Kuwa Mwanamziki miaka ya 70 ilikuwa ni Dunia nyingine kabisa

John Kitime

Verified Member
May 25, 2020
7
75
Leo nimekumbuka hali ilivyokuwa katikati ya miaka ya 70 wakati huo ambapo tayari nilikuwa mmoja ya wanamuziki kwenye kabendi ketu kadogo ka pale Iringa mjini. Kabendi kalikoitwa Iringa Jazz band lakini kutokana na mtindo wetu tuliouita Chikwala Chikwala, bendi iliishia kuitwa Chikwalachikwala kwa wapenzi wake. Nakaita kabendi kwa kuwa tulikuwa na magitaa mawili tu, gitaa la solo, gitaa la rythm na ngoma moja kubwa, vyombo hivi vilikuwa masalia ya vyombo vya bendi kubwa iliyowahi kuwa Iringa iliyoitwa Highland Stars, sisi tulijiona ni bendi kamili na kila Jumapili mchana kuanzia saa nane mpaka saa kumi na mbili jioni tulipiga muziki pale Iringa Community Center, wengi walioingia katika muziki huo walikuwa watoto wadogo kwa kiingilio cha senti 30 tu .

Sikumbuki kwa nini tulijita Chikwala chikwala lakini miaka hiyo kama ilivyokuwa kawaida miaka ile tuliiga namna ya kuita majina ya bendi au mtindo wa bendi kwa jina kujirudia mara mbili. Hii ilitokana na kuiga bendi za Kongo maarufu wakati ule, za Orchetra Bela bela na Orchestra Lipua lipua. Bendi nyingi hapa nchini ziliga mtindo huo, kulikuwa na bendi kama Orchestra Zela Zela, Vina Vina na bendi ya polisi ikawa na mtindo wa Vanga Vanga, bendi ya Idara ya Uhamiaji ikawa na mtindo wa Hama Hama, wakati Vijana Jazz Band walikuwa na mtindo wao wa Koka Koka na kadhalika.

Madansi ya mchana yalikuwa maalumu kwa watoto, pombe hazikuruhusiwa, na dansi hilo maarufu kwa jina la bugi lilikuwa likianza kati ya saba au saa nane, na mara nyingine siku za siku kuu dansi lilianza hata saa sita mchana na ilikuwa lazima liwe limekwisha kufikia saa kumi na mbili jioni. Mara nyingi baada ya dansi kama hili tulienda kupumzika na kisha kurudi usiku kwa ajili ya dansa la usiku ambalo lilikuwa la watu wazima.

Hakika muziki tuliopiga wakati huo tuliupiga tu kutokana na mapenzi ya muziki, kipato kilikuwa kidogo sana, na mara nyingi pesa zilizopatikana zilitumika kununua nyuzi za magitaa na vifaa vingine vidogo vidogo ili kuhakikisha bendi inaendelea kupiga. Msaada mkubwa ulikuwa pia unatoka kwa Afisa Utamaduni wakati huo, tukikosa chombo chochote tulikuwa tunamuendea nae aliweza kufanya jitihada ya kuweza kututafutia, hata ukumbi tuliokuwa tukipiga ambao ulikuwa wa serikali, haukuchukua fedha zozote zaidi ya pesa kidogo kusaidia malipo ya umeme, Afisa Utamaduni alikuwa msaidizi mkuu wa wasanii.

Bendi yetu ilikuwa pia inafanya ziara kwenye vijiji mbalimbali vilivyoizunguka Iringa, tulisafiri tukiwa na jenereta na kuweza kupiga katika maghala matupu ya mazao ambao yalikuwa kwenye vijiji mbalimbali. Maghala hayo pia yalikuwa ndio sehemu ya kulala baada ya kumaliza dansi. Safari za vijijii zilikuwa na manufaa kwani tulizawadiwa mazao mbalimbali na wapenzi wa muziki, bendi ilikuwa ikirudi mjini ikiwa na magunia ya mahindi, maharagwe na mazao mengine.

Karibu kila mwanamuziki alikuwa na kazi yake nyingine, mimi nilikuwa mwalimu, kulikuweko na fundi saa, fundi baiskeli, wafanyakazi wa serikalini na kadhalika, hii ilituwezesha kuendelea kupiga muziki japokuwa ulikuwa hauleti kipato chohcote.

Siku muhimu kwa bendi ilikuwa na siku ambazo bendi kubwa zilitembelea mji wetu, kati ya bendi ambazo nakumbuka ziliwahi kutembelea pale Iringa ni Morogoro Jazz Band chini ya uongozi wa Mbaraka Mwinshehe, Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza, Jamhuri Jazz Band, Butiama Jazz band, NUTA Jazz band, STC Jazz Band, Baba Gaston, JKT Kimbunga, Polisi Jazz na bendi nyingine nyingi sana. Kulikuwa na mahusiano mazuri kati ya bendi kubwa na bendi ndogo ambazo zilikuwepo kwenye kila mji, wanamuziki wenyeji walihakikisha wageni wanajisikia nyumbani kwa kuzungusha sehemu mbalimbali za mji.

Madansi ya zamani yalikuwa na kipindi cha mapumziko, ambapo wanamuziki walikuwa na kawaida ya kupumzika kwa muda wa robo saa hadi nusu saa kila dansi. Hii haikuwa sababu ya uchovu, bali ilikuwa lazima kwani amplifaya za zamani zilikuwa zikipata moto sana hivyo ilikuwa muhimu kuzizima kidogo ili ziweze kupoa. Ilikuwa ni baada ya mapumziko haya ambapo ilikuwa kawaida bendi ambayo ni wenyeji wa mji walikuwa wakikaribishwa nao waweze kupiga nyimbo mbili tatu. Kwa bendi yetu ya Chikwala Chikwala hii ilikuwa nafasi ambayo ni kama ndoto, kuweza kupiga muziki katika vyombo halisi. Lakini kulikuwa na jambo jingine kubwa zaidi, kupiga vizuri kulikuwa kunakupa nafasi ya kuchukuliwa na bendi kubwa.

Mpiga gitaa maarufu marehemu Ally Makunguru tulikuwa nae miaka hiyo na siku bendi ya JKT Kimbunga walipoturuhusu Chikwala Chikwala tupige nao matokeo yake walipenda sana upigaji wa Makunguru na kuondoka nae siku hiyohiyo. Makunguru alikuja kutokea kuwa kati ya wapiga magitaa bora Tanzania alikuja kupiga bendi za DDC Mlimani Park, Orchestra Safari Sound wana Ndekule, na hatimae alihamia Kenya ambako nako alijizolea sifa nyingi sana kabla ya kukutwa na mauti.
 

Attachments

Guasa Amboni

JF-Expert Member
Aug 13, 2015
8,037
2,000
Mzee kitine kila jambo na waqt wake dunia mlopiga muziki na leo tofauti zamani utahitaji kundi la watu ili ufanye muziki leo kijana anajifungia ndani siku mbili anatoka na album nzima. .Ukija kwenye kipato ndio hivyo ilikuwa khiyari ya moyo na khaswa kuupenda huo muziki ila jambo ambalo halitabadilika ni kuwa mlikuwa wanamuziki na sio waimbaji (yenye upeo watanielewa )tungo zenu mpaka leo zimesimama wima wala si bazoka poleni sana kwa njia mlopitia.
 

Guasa Amboni

JF-Expert Member
Aug 13, 2015
8,037
2,000
Enzi zenu mlikuwa mnasema mna tune mitambo aah siku hizi hicho kitendo cha ku tune au majaribio kijana wa sasa kwa muda huo wa kutest tayari zamani gani kaisha maliza wimbo.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom