Kwa hili la wasaidizi wa Rais Samia, namtetea Rais Rais Mstaafu Jakaya Kikwete

Phillipo Bukililo

JF-Expert Member
Dec 29, 2015
18,488
13,608
Mheshimiwa Jakaya Kikwete Rais wa awamu ya nne amekuwa akishikwa uchawi siku za karibuni baada ya kifo cha Rais wa awamu ya Tano John Magufuli. Zinatembea mitandaoni sauti za kurekodiwa (audios) pamoja na zile za Youtube zikimshambulia Mzee wa Msoga kama vile ni mhusika wa yaliyolikuta taifa hili mwezi uliopita.

Zinajengwa hoja kwamba wapo wasaidizi wa Mama Samia ambao waliingia katika ulingo wa siasa na uongozi kipindi cha awamu ya nne. Wanasema Dr Phillip Mpango ni matunda ya Mzee JK. Wanasema Mwigulu Nchemba ni matunda ya JK, wanasema Mama Liberata Mulamula ni matunda ya JK. Kwamba JK anaweza kuwa yupo nyumbani kwake akiongea na wazee wenzake lakini uwepo wake kimawazo na kimtazamo bado upo hai.

Nachoweza kuwakumbusha hawa watu wenye vinyongo na ile roho ya kupenda kutafuta mchawi ni kwamba Rais pekee ambaye hakufaidika na kizazi cha viongozi na wanasiasa waliokuwa wameandaliwa na mtangulizi wake, ni Hayati Julius Nyerere rais wa awamu ya kwanza. Ni yeye pekee ambaye alifanya kazi na kundi la wasomi lilikuwa limetoka vyuoni moja kwa moja na kuingia kwa mara ya kwanza katika masuala ya uongozi.

Ali Hassan Mwinyi aliwatumia wanasiasa kama Cleopa Msuya, John Malecela, Kirigini, Mustafa Nyanganyi na Salim Ahmed Salim wakiwa na matunda ya mtangulizi wake Julius Nyerere.

Benjamin Mkapa aliwatumia wanasiasa kama Amrani Mayagila, Jackson Makweta, Joseph Rwegasira na wengine wengi wakiwa ni matunda ya mtangulizi wake Mzee Mwinyi.

Jakaya Kikwete aliwatumia wanasiasa wengi tu ambao waliibuliwa na kukuzwa kisiasa na kiutendaji kama viongozi na watangulizi wake watatu.

Ni vigumu sana kwa Rais mmoja kufanya kazi na kundi jipya kabisa la wasaidizi ambao hawana makandokando ya uhusiano na waliomtangulia haswa kwenye nchi kama yetu ambayo inayo historia nzuri sana ya kurithishana mamlaka kwa amani (succession plan). Hatujawahi kuwa na tamaduni za mapinduzi japo tumewahi kuwa na siasa za mitandao ya kiurafiki.

Wenye kujenga hoja kwamba 'watu' wa JK bado wapo ni hivyo eti anaiongoza nchi kupitia mlango wa siri usioonekana kwa wote ni waendelezaji wa dhana za kujifurahisha tu (conspiracy theorists).

Kama Dr Mpango anao uwezo kichwani na anao umuhimu mkubwa kwa Taifa, asitumiwe kisa tu aliyempa cheo kwa mara ya kwanza alikuwa ni Mzee JK?.

Kama Mwigulu anayo elimu na umri unamruhusu, kwake kupewa wizara ya fedha ni nongwa eti kwa kigezo cha aliyempa cheo na kumkuza kama kiongozi ni Mzee JK?.

Hizi dhana za kutafuta mchawi zina madhara yanayodumu kwa muda mrefu, kwani uwezo wa kila anayesikiliza hizi audio unatofautiana katika namna za kuzama kwa kina na kukipima kile kinachozungumzwa.

Inatubidi Watanzania tujivunie namna ambavyo tumekuwa na marais wanaotoka Ikulu na kuachia ofisi kwa wanaowafuatia huku wakiwarithisha hazina pana ya wasaidizi wenye elimu na maarifa makubwa.

Yapo mataifa afrika hii hii ambayo hawana uzoefu wa kuona vizazi mbalimbali vikitoa mchango katika ujenzi wa uchumi na ustawi wa jamii zao. Hili la kumzonga Mzee JK halina tija sana sana ni kujaribu kutafutia mahali pa kupunguzia hasira.

Mungu ni mwema naamini Tanzania itadumu hata baada ya wenye nguvu za kimwili na kiakili wa leo watakapokuwa wameshatangulia mbele za haki.
 
Back
Top Bottom