Kwa nini FATHER CHRISTMAS wa KIBONGO asivae Kimasai?Bongo joto bana!

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,072
1,250
Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.



Vipi huko mpenzi wangu?

UNAENDELEAJE? Unajiandaaje kwa Krismasi teh teh? Maana hapa utadhani Krismasi ni kesho tu.

Kila mahali nyimbo za Krismasi hadi zinakifu. Miti ya Krismasi! Taa za Krismasi! Na sanamu za jamaa mwenye ndevu nyeupe na nguo nyekundu ambaye hajui kucheka teh teh, anacheka ho ho ho! Hivi yote hayo yana mahusiano gani na maisha yetu hapa.

Kama Krismasi ni muhimu kiasi hicho hapa petu, hatuwezi kuwa na Baba wa Krismasi anayefanana kidogo na sisi Wabongo? Kwa nini asivae Kimasai? Angalau nguo zitafanana na hali yetu ya joto. Juzi tulienda duka moja na masikini jamaa amevaa hizi nguo zake nzitonzito hadi ameloa jasho! Mama mmoja alitaka kumpeleka mtoto wake amshike mkono lakini mtoto akasema kwa sauti kubwa.

‘Sitaki mama, sitaki, mbona ananuka!’

Nadhani jamaa Krismasi Jasho aliona aibu hadi basi. Waswahili si wanasema iga ufe! Labda ni iga wakubwa wafe wadogo, maana bila shaka yule jamaa hakupenda sana kuvaa kama mwehu lakini mbele ya hali ngumu afanye nini.

Na si lazima Kimasai maana wanavyopenda kutangaza Bongo yetu na picha za Wabongo utadhani nchi nzima ni Wamasai. Kwa nini asivae nguo za vitenge au nini sijui? Ingawa kuna jamaa mmoja msanii maarufu alikuja kumwona bosi akiwa amevaa nguo za batiki. Bosi kama kawaida yake alikuwa amevaa suti na tai.

Hili nalo nimefikiria. Kwa watu wanaoishi katika nchi ya viyoyozi inawezekana. Nyumbani viyoyozi, garini viyoyozi, ofisini viyoyozi. Hivi suti ni kama kitambulisho kwamba mimi si mtu wa kawaida. Ni bosi. Naweza kuvaa nguo za ajabuajabu kwa sababu sionji joto la daladala, au la ofisi zenye feni tu.

Basi yule mgeni, katika kuongea na bosi akamtania;

‘Lakini mheshimiwa, mbona wapenda kujinyonga hivyo? Kwa nini usivae Kiafrika?’

Bosi akacheeeeka.

‘Wacha wewe! Hujui dunia imebadilika? Umemwona Mswahili gani amevaa mashati hayo?’

‘Nimeona wasanii wenzangu wengi …’

‘Ah, msanii si Mswahili Bwana. Kazi yenu kujifanya tofauti na wenzenu!’

‘Nyinyi ndio tofauti. Mimi nadhani sisi angalau tunatetea utamaduni …’

‘Utamu duni. Asili imebadilika. Sasa kwa kuwa Wazungu wengi mmekana suti, na wanaokuja hapa wanataka kuvaa tofauti, basi ni suti ambayo imekuwa vazi la Kiafrika. Na tai. Na hizi batiki zote ni kwa ajili ya Wazungu. Batiki, kitenge vazi lenu, suti vazi letu. Ndiyo mapinduzi ya dunia.’

Bosi akacheka kwa nguvu na kuendelea kunywa wiski yake ya kiasili vilevile. Hata maji aliyoweka ndani ya wiski yanatoka nje.

Lakini yule msanii akacheka pia.

‘Sawasawa mheshimiwa. Ndiyo maana siku ya Krismasi watu watavaa masuti na kwenda kwenye tanuru ya kanisa na kutoka kama vile nyama choma. Nasikia kanisa moja kidogo wapate mafuriko ya jasho.’

Bosi akacheka tena lakini naona kidogo alishtuka.

‘Kwani kuna ubaya gani. Ni heshima kwa Mungu.’

‘Au ni kutambiana? Anayekwenda bila suti anaonekana lofa!’

‘Hapo umenena. Suti ni hadhi. Ni vazi la heshima la Kiafrika!’

‘Ndiyo maana hata kwenye sherehe nyingine, watoto wanavalishwa visuti vya vipande vitatu? Hadi haviwakai, watoto hawana raha maana kimoyomoyo wanajua ni kituko, lakini kwa hadhi ya baba lazima wavae. Hadi kijijini siku hizi lazima avalishwe suti. Suti yenyewe imebebwa kimzobemzobe kutoka Dar ili mtoto awatambie wenzie huko, au asione aibu kwa kuvaa nguo za kawaida. Ama kweli utamaduni mpya.’

‘Lakini wewe Bwana mbona unakashifukashifu namna hiyo? Mambo yetu tuachie sisi. Tukiona suti inafaa wewe ni nani kulalamika?’

Yule msanii akashtuka.

‘Haya mheshimiwa. Nilifikiri utamaduni wa Tanzania unawaruhusu watu kutoa maoni yao bila ubaguzi. Kumbe wenye ruhusa ya kufikiri na kusema ni wenye uwezo tu. Sisi tuwe bubu.’

‘Simaanishi hivyo. Lakini watu wakitaka kuwa watanashati na mashati na tai, si vizuri kuwakejeli.’

‘Mtu anaweza kuwa mtanashati na mashati ya batiki pia. Tena sana. Mbona wanawake wanapendeza kwa rangi za kila aina wakati wanaume tunataka kujifunga tu ndani ya vazi kama hilo. Lakini siwaingilii. Kama wapenda kuvuja jasho ni sawa. Na hayo yote ya Krismasi, kama ya masuti ni biashara tu. Tena naona ya Krismasi ni mbaya sana maana inawalenga watoto hivyo wazazi wanaogopa kutofuata mkumbo. Na sasa Valentine, na siku ya mama duniani na siku ya baba duniani.

Mwisho kutakuwa na siku ya shemeji, na ya mpwa na binamu. Karibu sikukuu zote hizo zimetengenezwa nje ya Tanzania kwa ajili ya biashara kisha kuletwa kwetu ili tuige tufe. Pesa za Tanzania zinaenda kutunisha mifuko ya wengine.’

‘Lo Bwana naona unastahili kuwa mwanasiasa badala yangu. Maneno kibao.’

‘Labda wa enzi zile, si enzi hizo Bwana. Mwanasiasa wa leo lazima abwatie kwamba maisha siku hizi ni nje ndani tu. Mambo ya nje yajae ndani, kuanzia suti za Baba Krismasi hadi kadi za kumpongeza mama.’

Basi sijui waliendeleaje maana ilibidi nirudi jikoni lakini kesho kutwa yake nikashangaa bosi aliamuru mama bosi na mimi tumsindike hadi kijijini kwao. Alidai anataka kwenda kuwashukuru wapiga debe na wapiga kura wake.

Kumbe lengo lilikuwa jingine kabisa. Usiku wa kwanza tulilala kwenye ‘kibanda chake’ cha ghorofa ndani ya geti kali. Bila shaka huu ni utamaduni mpya wa Kiafrika pia. Sasa nilipoamka na kuanza kufanya usafi nilishangaa sana kuona foleni nje ya geti. Wengine wamevaa tumbo asilia … yaani nusu uchi na matunguli kama mkufu lakini wengine wamevaa masuti pia (kweli mpenzi, hata waganga wanavaa masuti siku hizi, na kujiita maprofesa. Kuna mmoja alibeba hata kompyuta!).

Laiti ungekuwapo mpenzi. Maana kweli wote walikuwa waganga. Kumbe bosi alikuwa ametangaza usaili wa waganga, amjue nani wa kumlinda vizuri kama bosi. Basi niliona maajabu. Mara nyumba inatingishika, mara nasikia vicheko vya kutisha, mara miti bustanini ikanyauka, mara ndizi zikaiva palepale mgombani.

Kila mmoja alikuwa anajaribu kumwonyesha bosi kwamba anao uwezo kuliko mwingine. Sasa sijui hata mshindi alishinda kwa kitu gani lakini alikuwa wa matunguli, si wale wa masuti. Kumbe masuti wanang’ang’ania utamu duni wa ushirikina tu, huku wakikataa mila zote nyingine. Ama kweli wanajua kubakisha mazuri na kutupa maovu.

Ningependa kukuambia zaidi mpenzi lakini hata mimi nimetishwa. Yule mganga mshindi alinilazimisha kunywa kinywaji fulani. Kisha akaniambia kwamba nikitoa siri zake, masikio yangu yatageuka masikio ya punda na hata nikiongea nitakuwa natoa kelele kama punda. Ningependa kujaribu lakini ….

Akupendaye kwa moyo wote usio na ushirikina hata chembe, mwenye kupenda utamaduni wetu wa kujenga si wa kuwadhuru wengine,
 

malisak

JF-Expert Member
Mar 16, 2006
536
500
vizuri na wazo zuri lakini kwa jinsi tusivyojipenda wenyewe na kuuendekeza uzungu lazima watu wataponda
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom