Kwa kusutwa huku serikali sasa ione aibu

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,113
KATUNI(681).jpg

Maoni ya katuni


Mkutano wa saba wa Bunge la 10 unalifikia ukomo wake jana. Katika mkutano huu mambo makubwa ya kihistoria yaliibuka, yote yakijikita katika wajibu muhimu wa Bunge katika kusimamia serikali. Ni mkutano ambao wabunge bila kujali tofauti zao za kiitikadi

walikuwa kitu kimoja kuihoji serikali juu ya utendaji usoridhisha wa baadhi ya mawaziri.

Hali hii ilijitokeza kutokana na taarifa za kamati za Bunge zilizowasilishwa zikichambua ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu

za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2009/10. Kamati hizi ni ile ya Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC na ile ya Mashirika ya Umma (POAC). Kwa ujumla wake ziliwasilisha kitu kimoja, watumishi wa umma wamekosa uaminifu kwa kiwango kikubwa.


Mawaziri nao hawakusalimika katika moto uliowashwa bungeni, baadhi wametajwa kwa majina jinsi walivyo vikwazo katika utekelezaji wa majukumu ya wizara zao, wengine wametajwa wazi kuwa ni waongo, wezi na wanaoendesha taasisi za umma kwa maslahi yao, ikiwa ni pamoja na kuwakingia vifua watu wanaotekeleza matakwa yao binafsi kwa faida binafsi.


Kama ni kusemwa, hakika serikali nzima ilisemwa; imesutwa, lakini kibaya zaidi katika historia ya utawala wa nchi hii tangu ijitawale Desemba 9, 1961 Waziri Mkuu amejikuta katika jaribio la kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye; wabunge wamejiorodhesha wazi wazi kutaka kumpigia kura ya kutokuwa na imani Waziri Mkuu.


Hawakujiandaa kwa uficho, walifanya hayo mbele ya macho yake, walimweleza wazi kuwa ameshindwa kazi kwa kuwa kama tabia ya mawaziri anaowasimamia ndiyo iko hivyo, basi hana anachokifanya.

Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya ughali wa maisha; mfumuko wa bei umewapiga sana watu wetu; gharama

za maisha kila uchao zinakwenda juu; serikali kwa ujumla wake imekuwa na maelezo ya ujumla sana juu ya hali hii, kwamba inasababishwa na mdororo wa uchumi duniani kote.

Ingawa ni kweli uchumi wa dunia umedorora, na pamoja na ukweli kwamba Tanzania kama sehemu ya mfumo wa uchumi wa kimataifa haiwezi kukwepa athari za matatizo yanaoikumba dunia, lakini ni vema na haki pia kujenga mipaka ya madhara ambayo yanasababishwa na nguvu za kiuchumi za dunia na yale yanaochochewa na udhaifu wa kiutendaji wa watumishi wa umma.

Kwa mfano, itakuwa ni jambo la ajabu kusema kuwa wizi wa fedha za umma, kutokuwajibika na udhaifu mwingine wa kiutendaji katika taasisi za serikali ni matokeo ya kudorora kwa uchumi duniani.

Haiingi akilini kwamba mabilioni ya fedha za umma yanapotea katika mikono ya watumishi wa umma na mawaziri wakijua hayo, kama

vile mishaha kwa watumishi hewa, kushindwa kusimamia mikataba ya kazi zilizotolewa na serikali kwa wakandarasi mbalimbali, kuwa ni matokeo ya mdororo wa uchumi duniani.

Kilio na kelele zilizopigwa na wabunge hazijahusisha kwa vyovyote vile na hali ya mdororo wa uchumi duniani, ni maelezo yanaoonyesha jinsi watu walivyokabidhiwa ofisi za umma wamezigeuza kuwa za binafsi, kuendekeza wizi, ubinafsi na ufedhuli ambao ni vigumu kupata maneno sahihi ya kuuelezea.

Ni kwa kutafakari hali hii ya joto la Mkutano wa saba katika Bunge la 10, tunashindwa kujizuia kuwaomba wabunge wetu wakaze buti zaidi ili kuiadabisha serikali. Wabunge wakaze buti kwa sababu uwaziri ni kazi yenye dhamana kubwa, ni heshima ndani ya jamii ya mamilioni ya watu wenye sifa ya kupewa majukumu hayo; pamoja na ukweli kwamba kazi ya uwaziri haisomewi kokote, lakini pia

uzembe, ubadhirifu na kila aina ya uovu ndani ya ofisi za umma si kielelezo cha uadilifu, ni sifa tosha kabisa ya kuachia ofisi ya umma.

Tungependa pia kuchua wasaa huu kuwakumbusha viongozi hasa mawaziri kwamba hata kama watakuwa wamepona katika wimbi hili la kutaka mawaziri wanane wajiuzulu na jaribio la kumpigia kura ya kutokuwa na imani Waziri Mkuu, bado mapambano hayajaisha kama hakutakuwa na mabadiliko katika utendaji wao wa kila siku; tunautazama huu kama mwanzo tu wa kuhimiza uwajibikaji kwa wote waliokubali kukalia ofisi za umma. Bila kufanya hivyo, hakika watarajie mabaya makubwa na magumu zaidi huko tuendako.


CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom