Kuvuja kwa mitihani ya muhula wa pili kwa kozi za uuguzi na utabibu; Tumebaini chanzo, tutafute suluhu haraka

Travelogue_tz

JF-Expert Member
Sep 28, 2010
848
1,212
Habari JF

Mnamo tarehe 15 Oktoba 2021 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) walitangaza matokeo ya awali ( provisional results) ya mitihani ya muhula wa pili iliyofanyika mwezi Agosti , 2021.

Katika taarifa yake, ilieleza kuwa matokeo yote ya wanafunzi wa ngazi ya 5 (NTA Level 5), program ya Utabibu (Clinical Medicine) yamezuiwa mpaka taarifa ya uchunguzi kutoka Wizara ya Afya itakapokamilika na kuwasilishwa NACTE kwa ajili ya maamuzi. Pia wanafunzi takribani 35 kutoka vyuo mbalimbali walifutiwa matokeo yao na wanafunzi hao kusimamishwa kuendelea na masomo (Discontinued) kutokana na kufanya udanganyifu kwenye mitihani.

Aidha taarifa hii ambayo ilifanywa kuwa siri kwa takribani wiki nzima, imetolewa kupitia Gazeti la Mwananchi la tarehe 25/10/2021.

Ni muhimu Viongozi wetu na watumishi wa umma kufahamu kwamba nchi yetu imekuwa na kilio cha muda mrefu juu ya ubora wa kitaaluma na kitaalamu miongoni mwa wahitimu, ambapo tatizo limeendelea kuwa kubwa zaidi kwa kadri siku zinavyosogea. Hivyo jitihada za kubaini vyanzo vya kuvuja kwa mitihani ili kupata suluhu ni jambo la msingi sana endapo tunataka nchi yetu kuzalisha wasomi wenye tija na hivyo kushindana katika somo la ajira.

Makala yangu itajikita zaidi katika tukio hili, ambapo pengine linaweza kutumika kama nyenzo muhimu kwa ajili ya kuboresha katika matukio mengine yenye sura hii.

Nini chanzo cha kuvuja kwa mitihani hii?

Kabla ya kufahamu chanzo chake ni muhimu kutambua mchakato (process) ya uchakataji wa mitihani kabla ya kumfikia mwanafunzi katika chumba cha mitihani.

Kwa kawaida mitihani ya mwisho wa muhula wa pili kwa fani zote za afya zinaratibiwa na kusimamiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto kupitia idara yake ya Mafunzo.

Idara hii imekuwa na kazi ya kuratibu utunzi, uchapishaji, usambazaji, kuteua wasimamizi( external examiners) na usahihishaji wa mitihani.

Wizara ndio mhusika mkuu wa zoezi la mitihani kutokana na kwamba hatua zote hizo zinafanyika chini ya uangalizi au usimamizi wake au kupitia watumishi walioteuliwa. Zoezi hili linapitia katika hatua kadhaa za utekelezaji;
  • Wizara inateua wakufunzi, wengi wao kutoka katika Vyuo vya umma kwa ajili ya kushiriki zoezi la kutunga mitihani hii ambapo nakala zaidi ya tatu (version) zinaweza kuzalishwa kwa kila mtihani mmoja.
  • Wizara kupitia Mkurugenzi wake wa mafunzo, na baadhi ya watu anaowaamini wanaamua nakala ambayo ndio itakuwa mtihani utakaochapishwa na kusambazwa.
  • Baada ya kuamua aina ya mtihani utakaofanyika linafuata zoezi la uchapaji, ambalo linafanyika katika taasisi za uchapaji za umma chini ya uangalizi wa vyombo vya usalama na watumishi wa wizara. Hii huambatana na kufungasha mitihani hiyo katika parcel kwa ajili ya kuisambaza katika vituo vilivyotengwa na Wizara (Examination collection centres) ambazo mara zote huwa ni Vyuo vya afya vya vilivyopo chini ya Wizara ya Afya.
  • Baada ya mitihani kufika katika vituo vya Kuchukua mitihani, Vyuo vinatakiwa kwenda katika kituo husika kwa ajili ya Kuchukua kifurushi chake cha mitihani, ambapo taratibu zinataka kuwa na usimamizi wa askari polisi wasiopungua Wawili.
  • Vifurushi hivyo vya mitihani vinasafirishwa na kwenda kuhifadhiwa katika vyumba vigumu (strong room) vilivyopo katika Vyuo siku moja kabla ya mitihani kuanza.
  • Siku ambayo vifurushi hivyo vinahifadhiwa katika Vyuo, wasimamizi walioteuliwa na wizara (external examiners) anakuwa amefika katika eneo la Chuo na kuhakiki vifurushi vyote.
  • Baada ya kuhakiki vifurushi hivyo anatakiwa kutuma taarifa ya siri kwenda idara ya mafunzo kuhusu hali ya utunzaji wa mitihani.
  • Wasimamizi hao watatakiwa kukagua mitihani hiyo kabla ya kuifungua , mbele ya wanafunzi na wanafunzi Wawili kutakiwa kuhakiki kama mitihani ipo katika usalama unaotakiwa. Zoezi hili hufanywa kwa mitihani yote.
  • Pia wakati wa uendeshaji wa mitihani, wasimamizi wa wizara wanatakiwa kuchunguza mwendendo wa mitihani na kutakiwa kutoa taarifa juu ya mwenendo usiofaa (examination irregularities) kwa Wizara.
  • Kazi zote hizi za mitihani hufanywa chini ya kiapo cha Serikali.
Kwa utaratibu huu, wadau wengi wa elimu wameshindwa kuelewa sababu ya msingi ya Wizara kuzuia matokeo ya ngazi ya 5 (NTA Level 5), program ya Utabibu (Clinical Medicine) pekee na kuruhusu matokeo ya program nyingine ilhali mitihani yote imepita katika mkondo mmoja. Je Wizara inataka kutuaminisha kuwa mitihani mingine haikuvuja bali ni hii pekee?

Kwa taarifa zilizopo, imethibitika kwamba mitihani hii haikuvuja katika vyuo kwa kuwa hakuna taarifa yeyote kutoka kwa wasimamizi wa nje (external examiners report) inayothibitisha hilo. Aidha taarifa ya gazeti la mwananchi imeeleza kuwa wanafunzi walitumiana mitihani hiyo kwa njia ya WhatsApp na Telegram bila kutaja chanzo cha kuvuja mitihani hiyo.

Taarifa ya kamati ya Uchunguzi iliyoundwa na Wizara imebaini kuwa chanzo cha kuvuja kwa mitihani hiyo ni kutoka kwa moja ya mtumishi wa idara ya mafunzo ambaye alituma mwongozo wa majibu (answer guides) kwa mmoja ya ndugu yake anayesoma katika moja ya Chuo cha Utabibu cha Serikali kilichopo Kusini , japo katika taarifa waliyoiwasilisha kwa Wizara wamebadili na kuhusisha baadhi ya Vyuo vya Serikali kama chanzo cha kuvuja kwa mitihani. Aidha imebainika kwamba takribani mitihani yote imevuja na sio hii iliyofutwa pekee.

Je nini suluhu ya hili?
  • Kuanzisha uchunguzi huru; Kwa kutambua mchakato wa uratibu na usimamizi wa mitihani ni wazi kuwa Wizara ya Afya ambao ndio wahusika wakuu hawawezi kujichunguza wenyewe katika tuhuma hii. Ni busara kwa watendaji wake na wale wote wanaohusika katika mnyororo wa mitihani kupisha uchunguzi huru ili kubaini uhusika wao katika kashfa ya kuvuja kwa mitihani.
  • Wizara ya Afya kuacha kujihusisha na zoezi la uratibu na usimamizi wa mitihani badala yake ijikite zaidi katika kusimamia na kuthibiti ubora wa wahitimu kupitia Mabaraza yake ya kitaaluma.
  • Kazi ya usimamizi na uratibu wa mitihani iwe chini ya Kanda za NACTE kwa kushirikiana na Vyuo au Vyuo vyenye ithibati kamili vipewe mamlaka yake kwa mujibu wa sheria kuendesha mitihani yake kama ilivyo kwa mitihani ya mwisho wa muhula wa kwanza, huku Wizara kupitia Mabaraza ikituma wasimamizi wa nje (External examiners) kwa ajili ya uhakiki wa ubora wa uendeshaji wa zoezi la mitihani. Utaratibu ambao utasaidia kwa kiwango kikubwa kutua mzigo wa gharama kwa Vyuo na wanafunzi.
 
Sina hakika kama swala la wizi wa mitihani serikali iliwahi kulikomesha kabisa! Iwe Vyuoni au Mashuleni.
 
Back
Top Bottom