Kwa nini mchezo wa soka ni mzuri kwa watoto | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kwa nini mchezo wa soka ni mzuri kwa watoto

Discussion in 'Sports' started by kilimasera, Apr 9, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Apr 9, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  DUNIANI kuna michezo mingi inayopendwa kuchezwa na watoto ikiwa kama sehemu yao ya kujiburudisha, kujifurahisha na kutengeneza undugu na urafiki wa dhati baina yao.

  Tanzania mchezo unaopendwa zaidi na watoto ni soka kwani ukipita kwenye mitaa nyakati za jioni au siku za likizo na mwishoni mwa wiki si ajabu kuwaona watoto wadogo wakicheza soka kwenye barabara za mitaani, kwenye viwanja vyao vidogo au pembeni mwa viwanja vya soka.

  Hali hiyo inaonyesha watoto wanapenda mchezo wa soka ingawa hawana sehemu maalum walizopangiwa kwa ajili ya kucheza mchezo huo, pia inaonyesha soka ni mchezo mzuri kwa watoto.

  Watoto wengi utawakuta wakicheza mchezo wa soka wenyewe bila ya kulazimishwa na wakiwa hawana vifaa maalum vya kucheza mchezo wa soka, ila wao wakiwa na mpira soka linaanza.

  Mchezo wa soka pia ni maarufu sana kwa watoto kwa sababu ni mchezo rahisi kujifunza na mchezo ambao unafurahisha na huwasaidia sana kiafya.

  Kutokana na mendeleo ya teknolojia hivi sasa watoto wengi hasa wale wanaotoka katika familia zenye uwezo wanaathiriwa na kuangalia sana televisheni na kucheza video games hivyo kuwa na wakati mgumu kiafya na kuwa imara kwa sababu hawafanyi michezo inayochangansha mwili.

  Pia aina za vyakula, maisha ya watoto kukaakaa na wazazi kutojihusisha na watoto wao kwa karibu ili kuwahamasisha kufanya michezo kunasababisha watoto wengi kunenepa ovyo na wengine kuota vitambi.

  Tatizo la watoto kunenepa ovyo aliwaathiri watoto hao utotoni tu, ila huwaathiri hata wanapokuwa wakubwa na kuwapa matatizo ya ugonjwa wa moyo, kisukari na maradhi mengine yanayotokana na unene wa ovyo.

  Suala hapa la kuzingatia ni wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata chakula sahihi na kuwatoa watoto wao wanaoshinda kwenye makochi kuangalia televisheni au kucheza video games na kuwaruhusu wakacheze michezo mbalimbali ukiwepo mchezo wa soka.

  Ninasema wakacheze mchezo wa soka kwa sababu ni mchezo ambao ni rahisi kucheza na unawafanya watoto waweze kukimbia na kuruka ruka hali ambayo itawawezesha watoto kuwa na afya nzuri na kupata hamu ya kula chakula.

  Pia, ninasema watoto wakacheze soka kwa sababu kama umewahi kufundishwa mchezo wa soka utagundua kwamba mchezo wa soka unachezwa kitimu na unahitaji ujuzi ambapo mambo hayo mawili yaani timu na ujuzi hukusaidia katika maisha ya baadaye kufahamu kufanya kazi kitimu na kuzingatia ujuzi.

  Vile vile mtoto akicheza mchezo wa soka atajifunza namna ya kuwasiliana na wenzake kwa heshima na kujibu kwa heshima kwa sababu wao kama timu inabidi wafanye kazi pamoja.

  Mtoto akicheza soka pia atajifunza kushirikiana kwa sababu wanatakiwa kuwa kitu kimoja ili kufanikisha lengo lao la kupata ushindi.

  Mambo hayo yote humuwezesha mtoto kukua vizuri na kuwa na marafiki wa aina mbalimbali, kujifunza tamaduni tofauti, imani tofauti na uelewa tofauti hivyo akipata na ushauri mzuri wa wazazi na elimu nzuri ya darasani hujitambua na kuitambua dunia vizuri.

  Ninasema mchezo wa soka kwa watoto ni mzuri pia kwa watoto wale wenye aibu shuleni kwa sababu wakicheza soka na wenzao watakuwa wamejichanganya na watoto tofauti ambao watawachangamsha katika mazingira yaliyo salama na yaliyo ya kiafya.

  Mtoto kuishi akiwa na afya bora na kuwa na marafiki ni vizuri, lakini ikumbukwe pia mchezo wa soka ni furaha, ni kujifurahisha ni burudani.

  Mchezo wa soka hujenga hali ya kujiamini ambapo kama mtoto ataanza kucheza soka akiwa mtoto anakua na hali hiyo na anapokuwa mkubwa hujiamini zaidi na kuweza kufanya maamuzi makubwa bila kuyumbishwa.

  Zaidi ya hapo mchezo wa soka huusisha akili na mwili, kwa hiyo mtoto anayekua huku akicheza soka huusisha akili na mwili kwa kiwango cha juu kuliko mtoto aliyekaa kwenye kochi akiangalia televisheni au kucheza video games.

  Ndiyo maana ninaona kuliko kumuacha mtoto wako akae kwenye kochi hapo sebuleni kwako na kucheza michezo ya kupigana au vurugu kwenye video games, au mtoto wako kutazama sana televisheni au kumnunulia madoli mengi, ni bora kama amemaliza kujisomea aende kucheza na wenzake mtaani au kwenye viwanja vya michezo ili aweze kujenga afya yake ya mwili, afya ya akili na uwezo wa kujiamini.

  Sisemi sifurahii teknolojia mbalimbali zinazogunduliwa duniani ambazo zinatusaidia kurahisisha kazi zetu au zile za kufurahia zaidi zikiwemo video games na televisheni, ila ninaona kutokana na teknolojia hizi tumekuwa tukikakaa tu na kuwafanya watoto wetu wakaekae tu na wawe hawana afya bora, pia wamejikuta wakiwa wanajifungia ndani na kushindwa kushirikiana na wenzao.

  Ninaamini tukiwaruhusu watoto wacheze soka na kuwafundisha vizuri mchezo wa soka tutawaweza kuwachangamsha watoto na kuwajengea mazingira mazuri ya maisha yao ya baadaye.

  Pia watoto wengi wakicheza mchezo wa soka itakuwa ni hazina kubwa ya vipaji vya mchezo wa soka ambavyo taifa la Tanzania litavitegemea siku za mbeleni katika ngazi ya klabu na timu ya Taifa.

  Kwa hiyo ninatarajia wazazi watahakikisha watoto wao wanashiriki katika michezo hasa hasa mchezo wa soka na kuwasisitiza kuzingatia masomo yao, lakini pia serikali iweke miundombinu mizuri ya viwanja vya kuchezea watoto pamoja na kuhakikisha vifaa vya michezo kwa watoto vinapatikana kwa wingi nchini.

  Allan Goshashy ni mwandishi wa michezo wa Gazeti la Mwananchi anapatikana kwa 0652254845
   
 2. Mphamvu

  Mphamvu JF-Expert Member

  #2
  Apr 10, 2011
  Joined: Jan 28, 2011
  Messages: 10,708
  Likes Received: 933
  Trophy Points: 280
  Nimependa hiyo, kikubwa ni mazingira ya mchezo. Kucheza soka ni rahisi kuliko michezo mingine, mkiwa na mpira tu(hata wa karatasi) mechi huanza. Tofauti na mkapu kwa mfano, unahitaji sakafu laini, mpira wenye kudunda na magoli ya juu, nani anaweza hiyo shughuli... Vive le futbol!
   
Loading...