Kwa CCM hii, tutarajie kuona vituko vingi zaidi

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,082
Kwa CCM hii, tutarajie kuona vituko vingi zaidi

Johnson Mbwambo Juni 25, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

WIKI kadhaa zilizopita Jaji Joseph Sinde Warioba, alitamka katika mahojiano maalumu na gazeti hili kwamba viongozi wetu wa nchi ni dhaifu. Alikuwa akitoa maoni yake kuhusu namna matatizo mazito ya nchi yanavyoshughulikiwa na viongozi wetu; kuanzia yale ya ufisadi, kama vile EPA, hadi kwenye suala la mwafaka wa CCM na CUF.

Ilikuwa ni kauli nzito ambayo, bila shaka, Jaji Warioba alifikiria mara mbili au tatu kabla ya kuitoa. Ni kauli ambayo alijua mapema kabisa kwamba ingetafsiriwa vibaya na wanasiasa wasioitakia mema nchi yetu, na pengine kuitumia kumgonganisha na wengine.

Lakini pamoja na hatari hiyo kubwa, kero ya namna mambo yanavyokwenda; hususan suala la mwafaka wa CCM na CUF ilimkaba koo Jaji Warioba kiasi cha kuamua liwalo na liwe, na ndipo alipoitoa kauli hiyo ya kwamba viongozi wetu ni dhaifu.

Siku chache tu baada ya kuitoa kauli hiyo, kile alichohofia mapema kwamba kingetokea kweli kikatokea: Mkongwe mwenzake katika siasa, Kingunge Ngombale Mwiru akaitisha press conference na kumshutumu kwamba kauli aliyoitoa kuhusu mwafaka wa CCM na CUF, ilikuwa ni ya kukurupuka na kwamba (yeye Jaji) haijui vizuri CCM.

Hata hivyo Jaji Warioba, kiungwana kabisa, alimjibu Kingunge na wana CCM wengine wote wenye mtazamo kama wake, kwamba watakuwa njozini kama wanaamini kuwa CCM kina hodhi ya maoni, si tu ya wanachama wake, bali Watanzania wote.

Pengine shutuma hiyo ya Kingunge kwamba yeye Warioba haijui vizuri CCM, ndiyo kielelezo na ushahidi wa wazi kabisa wa jinsi chama hicho sasa kisivyothamini tena maoni au hoja mbadala za wanachama wake; na hiyo ni dalili ya wazi ya chama kukosa mwelekeo na viongozi makini.

Inapofika mahala mzee aliyekuwa kiongozi CCM kwa miaka mingi, na ambaye karibuni tu alikuwa Mshauri wa Rais wa Masuala ya Siasa, anamjia juu mtu anayeheshimika katika jamii kama Warioba kwa sababu tu ya kutoa maoni yake binafsi ya namna asivyoridhishwa na mambo yanavyokwenda, ujue kuna mushkeli mkubwa ndani ya chama hicho.

Si lengo langu kurudia kujadili ‘kituko' hicho cha Kingunge, kwa sababu wachambuzi wengine walishafanya kazi hiyo vizuri tu, lakini kinachonikera ni kwamba bado CCM inaiendeleza hulka hiyo ya kujaribu kuwaziba watu midomo kwa kuwatisha; na hivyo kuwanyima haki yao ya kimsingi ya kikatiba ya kutoa maoni yao.

Tushukuru tu Mungu kwamba kama ambavyo Jaji Warioba alivyokataa kuzibwa mdomo na Kingunge, vivyo hivyo wamejitokeza wabunge kadhaa wa CCM ambao nao wamekataa kufungwa na chama chao "kufuli" midomoni.

Nawazungumzia wabunge kama Aloyce Kimaro (Vunjo), Fred Mpendazoe (Kishapu), Stella Manyanya (viti maalumu), na hasa hasa mbunge wangu wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ambao wiki iliyopita walikataa kufungwa midumo na CCM na wakajenga ujasiri wa kulizungumzia suala la ufisadi bungeni; suala ambalo hakika chama hicho kinajaribu kulisukumia chini ya zulia.

Nilisisimshwa na mbunge wangu Anne Kilango; hasa pale alipowasihi wabunge wenzake wasiogope vitisho vya NEC. (Na wengi wametishika kweli kweli – kila mmoja sasa anafikiria ka-muhogo kake 2010!)

Bado nayakumbuka kichwani maneno mazito ya Anne Kilango Malecela wakati akichangia bajeti, Alhamisi iliyopita, Juni 19. Miongoni mwa mambo mengine, Mama huyo machachari alisema hivi: "Wabunge tusimame imara, tusiogope vitisho tukauachia utajiri wa nchi hii kwa kundi dogo…"Ni maneno machache lakini yaliyoeleza kila kitu.

Lakini nilitiwa zaidi moyo na maneno ya nyongeza ya Spika Samwel Sitta alipowaambia wabunge kwamba wana bahati ya kuongozwa na Spika asiyeogopa vitisho. Kauli hiyo ya Spika ni uthibitisho kwamba vitisho kwa wabunge wa CCM vipo, na vitaendelea kuwepo.

Kauli za wabunge hao niliowataja na kauli ya Spika Sitta, zimetolewa ikiwa ni siku chache tu baada ya kumalizika vikao viwili vya CCM mjini Dodoma – Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM kilichohudhuriwa pia na wajumbe wa NEC.

Habari zilizozagaa kote nchini ni kwamba vikao hivyo viwili vilitumika kujaribu kuwasafisha viongozi na wanachama wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi, na pia vilitumika kuwatisha wabunge wa CCM wasishupalie suala hilo la ufisadi bungeni wala kuwanyooshea vidole watuhumiwa hao wa kashfa za EPA, Richmond, Kiwira nk.

Nasema tushukuru Mungu kwamba pamoja na vitisho hivyo - pamoja na jaribio hilo la kuwasafisha mafisadi, bado tuna kina Anne Kilango, kina Fred Mpendazoe na kina Sitta ambao wamegoma kusutwa na dhamira zao, na hivyo wameamua kusimama kidete kupigania haki za Watanzania; hususan masikini wanaoishi maisha ya mateso vijijini.

Kwa mtazamo wangu, chama hiki CCM kinahitaji mageuzi makubwa; kwa sababu katika historia yake hakijawahi kupata uongozi dhaifu kama kilionao hivi sasa. Na ushahidi kwamba kimekuwa dhaifu kupindukia ni matukio kama hayo ya kujaribu "kuzificha chini ya zulia" tuhuma za ufisadi zinazowaandama baadhi ya wanachama wake maarufu.

Badala ya kuzishughulikia tuhuma hizo kikamilifu na kujisaficha, Chama kinajaribu kuwasafisha watuhumiwa, na pia kinajaribu kuwaziba midomo na kuwatisha wanachama wengine wenye ujasiri wa kukikosoa kwa hatua hiyo.

Mara nyingi vitisho ni mbinu ya mwisho kabisa inayotumiwa na mtu au asasi ambayo ni dhaifu. CCM ni dhaifu, na ndiyo maana hoja hazijibiwi kwa hoja bali kwa vitisho.

Hebu fikiria chama ambacho mjumbe wake wa Kamati Kuu (Andrew Chenge) amekiri mwenyewe kwamba ana akaunti ya dola milioni moja katika benki iliyoko katika kisiwa kimoja Uingereza ambacho ni maarufu kwa kupokea pesa chafu, lakini bado hashinikizwi na vikao vya juu vya CCM kujieleza alipata wapi pesa hizo; achilia mbali kwamba anachunguzwa na asasi ya nje kwa ufisadi.

Hebu fikiria chama ambacho mtu huyo huyo (Chenge) anayechunguzwa kwa ufisadi na asasi ya nje, bado anaachwa aendelee kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na mjumbe wa Kamati ya Maadili ya NEC ; tena hata baada ya tuhuma za hivi karibuni za madai kwamba kamera za bunge zilimnasa akifanya vitendo vya ushirikina bungeni! Hivi huyu anaweza kusimamia maadili gani ndani ya CCM?

Hivi ni mpaka kiongozi atende maovu gani mengine makubwa au aandamwe na tuhuma zipi nzito zikiwemo za kimataifa (ya rushwa ya rada ni ya kimataifa) ndipo CCM impumzishe pembeni?

Fikiria chama ambacho mmoja wa watuhumiwa wakubwa katika kashfa ya ufisadi anakuwa na ujasiri (audacity) wa kusimama kwenye kikao cha Chama na kumtetea mtuhumiwa mwenzake wakati yeye mwenyewe si safi hata kidogo!

Yaani CCM imefika mahali ambapo mafisadi kwa mafisadi wanateteana wenyewe kwenye vikao vya Chama, na mwisho wa yote kikao kinamalizika bila maazimio yoyote, bila hatua zozote… ni business as usual. Kilikuwa ni kikao cha kupiga soga?

Hebu fikiria chama ambacho Katibu Mkuu wake, Yusuf Makamba anatoa kauli katika vikao vya juu vya chama kutetea vituko vya watuhumiwa wa ufisadi kukimbilia majimboni na kupokelewa kwa shangwe na vifijo – mapokezi ya mbwembwe yenye baraka zote za CCM mkoa!

Chama chenye kiongozi mkuu anayediriki kuhalalisha vitendo kama hivyo vya kuwaenzi watuhumiwa wa ufisadi wanaokitia aibu, ni chama kinachokejeli uwezo wa kufikiri wa si tu wanachama wake; bali Watanzania wote. Na malipo ya kejeli hizo yanaweza kuonekana kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Hebu fikiria chama ambacho wiki hiyo hiyo, mwenyekiti wake mmoja wa mkoa anatuhumiwa kushiriki katika biashara haramu ya nyara za serikali, na bado kwa uongozi wa Chama wa kitaifa, hiyo si issue.

Kwa hakika, ninapotafakari suala hili ndivyo ninavyozidi kukubaliana (tena na tena) na kauli ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka kwamba sasa kuna madaraja mawili ya wanachama katika CCM – Wasiogusika na Wanaogusika ("CCM A" na "CCM B"). Wasiogusika ni kama huyo Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, ni kama watuhumiwa wa kashfa za Richmond, EPA na Kiwira, ni kama kina Chenge na wengine wengi. Wanaogusika ni kina Lekule Laizer, Elissa Mollel na kina Abiud Maregesi na wengine wengi.

Hapa ndipo CCM ilipofikishwa na uongozi wake dhaifu wa sasa. Na kosa kubwa inalolifanya, hivi sasa, ni kujaribu kuzinyamazisha sauti hizi chache za kina Anne Kilango zinazojaribu kueleza ukweli na zinazojaribu kukizindua Chama usingizini.

Na kama chama hiki hakitazinduka kutoka katika usingizi mzito uliotokana na madawa ya usingizi kiliyonyweshwa na mafisadi, tutarajie kuona vituko vingi zaidi ndani ya CCM huko mbele ya safari!

Tafakari.

Email: mbwambojohnson@yahoo.com
 
Kwa CCM hii, tutarajie kuona vituko vingi zaidi

Johnson Mbwambo Juni 25, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo


Kwa mtazamo wangu, chama hiki CCM kinahitaji mageuzi makubwa; kwa sababu katika historia yake hakijawahi kupata uongozi dhaifu kama kilionao hivi sasa. Na ushahidi kwamba kimekuwa dhaifu kupindukia ni matukio kama hayo ya kujaribu “kuzificha chini ya zulia” tuhuma za ufisadi zinazowaandama baadhi ya wanachama wake maarufu.

Naam, huo ni ukweli usiofichika.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom