Kwa marais hawa tuzo ya Mo Ibrahim itapotea bure

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Posted Date::9/29/2007
Kwa marais hawa tuzo ya Mo Ibrahim itapotea bure
Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi

OKTOBA 22 itakuwa ni siku muhimu duniani, lakini hasa Afrika ambapo Rais Mstaafu bora ambaye atapata dola 5 milioni (sh 6 bilioni) na dola 200,000 (Sh 240 milioni) kila mwaka hadi mwisho wa maisha yake atatangazwa.

Mpango huu wa kumpata Rais mstaafu bora ambao ni kuanzia kati ya mwaka 2004 na 2006, umeanzishwa na Taasisi ya Mo Ibrahim ( Mo Ibrahim Foundation).

Uzinduzi wa tuzo hiyo ulitangazwa mwaka jana na Taasisi hiyo ambayo inamilikiwa na bilionea mzaliwa wa Sudan, Mohamed Ibrahim maarufu kama Mo Ibrahim.

Huu ni mpango mpya na mkubwa ambao unaangalia mambo matatu ya msingi, kuchochea mjadala wa utawala bora katika nchi za Afrika na duniani kwa ujumla.

Kutoa nguvu na mamlaka ya raia kuamua mambo katika serikali zao katika nchi, na kutambua na kuthamini mchango wa marais wa wastaafu katika kuleta maendeleo na kuongoza kwa vipindi maalumu.

Hii ndiyo nia na mtazamo wa Mo Ibrahim Foundation, ambao msingi wake ni kuonyesha mfano hai kwa kujaribu kushawishi marais waliopo madarakani duniani, wazingatie demokrasi na kujenga utawala bora.

Ni mtazamo mzuri, ambao lengo kuu ni kusaidia nchi za Afrika lakini wenye maswali mengi kuliko majibu, ikilinganishwa na hali halisi ya mwenendo wa mambo katika bara letu hili ambalo wakoloni waliita bara la giza.

Hapa nitazungumzia bara langu la Afrika tu, utoaji wa tuzo hii umemfanya mzee Nelson Mandela 'Madiba', Rais mstaafu wa Afrika Kusini, kutahadharisha kuhusu umakini wa kumpata mshindi.

Mtazamo na tathimini ya mzee Madiba, imezingatia kwa kina uzoefu wake katika uongozi wa kiti cha Urais katika Afrika Kusini huru ya mwaka 1994 na hata harakati zake, akijua uchungu wa kupigania uhuru na thamani yake.

Katika mtazamo na tathimini yake, mzee Madiba anasimama katika jambo moja kubwa la msingi kwamba, tuzo hiyo itolewe kwa kiongozi aliyeongoza kwa umakini.

Hii maana yake nini, kiongozi huyu anayetajwa na Mandela si tu ambaye aliachia madaraka baada ya muda kuisha, au aliyetekeleza eneo moja la demokrasi au utawala bora, huyu lazima uongozi wake uwe uliokubalika na wananchi.

Kukubalika maana yake nini, ni kuongoza kwa matakwa ya umma, kushughulikia kero zao, kutotumia madaraka ya umma vibaya au kwa maslahi binafsi, kutojihusisha wala kukubali kuwa na watendaji mafisadi katika serikali.

Uongozi makini hapa anaoutaja Mandela ni zaidi ya hapo, ni pamoja na kuhakikisha rasilimali za nchi zinanufaisha wananchi na kuwaondolea umaskini na ufukara, kusomesha watoto, kujenga miundombinu na kuboresha huduma zote muhimu za kijamii.

Huu ndiyo uongozi makini na uliotukuka ambao unatajwa na mzee Mandela kama ambao kiongozi wake anapaswa kupewa tuzo.

Binafsi, kabla ya kusoma mtazamo wa mzee Mandela, nimekuwa nikijiuliza swali moja la msingi kuwa, ni rais gani hasa anayepaswa kupewa tuzo hii kwa Afrika hii i isiyokuwa na akina Kwame Nkrumah, Mwalimu Julius Nyerere na wengineo waliopigania nchi zao kwa uwezo wao wote.

Je, ni rais aliyeongoza kwa mujibu wa katiba kisha akaondoka madarakani, je, ni aliyekuwa na uongozi makini kwa ujumla, aliyeruhusu vyama vingi kama utitiri, aliyekuwa akitoa fursa kwa wananchi kutoa maoni kisha yanaishia Ikulu au wizarani?

Nikapata jibu kama la mzee Mandela kwamba Afrika inahitaji kiongozi aliyeongoza kwa umakini, lakini bado nikajiuliza tena, hao viongozi makini wapo?

Hapa ndipo ninapogota, nashindwa kupata jibu nani hasa anaweza kuwa kiongozi makini na kupaswa kupewa mabilioni hayo!

Nakaa nakuna kichwa naona nywele zinakaribia kunyonyoka, naona majina mbalimbali yanatajwa miongoni mwao ni Benjamin William Mkapa Rais mstaafu wa Tanzania.

Hapa ndipo nakataa kabisa, ingawa najua anaweza kushinda kwani anatajwa na mabwana wa Ulaya kama mtu makini na aliyeleta mageuzi Tanzania, lakini msimamo wangu unashindwa ukubaliana nao.

Naona ni vema pesa hizi wapelekewe watoto yatima au zitumike kujenga barabara, miundombinu ya mawasilino ya kompyuta (ICT) hadi vijijini, kuushambulia ufukara na umaskini na kutoa elimu ya uraia kwanza.

Hapa naona kiza, sipati nuru, naona kutoa mabilioni hayo ni sawa na kuyatupa au kuzidi kuwanemeesha waliokwipataa neema.

Nafahamu azma ya tuzo hii ni kuondoa matatizo kama ya ufisadi, lakini naamini kwa viongozi hawa wa Afrika wa sasa pesa hizo ni bora zingepelekwa katika maeneo niliyoyataja hapo juu.

Kubwa naona hapa hakuna cha mabadiliko bali itakuwa ni kumuongezea aliye nacho, kwa maana Afrika ya sasa na kuanzia miaka ya 1990 haina viongozi bali ina watawala na viongozi wafanyabiashara.

Naona jambo moja tu kwamba kama ni kutoa tuzo, basi ilipaswa kushindanishwa kwa waasisi wetu kama akina Mwalimu Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Patrice Lumumba, Mandela nk.

Naona dhahiri mpango huu wa Mo Ibrahim na taasisi yake, haukufanyiwa utafiti wa kuona mahitaji halisi ya maendeleo ya bara la Afrika.
Ninashangazwa pale Mo Ibrahim anapodhani demokrasia na utawala bora Afrika unajengwa na rais, hili ni kosa. Mambo haya yanategemea uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu (Rights and Responsibilities), vitu hivi vinakosekana na vinaweza kupatikana kwa kutoa elimu ya uraia.

Lakini si elimu ya uraia tu, huwezi kujenga utawala bora na demokrasi kwa mtu masikini anayeweza kuuza kura kwa sh 2,000 au kopo la pombe ya asili, khanga, mpango huu umesahau kuondoa kero hizo kwa kujengea wananchi uwezo kiakili.

Hapa ndipo nasikitika kuona Mo Ibrahim anataka kushindanisha marais, badala ya kuweka misingi hiyo kwanza kisha akaanza tuzo hiyo miaka 30 baadaye.

Kwa mfano, unaweza kumpa Mkapa Sh6 bilioni kwa sababu tu aliachia madaraka kwa kipindi cha miaka kumi kisha akaondoka madarakani na pia kuwa rafiki wa akina Tony Blair, lakini ni huyu katika uongozi wake nchii hi ilishuhudia mauaji ya kisiasa visiwani Zanzibar mwaka 2001.

Ni huyu ambaye alitenda aliyoamini yeye, hakutaka kusikia maoni ya wananchi wala vyombo vya habari vya ndani, kwa kifupi hakuweza kujenga utawala bora wala kuruhusu demokrasia ya kweli, wananchi walipinga uuzaji wa nyumba za umma serikali ikaziba masikio, ikaziuza. matokeo yake viongozi wa sasa hawana makazi.

Lakini huu ni mfano hai tu, najua kuna wengine wanatajwa kama akina Joaqium Chissano (Msumbiji), huyu licha ya kumaliza vita kati ya serikali na waasi wa Renamo, bado ana kasoro nyingi ambazo ni pamoja na mwanae Nyimpine kudaiwa kumua mwandishi wa uchunguzi Carlos Cardos, na kisha kuiba Sh 14 milioni, lakini kesi ikazimwa.

Wengine ni akina Alhaji Bakili Muluzi (Malawi), huyu kwanza hataki kuitwa Rais Mstaafu kwani anataka kugombea tena, pia anatuhumiwa kwa ufisadi, wengine ni Albert Rene (Shelisheli), huyu ingawa anaelezwa kuimarisha utawala bora katika visiwa hivyo, lakini bado hapaswi kupata fedha.

Kuna akina Methew Kerokou wa Benin ambaye anaelezwa kuruhusu demokrasi ya vyama vingi, lakini bado hapaswi kupata fedha hizi kwani nchi yake bado inanuka umaskini.

Mifano hii ya viongozi hawa wanaotajwa kuweza kutwaa tuzo hiyo ni ishara tosha kwamba mabilioni haya yatatupwa au kupelekwa kusiko, badala ya kutumika kusaidia yatima, akina mama wanaojifungulia vichakani au kusaidia kujenga huduma za kijamii.

Ndiyo maana naona, hakuna mantiki wala haiingi akilini leo hii mtu apewe Sh6 bilioni eti tu, leo hii nchi za bara hili zinashindwa kuungana na kuhujumiana zenyewe kwa zenyewe.

Unampa Rais tuzo wakati katika serikali yake alikuwa na mawaziri mafisadi au waziri mkuu fisadi, hi maana yake nini?

Ndiyo maana naona tuzo hii itatolewa kimakosa au Mo Ibrahim kutokana na kukosa washauri au kutofanya utafiti, anafikiri marais ndiyo wananchi.

Msingi ni wananchi, hawa wakijitambua ndipo bara la Afrika litapata viongozi bora, zaidi ya hawa wanaotajwa sasa na kushuhudia mapinduzi ya maendeleo na uongozi katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (Sub Saharan Africa), kama anavyotaka Mo Ibrahim vinginevyo pesa hizi ni kuzitupa!


Ramadhan Semtawa ni mwandishi wa Mwananchi: semtawa.blogspot.com, semtawa@yahoo.co.uk.0782-528229
 
Marais wengi ni kukandamiza demokrasia na walimaliza kukandamiza wanachezea katiba zao kuongeza muda wabakie madarakani.

Hii ndiyo Africa.
 
Back
Top Bottom