Kuwasifu Nyerere na Mandela ni kazi rahisi kuliko kuwaiga

sulphadoxine

JF-Expert Member
Nov 1, 2010
2,257
644
NDANI ya kipindi cha miongo miwili sasa, Bara la Afrika limepoteza watu wawili ambao maneno na matendo yao, yanachochea udadisi ili kubaini kama kweli hao ni binadamu wa kawaida, au ni malaika walioshushwa toka mbinguni na Mungu kuwapa sura ya ubinadamu uliozoeleka machoni pa watu.

Tofauti na wengi wetu tunaosema hili midomoni, lakini mioyoni mwetu tukimaanisha lile, Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza na Mwasisi wa Taifa la Tanzania na Nelson Mandela, Mpigania uhuru wa Afrika na Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika ya Kusini, wao wamekuwa wakiishi juu ya viwango vya maneno adilifu waliyoyasema wakisisitiza haki, maelewano, msamaha na upendo wa kweli kwa wote. Kwangu mimi, nawaona Mandela na Nyerere walikuwa mapacha wasiolingana na kufanana kwa sura na umri, lakini mapacha wanaofanana na kupendana kutokana na imani zao haki, uhuru na utu unaofunikwa na mwavuli wa upendo usioruhusu ubaguzi.

Mandela na Nyerere nawatazama kama mapacha wa imani waliomuona Mungu maishani mwao, wakasikia sauti yake ndani yao na kutenda kadiri ya maagizo yake. Hawa, ni watu wa Mungu uwe usiku wa giza, au mchana wa mwanga. Kifo cha watu kama hao hasa viongozi wakuu na maarufu kama Nyerere na Mandela, mara nyingi ni simanzi kwa wengi hasa waadilifu, lakini waliao msibani ni wengi ingawa kila mmoja ana sababu ya kulia kwake katika msiba husika. Wapo wanaolia kwa sababu wamepoteza shujaa, mwadilifu na mpenda watu, lakini pia wapo wanaolia kwa sababu ya furaha maana huenda uadilifu wake ulikuwa kikwazo cha hao kufanya ukiukwaji wa maadili na hao, ndio huwageuza watu kama Mandela na Nyerere kuwa mitaji yao ya siasa jukwaani.

Hao, watasahau mambo yote yanayowapasa kuyafanya ili kumuenzi Nyerere au Mandela, lakini katu hawatasahau na daima wataendelea kila siku kusema, "Tumuenzi Nyerere/ Mandela kwa vitendo" lakini kwao, hayo ni maneno ya mdomoni ambayo hata kanga zinayo, lakini mioyoni mwao, kuna mengine. Hao, watazimimina kama maji ya bomba sifa za viongozi hao, lakini itakuwa ngumu kama ngamia kupenya tundu la sindano kusikia au kuona hao wakiiga uadilifu na uchapakazi wa hao wanaowasema. Mandela ana haki zote za kufa sasa kwani hata umri alioufikia unastahili kumshukuru Mungu.

Matunda ya uzao aliouacha duniani, ni Mungu pekee wa kumshukuru kwa maneno maana kama ni kitu, utamrudishia nini Mungu kwa ukarimu wake na kama ni utumishi, acha Mandela aende, ametumika vya kutosha na kwa namna sahihi inayohiari kujitoa kwa ajili ya faida ya wengine. Kwa vipimo vya ubinadamu, niseme kuwalilia Mandela na Nyerere ni kutowatendea haki kwani kwa utumishi wao, ni wazi wameitenda vema kazi waliyotumwa na Mungu na kutaka wachelewe kufa kama tungeweza, huenda tungewaweka katika vishawishi vya kuanguka.

Hivi unafikiri kama sio upendo na uadilifu wao na wenzao akina Nkwame Nkrumah na wengine, nani angelitetea Bara la Afrika? Nani angeitetea Tanzania mbele ya Mungu au nani angeitetea Afrika Kusini mbele ya Haki. Acha Nyerere na Mandela waende. Wamefanya kazi njema. Kifo cha Nelson Mandela maarufu kama Mzee Madiba, kimewaliza si Wana Afrika ya Kusini pekee, bali hata Tatanzania na dunia nzima na ndiyo maana Afrika Kusini sasa imetapakaa watu kutoka kona mbalimbali duniani wakiwamo viongozi maarufu duniani. Bunge la Jamhhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kumlilia Mandela limejikuta likitoa azimio la kumlilia shujaa huyo wa Afrika aliyefariki usiku wa Desemba 5, 2013 na mwili wake utapata pumziko katika kitanda chake cha milele Desemba 15, mwaka huu.

Akisoma Azimio hilo Jumamosi Desemba 7, 2013, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Edward Lowassa alisema, "Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaazimia kuungana na familia yake (Mandela), wananchi wa Afrika Kusini na dunia nzima katika kuomboleza msiba wa Hayati Mandela. Madiba amekufa, lakini ataendelea kuishi katika mioyo yetu kwa miaka mingi."

"Tuendelee kumuenzii kwa kuiga na kufuata nyayo zake za kuwa kiongozi mzalendo aliyeithibitishia dunia kujali utu na kuthamini wengine, mpigania haki na usawa kwa binadamu na kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi." Kifo cha Nyerere kilipotokea Oktoba 14, 1999 na kuukusanya ulimwengu mzima kuja na kuitazama Tanzania, zilitolewa ahadi nyingi zilizogeuka kuwa mtaji wa kisiasa na kibwagizo cha hotuba mbalimbali kuhusu kumuenzi Nyerere, lakini je, nani anamuenzi Nyerere?

Nani anaishi kama Nyerere? Nani anaongoza au kutumikia kwa moyo wa upendo wa dhati kama Nyerere? Nani anafuata nyayo za Nyerere? Nani anamuenzi kama sio tu kunukuu hotuba zake ikiwamo ile inayokemea rushwa anaposema enzi zao mtoaji na mpokeaji wa rushwa "bhonswe n' mabhi gha nyange" yaani wote ni mavi ya ndege waitwao nyangenyange.

Nani asiyependa hotuba hiyo kwa vile tu alisema aliyebainika alihukumiwa kifungo jela lakini siku ya kuingia alichapwa viboko 12 na siku ya kutoka akachapwa viboko vingine 12 ili akamuoneshe mkewe? Nanii anayaheshimu maneno hayo na kuikataa rushwa kwa dhati kama njia ya kumuenzi Nyerere? Kama hakuna, basi tusiomboleze kifo cha Mandela na kumdanganya "Mzee wa Watu" kwa hotuba na maneno mengi yanayoonekana kwa macho kuwa ni matamu, lakini kwa matendo mdomoni ni makali kama pilipili na machungu mithili ya mwarobaini.

Twendelee kuomboleza kama ilivyo ada wanadamu, lakini tujue kuwa kuwaahidi marehemu ahadi za uongo, ni kuwatesa na kuwaonea kama sio kuwanyanyasa kwa vile wamekufa. Hivi nani atafurahi siku akifa naye akanyanyaswa kama tunavyomnyanyasa Nyerere kwa maneno ya uongo na sasa tumemgeukia Mandela? Nani kweli atamuenzi Mandela kama ameshindwa kumuenzi Nyerere wa nyumbani kwa matendo? David Kafulila, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Magezu) amesema, "Tunahitaji watu wa aina yake (Mandela) ili walifanye taifa hili kuwa moja kama Mandela alivyoifanya Afrika Kusini."

Sawa Kafulila, lakini Kafulila anavyoiona Tanzania hii, nani mwenye upendo wa dhati kiasi hicho? Mfano, ni kiongozi gani ambaye hajaliwa na mchwa aina ya u-chama? Nani hajaliwa na mchwa na kupe aina ya u-dini? Viongozi wangapi hawajaliwa na mchwa ina ya u-kabila na u-majimbo? Nani anamuenzi Nyerere; nani atafuata nyayo za Nyerere na Mandela? Nani haoni namna hata ukabila unavyoanza kuitafuna nchi? Kwanini watu wakiwamo viongozi wa dini wamwagiwe tindikali, wapigwe risasi na kuua na wengine wakichinjwa mithili ya kuku huku makanisa yakichomwa kama mishikaki? Nani anaweza kuwaenzi Nyerere na Mandela? Nani? Kuwasifu Mandela na Nyerere kwa vile wamekufa, ni kazi rahisi na tamu, lakini kuiga matendo yao ni kazi ngumu kama chuma cha pua na yenye maumivu makala kama kung'oa jino au kucha bila sindano ya ganzi.

Hivi nani asiyeona hata namna tunavyoibaka demokrasia yetu kwa siasa za majitaka wakati zipo siasa za majisafi na zinawezekana? Tumeshindwa kumuenzi Nyerere wa nyumbani tutamuenzi Mandela wa jirani? Watanzania wote tangu ngazi ya uwayo hadi kilele cha nywele kichwani tunaimba kwa kibwagizo cha kumuenzi Nyerere, lakini nani anamuenzi Nyerere kama wawekezaji wanakuja nyumbani na kutuondoa kwa gharama ya machozi yanayoyeyushwa na jua na mengine kupotea kama yale ya samaki? Nani anamuenzi Nyerere?

Kumuenzi Nyerere kuna gharama zake bwana tusidanganyane msibani ili kumfariji maiti. Mwandishi Ani Jozeni ameandika katika Nipashe Jumapili iliyopita akisema, "Maisha ya Madiba (Mandela) ni kielelezo kuwa dhamira njema haileti faraja kwa walio na chuki, haiwainui mbele ya wenzao walio na chuki, lakini mikusanyiko yote ya wenye chuki huishia katika uharibifu na vilio. Huzaa udhalimu unaodumu kwani utawala unaojengwa katika chuki hujiinua kwa udhalimu, na hauwezi kuruhusu kundi lingine lianze kupitia majalada ya udhalimu wao."

Nani asiyejua kuwa barani Afrika hata mikataba yote ya kuuza au kununua vitu ni siri; siri dhidi ya nani na vinanunuliwa au mikataba ni ya nani? Nelson Mandela aliyezaliwa 1918 na kufariki 2013 amemfanya Rais wa Marekani Barack Obama katika moja ya hotuba zake mwaka 2012 aseme, "Kwa viwango vyovyote, Nelson Mandela ametengeneza historia, ameibadili Afrika na dunia kwa jumla…"

Ndiyo maana ninasema, Watanzania tumemdanganya Nyerere kwamba tutamuenzi, lakini hatufanyi hivyo japo tunaadhimisha kumbumbuku ya kifo chake hivyo, ni vyema tusimdannganye na Mzee Madiba, akaenda kaburini na matarajio mengi kumbe tunampiga changa la macho atoke maana, kuwasifu Mandela na Nyerere ni kazi rahisi kuliko kuwaiga kwa maneno na vitendo sahihi.
 
walikuja hapa duniani kwa malengo maalum, wameianzisha na kuwka misingi imara ya kazi walizoanzisha; Tanzania ilibidi isubili mpaka Nyerere aungane na Watz watangulizi ktk kudai uhuru wa Tanganyika, na mara ukapatikana

Vivo hivyo SA nayo iliendelea kusubili pamaja na harakati za wapigania uhuru wengi, mpaka Mandela alipokuwa huru na uhuru wao ukapatikana.

Kwangu ndo naona kama vile hawa watu walizaliwa waje waongoze hizi nchi kwani tayari baada tu ya kuondoka kwao,(achilia mbali kuaga dunia) madarakani tumeshuhudia watawala walioibuka na waliyoyafanya hadi kuzomewa ama mikutano yao kuwa ya kubembeleza watu wahudhurie hata kama ni kuwabeba ktk magari.

Wanasiasa wanawataja tu majina yao ili kujiongezea umaarufu kuwa wanautambua kuwa kulikuwa na utawala thabiti wa hao watangulizi. Hawawezi kuwaenzi ktk matendo yao kwa vile hawana hizo hisia zao juu ya maisha ya wananchi wao
 
Back
Top Bottom