunalipa watumishi hewa, bado tuna watu wengi katika ajira ya umma ambao wengine kwa kweli wangeweza kabisa kubadilishwa nafasi zao au kupunguzwa.
Serikali ya CCM haina mpango wa kubana matumizi. Kwa miaka sasa imezidi kuwa kubwa zaidi ikitumia fedha nyingi zaidi. Na bahati mbaya sana bado hatujaona chama chenye sera ya kubana matumizi na kupunguza ukubwa wa serikali.
Na kwa kadri ninavyoona, kama Watanzania watairudisha tena serikali hii madarakani ni wazi kuwa haiwezi kupungua tena; CCM inahitaji serikali kubwa!
Tunahitaji chama chenye sera na itikadi tofauti ya CCM; Chama ambacho kina lengo kweli la kumpigania mfanyakazi na mkulima wa Tanzania; chama ambacho hakitaogopa kupunguza mishahara ya juu ya watendaji na hakitasita kubana matumizi ili kuleta ubora na tija ya kweli huku kikiinua mishahara ya chini.
Ni lazima tuwe na chama ambacho kitakuwa na lengo la kuwainua Watanzania wote na kuhakikisha kuwa wafanyakazi wa Tanzania hawalazimiki kuishi kiujanjaujanja ili mradi maisha yaende mbali. CCM siyo chama hicho; CCM kimekuwa ni chama cha kutetea waajiri na mabepari mamboleo.
Kama kuna mwana CCM anafikiria CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi, mtu huyo itabidi apepewe!
Lakini kwa kadri tunavyoendelea, ni lazima tutarajie kile kisichoepukika. Mgongano kati ya wafanyakazi na mabepari utakuwepo, na ni lazima utokee; kwani hiyo ndiyo asili ya ubepari duniani pote. Mgongano kati ya vyama vya wafanyakazi na serikali ya CCM utatokea tena kama ulivyotokea 1994!
Ni mgongano wa lazima; kwani ni kutokana hapo ndipo fikra mpya za mabadiliko zitazaliwa. Mgongano huo hauhitaji baraka ya vikao vya CCM.
Ni muhimu serikali ikumbuke kuwa kwa kuchagua vitisho, imeonyesha kuwa imeishiwa hoja; kwa kutumua nguvu itajikuta inalazimisha vurugu yenyewe. Wakati umefika kwa Kikwete kuwaomba radhi Watanzania kwa uchaguzi wake wa maneno, na hasa kwa kuhutubia akiwa amezungukwa na wakuu wa vyombo vya usalama jambo ambalo hajawahi kulifanya huko nyuma isipokuwa kama alikuwa na kusudio la kutuma ujumbe.
Lakini zaidi, vyombo vyetu vya usalama visiingizwe katika malumbano ya kisiasa. Kikwete akitaka kuzungumza kwa ukali azungumze apendavyo, lakini asifanye hivyo kwa kulazimisha wakuu wa vyombo vya usalama kuwa wamemzunguka.
Vyombo vya usalama viachwe vifanye kazi yake, na ni matumaini yangu wakuu wetu wa vyombo vya usalama hawatakubali kuingizwa katika hotuba za kisiasa; kwani kwa kufanya hivyo wataonekana wameshachagua upande na watakuwa tayari kulazimisha maamuzi mabovu ya serikali katika vinywa na migongo ya wafanyakazi wa Watanzania.
 
hiyo hekima haipate wapi???Prezidaa wetu hana hekima jamani kumfananisha na Mwl.Nyerere ni kama kulinganisha mrija wa mbu na mkonge wa Tembo
 
Ubinafsi umetawala sana nchini. Viongozi wa CCM na Serikali yake ndio wanaoongoza kwa ubinafsi na kwa ubinafsi wao ndio maana wanatuambia kwamba CCM itatawala milele wakiamini kwamba wao tu ndio wanaoweza kutawala na si watu wengine.

Ninaamini kabisa kwamba CCJ kitakuwa chama cha ukombozi na tumaini litakalorejea iwapo viongozi na wananchama watarajiwa wa CCJ watakuwa makini na kuanza kukanyaga nyayo za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye aliiongoza nchi kwa mapenzi makubwa kwa wananchi aliokuwa akiwaongoza na Taifa kwa ujumla. Tukumbuke jinsi ambavyo aliweza kuwakumbuka "Watanzania wake" hata pale alipoelewa kwamba sasa muda wake wa kuishi duniani umekwisha. Ni kiongozi gani wa CCM ambaye anaweza akakumbuka dhiki na shida za Watanzania wengine hata anapokuwa kwenye death bed?
 
Back
Top Bottom