Kuzama Mv Skagit, ziri nzito yafichuka *Yadaiwa usalama wake ulikuwa mdogo *Serikali Z'bar yabebeshw | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kuzama Mv Skagit, ziri nzito yafichuka *Yadaiwa usalama wake ulikuwa mdogo *Serikali Z'bar yabebeshw

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Jul 21, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Jul 21, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  [h=2]20 JULY 2012[/h][h=3]Kuzama Mv Skagit, ziri nzito yafichuka *Yadaiwa usalama wake ulikuwa mdogo *Serikali Z'bar yabebeshwa lawama *Maiti 58 zaopolewa, 128 wanasakwa *Bunge laomboleza, bendera nusu mlingoti siku 3[/h]  Na Benedict Kaguo, Dodoma

  MBUNGE wa Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bw. Haji Khatib Kai (CUF), amefichua siri nzito ya kuzama meli ya Mv Skagit na kudai kuwa, tayari ilifungiwa isifanye kazi ya kubeba abiria kutokana na ubovu uliokithiri lakini wamiliki wake wameihonga fedha Serikali ili iendelee na kazi.


  Akizungumza na Majira jana, Bw. Kai alisema katika ripoti ya uchunguzi wa ajali ya Meli ya Mv Spice Islander I, ambayo ilizama miezi 10 iliyopita, tume iliyoundwa ilitoa mapendekezo kadhaa likiwemo la kuzuia meli zinazomilikiwa na Kampuni ya Seagul ikiwemo Mv Skagit (iliyozama) na kusababisha vifo.

  Alisema inasikitisha kuona meli hiyo imeachwa ifanye kazi ya kubeba abiria wakati uchunguzi tume ilishaagiza meli za kampuni hiyo zifungiwe kwa sababu zimekuwa zikizima na kupoteza uelekeo baharini.

  “Inavyoonekana, wamiliki wa kampuni hii wametoa hongo ili meli zao ziruhusiwe kubeba abiria hata kama hazifai hivyo ajali hii ilitegemewa kabisa kwa siku za usoni na kuua watu wasio na hatia.

  “Tukio hili si la bahati mbaya kwani tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa ilishatoa tahadhari juu ya kuchafuka kwa bahari, iweje meli hii iruhusiwe kuondoka kwenda Zanzibar kwa sababu ya kutaka fedha na kusababisha maafa kama haya,” alihoji Bw. Kai.

  Kwa Upande wake, Mbunge wa Konde, Bw. Khatib Said Haji (CUF), alisema ajali hiyo ni matokeo ya Serikali kushindwa kuchukua hatua stahiki za kulinda maisha ya raia wake.

  Alisema Zanzibar ni visiwa hivyo kwa vyovyote Serikali ilipaswa kuweka mfumo mzuri wa vyombo vya usafiri majini lakini imekuwa ikifumbia macho hali hiyo kwa kisingizio cha ufinyu wa bajeti.

  “Ni takriban mwaka mmoja tangu janga kama hili litokee, ilikuwa fundisho kwa Serikali ambayo ilipaswa kuchukua hatua stahiki za kuokoa maisha ya watu...hii ni makusudi ya Serikali kutochukua hatua ili kulinda maisha ya raia wake,” alisema.

  Aliongeza kuwa, kitendo cha Serikali kutolinda raia wake kwa kisingio cha ufinyu wa bajeti, umefika wakati wa Baraza la Wawakilishi liiwajibishe Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

  “Majanga kama haya yanawafanya wananchi wapoteze imani na Serikali yao kwani tunakumbusha makovu ya ajali ya mwaja jana ambayo watu hawajaisahau,” alisema.

  Mbunge wa Kisarawe, Bw. Suleiman Jaffo (CCM), alisema wanaohusika na vyombo vya majini wawajibike kwa kashfa hiyo kabla ya kusubiri wananchi kuwanyooshea vidole.

  Alisema uzembe wa usimamizi wa vyombo vya majini unaonekana kuota mizizi ambapo Serikali bado haijaweza kuweka mkakati wa kukabiliana na majanga.

  Mbunge wa Viti Maalumu Bi. Magdalena Sakaya (CUF), alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuivunja Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), kwani imeonesha kushindwa kusimamia vyombo vya majini hivyo kusababisha maafa.

  Alisema viongozi wa SUMATRA, wameshindwa kazi na kutilia shaka uteuzi wao kuwa huenda haukizingatia sifa ila masuala ya kisiasa ndio maana wanashindwa kutekeleza majukumu yao.

  “Watu wanasafirishwa kama magogo, hakuna usimamizi makini, Serikali imekuwa ikichukulia mambo kirahisi tu…ajali za Mv Bukoka, Mv Spice Islander I, zilitosha kabisa kuwa fundisho,” alisema Bi. Sakaya.

  Mbunge mwingine wa Viti Maalumu Bi. Christowaja Mtinda (CHADEMA), alisema ajali hiyo imechangiwa na Serikali kutosikiliza ushauri wa wabunge.

  “Kwa muda mrefu wabunge wamekuwa wakilalamikia vyombo vya usafiri kama ndege na meli lakini Serikali bado inarudusu kuingizwa mitumba, wakati tunapitisha Sheria ya Manunuzi, tulikataa vyombo vya mitumba visinunuliwe kwani haya ndio madhara yake iwe kwa watu binafsi au serikalini, tununue meli mpya sio mitumba,” alisema.

  Alisema meli hiyo inapandwa na wananchi wa kipato cha chini kutokana na ubovu wake ambapo Serikali imekuwa ikiona na kushindwa kuchukua hatua.

  Spika Makinda aahirisha Bunge

  Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda, jana ameahirisha kikao cha bunge na kueleza kuwa, posho za wabunge wote zitapelekwa kwa waathirika wa ajali ya Meli ya Mv Skagit, iliyozama juzi eneo la Chumbe Zanzibar, kama rambirambi.

  Bi. Makinda alitangaza uamuzi huo baada ya wabunge kuingia ukumbini, kusomwa dua ya kuliombea Bunge na kumwita Waziri wa Nchi, Sera Uratibu na Bunge, Bw. William Lukuvi, ambaye alitoa taarifa ya Serikali kuhusu tukio la kuzama kwa meli hiyo.

  Alisema taarifa za awali hadi kufikia juzi jioni, zinasema meli hiyo ilibeba abiria 290 ambapo kati ya hao, watu wazima walikuwa 250, watoto 31 na wafanyakazi tisa wa meli hiyo.

  Aliongeza kuwa, hadi jana asubuhi watu waliokuwa wameokolewa wakiwa hai ni 146 ambapo jumla ya maiti 31, ziliopolewa na zote zimetambuliwa na ndugu zao.

  Bw. Lukuvi alisema, miongoni mwa waliookolewa wako watalii 16 ambapo mmoja aliopolewa akiwa amekufa na watu wengine 113 wanaendelea kutafutwa ambapo shughuli za uokoaji zilisimama
  jana kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa baharini.

  Kutokana na tukio hilo, Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo na bendera zote zitapepea nusu mlingoti na kuwataka wakazi wa Bara, wafike Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kupata taarifa za ndugu zao waliokuwa katika meli hiyo.

  Baada ya taarifa hiyo, Bi. Makinda alisemama na kueleza kuwa tangu kutokea kwa ajali hiyo juzi, wabunge 18 walisafirishwa kwenda Zanzibar kuungana na wananchi na kundi jingine la wabunge limeondoka jana.

  “Tulidhani kutakuwa na mazishi ya halaiki lakini Serikali ya Zanzibar imesema bado kwani maiti nyingi zimetambuliwa na ndugu zao na idadi ya watu ambao bado hawajapatikana ni kubwa.

  “Kwa hali hiyo, hatuwezi kukwepa kuwepo kwenye mazishi ya
  halaiki...sasa naahirisha bunge hadi kesho saa tatu asubuhi,” alisema.

  Nje ya ukumbi wa Bunge, Bw.Lukuvi alikutana na waandishi wa habari na kuwasilisha taarifa ya Rais Jakaya Kikwete ambaye ametoa salamu za rambirambi na kuwataka wananchi wawe na subira wakati huu ambao kazi ya uokoaji inaendelea.

  Alisema uchunguzi wa kina wa tukio hilo unafanyika ili ifahamike nini kilichangia ajali hiyo ambapo kazi ya uokoaji bado inaendelea kufanywa na kwa ushirikiano wa Vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), KMKM, Polisi na wananchi.

  Alisema taarifa za watalii hao zinaendelea kufuatiliwa kwani hadi sasa haijafahamika ni raia wa nchi gani.

  Maiti zaidi zapatikana

  Hadi jana jioni, miili ya watu 58 ilipatikana baada ya kuopolewa katika eneo la tukio kukiwa na matumaini ya kupatikana wengine 124, ambao hadi sasa hawajulikani walipo.

  Juhudi za kuokoa abiria waliozama, jana ziliingia siku ya pili. Mwandishi wetu aliyepo Zanzibar, alisema kazi ya uokoaji bado inaendelea ingawa hadi jana jioni hakuna aliyepatikana akiwa hai.

  Mganga Msaidizi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar, Dkt. Abdurahaman Khalfan Said, alisema juzi walipokea majeruhi 145, wa ajali hiyo kati hao, 22 ndio wanaoendelea na matibabu ambapo wengine walitibiwa na kuondoka.

  Alisema kati ya watu walioruhusiwa baada ya kupata matibabu, sita hawana ndugu Zanzibar, hivyo wanaendelea kubaki hospitalini hapo wakati taratibu zingine zikiendelea.

  Dkt. Said alisema walipokea miili ya watu 20, mmoja alikuwa raia wa Israel, wawili Tanzania Bara na mmoja Mwera, Unguja.

  Katika hatua nyingine, yalitokea malalamiko ya wapigambizi wa kujitolea wakidai kuwa wameshindwa kwenda eneo la tukio kutoa msaada kutokana na kukosa mafuta.

  Kwa upande wa wananchi, baadhi yao wameilalamikia Serikali kwa kuchelewa kupeleka waokoaji eneo la tukio kwa sababu ya kuchelewa kupatikana kwa mafuta.

  Walitoa mwito kwa Serikali kuhakikisha matukio ya ajali za aina hiyo hayatokei tena.

  SUMATRA yatoa taarifa

  Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), jana imetoa ufafanuzi wa ajali hiyo.

  Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisa Uhusiano wa SUMATRA, Bw. Devid Mziray, alisema meli hiyo inamilikiwa na Kampuni ya Seagul Transport.

  Alisema usajili wa meli hiyo ulifanyika katika Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) na ina uzito wa (GRT) 96.

  Aliongeza kuwa, cheti cha ubora wa meli hiyo kimepatikana Agosti 24, 2011, kinamalizika Agosti 23, 2012 na ina uwezo wa kubeba abiria 300 wakati mizigo ni tani 26

  “SUMATRA kupitia Kituo cha Utafutaji na Uokoaji-MRCC, ilipata taarifa kuwa meli hii ambayo ilikuwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, inazama kwenye karibu na Kisiwa cha Chumbe, Zanzibar, eneo ambalo lipo umbali wa kilomita za bahari 13.8 kutoka Bandari ya Zanzibar,” alisema Bw. Mziray.

  Alisema baada ya kupata taarifa hizo, kituo cha MRCC kilitoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama na vyombo vya usafiri majini ambavyo vilikuwa karibu na eneo la tukio.

  Bw. Mziray alisema meli hiyo iliondoka bandari ya Dar es Salaam saa 06.05 mchana ikiwa na abiria 248, watoto 31 na mabaharia tisa kwa mujibu wa orodha ya abiria.

  Taarifa za ajali hiyo zilisambazwa kwa wadau mbalimbali wakiwamo Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Kikosi cha Polisi cha Maji, Kikosi cha Wanamaji, Vituo vya Ishara Zanzibar (Signal Station) na Shirika la Bandari Zanzibar.

  “Kazi ya uokoaji inaendelea katika eneo la tukio kwa msaada wa vyombo mbalimbali zikiwamo boti za Mv Flying Horse, Mv Kilimanjaro III, Tug Bandari ya Zanzibar, KMKM, Mv Zanzibar I, Polisi, boti za doria, Kikosi cha Wanamaji na Kituo cha MRCC ambacho kinaendelea kufuatilia na kutoa taarifa ya uokoaji.

  Rais Kikwete atuma salamu

  Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi kwa Rais wa Serikali ya Mapiduzi Zanziba (SMZ), Dkt. Ali Mohamed Shein, kutokana na ajali hiyo ambayo imesababisha vifo na majeraha kwa Watanzania na raia wa kigeni.

  “Huu ni msiba wetu sote, majonzi yao ni majonzi ya Watanzania wote, kwa ndugu zetu waliojeruhiwa tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape ahueni na wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli za kujiletea maendeleo na kulijenga Taifa letu,” alisema Rais Kikwete katika taarifa yake.

  Alimpongeza Dkt. Shein na viongozi wote wa ngazi mbalimbali kwa uongozi wao thabiti tangu wapate taarifa ya ajali hiyo, maofisa, askari wa vyombo vya ulinzi na usalama na wafanyakazi wa meli binafsi kwa juhudi kubwa za uokoaji watu waliopatwa na maafa.

  Atamko wananchi wawe na moyo wa subira na uvumilivu wakati kazi ya uokoaji ikiendelea kama ilivyofanyika katika ajali ya Mv Spice Islander, miezi 10 iliyopita ambapo uchunguzi wa kina utafanyika kubaini chanzo cha ajali.

  Dkt. Shein azungumza

  Akizungumzia ajali hiyo, Dkt. Shein alisema tukio hilo ni msiba mkubwa kwa wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

  “Ni wakati mgumu kwetu sote, napenda kutoa mwito kwa watu wote tuwe na subira na wastahamilivu, huu ni wakati wa kufikiria ndugu na watoto wetu waliopoteza maisha na tuwatakie rehema za mola wetu,” alisema Dkt. Shein.

  Aliongeza kuwa, kwa niaba yake binafsi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, anatoa pole kwa wafiwa wote na anamuomba Mwenyezi Mungu awape subira.

  “Wale ambao bado hawajapata taarifa za watu waliokuwa katika safari hii, kuweni wavumilivu wakati juhudi za uokoaji zikifanyika, natoa shukurani zangu kwa wamiliki wa vyombo vinafsi vya bahari ambavyo vimeshiriki katika kazi za uokoaji maiti na wananchi.

  “Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasimamia gharama zote za mazishi ya watu waliokufa na kutoa huduma za afya, matibabu na nyingine kwa wote waliopata majeraha,” alisema na kuongeza kuwa kutokana na msiba huo, Serikali yake inatangaza siku tatu za maombolezi kuanzia jana.

  Tume ya Katiba yasitisha kazi

  Kutokana na tukio hilo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya imesitisha mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu iliyokua inaendelea katika Mkoa wa Kusini Pemba.

  Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilisema mikutano iliyositishwa ni ile iliyopangwa kufanyika kuanzia jana, leo na kesho katika maeneo ya Wawi, Vitongoji, Chanjamjawiri, Pujini, Gombani na Wara.

  “Tume imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya ajali hii na imesitisha mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya iliyokuwa inaendelea Mkoa wa Kusini Pemba,” ilisema taarifa hiyo.   
Loading...