Kwa hili Jenerali Uimwengu umewaacha mashabiki wako njia panda

Byendangwero

JF-Expert Member
Oct 24, 2010
871
56
Jana nilisoma katika safu hizi, barua ndefu iliyoandikwa na Jenerali Ulimwengu kwa JK. Nianze kwa kukiri kwamba barua ya aina hiyo hiyo, niliwahi kuiona katika gazeti la Rai ama mwishoni mwa mwaka 2005 au mwanzoni mwa mwaka 2006. Kwa maoni yangu,barua hii ilipotokea kwa hiyo mara ya kwanza, ilikuwa inastahili. Lakini kwasasa, kwa baadhi yetu barua hiyo inatia kichefuchefu, kwani inapindisha ukweli ulivyo. Mwaka 2005 wakati JK anaingia madarakani watu wengi tuliamini ya kwamba sasa tumempata mkombozi wa kweli, ambaye angeliondoa nchi yetu katika shimo la ukoloni mamboleo, ambamo ilitumbukizwa na utawala wa Mkapa, na kuielekeza katika njia ya uhuru kamili kiuchumi. Miaka mitano ya uongozi wake, imekuwa ni ya kukatisha tamaa kwa yeyote yule mwenye mapenzi mema na nchi yetu. Chini ya uongozi wake siyo tu kwamba nchi yetu imeendelea kupoteza rasilimali nyingi kwa uporaji na matumizi mabaya ya serikali, lakini pia kuna kila dalili zinazodhihilisha ya kuwa nchi yetu kama taifa imepoteza mwelekeo.Hali hiyo imesababisha watu wengi kupoteza imani waliyokuwa nayo kwa JK. Kwanini basi, mtu kama Jenerali, kwa wakati huu tulionao, anaamua kupindisha ukweli huo na kuaanza kumuita JK mkombozi! naomba kwa yeyote mwenye jibu anitegulie kitendawili hicho.
 
Samahani,
Hebu iweke barua hiyo hapa tuidodose maana wengine tuko mbali na magazeti ya Bongo.

Lakini, usiwe na matumaini sana na Ulimwengu. Alipata matatizo na utawala wa Mkapa na ktk utawala huu akawa na amani sana. Akawauzia hata gazeti wana mtandao. Nadhani anasumbuliwa na urafiki wa kudumu ili waendelee kumpa upendo wa kudumu. Lakini nyingine ya mwandishi huyu, kwangu mimi ni aina ya themes zake. Mara nyingi naziona zina misingi ya theories anazozifahamu au alizozifahamu siku zote za maisha badala ya uhalisia wa maisha tuliyonayo sasa hivi.

Tumuite tu kwamba ni mwana historia.
 
Kamwita JK mkombozi!? Nafikiri Ulimwengu anazeeka vibaya

jamini mkombozi ni mkombozi tu lakini yawezekana amemwita mkombozi wa mafisadi toka kwenye kibano
kilichokuwa kinawakabiri dhidi ya ufyolo waliolifanyia taifa, kikubwa ni sasa kuweza kuangalia ni
ukombozi wa aina gani? ambao jk anastahili kuitwa
 
Twaha Ulimwengu alipanda cheo katika medani ya habari na kuwa four-star General. Sasa anaporomoka na kuwa foot soldier, juzi aliandika lead story kwenye East African kama special correspondent!! Yaani from editor-in-chief of leading media house to a newspaper correspondent. Hii ya barua kwa JK nadhani anajipendekeza... amerudia hadithi ya walivyokutana Bulgaria, hivi kweli JK na English yake ilivyopinda na hoja nyepesi hali ilikuwaje alivyokuwa kijana hajapata exeperice? Bulgaria huko aliongea nini? ahahahahaha
 
Tatizo la Jenerali Twaha Ulimwengu ni "OPPORTUNISM" anataka aonekane yuko upande wa watawaliwa at the same time hataki kuwaudhi watawala, haiwezekani!! He wants to eat his cake and still have it!! Ukiila keki yako ndio basi inakwisha mpaka ukaitolee maliwatoni.!!
 
Mwaka 2005 siku chache baada ya Jakaya Kikwete kushika madaraka ya Rais wa Tanzania kutokana na uchaguzi uliompa ushindi wa Oktoba mwaka huo, nilimwandikia Barua Ndefu ya Wazi kupitia katika gazeti la Rai. Kwa kuwa mazingira ya wakati huo na ya leo yanashabihiana sana, na kwa kuwa bado Barua ile Ndefu ya Wazi ina hoja ambazo zinatukumbusha yaliyopita na kututabiria yajayo, tunairejea barua hiyo ambayo maudhui yake yanabaki yaleyale hata kama imehaririwa hapa na pale kusahihisha makosa ya chapa.

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,
Ikulu.

Ewe Jakaya mwema, Salaam.

AMA baada ya salaam, nakuomba upokee dua zangu za kukutakia heri na fanaka katika Mwaka Mpyana maisha marefu na afya njema katika utumishi wa Taifa letu.

Pili, napenda kukupongeza kwa ushindi uliopata katika uchaguzi uliopita, ushindi uliodhirisha kwa mara nyingine tena jinsi ambavyo wewe kama mwanasiasa. unakubalika machoni mwa Watanzania. Umekuwa ushindi unaodhihirisha imani iliyojengeka katika nyoyo za Watanzania kwamba wewe, Jakaya, utawaongoza vyema ili waondokane na adha zilizowazingira, hususan ufukara uliokithiri na unaoendelea kujijenga kila siku miongoni mwao bila ya kuwapo kwa ishara kwamba viongozi wao wanajua au kujali hali zao.

Tatu, naomba radhi kwa kuamua kukuandikia waraka huu, ulio wazi na mrefu. Si nia yangu kukuchosha na maneno mengi ambayo sina shaka umekwisha kuyasikia au kuyasoma katika sura moja au nyingine, na wala si kusudi langu kushusha hadhi ya nafasi yako ya juu kwa kukuandikia kupitia magazeti.

Nimeteua njia hii ya mawasiliano kwa sababu tu haya ninayokusudia kuyajadili ni masuala ya umma, na ni masuala ambayo naamini kwamba yanao uzito mkubwa, na kwa hiyo yanastahili kujadiliwa kadamnasi, wala si masuala binafsi baina yangu na wewe ambayo yangeweza yakajadiliwa faragha. Napenda kuamini kwamba ubinafsishaji wa amali hapa nchini, pamoja na jitihada za baadhi yetu, bado haujafikia viwango hivyo.

Nne, naomba unielewe kwamba sithubutu, wala sidiriki, kukufundisha kazi. Kazi hiyo uliyopewa sijawahi kuifanya, sijawahi hata kuikaribia, na wala sijawahi kuiota. Lakini ninaamini kwamba unanijua vyema na unaelewa kwamba kujadili masuala kama haya ni sehemu ya jinsi nilivyo. Iwapo kati ya mambo nitakayoyasema katika waraka huu yatakuudhi, natanguliza kuomba radhi; na iwapo yatakuchosha, naomba uyatupilie mbali.

Napenda kurejea lile nililolitaja kama la pili, nalo ni pongezi kwako kwa ushindi uliopata katika uchaguzi. Pongezi hizi hazina budi kutangulizana pamwe na pole. Pole, si tu kwa kuwa umefanya kazi kubwa ya kampeni. Hiyo pia ni kweli. Na wala si kwamba kazi hiyo imeanza karibuni, bali imechukua muda wa miaka kadhaa ya maandalizi, wakati mwingine ya mashaka, lakini hili nitalijadili mbele ya safari.

Pole, kimsingi, kwa sababu ushindi waliokupa wananchi wa Tanzania ni mzigo mkubwa uliobebeshwa. Najua unaelewa fika kwamba hamasa na mapenzi waliyoonyesha Watanzania kwako tena ni kielelezo kwamba wanayo imani kuwa bado unaweza kuwa mkombozi wao. Kwa nini wanaamini hivyo, mimi sijui, lakini ukweli ni kwamba hivyo ndivyo wanavyoamini. Watu wanataka mkombozi.

Kwa bahati mbaya, watu wote wanaotaka mkombozi ni watu walio katika utumwa wa aina moja au nyingine. Misahafu imejaa aina mbalimbali za utumwa zilizowafanya watu wadai mkombozi, ambaye walimpata au hawakumpata, na pia mifano ya zahama zinazoweza kujitokeza pindi watu wanapofadhaishwa na ucheleweshaji wa ukombozi. Mfano mmoja ni pale wana wa Israeli walipofadhaishwa kutokana na kuchelewa kwa Nabii Musa kurejea kutoka kilimani alikokwenda kupata maelekezo ya Bwana Mkubwa, wakaamua kuchanga vidani vyao, wakaviyeyusha na kuunda kijindama cha dhahabu, kisha wakakiabudu.

Kwa maneno mengine, watu wanaotaraji ujio wa mkombozi hawana subira, kimsingi kwa sababu wamechoshwa na hali zao na wanataka mabadiliko ya haraka, ya mara moja. Wanapohisi kwamba ukombozi wao umo katika hatari ya kuahirishwa, huwa ni wepesi wa kutafuta ukombozi mbadala, kama yule ndama wa wana wa Israeli.

Wakati mwingine mchakato wa ukombozi huenda mrama, watu wakahamanika kwa kutoona matunda, "wakubwa" wakaogopa kwa sauti kubwa zaidi za madai, na hatua kali zikachukuliwa na "wakubwa" dhidi ya mkombozi mtarajiwa, huku wale waliotaraji ukombozi wakishangilia hatua hizo na kumkejeli mkombozi mtarajiwa aliyeshindwa. Hapo ndipo mkombozi huvishwa taji la miiba na kubebeshwa msalaba hadi Kalvari.

Naam, Jakaya, ukombozi una madhila yake kwa maana nyingi. Kwanza, tukiacha matapeli wachache wenye uwezo wa kisanii wa kughilibu akili za binadamu, ukombozi hautafutwi. Ukombozi humzukia mtu asiyeutaraji. Mara nyingi kinachotafutwa ni fursa ya kawaida tu ya kufanya yale unayoamini yanaweza kufanyika na yakazaa manufaa kwa jamii yako na watu wako. Unaamini kwamba utawala uliopo haujafanya kazi ya kutosha katika hili au lile, yako masuala mengi ambayo hayajashughulikiwa, na iwapo ungepata nafasi ya uongozi wewe ungerekebisha mambo.

Lakini unapojitokeza tu, kwa sababu ambazo hazijawahi kuelezwa, watu wanakutambua kama yule mkombozi waliyekuwa wakimsubiri kwa karne. Utajitahidi kuwaambia kwamba wewe si mkombozi, kwamba unachoweza kufanya ni kuunganisha nguvu na akili zao na kuwaongoza na wao wakishiriki, wapi! Hawatokusikia, na hayo maelezo yako yatamezwa na nderemo na vifijo vinavyomshangilia mkombozi, na kila unavyojitahidi kuwaelimisha kuhusu ukweli wako ndivyo watakavyozidi kuamini kwamba wewe ni mkombozi kweli kweli, na watayachukulia maelezo yako kama sifa ya kutopenda utukufu, alama nyingine ya mkombozi.

Sijui kama umeliona hili, lakini wewe ulikuwa katika hatari kubwa zaidi ya kufanywa mkombozi kuliko wenzako wawili waliokutangulia. Nasema kweli ninaposema kwamba tangu Baba wa Taifa, Kambarage, nchi hii haikuwahi kupata kiongozi aliyeingia madarakani kwa ridhaa ya wazi wazi kabisa ya raia karibu wote wa Tanzania, kama wewe.

Kilichokuwa kikifuata baada ya ridhaa hiyo ni wewe kufanya kazi ya ukombozi, kazi ya kufanya mambo yasiyo ya kawaida, miujiza. Ingawaje sote tunajua kwamba miujiza hutokea kwa nadra sana siku hizi, hiyo ndiyo iliyotarajiwa. Matapeli wa kisiasa wanalijua hili, kwamba watu wanataka miujiza. Wataahidi kila wanachodhani wananchi wanataka kuahidiwa huku wakijua kabisa kwamba hawawezi kutimiza ahadi zao. Hawa ndio wale wanaoahidi kujenga daraja katika kijiji kisicho na mto.

Mwanasiasa wa kweli naye anaahidi, lakini anaahidi huku akiamini kwamba anayoahidi kuyafanya ni mambo yanayohitaji kufanyika na pia yanawezekana, hata kama si katika miaka miwili au mitatu. Ni mambo ambayo yakiwekewa mikakati thabiti yanaweza yakafanyika kwa urefu mbalimbali wa mitazamo ya muda, muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Anajua kwamba iwapo falsafa ni imara, sera ni safi, mikakati ni madhubuti, mbinu ni sahihi na utekelezaji ni makini, hakuna lisilowezekana.

Nimefuatilia kwa makini ahadi ulizozitoa katika kampeni yako yote. Ahadi hizo ni nyingi, hakuna ubishi, na ni kuhusu mambo makubwa makubwa. Lakini hazinitishi, kwa sababu mambo uliyoahidi kufanya kwa kweli ndiyo mambo kiongozi wa nchi anatakiwa ayafanye, na asipoyafanya anakuwa ameshindwa kuiongoza nchi yake.

Kwangu mimi, ahadi zote ulizozitoa kuhusu maeneo muhimu kama vile elimu, afya, maji, kilimo, miundombinu, mazingira, uendeshaji wa migodi ya madini, ajira kwa vijana, michezo, rushwa, na kadhalika, yote ni masuala ambayo mkuu wa nchi yo yote hana budi kuyashughulikia.

Kwa kweli tungeweza hata kusema kwamba mwanasiasa anayetafuta uongozi wa nchi hana haja ya kuyataja hayo, kwani yanaeleweka kama majukumu ya ye yote yule atakayeingia madarakani. Lakini ni lazima yatajwe mara kwa mara, ili tujikumbushe na tusije tukayasahau, kwani yanaweza kusahauliwa. Tulimsikia Rais Mstaafu kabla yako akisema kwamba katika uongozi wake wa miaka kumi alisahau kilimo. Sasa, kama inawezekana kusahau kile kinachoitwa "uti wa mgongo" wa uchumi wa taifa, sembuse "kucha" kama michezo!

Hivyo, basi tukumbushane kila wakati majukumu yetu. Nasema yetu, kwa sababu si yako peke yako. Hili ni jambo ambalo linahitaji kusisitizwa. Majukumu haya ni yetu sote, sote raia wa Tanzania, na kila anayetutakia mema. Tukilitambua hili, tutakuwa tumeepuka mtego wa kukusabilia wewe na serikali yako kila mzigo wa Taifa.

Hata hivyo, ni wewe unayetakiwa kutupa uongozi. Baada ya uteuzi wa mawaziri utakuwa katika shughuli nzito ya kuwateua wananchi wengine wengi wa kukusaidia katika kazi yako nzito. Katika barua hii ndefu nitapata wasaa wa kutoa maoni yangu juu ya Baraza la Mawaziri na watendaji wengine, pamoja na masuala mengine ya kiutawala na kiuongozi.

Kwa sasa inatosha kusema kwamba mawaziri utakaowateua, na watendaji wengine wengi unaoruhusiwa kuwateua, hao ndio watakaounda timu yako. Hawa wote ni wachezaji; wewe ndiye kocha au meneja. Timu ikicheza vibaya, ikafungwa wewe ndiye wa kulaumiwa. Ikicheza vizuri ikashinda, wewe ndiye wa kusifiwa.

Kama kocha na meneja, unao uwezo wa kuona ni namba gani inapwaya ukamtoa mchezaji na kumwingiza mwingine. Haitarajiwi kuwa utachezesha timu hiyo hiyo, kama hii iliyopita, kwa miaka kumi hata kama haifungi mabao. Kitendo kama hicho kinaashiria kwamba ama kocha kalala usingizi, ama haelewi mchezo unaochezwa, ama hajali kama timu inafunga au inafungwa, ama si kocha bali ni shabiki namba moja wa timu. Ni dalili ya nakisi kubwa katika uwajibikaji.

Huna haja ya kuelezwa kwamba ulirithi nchi ambayo wananchi wake wamezama katika umasikini usioelezeka hata kama nchi yenyewe ni tajiri. Nchi hii ina kila kitu kinachohitajika kwa maendeleo ya watu wake, lakini bado maendeleo ni ndoto ya mbali. Umerithi nchi ambayo wananchi wake walianza tena kukata tamaa kwa kuelemewa na maadui wakubwa wanne, baada ya wale watatu tuliowatambua wakati tunapata Uhuru kuongezewa wa nne, rushwa.

Umerithi Taifa ambalo limeshuhudia katika miaka ya hivi karibuni mpasuko mkubwa kati ya matajiri wa kufuru na masikini wa kutupa, kiasi kwamba ipo hatari ya kweli ya amani kuvurugika.

Umerithi Taifa ambamo viongozi walikwisha kujisahau, wakawa watawala tu, wakajenga jeuri ya shibe haramu, wakaamini kwamba wao ndio wanawamiliki wananchi, wakawaambia wananchi na wakale majani bali wao lazima waishi maisha ya anasa. Umerithi nchi ngumu.

Simulizi ifuatayo unaikumbuka vyema. Hata hivyo, nitairejea ili nipate urahisi wa kusema ninachotaka kusema:

Mwezi Julai mwaka 1974 niliondoka Dar es Salaam kwenda Algiers, Algeria kufanya kazi makao makuu ya Umoja wa Vijana wa Afrika. Siku chache baada ya kuwasili Algiers, niliondoka kwenda Bucharest, Romania, kuhudhuria mkutano wa vijana wa dunia kuhusiana na Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya Idadi ya Watu (UN Conference on Population).

Nilipofika hotelini niliambiwa na wenyeji wangu kwamba kulikuwa na mjumbe kijana kutoka Tanzania akiwakilisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nami nikawa na shauku ya kumwona kijana huyo. Ilikuwa ni miaka miwili tu tangu nilipoondoka chuoni hapo, na nilikuwa bado na mapenzi makubwa kwa shule yangu, kwa hiyo nilikuwa na hamu ya kukutana na mwakilishi wake.

Tulipokutana na kijana huyo nilimkuta ni kijana mcheshi, mwenye haiba ya kupendeza na mwenye uwezo wa kujieleza vizuri na kwa ukweli. Siku chache tulizokaa pamoja mjini Bucharest zilinifanya nivutiwe na kijana huyu, hasa katika mijadala mikali katika mkutano, kama ilivyo siku zote katika mikutano ya vijana wa dunia, ambao wana mawazo ya kila aina yanayokinzana kwa ari na jazba.

Labda niseme tu kwamba jambo moja pekee lililoniudhi kuhusu kijana huyo ni kwamba alikuwa bado anashangilia ushindi wa timu ya Yanga dhidi ya Simba katika mechi ya kihistoria iliyochezwa siku chache kabla katika Uwanja wa Nyamagana, mjini Mwanza. Siku hizo nilikuwa bado shabiki mkubwa wa mambo haya, na kijana huyo hakuisha kunicheka kila alipopata mwanya.

Mbali na hilo, tulipatana sana, kiasi kwamba nilipoondoka nchini Romania na kuwasili Algiers nilipofungua mkoba wangu niligundua kwamba niliondoka na pasi yake ya kusafiria, jambo ambalo lilinihamanisha hadi pale nilipopata njia ya kuirudisha Bucharest, ambako yule kijana alikuwa kakwama, hawezi kuondoka kurudi Tanzania. (Nilijiuliza baadaye kama kijana huyo angeweza kudhani kwamba kuondoka na pasi yake ilikuwa ni njia ya kumwadhibu kwa ushabiki wake wa Yanga!)

Kijana huyo wa Bucharest aliitwa Jakaya Mrisho Kikwete. Miaka kadhaa iliyopita nilikuomba unikumbushe ilikuwa vipi hadi nikaondoka na pasi yako, ukasema ni kwa sababu wewe hukuwa na mkoba, na ulikuwa unatembea na pasi yako mfukoni, nami nikajifanya Msamaria Mwema kwa kukutunzia.

Baada ya hapo tulipata fursa kadhaa za kukutana, katika mikutano ya Umoja wa Vijana wa Afrika na kwingineko. Tumefanya kazi pamoja bungeni na ndani ya Halmashauri Kuu ya CCM, na kwa wakati wote nilipokujua umekuwa mtu yule yule niliyekutana naye mjini Bucharest, uchangamfu ule ule, uungwana ule ule, ujasiri ule ule wa kusema unaloliamini.

Hujabadilika, na wala nyadhifa mbalimbali ulizozishika hazijaathiri haiba yako ya asili. Kwa hili nakupongeza, kwa sababu katika mazingira yetu tumewaona watu waliojitutumua na kupandisha mabega kwa sababu tu wamepewa cheo kidogo – ukuu wa wilaya, unaibu waziri, au uwaziri. Ghafla huumuka kama vile wametiwa hamira na kutaka waabudiwe na wapewe enzi wasizostahili. Wewe umeshinda katika hilo.

Lakini bado. Mtihani mgumu kuliko yote uliyowahi kuipitia unaanza baada ya kushika madaraka ya juu kabisa nchini. Nafasi ya urais katika nchi yetu (na nchi karibu zote za Afrika) ni nafasi inayompa mtu mmoja uwezo mkubwa mno ambao wakati mwingine unamfanya aonekane kama vile mungu-mtu. Haishangazi kwamba baadhi yao hushikwa na kiwewe, wakawa wendawazimu kabisa.

Huu ndio mtihani wako mkubwa. Hutakuwa na nakisi ya watu watakaotaka kukushawishi nawe uwe kama watawala wengine wa Afrika, kwa maslahi yao. Hii ni kwa sababu nafasi uliyo nayo inakupa uwezo wa kumjenga huyu au kumbomoa yule kwa njia mbalimbali. Watu wengi mno wanajua kwamba chakula chao kitatoka moja kwa moja mezani kwako. Baadhi yao ni wale ambao uteuzi wao unakutegemea wewe moja kwa moja au kupitia watu wengine uliowateua.

Katika miezi michache ijayo utakuwa unateua mamia ya watu wa kukusaidia katika nafasi mbali mbali, na sina shaka kwamba watu tayari wanapigana vikumbo ili wateuliwe katika nafasi hizo. Katika kupigana vikumbo huko, watajipendekeza kwako au kwa watu walio karibu yako, watapakana matope na kupikiana kila aina ya majungu, alimradi wapate "kula" yao kutoka kwako.

Ni "kula" kwa maana zaidi ya moja. Kwanza serikali ndiyo tajiri mkubwa kuliko wote, ndiyo inatoa ajira nyingi kuliko sekta nyingine yo yote. Pili, ajira ya serikali katika nafasi fulani inaleta uhakika wa kipato na maisha yenye neema-malazi, usafiri, masurufu kem kem. Tatu, kwa wale ambao si waaminifu (na hawa si wachache) ajira serikalini inatoa mwanya wa "kujitengeneza", kwa maana ya kutumia cheo kwa manufaa ya mtu binafsi.

Nakuombea busara, subira na uvumilivu. Nakuombea upate uwezo wa kuwasikiliza wote watakaokuletea taarifa kuhusu huyu au yule bila kulazimika kuwaamini wote. Wengi wao ni waongo, wanafiki na wazandiki.

Sina ubavu wa kukufundisha lo lote katika medani ya majungu kwa sababu wewe mwenyewe umekuwa mhanga wa majungu kwa kipindi kirefu katika awamu iliyopita. Ni matumaini yangu kwamba ujasiri ule ule uliokuwezesha kuyashinda majungu dhidi yako utakusaidia katika kupima na kusaili kila unaloambiwa.

Ofisi unayoiendesha ni nyumba ya upweke mkubwa, na bila shaka kama mtu uliyezoea kuchanganyika kirahisi na watu upweke huo utakupata. Wale wachache watakaokuwa na fursa ya kukukaribia mara kwa mara watakuwa ni watu adimu hapa mjini, nao watatafutwa kama lulu na wale wote wanaotaka kupata cho chote kutoka Jumba Kuu.

Watanzania watakuwa wanakuombea dua zote ili uwe kiongozi mwema kama vile ulivyokuwa binadamu mwema. Mwanafalsa mmoja aliwahi kusema kwamba haiwezekani kutawala kwa haki. Labda hili ni kweli, kwa sababu si dhima ya mtawala kutenda haki, lakini kiongozi hana budi kuongoza kwa haki.

Naamini kwamba iko tofauti kubwa katika utawala na uongozi, na kwamba wewe katika ngwe hii ya mwisho utakuwa kiongozi zaidi kuliko mtawala, kwa sababu hiyo ndiyo silika yako, kwa sababu wewe ni muungwana.

Kwa kuwa kuongoza ni kuonyesha njia, tuongoze, basi, kwa kutufundisha. Mojawapo ya mambo mengi unayotakiwa kufanya katika uongozi wako ni kuwa mwalimu wa Taifa zima. Lakini papo hapo itabidi wewe mwenyewe uendelee kujifunza sana kuhusu watu wako na matatizo yao. Kwa jinsi hii wewe kama mwalimu na sisi kama wanafunzi tutakuwa tunajazana maarifa na hekima.

Mojawapo ya mambo yaliyonifurahisha katika matamshi yako ni lile la kuwataka watendaji wako wasije wakakosea kwa kudhani sura yako ya tabasamu ni dalili ya udhaifu. Na kweli wasije wakarogwa wakaamini hivyo.

Sote tulishuhudia mwaka 1995 ulipochukua hatua isiyokuwa ya kawaida ya kutamka hadharani kwamba Katibu Mkuu wa CCM alikuwa hawatendei haki wagombea wote kwa sababu alikuwa anampendelea mmoja wenu.

Ulisema hayo huku ukitabasamu ingawaje yalikuwa maneno mazito. Mwaka 2003, ulipoona umezidi kuonewa na kuchimbwa uliamua kuchukua ukumbi katika kikao cha juu cha chama chako na kusema kwamba unaonewa, wazi wazi, bila kumung'unya maneno wala kumwonea haya mtu. Sikuwapo, lakini naamini kwamba hata siku hiyo ulikuwa unatabasamu. Kwa hiyo endelea kutabasamu huku ukifanya mambo mazito kuliongoza Taifa lako. Na kama Mungu kakujalia tabasamu zuri kwa nini unune ili kuonyesha kwamba u makini?

Wako watawala wanaoamini kwamba kukunja uso, kuonyesha hasira na kuwafokea wananchi ndizo njia za kuonyesha umakini. Hawa ni wale ambao pia hushindwa kutambua kwamba ukatili si dalili ya uimara wa utawala bali ni uovu tu. Ama kwa hakika wengine huficha udhaifu na woga wao kwa kujivisha sura za kutisha na kuazima sauti za kufoka. Halafu wanawafokea wananchi, ambao tunaambiwa ndio waliowaweka madarakani.

Bila shaka utahitaji kufoka mara moja moja, lakini mfoko huo unatakiwa uwahusu watendaji na wasaidizi wako waliozembea katika utendaji. Kuwakaripia wananchi na kuonyesha dharau kwao si uungwana na wala hakuonyeshi uelewa mzuri wa mahusiano baina ya kiongozi na raia wake. Baadhi ya watu utakaowateua katika Baraza la Mawaziri wanaweza kuwa ni wale tuliowahi kuwasikia wakiwabeza wananchi kwa kuwaambia watakula majani alimradi matakwa ya wakubwa yatimizwe, au kuwaambia wale wanaohoji uuzaji wa nyumba za Serikali kwamba wanalia wivu. Ni matumaini ya watu wengi kwamba kuropoka kama huko hakutavumilika chini ya uongozi wako, na kwamba utamkaripia ye yote atakayethubutu kutoa matamshi hayo yanayodhihirisha utovu wa nidhamu.

Lakini kama nilivyosema awali, timu inacheza jinsi ilivyoelekezwa na kocha. Iwapo kocha kailekeza timu yake ipige "daluga" itafanya hivyo, hasa iwapo wachezaji watamwona kocha mwenyewe kamkwida refa au mchezaji wa timu pinzani. Kuwa mwema, ukiondoka raia wakujutie.

Itaendelea.



My Take:

Sio kwamba jenerali hajui kinachoendelea...Ila huyu bwana anaijua hii nchi kwa uunje wake na undani wake, kuanzia viongozi wake, Rasilimali zake na watu wake kwa ujumla wake... na anajua kabisa vyovyote itakavokua bado JK atatuongoza kwa maiaka mingine mitano.....So kwa kuljua hilo bado anajua maendeleo ya nchi hii bado yanamtegemea kikwete....so bado kikwete atahitajika kuwa mkombozi wa wanyonge ambao ndio wengi upo katika kundi hilo........

Hapo amemuelezea Kikwete kwa uhalisia wake na kwa jinsi nilivyomuelewa ni kuwa JK wa Uhalisia sio jinsi alivyo kwa sasa..... yeye alimfahamu JK since 70's...So anamtaka yule JK wa 70's awe JK wa sasa.....Kifupi sioni ubaya wowote wa barua hii......
 
Twaha Ulimwengu alipanda cheo katika medani ya habari na kuwa four-star General. Sasa anaporomoka na kuwa foot soldier, juzi aliandika lead story kwenye East African kama special correspondent!! Yaani from editor-in-chief of leading media house to a newspaper correspondent. Hii ya barua kwa JK nadhani anajipendekeza... amerudia hadithi ya walivyokutana Bulgaria, hivi kweli JK na English yake ilivyopinda na hoja nyepesi hali ilikuwaje alivyokuwa kijana hajapata exeperice? Bulgaria huko aliongea nini? ahahahahaha

U misunderstood the guy....reread his letter then u will understand.....Sidhani jamaa kwa jinsi alivyojijenga kiuchumi atahitaji chochote kwa JK anachohtaji nikuona JK anabridge gap btn the have's and dont have's....take ur time and reread that letter....make sure while rereading uwe stress free with political views....reflect maendeleo ya nchi hii.....
 
My take, hapa jenerali anataka kuanzisha mjadala mrefu, tulipotoka na tulipozamia. 2 step forwad, 2 backwards
 
Barua ndefu sana siwezi kusoma yote kwa hiyo sina cha kucoment

Nawe ipo siku utataka uwe kiongozi????? mvivu wa kusoma hata Kisahili????? lugha zingine je???? jenga utamaduni wa kujisomea broda........
 
Jana nilisoma katika safu hizi, barua ndefu iliyoandikwa na Jenerali Ulimwengu kwa JK. Nianze kwa kukiri kwamba barua ya aina hiyo hiyo, niliwahi kuiona katika gazeti la Rai ama mwishoni mwa mwaka 2005 au mwanzoni mwa mwaka 2006. Kwa maoni yangu,barua hii ilipotokea kwa hiyo mara ya kwanza, ilikuwa inastahili. Lakini kwasasa, kwa baadhi yetu barua hiyo inatia kichefuchefu, kwani inapindisha ukweli ulivyo. Mwaka 2005 wakati JK anaingia madarakani watu wengi tuliamini ya kwamba sasa tumempata mkombozi wa kweli, ambaye angeliondoa nchi yetu katika shimo la ukoloni mamboleo, ambamo ilitumbukizwa na utawala wa Mkapa, na kuielekeza katika njia ya uhuru kamili kiuchumi. Miaka mitano ya uongozi wake, imekuwa ni ya kukatisha tamaa kwa yeyote yule mwenye mapenzi mema na nchi yetu. Chini ya uongozi wake siyo tu kwamba nchi yetu imeendelea kupoteza rasilimali nyingi kwa uporaji na matumizi mabaya ya serikali, lakini pia kuna kila dalili zinazodhihilisha ya kuwa nchi yetu kama taifa imepoteza mwelekeo.Hali hiyo imesababisha watu wengi kupoteza imani waliyokuwa nayo kwa JK. Kwanini basi, mtu kama Jenerali, kwa wakati huu tulionao, anaamua kupindisha ukweli huo na kuaanza kumuita JK mkombozi! naomba kwa yeyote mwenye jibu anitegulie kitendawili hicho.



Hivi ni mwaka gani walisema Ulimwengu sio raia?
 
Mara nyingine nafikiria niweke blocking mechanism kwenye masikio yangu nisizisikie kabisa hizi kelele za siasa, ila nimeshindwa. Pengine sasa umefika wakati wa kufikiria namna nyingine ya kuongezea thamani ya maisha yangu na nchi yetu ya Tanzania.
Yanayoendelea nashindwa kuyaelewa kabisa, duuh!
 
Barua zanamna hii zinahitaji kuandikwa kwa watu wenye uwezo wakutafsiri fasihi simlizi vizuri vinginevyo sina uhakika aliye andikiwa barua hii na rafiki yake kama anamuda wa kuisoma na kuchukua maudhui yake nakuyaweka katika picha halisi.pia siamini kama ulimwengu analengo lakuleta mabadiriko yoyote katika taifa hili kupitia barua yake, kwa mfano ameomba msamahaa hata kabla aliyeandikiwa barua hajaisoma kana kwamba akimwudhi,je Ulimwengu unategemea usimwudhi?je hayo uliyo yaandika unategemea yawe na mtazamo chanya kwa huyo rafiki yako?lengo lako ni lipi? kukosoa, kushauri,kutoa mwelekeo au kueleza hali halisi iliyopo? kama lengo lako ni miongoni mwa hayo maswali una ombaje msamahaa?.
Pia unasema kama mheshimiwa rafiki yako atupilie mbali walaka wako kama ataona unamchosha kwa vile nimrefu.Hapo mantiki ya kuandiaka walaka wako ni nini? kama una mwandikia mtu walaka halafu hujari kama atasoma hivi lengo lako linakuwa ni lipi? hapa naona unatimiza wajibu wa nafsi yako lakini sidhani kama una nia dhabiti kama inavyo tafsiriwa nawengi

@kereng'ende
 
Mkuu nafikiri hujaelewa mantiki ya Ulimwengu kurudiaile barua aliyomwandikia JK mwaka 2006 mara tu ya Jk kula kiapo cha kuiongoza Tanzania.

Ukiielewa kwa makini utagundua kwa nini Ulimwengu ameamua kuichapisha tena barua hiyo kwenye toleo la Raia Mwema la wiki iliyopita.

Jaribu kufuatilia makala ama hata mijadala ya Jenerali Ulimwengu na utagundua ni mtu wa calibre gani!!
 
:nono: Hili la uraia haliwezi kumfanya mtu aandike hivi ama sivyo nadhani ange kaa kimya kabisa.Kuna kitu kinacho msukuma kwenye nafsi yake na ndicho anacho taka kukitimiza.
 
Twaha Ulimwengu alipanda cheo katika medani ya habari na kuwa four-star General. Sasa anaporomoka na kuwa foot soldier, juzi aliandika lead story kwenye East African kama special correspondent!! Yaani from editor-in-chief of leading media house to a newspaper correspondent. Hii ya barua kwa JK nadhani anajipendekeza... amerudia hadithi ya walivyokutana Bulgaria, hivi kweli JK na English yake ilivyopinda na hoja nyepesi hali ilikuwaje alivyokuwa kijana hajapata exeperice? Bulgaria huko aliongea nini? ahahahahaha
:smile-big::smile-big: Jamani muwe mnasoma alama za nyakati... wakati anaandika hiyo makala kwani wabunge wa kuteuliwa walishateuliwa??? kuna nafasi ya uwaziri wa habari pale.:smile-big:

Tuukirudi kwenye MADA, ni barua njema nzito na yenye maana PANA.
 
brooklyn
Acha polojo mtazamo wangu uko pelepale haijarishi alindika lini walaka huu kwa mara yakwanza. ukifanya kosa basi uendelee kufanya tena kwasababu una rudia? basi lako sipandi

@kereng'ende
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom