Kuuelewa Mgogoro wa CHADEMA na Kuumaliza Kuuelekea 2015

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,474
39,987
Utangulizi

Mgogoro wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CDM) ambao umesababisha baadhi ya viongozi wake waandamizi kung'olewa, wengine kujiuzulu na kugawa makundi ya wanachama na kuhatarisha hata usalama wa viongozi wengine ni lazima ufikie tamati.

Japo ambao wanataka tuamini kuwa hakuna mgogoro si kwa sababu hatuuoni bali kwa sababu wanataka tusiutazame ni muhimu kuwa wakweli kwa nafsi zetu kuwa kinachoendelea na ambacho kimedumu muda mrefu ni mgogoro ambao umetishia umoja wa chama, umelegeza harakati za kuing'oa CCM madarakani na kwa hakika umeacha majeraha ambayo kwa siku kadhaa sasa yanazidi kutoneswa toneswa na jitihada za kuyaponya hazijafanyika zikatosheleza. Katika mfululizo wa makala yangu hii nitajaribu kushirikisha mawazo yangu kuhusiana na mgogoro huu. Kwa muda mrefu watu wengi – wa pande zote za mgogoro – wameniuliza maoni yangu kuhusu kinachoendelea CDM na kwa wote jibu langu limekuwa "bado nafikiri". Ni kweli nilikuwa bado nafikiri kwa sababu naamini bila kutumia muda kufikiri kwa kina kuhusiana na tatizo, kulielewa chanzo chake na kulikabili lilivyo itakuwa vigumu kupata suluhisho la kudumu. Makala hii hadi hivi sasa ina sehemu nne – sidhani kama nitaifanya izidi sehemu tano; kwa wale wasiona mazoea ya kusoma maandishi mengi nashauri wanaweza kusubiri sehemu ya tatu nay a nne kuweza kuona mambo ambayo ninayapendekeza kufanyika. Lakini kwa wale ambao wanapenda kujua nilifikia vipi mapendekezo hiyo watajitendea hisani kunisoma toka mwanzo kuweza kuelewa msingi wa hoja yangu.

Katika Makala hii hasa hapo mbeleni nitajikita kwa kina kuonesha kwanini viongozi wakuu wa CDM ni sehemu ya mgogoro huu lakini pia ni wao ndio ambao wanaweza kuupatia suluhisho la kudumu; suluhisho ambalo litakuwa linatenda haki, linazingatia misingi ya kidemokrasia lakini pia suluhisho ambalo litasababisha wanachama wote kutambua kuwa kuelekea 2015 migogoro haikubaliki, haitavumiliwa na yeyote ambaye atakuwa sehemu ya mgogoro atashughulikiwa ipasavyo kwa staili ya kumkomo nyani giledi, mchana kweupe.

Katika sehemu ya kwanza nitaangalia nadharia ya nidhamu ya chama (party discipline), katika sehemu ya pili nitaangalia sehemu ya kwanza ya chanzo cha mgogoro, katika sehemu ya tatu nitaangalia sehemu ya pili ya chanzo cha mgogoro (ambayo inatokana na nadharia ya nidhamu ya chama) katika sehemu ya nne nitachambua viongozi wa CDM ambao naamini wamekuwa sababu ya mgogoro na kwa namna gani vyanzo vya mgogoro vimewaweka katika hili; katika sehemu ya mwisho (natumaini sitaenda zaidi ya hapo) nitaangalia namna ya kuutatua mgogoro huu kwa kutoa mapendekezo ambayo ni ya kuthubutu, yasiyo angalia sura na ambayo hayana haja ya kuomba radhi kabla ya kuyatoa.

Matumaini yangu ni kuwa hoja nitakayoiweka hapa itatoa pendekezo bora zaidi la kumaliza mgogoro CDM (na wengine wanaweza kujifunza) kuliko mapendekezo mengine yote yaliyowahi kutolewa na wengine kabla.

Fuatana nami katika sehemu ya kwanza.


NADHARIA YA NIDHAMU YA CHAMA (Party Discipline Theory)

Mambo haya matatu yanatusumbua sana na yanaligharimu taifa. Yanatusumbua kwa sababu hayaonekani kumalizika bali yanaonekana kama kuzidi na kuzidi kila siku iitwayo leo; na yanaligharimu taifa kwa sababu matokeo yake kwa ujumla wake kwenye uongozi na utendaji wa taifa letu ni hasi. Ukiangalia kwa karibu mambo yanayoendelea ndani ya chama tawala na kwenye chama kikuu chaupinzani nchini – CDM – mambo haya yameota mapembe ambayo kwa kweli hayakatiki, hayakatwi bali zaidi yanaonekana kuchongwa.


Mfano wa Jeshi

Jeshi lolote duniani ambalo limeundwa kwa ajili ya kutoa ulinzi na kupigana vita linahitaji vitu hivi vitatu kama nguzo zake kuu za kiutendaji ili kuweza kupata ushindi vitani. Majeshi yote duniani kati ya vitu ambavyo wanamfundisha askari mtarajiwa (kuruta) ni kuwa na nidhamu, kutii mamlaka iliyo juu yake na kutotumia madaraka vibaya. Makuruta wanapojiunga na jeshi wanatoka katika mazingira tofauti, wana tabia tofauti na wana mitazamo tofauti; kazi ya kwanza ya wakufunzi wa kijeshi (drill sergeants) ni kuwatengeneza hawa watu kutoka walivyokuwa na kuwapeleka wanakotakiwa kuwa.

Kwa wale tulioshuhudia kwa karibu Vita ya Kagera na harakati za Ukombozi wa Nchi zilizoko Kusini mwa Afrika tunajua ni kwa kiasi gani jeshi letu lilijipatia heshima katika kushiriki mapambano, kutoa mafunzo na kulinda usalama wa nchi yetu. Kiasi kwamba tulijiaminisha kuwa jeshi letu ni mahiri kabisa katika eneo letu hili. Kutokana na ujuzi huo tumekuwa na kiburi cha ufahari wa jeshi letu; ndio maana tunapochokozwa na majirani zetu hatuchelewi kuanza kushadadia vita na mapambano kwa sababu tunaamini kabisa kuwa katika eneo letu hakuna nchi ambayo inaweza ikaingia vitani na sisi ikatupiga; siyo Malawi, siyo Rwanda wala siyo nani.

Siri ya mafanikio haya ya jeshi letu ni nini hasa? Je ni kwa sababu tumewekeza kwa kiasi kikubwa katika vifaa vya kijeshi? (hili si kweli); je inawezekana ni kwa sababu tuna silaha za kisasa zaidi kuliko wengine? au kwa sababu sisi ni Tanzania kana kwamba kwa kuwa Tanzania basi automatically jeshi letu ni bora zaidi? Au kuna siri kubwa zaidi na ya msingi?

Naomba kupendekeza kwa msomaji kuwa siri ya mafanikio ya jeshi lolote duniani (likiwemo la kwetu) imelala kwanza kabisa katika nidhamu (discipline). Jeshi lisilo na nidhamu haliwezi kushinda vita hata kama lina silaha, wataalamu au mabilioni ya pesa. Vitu vingine ni muhimu sana katika kufanikisha mapambano lakini hakuna kitu muhimu kama kuwa na wapiganaji walio na nidhamu iliyopitiliza; ambao wanatambua majukumu yao barabara na ambao pamoja na makamanda wao wako moyo mmoja kutafuta ushindi. Hakuna brigedi, hakuna kikosi, hakuna company ambayo inaweza kusimama peke yake au kujifanyia mambo yake kwa ajili ya sifa zake yenyewe. Jeshi lote na sehemu yote chini ya majenerali husika ndio linaenda kutafuta ushindi. Jeshini hakuna sifa ya kikosi moja au kapteni mmoja!


Nidhamu na Demokrasia

Mojawapo ya mambo ambayo yananitatiza siku za karibuni – hasa kufuatia mgogoro wa ndani wa CDM – ni ile imani ya baadhi ya watu kuwa demokrasia na nidhamu haviendani (the incompatibility of democracy and party discipline). Kwamba, katika nchi ya kidemokrasia vyama vya siasa haviitaji kuwa na nidhamu ya ndani kwani kuweka nidhamu au kusimamia nidhamu ni kuminya au kufinya demokrasia. Wenye kuamini hivyo ni wepesi kuona tishio kwa demokrasia wakati wowote chama cha siasa kinapojaribu kusimamia nidhamu ndani yake.

Matokeo yake ni kuwa wanasiasa – viongozi na wasio viongozi – wanajaribu na wengine wameshajaribu kufanya mambo bila kujali chama chao cha siasa. Kwamba, kwa vile mtu ana mawazo Fulani basi yuko tayari kuyafanyia kazi mawazo hayo (haijalishi kama ni mazuri au la) bila kujali, kukihusisha au kupata kuungwa mkono na chama chake. Hili linasababisha tujiulize swali la msingi kweli; je ni kweli kwamba demokrasia na nidhamu haviendani pamoja?

Naomba kupendekeza kwa mpendwa msomaji kuwa bila nidhamu demokrasia haiwezi kuchipuka, kustawi na kuzaa matunda. Nidhamu ni gundi inayokishika chama pamoja na siyo chama tu bali jumuiya yoyote ya watu ambao wameamua kuunganisha nia zao ili kufikia lengo moja. Hili ni kweli kwenye kwaya, bendi ya muziki, timu ya mchezo, na ukiangalia sana hata kwenye familia. Wakati wowote kunatokea kukosekana kwa nidhamu basi kikundi hicho cha watu kitaanza kuwa na nyufa, misukosuko na kama wahusika hawatawajibika ipasavyo basi kikundi au jumuiya ya watu inaweza kabisa kuparaganyika. Hapa basi kuna haja ya kuielewa hii nidhamu ya chama (party discipline)

Nidhamu ya Chama Ni Nini Basi?

Hii inaweza kutafsiriwa kama mfumo na utaratibu unaotumiwa na chama cha siasa kuhakikisa kuwa wanachama (viongozi na wasio viongozi) wanafuata msimamo wa chama badala ya kufuata tu vitu vingine ambavyo navyo vyaweza kuwa vya muhimu. Katika nchi zenye utawala wa kidemokrasia nidhamu ya chama ni utaratibu wa kichama wa kuhakikisha kuwa watendaji na viongozi wanaotokana na chama cha siasa wanazingatia na kufuata misimamo, misingi, itikadi na mwelekeo wa chama.

Kama nilivyosema hapo juu, lengo la kuwa na nidhamu ya chama ni kuhakikisha kuwa chama kinasimamia malengo yake na hatimaye kuhakikisha kuwa kinayafikia malengo hayo. Mgawanyo wa Nidhamu ya Chama

Naweza kuigawa hii nidhamu ya chama katika makundi makubwa matatu.

a. Nidhamu ya Wanachama kwa Chama


Kila mwanachama anapojiunga na chama cha siasa anakuwa amekubali malengo, nia, na madhumuni ya chama hicho. Katika kukubali mambo hayo mwanachama anakuwa amekubali kufuata Katiba ya chama, taratibu zake na miongozo yake. Hii ndiyo sababu mtu anachukua kadi ya chama na kuilipia; anaonesha kukubali kwake yaliyomo ndani ya Katiba hiyo. Kimsingi, anakuwa amekubali kufungwa na Katiba hiyo. Hili ni kwa kila mwanachama. Hivyo, kila mwanachama bila kujali uwezo wake, hali yake ya kimaisha, jinsia yake n.k anatazamiwa kufuata Katiba ya chama, taratibu zake na uongozi wake.

Kila mwanachama anapaswa kuwa na nidhamu kwa chama chake; kuanzia tawi alipo hadi ngazi za juu za chama chake. Kwa upande wa CDM Mwanachama ni lazima akubaliane na Katiba, Itikadi, na Kanuni za chama kwa mujibu wa Ibara ya 5.1.4 na 5.1.5 ya Katiba ya CDM.

b Nidhamu ya Wanachama kwa Viongozi na Viongozi kwa Wanachama

Chama cha siasa ili kiweze kusonga mbele kinahitaji kuwa na nidhamu ya viongozi kwa viongozi na viongozi na wanachama wao. Hii ina maana ya kuwa wanachama wanakuwa tayari kufuata uongozi na viongozi wanatarajiwa kuwaongoza wanachama wao vizuri na kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa wazi. Bila ya nidhamu ya aina hii kila mwanachama atakuwa kiongozi na kile kiongozi atakuwa na wanachama wake. Ni lazima kuwe na nidhamu ya aina hii ili kuhakikisha kuna utulivu, umoja, na ufanisi katika utendaji kazi au katika kusimamia majukumu mbalimbali. anatazamiwa kufuata Katiba ya chama, taratibu zake na uongozi wake.

Wanachama wanatakiwa kuwa na nidhamu ya kukubali kuongozwa; ndio maana ya kuwa na viongozi. Wanachama wasiokubali kuwa chini ya uongozi ulio halali juu yao ni sawasawa na kuwa na kundi la mifugo lisilokubali kuchungwa. Mfano huu waweza kuelezea vizuri haja ya kuwa na nidhamu kama kundi; mchungaji mzuri anajua jinsi ya kulinda mifugo yake, kuipatia lishe nzuri, kuhakikisha ina afya na inaongezeka na hatimaye kumpatia faida. Mchungaji ambaye kila wiki anachinja mifugo kwa ajili ya kufurahia tu au anauza kwa bei chee au haipi matunzo yanayostahili ni mchungaji wa hatari.

Uongozi ni hivyo hivyo; viongozi wanatakiwa kutoa uongozi mzuri kwa wale wanaowaongoza na wale wanoongozwa kukubali kuongozwa vizuri. Wanachama wasiopenda kuongozwa na wanaojifanya na wao ni viongozi wakati siyo ni sababu moja ya kukosekana kwa nidhamu. Mwanachama anayeamini anaweza kuongoza vizuri zaidi kundi anapewa nafasi katika uchaguzi kuwashawishi wanachama wenzake kumpa uongozi. Kabla ya hapo anatakiwa awe na nidhamu kukubali kuongozwa.

Viongozi nao hata hivyo kwa vile ni viongozi haina maana wanaweza kuongoza vibaya wakaachwa; ni lazima waoneshe kuwa na nidhamu ya kuongoza vizuri makundi yao. BIla kufanya hivyo watajikuta wanapata shida kusimamia wale wanaowaongoza na matokeo yake wanaweza kusababisha uasi katika kundi.

c. Nidhamu ya Viongozi kwa Viongozi


Kila chama kina ngazi mbalimbali za uongozi; kuna viongozi wa ngazi za chini, wapo wa ngazi za kati na wapo viongozi wa ngazi za juu. Japo wote wanaitwa viongozi lakini kimsingi uongozi wao ni katika maeneo ambayo wamepewa uongozi na si vinginevyo. Katika elimu ya uongozi hii inaitwa ‘ngazi za uongozi/madaraka' (leadership hierarchy).

Ngazi za Madaraka katika demokrasia zinatoa nafasi kwa watu mbalimbali kushika uongozi katika ngazi mbalimbali na wakati huo huo kuweza kupata nafasi ya kusonga mbele katika nafasi nyingine zenye majukumu makubwa zaidi. Ni wazi kuwa kwa kadiri mtu anapanda ngazi hii ndivyo anavyozidi kukuta kuwa huku juu nafasi zinazidi kupunguza zaidi. Ndio maana uongozi wa kisiasa unakuwa kama pembetatu fulani hivi ambapo nafasi kubwa za kushika uongozi wa aina mbalimbali ziko chini kuliko juu.

Kwa mujibu wa Katiba ya CDM Ibara ya 7; Muundo wa chama unaanzia ngazi ya Msingi na kuishia Ngazi ya Taifa. CDM ina ngazi zifuatazo za muundo wa chama.

1. Msingi/Vitongoji
2. Tawi
3. Kata/Wadi
4. Wilaya
5.
Mkoa
6. Jimbo/Kanda
7. Taifa

Hata hivyo ukizingatia tangazo la hivi karibuni la uchaguzi wa ndani wa chama yawezekana kukaonekana kuwa kuna utata wa muundo huu wa chama hasa linapokuja suala la Kanda na Majimbo. Kwa mujibu wa tangazo la chaguzi hizo kuanzia 1-10 Aprili 2014 kutafanyika chaguzi za majimbo na tarehe 9 Julai utafanyika uchaguzi wa Kanda.

Kwa mujibu wa ufafanuzi wa maneno katika Katiba ya CDM "Majimbo" kimsingi ndio "Kanda". Katiba inatafsiri Majimbo kuwa ni "mkusanyiko wa mikoa yenye mahitaji yanayofanana kiuchumi kama itakavyoamuliwa na Baraza Kuu." Sasa ama kuna kurudia rudia chaguzi au majimbo kama yalivyotajwa kwenye suala la uchaguzi siyo kanda kitu ambacho kitatufanya tuulize ni nini hasa? Kama ni majimbo ya uchaguzi (constituencies) basi Katiba ya CDM haina ngazi hizo kwani Ibara ya 7:6 inapozungumzia majimbo inazungumzia kwa maana hiyo hapo juu isipokuwa kama kutatolewa ufafanuzi wa mahusiano ya kiutendaji kati ya majimbo ya uchaguzi na majimbo ya kanda. Hii ni kwa sababu katika suala la uchaguzi ‘uchaguzi wa majimbo' umewekwa kabla ya uchaguzi wa Wilaya na ule wa Mikoa na baada ya uchaguzi wa matawi kitu ambacho kinanifanya niamini kuwa uchaguzi uliosemwa ni wa "majimbo" ni uchaguzi wa ngazi ya Kata/Wadi na sio jimbo kwani jimbo ni kanda.

Katika ngazi hizi zote – kuanzia vitongoji hadi taifa; kutakuwepo na watu ambao wataomba nafasi ya kutumikia chama chao katika ngazi hizo za uongozi; wakati huo huo wao wenyewe watakuwa wanajiweka chini ya uongozi ule wa juu yao. Hii ndio ngazi ya uongozi; kila kiongozi wa chini anatakiwa kuwa na nidhamu na viongozi wa juu na wale wajuu wanasimama na kuwajibika kwa walio chini yao.

Nidhamu ya Chama ni Suala la Vyama vya Kijamaa?

Mtu anaweza kusema kuwa suala la nidhamu ya chama ni suala la vyama vya kijamaa; kwamba katika demokrasia au mfumo wa vyama vingi vyama vya siasa havitakiwi kuweka mkazo sana katika nidhamu; kwamba nidhamu inadumaza na kudunisha ukuaji wa demokrasia. Hivyo, katika fikra za baadhi ya hawa wanaweza kuona kuwa kila mtu kujifanyia, kujiamulia au kujiendea kivyake vyake katika chama ni sehemu ya demokrasia.

Hii si kweli. Wanasayansi wa elimu ya siasa wa nchi za kidemokrasia wameandika vya kutosha juu ya umuhimu na hata ulazima wa nidhamu ya chama. Nchi zenye muda mrefu katika demokrasia ya vyama vingi kama India, Australia, Uingereza, Marekani, New Zealand, Canada n.k zinatumia nidhamu ya chama katika kuhakikisha kuwa wanachama na viongozi wanakuwa katika mstari mmoja na wanakuwa katika lengo na mwelekeo mmoja wa kichama. Kwa Marekani hata hivyo mfumo wa nidhamu ya chama hauna nguvu sana kama ilivyo Canada, India, Japan au Uingereza na Australia. Kuna sababu za Kikatiba kwanini mfumo wa nidhamu ya chama Marekani ni dhaifu kulinganisha na nchi nyingine.

Manufaa makubwa kabisa ya mfumo na usimamizi mzuri wa nidhamu katika chama ni kukiandaa kushika madaraka na kutimiza ajenda yake ya uchaguzi kwa ufanisi, weledi, umoja na kuhakikisha matokeo yake yanakuwa mazuri.

KUUELEWA MGOGORO WA CHADEMA NA KUUMALIZA KUELEKEA 2015 - 2

VYANZO VYA MGOGORO


Kwa karibu miaka kadhaa sasa ndani ya chama kikuu cha upinzani nchini CDM kumekuwepo na mvutano wa ndani baina ya makundi mbalimbali. Mvutano huu ambao wakati mwingine umekuwa ukilaumiwa chama tawala cha CCM ni muhimu kueleweka ili hatimaye suluhisho la kudumu, kamili na thabiti liweze kufikiwa. Mgogoro uliopo ni vizuri kuelewa sio mgongano wa kiitikadi au kifikra; angalau sivyo unavyojionesha hivyo. Karibu wote wanaogongana na ambao wamewahi kugongana utaona kuwa hawagongani kwa vile wanatofautiana sana kiitikadi au sera za Chama kiasi kwamba mmoja anataka kubadilisha sera za mwingine. Ukiumulika kwa karibu utaona kuwa mgogoro huu unahusisha watu zaidi (personalities) kuliko fikra au itikadi. Chacha Wangwe dhidi ya Mbowe, Slaa dhidi ya Zitto na kinyume chake, kundi la vijana dhidi ya Mbowe au Dr. Slaa; na wengine dhidi ya Zitto n.k. Na hili ni kweli siyo kwenye ngazi za juu tu za chama bali pia tumeona kwenye ngazi za chini kama ilivyotokea Mbeya, Mwanza, Arusha n.k

Mgogoro huu wengine wanaweza kuuona pia ni mgogoro wa kimaslahi zaidi ambapo watu mbalimbali wanatafuta maslahi fulani zaidi huku wengine wakitaka kuendelea na maslahi fulani. Kama ni maslahi binafsi au ya chama au ya taifa hili ni jambo jingine lakini wao wenyewe wanaogongana kila mmoja anajaribu kusema anatetea maslahi fulani. Kama ni kweli ni mgogoro wa maslahi au maslahi yana sehemu zake kwangu si la maana sana; la maana katika hoja yangu ni kuwa mgogoro huu upo, umekuwa mkubwa (umekuzwa) na hatua ambazo zimechukuliwa hadi hivi sasa naamini hazitoshi kuumaliza kabisa. Lakini kabla hatujazama zaidi kuuelewa mgogoro huu naomba nioneshe kwanini mgogoro huu upo.

Kwanini kuna Mgogoro CDM?

Naomba kupendekeza kwa msomaji kuwa mgogoro uliopo CDM una vyanzo viwili vikubwa. Chanzo cha kwanza kikiwa Nina uhakika wapo wanaofikiria kuwa mgogoro huu chanzo chake ni ‘watu'; mimi naomba kutafutiana nao. Ni rahisi kutaja majina ya watu kama vyanzo vya mgororo lakini naamini mgogoro uliopo ni zaidi ya watu. NI sawasawa na watu wanaofikiria kuwa tatizo la utawala wa CCM ni watu kuwa wakibadilisha watu basi utawala utakuwa mzuri na kweli kwa miaka 52 sasa CCM imeendelea kubadilisha watu na namna ya utawala imeendelea kuwa vile vile. Nchi imekuwa na marais wanne, mawaziri wakuu 9 (na wapo wengine Bungeni wanataka waziri mkuu wa 10!); mawaziri wa nishati na umeme lukuki, kwenye afya wengi tu, elimu ndio usiseme kabisa!

Mtu yeyote anayetaka kufiriki vizuri ni lazima ajiulize; kama tunabadilisha watu hivi kwanini namna ya utawala haibadiliki? Je inawezekana kuwa tatizo ni zaidi ya watu? Binafsi naamini tatizo la mgogoro wa CDM kama ule ulioko CCM (ambao kwa leo naomba niuache kwani nilishawahi kuandika na mapendekezo yangu kuyatoa miaka kadhaa nyuma) lina sehemu kubwa tatu na kuzielewa sehemu hizo mbili au vyanzo hivyo viwili ndio njia pekee ya uhakika ya kuweza kuondoa mara moja na daima mgogoro huu bila kujali sura, majina, hadhi, ujiko, na vyeo vya wahusika. Vyanzo vya mgogoro ndani ya CDM ni vya pande tatu; upande mmoja ni mfumo na muundo wa chama, upane mwingine ni ukosefu wa nidhamu ya chama na upande wa tatu ni sheria ya vyama vya siasa (na Katiba ya sasa).

Hili la tatu hata hivyo siyo somo ambalo nitalizungumzia kwenye Makala hii kwani kwa wengi labda ni rahisi kueleweka zaidi kuliko haya mengine mawili. Na katika mada yangu hii kubwa ambalo nitazama ndani kidogo ni kuliangalia sana ni hilo la pili – la ukosefu wa nidhamu; la kwanza nitaliangalia kama kidokezo tu lakini pia kwa sababu litaganya hili la pili liwe bayana zaidi.

Mfumo na Muundo wa Chama

Mfumo na Muundo wa chama ni kama jukwaa ambalo juu yake wachezaji mbalimbali wanasimama. Jukwaa linalotaka kusimama mtu mmoja hutengenezwa kwa ajili ya mtu mmoja, jukwaa la kikindi kidogo huwa dogo vile vile; jukwaa ambalo linatarajiwa kuwa la kundi kubwa la watu, vifaa na vitu mbalimbali huwa kubwa na kila mojawapo hujengwa kwa kuhakikisha kuwa linakuwa imara. Jukwaa ambalo litachukua watu zaidi ya uwezo wake linaweza kuvunjika na kusababisha madhara makubwa. Jukwaa ambalo watu watakuwa wanaruka ruka n.k ni lazima liwe na uwezo mkubwa, kinga za kutosha na lililojengwa kwa ustadi mkubwa. Kile kinachofanyika kwenye jukwaa kinategemea sana ustadi, uimara na ukubwa wa jukwaa.

Katika hoja yangu hii mfumo na muundo wa chama ni kama jukwaa; udhaifu wowote katika eneo hili utajionesha katika watu wanaosimama kwenye jukwaa hilo na uwezo wake wa kuhimili mikikimikiki. Vyama vyote vya siasa vilivyoanzishwa kufuatia kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini vilijikuta vinahitaji kujijenga na kujiunda ili kuweza vyama vya kitaifa kama inavyotaka Katiba na sheria ya nchi. Tatizo ni kuwa chama pekee cha siasa kilichokuwepo na ambacho watu walijua mfumo wake kilikuwa ni CCM.

Matokeo yake ni kuwa karibu vyama vyote vilivyoanzishwa vimejikuta vikinakili kwa kiasi kikubwa sana muundo na mfumo wa CCM kiasi kwamba kuna kufanana kusiko kwa lazima kimfumo na kimuundo kati ya vyama hivi – ukiondoa tofauti kadha wa kadha. Mfumo na Muundo wa CDM umekaa kiCCM zaidi na hili ni tatizo kwa sababu ndilo pia limechangia matatizo ndani ya CCM vile vile na limechangia katika kuleta utawala mbovu nchini. Kufanana huko kwanza ni kwa mfumo wa ngazi za muundo wa chama. Hapo juu tayari nimeonesha muundo wa ngazi za CDM nioneshe jinsi muundo huu unavyoakisi muundo wa CCM.

CCM ina mfumo ufuatao wa kichama:
1.
Shina
2.
Tawi
3. Kata/Wadi
4. Jimbo
5. Wilaya
6. Mkoa
7. Taifa

Utaona kuwa CDM na CCM vinafanana muundo wao wa kingazi. Swali ambalo labda watu wengine wanaweza kulijibu ni hili: Kwanini CDM ilipoundwa hadi hivi sasa imekuwa na mfumo huu wa ngazi saba wa kichama? Swali jingine la kina zaidi ni kwanini CCM wamekuwa na mfumo huu wa ngazi za aina hii tangu enzi za TANU? Hili swali la pili ni rahisi kulijibu: CCM ilizaliwa na kuishi kwa muda mrefu kama chama cha kijamaa (socialist party) ambacho kama vilivyo vyama vingine vya aina yake hasa wakati wa vita baridi vilikuwa vinajaribu kuhakikisha kuwa chama kinamfikia kila mwananzi kuanzia kwenye nyumba mtaani (vitongoji na shina) hadi kufika ngazi ya taifa.

Vyama vyote vya kijamaa au kikomonisti kama vya China, Cuba, Vietnam n.k vina mfumo wa namna hii ambapo wananchi wana uchaguzi mmoja tu wa kujiunga na chama na uanachama wa chama hicho ni sharti kubwa la kuweza kufanikiwa katika mambo mengine mengi. CCM kwa muda mrefu ilinufaika sana na mfumo huu kwani ilihakikisha kuwa siasa zake zimeenea kuanzia ngazi za juu kabisa hadi kwenye mitaa. Ni mfumo ambao unataka kudhibiti siasa katika nchi; ni mfumo ambao hauendani na demokrasia japo unajionesha kana kwamba unatoa nafasi kwa watu kutoa maoni yao kwa wingi. Mfumo huu umeweka madaraka juu mno kama nitakavyoonesha hapa chini.

Nguvu ya Kamati Kuu

Japo ningeweza kuangalia muundo wa CDM na CCM ngazi kwa ngazi kwa namna ya pekee ningependa kuangalia madaraka ya Kamati Kuu katika vyama hivi vikuu nchini na kwanini muundo huu umepitwa na wakati na ni chanzo kimojawapo cha migogoro katika vyama vya siasa.

Kazi za Kamati Kuu ya CDM

Kwa mujibu wa Katiba ya CDM Ibara ya 7.7.16 Kamati Kuu ya chama imepewa majukumu mengi mno ya kuyasimamia kiasi kwamba inabidi mtu aulize ni kwa kiasi gani KK inaweza kuwa na ufanisi na kutimiza majukumu yake yote haya hasa ukizingatia kuwa wajumbe wake wengi pia wana wawajibu mwingine katika Bunge au chama.

Kazi za KK ya CDM ni hizi:

(a) Kufanya utafiti wa wagombea na wa Uraisi na Mgombea Mwenza na kuwasilisha ripoti zake kwa Baraza kuu kwa ajili ya mapendekezo yake kwa Mkutano Mkuu.
(b) Kuteua Wakurugenzi wa Idara Kuu za Chama Makao Makuu
(c) Kuteua Makatibu wa Wilaya na Mikoa
(d) Kuthibitisha uteuzi wa Sekretarieti za Wilaya.

(e) Kutoa mapendekezo kwa Baraza Kuu juu ya rufaa za uchaguzi na kinidhamu.
(f) Kuandaa na kutoa Mapendekezo kwa Baraza Kuu, Mikakati ya kuendesha shughuli za Chama kwa kila mwaka na kwa kipindi cha miaka mitano.
(g) Kuandaa na kutoa mapendekezo kwa baraza Kuu , Mikakati ya kupata mahitaji ya raslimali za kuendesha kampeni za wagombea wa Chama katika chaguzi za kiserikali.
(h) Kuandaa na kutoa mapendekezo kwa Baraza kuu ratiba na maelekezo ya uchaguzi wa kichama.
(i) Kupitia na kutoa kwa Baraza Kuu mapendekezo ya haja ya kuzifanyia marekebisho au maboresho Kanuni za Chama ama Katiba ya Chama.
(j) Kujadili taarifa za Sekretarieti ya Kamati Kuu na kutoa maamuzi na maelekezo kwa utekelezaji.
(k) Kusimamia utendaji kazi wa Sekretarieti ya Kamati Kuu
(l) Kufanya mapitio ya Sera za Chama na kutoa mapendekezo kwa Baraza Kuu kwa kuzingatia matokeo ya Utafiti uliofanywa na Sekretarieti ya Kamati Kuu.
(m) Kusimamia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Baraza Kuu na Mkutano
Mkuu.
(n) Kuwa kiungo na kudumisha mahusiano mema kati ya Chama na vyama vingine vya siasa nchini, Afrika Mashariki na nchi nyingine.
(o) Kuthibitisha ajira za watumishi wakuu wa Chama ngazi ya Taifa.
(p) Kuteua kamati au tume za kushughulikia masuala maalum ya kichama kwa muda
maalumu.
(q) Kuteua wakaguzi wa mahesabu ya Chama kwa kila mwaka
(r) Kuthibitisha uteuzi wa wagombea Uspika, Ubunge na Baraza la wawakilishi Zanzibar
(s) Kuandaa agenda za Baraza Kuu na Mapendekezo ya agenda za Mkutano Mkuu.

(t) Kufanya uamuzi juu ya mpendekezo ya kufukuza Mwanachama.
(u) Kuandaa hoja za kupelekwa Bungeni na Wabunge wa Chama

(v) Kumwachisha ujumbe wa Kamati Kuu mjumbe mteule ambaye ataenda kinyume na
katiba, kanuni na maadili au kushindwa kukidhi matakwa ya kuteuliwa kwake.
(w) Kuratibu utendaji wa ofisi ndogo ya Makao Makuu Zanzibar.

(x) Kusimamia utendaji kazi wa Mabaraza ya Vijana, Wanawake na Wazee.
(y) Kuteua wajumbe maalum wawili kuingia Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya.

Kwa upande wa CCM kazi za Kamati Kuu zimeanishwa katika Ibara ya 109 ya Katiba ya CCM. Kazi za KK ya CCM ni nyingi vile vile na baadhi yake ni hizi:

(1) Kutoa uongozi wa Siasa katika nchi.
(2) Kusimamia utekelezaji wa shughuli za kila siku za CCM.
(3) Kueneza Itikadi na Siasa ya CCM nchini.
(4) Kusimamia kampeni za Uchaguzi na kampeni nyinginezo.
(5) Kuteua Makatibu wa CCM wa Wilaya na Katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa.
(6) Unapof ika wakati wa Uchaguzi Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa itashughulikia mambo yafuatayo:-
(a) Kuf ikiria na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya Wanachama watakaosimama katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM.
(b) Kuf ikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu majina ya Wanachama wasiozidi watano wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

(c) Kuf ikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya Wanachama watakao-simama katika uchaguzi wa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM.
(d) Kuf ikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya majina ya Wanachama wasiozidi watatu ambao wanaomba kugombea kiti cha Rais wa Zanzibar.
(e) Kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya Wanachama wanaoomba nafasi za uongozi katika CCM na Jumuiya zinazoongozwa na CCM ambao uteuzi wao wa mwisho unafanywa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa.
(f ) Kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya Wanachama wanaoomba nafasi ya Ubunge na Wanachama wanaoomba nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.
(g) Kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya Taifa juu ya Wanachama wa CCM wanaoomba nafasi za uongozi katika Jumuiya za Wananchi zinazoongozwa na CCM, ngazi ya Mkoa na Taifa, ambazo uteuzi wake wa mwisho hufanywa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

(h) Kufikiria na Kufanya uteuzi wa mwisho wa wanachama wa CCM wanaoomba kugombea nafasi ya Spika wa Bunge/Baraza la
Wawakilishi, Meya wa Halmashauri ya Jiji/Manispaa.
(7) Kumsimamisha uongozi kiongozi yeyote isipokuwa Mwenyekiti wa CCM na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM endapo itaridhika kwamba tabia na mwenendo wake vinamwondolea sifa za uongozi.

(8) Kuona kwamba masuala ya Ulinzi na Usalama wa Taifa na Maendeleo yanazingatiwa.

(9) Kuandaa mikutano ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa.

(10) Kuwa na mikakati endelevu ya kuimarisha Chama kimapato, kudhibiti mapato na mali za Chama na kuthibitisha matumizi ya Chama katika ngazi ya Taifa .

Tuchukue kazi moja hapa na tuiangalie kwa karibu kidogo kama kwa kutumia darubini. Kwa upande wa CDM tuangalie kazi (a) ambayo inasema "Kufanya utafiti wa wagombea na wa Uraisi na Mgombea Mwenza na kuwasilisha ripoti zake kwa Baraza kuu kwa ajili ya mapendekezo yake kwa Mkutano Mkuu." Na kwa upande wa CCM tuangalie kazi (6b) ambayo inasema "Kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu majina ya Wanachama wasiozidi watano wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."

Kazi hizi mbili za KK za vyama hivi zinaonesha tu kuwa hakuna mtu anayeweza kuwa Rais wa Tanzania kama hatopata Baraka kutoka kwenye Kamati Kuu ya chama. Hii ina maana KK ya kila chama ni chombo ambacho kinavutia wengi na katika uendeshaji wa chama watu walioko kwenye KK ya chama ni watu wenye nguvu kubwa sana katika chama. Ukilielewa hili utaona kuwa mgongano karibu yote ambayo imetokea ndani ya CDM hadi hivi sasa inahusisha kwa kiasi kikubwa wajumbe wa Kamati Kuu. Ikumbukwe kuwa kinachoitwa Baraza Kuu kwa upande wa CDM ni sawasawa na kile kinachoitwa Halmashauri Kuu ya Taifa.

Tungeweza hata kulinganisha kazi za vyombo hivyo na tungeona jinsi ambavyo vinafanana. Na hata kwenye ngazi ya Mkutano Mkuu utaona kuwa CCM na CDM (kama ilivyo kwa vyama vingine) bado vinafanana sana. Na siyo kwenye ngazi hizi tu hata huku chini utaweza kuona kufanana huko na maana yake katika utendaji wa chama.

Tatizo la kufanana huku ni nini basi?

Kufanana huku kuna tatizo moja kubwa; kama mfumo wa CCM umekosewa kinadharia na kiutendaji basi vyama vilivyonakili mfumo huo vitajikuta vinaingia kwenye matatizo yale yale ya CCM. Ni sawasawa na watoto darasani ambapo mmoja anayedhaniwa kuwa ana akili anafanya makosa katika kujibu swali halafu mwingine pembeni yake naye ananakili kosa. Halafu itokee mtoto wa tatu ambaye anaangalia mtoto wa kwanza akinakili kosa amsahihishe na kumuambia "hujanakili sawasawa" akiamini kuwa kinachonakiliwa kiko sawasawa. Hili la muundo na mfumo wa chama ni pana na lenye kina cha kutosha; itoshe kusema tu kuwa mfumo huu wa chama kwa CDM unachangia sana kuanzisha, kuendeleza na kukoleza matatizo na migogoro.

Hali ingekuwa hivi hivi kwa CCM kama wasingekuwa madarakani kwani ni mfumo ule ule ambao umepitwa na wakati na ambao hauendani na hali halisi ya jitihada za kujenga demokrasia nchini. CCM kinga yao ni kuwa wao wana serikali na hivyo wanajua kuwa hawawezi kwenda mbali sana na malisho. Ningeweza kuliangalia hili kwa kina lakini kama ipo haja (kama watakuwepo wa kubishia hili) basi nitazama zaidi na kuonesha mlinganisho na utofauti (contrasting) mfumo wa chama chenye sera zilizoshindwa na kiko madarakani tunahangaika nacho na chama kinachotaka kushika madaraka lakini kina mfumo wa chama kilichoshindwa.

Muundo wa sasa wa CDM hauna chombo huru cha kushughulikia migogoro au masuala makubwa ya nidhamu. Katiba ya CDM imeweka vikao vya kichama kama sehemu ya kutatulia migogoro kwa kila ngazi ya chama. Kwa maoni yangu, kukosekana kwa chombo huru cha kichama ambacho kinaweza kuhusika katika kusimamia nidhamu kuliko ilivyo sasa ambapo kwa mujibu wa Ibara ya 6.3.6.

Kukosekana kwa chombo huru cha kutatua migogoro na kusimamia nidhamu


Kwa kiasi kikubwa yote yanayotokea sasa hivi ni matokeo ya hili vile vile; kwamba hakuna chombo huru ambacho kinaweza kushughulikia migogoro katika chama, kabla haijakua na chenye uwezo wa kupendekeza hatua za nidhamu kabla mambo hayajafika mbali. Mojawapo ya mambo ambayo yameikoroga sana CDM ni kuwa kusimamia nidhamu kunahitaji vikao vya chama; na vikao vya chama vinahitaji wajumbe na wajumbe ni lazima wafikie idadi inayotakiwa ili kufanya maamuzi mbalimbali. Na kwenye chama ambapo baadhi ya wajumbe wana nyadhifa nyingine nje ya chama wakati mwingine ni vigumu mno kuita vikao kwa wakati na kwa ufanisi unaotakiwa.

Mwisho utaona kuwa hadi matatizo yanapokuwa yamefikia pasipovumilika ndio vikao vinalazimika kuchukua hatua kali – kufukuzana au kunyang'anyana vyeo n.k – wakati kama tatizo lingeweza kushughulikiwa mapema zaidi hali isingefika huku. Fikiria mtu anaweza kuwa na tatizo na wajumbe wa Kamati Kuu na yeye ni Mjumbe wa kamati kuu na kamati kuu hiyo hiyo ndiyo chombo cha nidhamu kwa ngazi hiyo na hivyo kamati kuu hiyo ambayo ndani yake ina watu wanagongana inasimama kumshughulikia mjumbe mwingine.

Au unaweza kuangalia kinyume chake kwamba Kamati Kuu ina tatizo na mmoja wa wajumbe na kwa vile ndiyo chombo cha nidhamu inaamua kumshughulikia wakati huo huo mtu anayehusika naye anatafuta mahali ambapo ni huru (impartial) na anajikuta hana isipokuwa kusubiri kikao cha juu ambacho katika mfumo wa CDM ni kikao cha Baraza Kuu.Tatizo ni kuwa wajumbe wote wa kikao cha Kamati Kuu kwa mujibu wa Ibara ya 7.7.11a nao ni wajumbe wa Baraza Kuu! Yaani mtu anataka kukata rufaa ya kikao cha chini kwenda kikao cha juu ambacho wajumbe wake ni wale wale waliomhukumu kwenye kikao cha chini!

Mfumo huu hata hivyo unazaa chanzo cha pili cha migogoro ndani ya CDM; siyo tu kwenye ngazi ya taifa bali hadi kwenye ngazi za chini kabisa. Chanzo cha tatu kama nilivyosema hapo awali sitaangalia sana. Chanzo kikubwa kabisa na chenye hatari kwa chama ni ukosefu wa nidhamu ambayo nimezungumzia katika sehemu ya kwanza; nidhamu ya chama. Kama tumeliweka jukwaa letu wazi na tukaliona udhaifu wake basi yanayotokea juu yake hayawezi kuwa mema hata kama watu wake watakuwa wamevaa suti, wanaimba kwa furaha au wamevaa magwanda na wanazungumza kwa jazba. Kwamba jukwaa haliko imara yote wanayoyafanya yanahatari ya kuwaangukia na wanaweza kusababisha matatizo hata kwa wasio husika.

Nimesema hapo juu kuwa tatizo hili au chanzo hiki cha mfumo na muundo wa chama kinasababisha tatizo la pili ambalo wote tunaliona. Hili la kwanza linahitaji kutulia na kulichambua kwa kina kuweza kuona jinsi gani linasababisha migogoro lakini hili la pili ni rahisi kulionesha kuwa linasababisha migogoro kwa sababu wahusika wamesimama kwenye mfumo mbovu wa chama; mfumo ambao ulitakiwa ubadilishwe mara tu ya uchaguzi wa 2010; mfumo ambao sidhani kama utabadilika wakati wowote sasa hivi hasa kuelekea uchaguzi wa Serikali ya Mitaa mwakani. Mfumo huu unasababisha tatizo lisilokoma la Utovu wa Nidhamu (Indiscipline).


UTOVU WA NIDHAMU CHANZO KIKUU YA MGOGORO CDM – 3

Tumekwishaona nadharia ya nidhamu ya chama katika mwanzo wa mfululizo huu. Nimeonesha kuwa nidhamu na demokrasia ni vitu ambavyo haviwezi kutenganishwa. Huwezi kuwa na demokrasia ya kweli bila ya kuwa na mfumo mzuri wa kuhakikisha kuwa inakuwepo nidhamu katika chama. Kwamba nidhamu hii inahusu wanachama na chama chao, wanachama na viongozi/viongozi na wanachama na viongozi kwa viongozi.

Nimeonesha pia kuwa muundo na mfumo wa chama unachangia sana kutengeneza mazingia ya kuibuka, kukua na hata kuenea kwa migogoro ndani ya chama. Wakati mwingine katika mazingira ya nchi yetu ni rahisi sana kuituhumu na kuilalamikia CCM kuwa ni ‘chanzo' cha migogoro kama kwa kufanya hivyo kutatufanya tusijiangalie sisi wenyewe ndani tunafanya makosa gani ambayo yanasababisha na kuchochea migogoro. Ni kweli kama nilivyowahi kusema mahali pengine CCM haina nia au sababu yoyote ya kufanya Upinzani nchini uwe na Amani na ukomae; kwani, kwa kufanya hivyo CCM itakuwa inatengeneza mafuta ya kujikaangia. CCM kama chama ambacho kinafurahia madaraka kinajua kwa uhakika kabisa kuwa kukomaa na kupata nguvu kwa CDM ndio utakuwa ni mwisho wake.

Nimeonesha kwa njia ya mfano kuwa kuelewa chanzo cha migogoro ni vizuri kuangalia chama kama jukwaa ambalo juu yake mambo mbalimbali yanafanyika. Jukwaa ndilo linajenga mfumo na muundo wa chama (Katiba na kanuni mbalimbali vyote viko huku) na wanachama na viongozi wanasimama kwenye jukwaa hilo kutekeleza wajibu wao mbalimbali. Kama jukwaa ni legelege au lina nyufa, au limesimamishwa huku limepinda ni wazikuwa kwa kadiri watu wanaongezeka pale jukwaani au kwa kadiri mambo mengi yanafanyika basi uwezekano wa kutoka ajali ni mkubwa. Na kama watu hawajali kunesanesa kwa jukwaa ni wazi kuwa siku moja litawabomokea na kusababisha madhara. Haijalishi nani anasimama kwenye jukwaa hilo hatari iliyopi ni ile ile.

Nikasema kulegalega kwa jukwaa au ubovu wa jukwaa unasababisha tatizo la pili la chanzo cha migogoro; tatizo ambalo naamini ndio sababu kubwa ya migogoro ndani ya CDM. Ukweli ni kuwa huwezi kulitatua tatizo hili la pili kwa ukamilifu bila kutatua tatizo la kwanza kwa ukamilifu kwani japo mtu anaweza kushughulikia tatizo la pili (nidhamu) lakini kama hatoshughulikia tatizo la kwanza (mifumo na miundo) basi anachofanya ni kuahirisha tatizo tu kwani matatizo yale yale ya kinidhamu yatajitokeza tena.

Ni mgogoro wa nidhamu siyo wa madaraka

Baadhi ya watu wengi tu na wengine ni watu wa kuheshimika kabisa wanaamini kuwa mgogoro ulioko CDM sasa hivi ni mgogoro wa madaraka. Kwamba kuna kundi linataka "Uenyekiti" na jingine linataka kung'ang'ania uenyekiti ndio maana kuna mgogoro. Kwamba, kwa vile kiongozi mmoja alitangaza kuwa anataka kugombea urais 2015 tena akisema kuwa ni zamu ya vijana watu waliona kuwa anamlenga mmoja wa viongozi wake ambaye aliyegombea 2010 na ambaye wapo wanaoamini anapaswa kugombea tena 2015. Hapa nawazungumzia Dr. Slaa na Zitto Kabwe – Katibu Mkuu wa CDM na Mbunge wa Kigoma Kaskazini hao.

Naomba kupendekeza kwa msomaji wangu kuwa mgogoro mzima ulioko CDM kimsingi si mgogoro wa madaraka kama wengi wanavyoamini au walivyoaminishwa. Nina uhakika unaweza kushangaa kuwa inakuwaje siyo mgogoro wa madaraka wakati wapo watu tena wazito tu ndani ya chama wanaoona kuwa hili ni suala la madaraka?

Ni vizuri kuelewa kuwa wanasiasa wote duniani wanapenda madaraka. Hakuna mwanasiasa asiyependa madaraka; kila mwanasiasa ambaye anapata nafasi ya kupata madaraka zaidi anaichukua; na ni wanasiasa wachache sana ambao wamekaa madarakani muda mrefu ambao wanaweza kuona wakati umefika kuachia ngazi. Wakati mwingine hata wale ambao wameachia ngazi au kustaafu wanapopewa nafasi ya kupata madaraka tena hawailazii damu; ndio asili ya uanasiasa.

Ni mgogoro unaohusiana moja kwa moja na nidhamu ndani ya chama (a discipline crisis); kwamba kutokana na kutokuwepo kwa mfumo mzuri na usimamiaji mzuri wa nidhamu watu ndani ya chamakila mmoja anaamini anaweza kufanya lolote, popote, kwa yeyote na vyovyote vile.

Mgogoro huu matokeo yake yanaoonekana kila mahali na mengine ni makubwa mno kiasi kwamba kuyaponya kutahitaji hekima, uthubutu na ufundi wa hali ya juu. Mgogoro huu wa nidhamu unajionesha katika kile kinachojulikana kama utovu wa nidhamu (indiscipline) yaani watu kukosa nidhamu na hivyo kutishia namna ya utawala na uendeshaji wa chama. Utovu huu wa nidhamu unajionesha katika namna zifuatazo ambazo ni katika kuzielewa ipasavyo ndivyo pia tutaweza kuona huko mbeleni namna gani mgogoro utaweza kutatauliwa.

1. Kutokukubali Mamlaka ya Juu (Insubordination)
Kila mtu anayefanya kazi mahali – iwe kwenye sekta binafsi au ya umma – analazimika kujiweka chini ya mamlaka nyingine. Ni mfumo wa utawala na menegimenti ambao unataka kuwa watu kutii na kukubali mamlaka yaliyo juu yao ili watimize kazi na majukumu yao mbalimbali. Kukubali huku mamlaka ya juu kunalazimisha watu kutekeleza majukumu yao na pale wanaposhindwa kufanya hivyo basi mamlaka ya juu yao inatakiwa kutoa uongozi na kuwasaidia kufanya hivyo.

Sasa mtu – kiongozi au mtendaji mwingine – anaposhika madaraka fulani hili ni jambo ambalo anatakiwa kulielewa na analazimika kulikubali. Hakuna ufanisi mahali popote pa kazi au katika jambo lolote ambalo watu wanataka kulifanya kwa pamoja ambapo bila kukubaliana kimadaraka litaweza kufanikiwa.

Mtu asiyekubaliana na madaraka ya mtu au chombo kilicho juu yake anaonesha utovu wa nidhamu na kama anakataa kabisa kutii mamlaka ya juu yake mtu huyo ana uchaguzi wa kujiuzulu nafasi yake. Hii inatokea hata pale ambapo mtu anaona hakubaliani na kiongozi au chombo cha juu yake na njia zote za kutafuta suluhu zimeshindikana basi mtu anapaswa kuachia ngazi.

Katika CDM hili tatizo linaanza kujionesha zaidi na zaidi na baadhi yetu tumeona jinsi utovu huu wa nidhamu ulivyojionesha baada ya Kamati Kuu ya Chama kuwavua nafasi za uongozi baadhi ya viongozi wake akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Arusha. Mwitikio wa baadhi ya watu kufuatia uamuzi huo wa Kamati Kuu na agizo kwa wahusika kuandika maelezo yakwanini wasivuliwe uanachama umeonesha huku kutokutii madaraka ya juu ambako ni hatari kwa demokrasia na utawala bora.

Tuchukulie kwa mfano, baada ya wahusika kuvuliwa vyeo vyao na chombo halali jambo pekee walilotakiwa kufanya ni kutekeleza agizo la Kamati Kuu na kusubiri matokeo yake. Walitakiwa siyo tu watafutwe kupewa tuhuma zao (wengine wameziita mashtaka) wao wenyewe walitakiwa hata wazifuate ili waharakishe utetezi wao kwa chombo hicho. Badala yake wakaamua kwenda hadharani kutoa changamoto kwa uongozi uliowaadhibu – insurbodination.

Mtu anaweza akasema sasa ulitaka wasijetetee? Tuchukulie kwa mfano kidogo wa mtu anayefanya kazi kwenye taasisi au kampuni au shirika fulani. Wakubwa wake (sema bodi ya menejimenti) wanaona kuwa kuna jambo haliko sawa na wanataka maelezo ya kwanini jambo hilo haliko sawa na kwanini wasimfukuze kazi. Fikiria mtu huyu badala ya kutekeleza maagizo ya Bodi anaitisha vyombo vya habari na kuwashukia kwa ‘nondo' bodi na kuwaita kila aina ya majina kweli mtu huyo anapaswa kuendelea katika nafasi hiyo. Kimsingi, katika mazingira ya kawaida mtu huyo akifanya hivyo anatakiwa kujiuzulu siyo kuendelea kwa sababu maelekezo ya bodi yake ama hakuyaelewa au aliyapuuza.

Uamuzi wa KK kutaka maelekezo kutoka kwa wahusika ulitakiwa kutekelezwa kwanza kabla ya kulalamika. Wahusika walitakiwa kuandika maelekezo yao na utetezi wao na kusubiri uamuzi wa KK baada ya kuangalia utetezi wao. Kama uamuzi wa KK baada ya hapo unakuwa hasi hatua inayofuatia inachukuliwa yaani kukata rufaa kwa Baraza Kuu na baadaye ikibidi kwa Mkutano Mkuu.

Lakini hili la kutokujiweka chini ya mamlaka ya juu halijaishia kwa ndugu zetu hawa tu tunaliona pia katika viongozi wa chini na sehemu nyingine ambapo CDM imejikuta kwenye mgogoro. Kwa wanaokumbuka yaliyotokea Arusha kwa wale madiwani ambao baadaye walijikuta wanafukuzwa uanachama. Kundi la madiwani wa CDM Arusha waliamua kuingia makubaliano na CCM na kupokea vyeo kwenye halmashauri kwa mujibu wa makubaliano hayo. Madiwani hao walikuwa ni Estomih Mallah (Kimondulu), John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi (Themi), Rehema Mohammed (Viti Maalum), na Crispin Tarimo (Sekei).

Kamati Kuu ya CDM ilitoa maelekezo Julai 18, 2011 kwa viongozi hao kujitoa kwani maridhiano hayo hayatambuliwi na chama na kuwa madiwani hao walifanya hivyo bila kuwashirikisha viongozi wao wa juu. Hata walipoambiwa wajiondoe madiwani wale walijifanya kichwa ngumu (insurbodination) na kutaka kuendelea kiasi cha kulazimisha KK kuamua kuwavua uanachama. Pamoja na kuvuliwa uanachama madiwani wale walifungua kesi kutoa changamoto (challenge) kwa Kamati Kuu, kesi ambayo walipoteza na hatimaye kusababisha uchaguzi mdogo wa madiwani pale Arusha ambao CDM ilitetea viti vyake vyote.

Itoshe kusema tu kuwa mtu unapokubali wadhifa mahali popote unakubali vile vile kuwa chini ya ama waliokupa wadhifa huo au wale walio juu yako. Wakati wowote unapoona hukubaliani na bosi wako au viongozi wako unatakiwa kufuata njia halali za kuonesha hilo na kama hutaki kupoteza muda huo unatakiwa kujiuzulu ukipinga (resigning in protest).

2. Matumizi Mabaya ya Madaraka (Abuse of Power)
Njia nyingine ambayo utovu wa nidhamu unaonekana ni matumizi mabaya ya madaraka ambapo watu wenye madaraka wanajiaminisha kuwa wanaweza kufanya lolote kwa yeyote kwa vile wao wana madaraka. Hili nalo ni jambo baya sana katika taasisi yoyote ile na ni hatari kwa chama cha siasa zaidi kwani kama kiko madarakani wananchi watapata shida nacho (tayari tunaliona hili kwenye CCM).

Kiongozi unapopewa wadhifa fulani unatarajiwa kutumia wadhifa huo kutimiza malengo ya kazi uliyopewa. Ndio maana kiongozi anapopewa madaraka anapewa majukumu yake – yaani mambo ambayo anapaswa kuyafanya kwa wadhifa huo. Na mtu huyo anatakiwa kutekeleza majukumu yake hayo kwa haki, usawa, uwazi na kwa weledi. Wakati wowote kiongozi anatumia wadhifa alionao kufanya visasi, kujinufaisha, kunufaisha marafiki, ndugu na jamaa, au kuwanyanyasa watu wengine kiongozi huyo atakuwa anafanya ‘matumizi mabaya ya madaraka'

Japo mara nyingi tunapozungumza matumizi mabaya ya madaraka huwa tunaangalia kwa watendaji wa serikali lakini ukweli hili ni mojawapo ya matatizo yanayotokea sana na labda bila kushughulikiwa kwenye taasisi binafsi au makampuni binafsi ambapo watendaji wanajiona au wanaamini wanaweza kufanya lolote au kutofanya lolote na hivyo kuchangia kuibuka kwa migogoro.

Sehemu mojawapo ya matumizi mabaya ya madaraka ni kutumia vibaya raslimali za taasisi ama kwa kujipendelea au kwa kupendelea wengine. Lakini pia matumizi mabaya ya madaraka yanatokea pale viongozi au kiongozi anaamua kufanya jambo ambalo hana madaraka nalo kulifanya.

Mfano mzuri ni jinsi Mwenyekiti wa CDM Arusha Samson Mwigamba alivyokamatwa na ushahidi dhidi yake kukusanywa. Kwa yeyote aliyefuatilia kikao cha Kanda ambacho kilimsimamisha madaraka yake ya Uenyekiti wa Mkoa maswali kadhaa yanaweza kuwa yalijitokeza kubwa ni mwongozo gani kikao kilifuata katika kumkamata, kumpekua na kukamata ushahidi (search and seizure)? Kama watu kwenye kikao kwa vile wamehisi mmoja wao anavujisha habari na wanaamua kumkamata na kukamata kompyuta yake na papo hapo kumtolea hukumu (kumsimamisha uongozi) manake ni kuwa kikao ndicho kiligeuka kuwa waendesha mashtaka na hakimu. Hii haijalishi kama madai yalikuwa ni ya kweli; kwamba, watu walitumia madaraka ya kikao kufanya walichofanya ni wazi lazima maswali yajibiwe.

Hata hivyo hili nalo linaweza kuonekana katika kile nilichokisema hapo nyuma – kukosekana kwa chombo huru cha kuchunguza na kufuatilia migogoro na kusimamia nidhamu. Si lazima kiwe chombo cha kitaifa inawezekana hata kwa mfumo wa kikanda chombo cha namna hiyo kikawa katika kila kanda ili kuharakisha uchunguzi na maamuzi.

3. Kujifanyia Mambo Kila Mtu Kivyake (Maverickism)
Kati ya mambo ambayo yanasumbua sana CDM sasa hivi na labda nalo linatokana na hayo mawili hapo juu ya kinidhamu ni viongozi wanapoamua kufanya mambo kivyao vyao. Hili nalo ni sehemu ya matumizi mabaya ya madaraka lakini lapaswa kuangaliwa peke yake. Sijui kama watu wengine wameona hili au wameliona na kulipuuzia ni baadhi ya mambo ambayo yanatokea Bungeni kwenye kambi ya CDM.

Kwa wanaofahamu mfumo wa kibunge (parliamentary system) vyama vya upinzani kama kilicho chama tawala vinafanya kazi kwa mtindo fulani ambao unahakikisha kuwa wapinzani wanakuwa kitu kimoja katika kuibana serikali na hata ikibidi kuiangusha na kulazimisha uchaguzi mkuu. Bahati mbaya katika Tanzania mfumo huu haujatumika vizuri sana.

Kwa upande wa CDM kuna mambo yanafanywa na baadhi ya wabunge wake ambayo yanaonesha kukosekana kwa nidhamu ya kibunge ya kufanya kazi kwa pamoja. Mbunge mmoja anaweza kuwa na hoja nzuri sana lakini inakuwa ni hoja yake na si ya chama. Au utaona mbunge wa chama kile kile cha upinzani (chukulia mfano Godbless Lema) anasimama na kumrushia kijembe mbunge wa chama chake kwa vile hakubaliani naye. Au mbunge wa upinzani anaanzisha harakati za kumuondoa Waziri Mkuu wa Tanzania (hili alilifanya Zitto) bila kutumia mfumo wa kichama.

Labda turudi kwenye Katiba ya CDM Ibara ya 7.7.16 kifungu kidogo cha (u) ambacho kinaelezea mojawapo ya kazi za Kamati Kuu (orodha yote ya kazi za KK nimeziorodhesha hapo juu) na ni nii: Kuandaa hoja za kupelekwa Bungeni na Wabunge wa Chama. Kimsingi, wabunge wa CDM wanapaswa kuanzisha hoja zao kwenye Kamati Kuu ambapo zitapata baraka na wabunge wa CDM wote watatakiwa ama kuziunga mkono – hawawezi kuzipinga. Hoja inapokuwa ni ya chama basi wabunge wake – katika mfumo wetu wa kibunge ambao ni tofauti na ule wa Marekani – wanapaswa kuunga mkono.

Zaidi ya hilo utaona kuwa huko Bungeni usimamizi wa mnadhimu mkuu (sidhani kama ni jina sahihi hili) umechangia kwa wabunge kuja na hoja ‘zao' na wakati mwingine kurushiana vijembe bila matokeo. Jambo moja ambalo zina uhakika nalo ni kama ipo itifaki (protocol) ya kusimamia wabunge wa upinzani chini ya Chief Whip – ambaye ni Tundu Lissu. Ikumbukwe kuwa "Chief Whip" kama jina linavyoashiria ni ‘Mjeredi Mkuu' yaani ofisi ya nidhamu ya kibunge yenye kusimamia wabunge wa upinzani (au kwa chama tawala – anaitwa Majority Whip) kuhakikisha kuwa wanapiga kura kwa kusimama upande wa chama chini ya Ibara ile niliyoinukuu hapo juu. Hili nalo ni jambo ambalo linachangia migogoro kwa kile mtu kujipelekea hoja kwa Spika na sijui hata wabunge wa upinzani wanajua kuwa wanalazimika kupanga mikakati yao na uongozi wao Bungeni. Fikiria Lissu anapopingana na Zitto Bungeni si jambo zuri kwa chama Bungeni; ni dalili ya kila mtu "kivyake vyake". Ni ukosefu wa nidhamu ya Kibunge.

Jingine ambalo nalo limejitokeza na linaonesha tatizo hili ni jinsi ambavyo baadhi ya watu kufuatia uamuzi wa KK kuhusiana na kina kina Zitto walipoamua na wao kutoa matamshi mengine ya kejeli kana kwamba wao ni wasemaji wa Kamati Kuu. Huu ni ukosefu wa nidhamu. Kamati Kuu ina uongozi wake na iliwapa watu fulani jukumu la kuzungumzia maamuzi yake – yaani John Mnyika na Tundu Lissu.

Kinyume chake tumeona baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu nao wakitoa kauli zao nyingine za kuendelea kuwananga hawa na nyingine za kuhoji hata uamuzi wa KK ambayo wao ni wajumbe. Kauli za Prof. Baregu, Mchg. Msigwa na Godbless Lema ni kauli ambazo hazikupaswa kutolewa. Wote walionekana kujaribu kutetea maamuzi ya Kamati Kuu lakini kwa kufanya hivyo wameonesha ukosefu wa nidhamu; KK imetoa maamuzi ambayo yanasubiriwa kutekelezwa. Kama Msigwa au Lema ana shida na kauli za kina Zitto, Kitila na Mwigamba wana na nafasi hiyo katika kikao cha maamuzi.

Katika mazingira mengine hawa waliotoa kauli zao hizi zenye kuonesha upendeleo (bias) ya aina fulani wanatakiwa wajitoe kushiriki katika kikao kitachojadili barua za maelezo (statements) za Zitto na wenzake. Hii ni kuhakikisha kuwa wanachama hawa wanatendewa haki.

Siyo kwa hawa tu ambao ni wabunge; wengine kutoka mikoani nao wakaanza kutoa kauli zao na wao ni viongozi wa chama ati wanapinga "maamuzi ya Kamati Kuu". Kama nilivyosema hapo juu kuhusu surbodination. Ni matumaini yangu ofisi ya Katibu Mkuu itakuwa imewaandika barua viongozi hawa na kuwataka watoe maelezo au wajiuzulu. Wanachama wa kawaida wanaweza kutoa maoni haya tena kwa ukali wote kama wale waliojitokeza Kigoma kupinga ziara ya Katibu Mkuu – natumaini hakuwepo kiongozi wa ngazi yoyote. Viongozi wa CDM – ngazi yoyote ile – anapaswa kuheshimu vikao vya ngazi zote za chama na hasa vikao vya juu yake; unapokuwa na kiongozi – wa mkoa au jumuiya ya chama anasimama na kupinga hadharani maamuzi ya Kamati Kuu kiongozi huyo anapaswa kujiuzulu au kufukuzwa – vinginevyo, kila uamuzi wa Kamati Kuu au kikao chochote cha juu utajikuta unapingwa na watu ambao wataona mtu au watu wao wameathirika. Itaendeleza migogoro isiyo ya lazima. Ni lazima watu wajifunze kuheshimu madaraka yaliyo juu yao kwani wao pia kama viongozi wakati fulani wataitwa kuchukua maamuzi ambayo wasipoangalia wataona yanapingwa na viongozi wenzao.

Kama kiongozi yoyote ana tatizo na uamuzi wa chombo cha juu yake anapaswa kuandika kwa chombo hicho au chombo husika kuonesha malalamiko yake na kama anaona hawezi kuendelea uamuzi mzuri ni kujiuzulu na kuondoka kama alivyofanya Makamu Mwenyekiti wa CDM (Bara).

Nitaangalia Jumatatu hili suala la nidhamu kwa kuangalia viongozi watatu ambao wako katika kiini cha mgogoro huu, Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dr. W. P. Slaa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe.


PEMBETATU YENYE MATATIZO – 4

Tujikumbushe kidogo tulikotoka. Tumeona kuwa nidhamu ya chama ni msingi wa chama kufanya vizuri katika kutekeleza majukumu yake na mipango yake. Kwamba, bila nidhamu ni vurugu na hakuna taasisi yoyote ile inayoweza kukamilisha majukumu yake bila kuwa na nidhamu. Nimeonesha kuwa nidhamu hii ina pande nyingi – wanachama kwa chama, wanachama kwa viongozi-viongozi kwa wanachama, na viongozi kwa viongozi.

Nimeonesha pia kuwa mojawapo ya matatizo makubwa yanayoikabili CDM leo hii ni lile linalohusiana na mfumo na muundo wake ambao ulinakiliwa ukiwa na makosa kutoka CCM. Nimeonesha pia kuwa mfumo huu au muundo huu unazaa matatizo makubwa sana kwenye chama na kubwa kati ya hilo ni utovu wa nidhamu. Nimeonesha jinsi ukosefu wa nidhamu unaweza kujitokeza katika chama kama kwa kutokutii madaraka ya juu, matumizi mabaya ya madaraka, kujifanyia mambo kila mtu kivyake vyake n.k

Katika sehemu hii ya nne ambayo naamini itakuwa ngumu kwa baadhi ya watu – lakini ya lazima – nitajaribu kuonesha kama nilivyoahidi jinsi gani uongozi wa Freeman Mbowe, Dr. Wilbrod Slaa na Zitto Kabwe kwa namna mbalimbali umechangia kuacha migogoro ikue na kuenea na hatimaye kutishia umoja wa chama na njozi ya CDM kuing'oa CCM madarakani. Kuweza kuelewa uzito wa hoja yangu hii ninatumaini msomaji atakuwa amesoma makala yangu ya Oktoba 18, 2010 kuhusiana na "Pembetatu ya Ushindi Kuelekea Kuyatikisa Malango ya CCM".

Hata hivyo, kabla sijazama kuwaangalia viongozi hawa watatu na maoni yangu jinsi ambavyo wanaongoza naomba niwachepushe pembeni kidogo kuangalia vitu viwili muhimu sana katika utawala wa demokrasia na ambavyo naamini vinahusiana pia na migogoro katika CDM na bila ya shaka katika vyama vingine vile vile.

Kupinga na Demokrasia (Dissent and Democracy)


Kipimo cha demokrasia ya kweli siyo jinsi watu wanavyoubaliana na wengi bali zaidi jinsi watu wanavyoweza kupingana na wengi. Kupingana na maoni ya wengi au maoni yaliyokubalika na wengi ni kipimo cha jinsi gani demokrasia au mfumo wa demokrasia unafanya kazi. Katika tawala za kibabe (tyrannical regimes) watu wanalazimishwa kukubaliana na maoni ya watawala au ya wengi na kupingana na maoni hayo kunaweza kumfanya mtu aonekane ni adui wa dola (enemy of the state). Tawala zote za kibabe duniani hazikubali kupingwa.

Katika demokrasia watu wasiokubaliana si lazima wawe na uadui wa kutokukaribiana katika mambo mengine. Tofauti ya maoni si sababu ya watu kuwa na tofauti ya moyoni. Mojawapo ya vitu ambavyo vinasumbua sana demokrasia yetu changa ni kutokuelewa ukweli huu kuwa watu wasiokubaliana si lazima wagombane au watengeneze uadui wa aina fulani. Hii ni kweli zaidi hasa ndani ya chama ambapo watu wanaweza kuwa na maoni tofauti juu ya jambo fulani na watu hao wakaonekana kuwa ni adui wa chama. Leo hii katika siasa zetu watu wanaodai kuamini katika demokrasia wanajikuta wanatofautiana kiasi cha kujenga uhasama ambao ni vigumu kuona jinsi gani utaweza kuondolewa na mahusiano kuponywa.

Kwa zaidi ya miaka kumi na tano ya kufuatilia kwa karibu siasa za Tanzania, wanasiasa wake namwelekeo wa kisiasa wa nchi naweza kusema kuwa mahusiano ya wanasiasa wetu yamefika mahali pabaya na wakati umefika tuanze kuwalazimisha kurudi kwenye staha, kuheshimiana na kujenga tunu ya kupingana bila kupigana. Siasa zetu sasa hivi zimefika mahali kuwa watu wanapokosoana huishia kukosana; yaani hakuna tena kukosoana bila kukosana. Na siyo tu watu wanakosana bali wanajenga uhasama wakati mwingine wa wazi kabisa kisa ni tofauti za kimtazamo au mwelekeo. Kwa upande wa CDM (kama ilivyo hata ndani ya CCM) baadhi ya viongozi na wanachama wamefika mahali wana uadui wa wazi.

Sisi tunaopitia mitandao mbalimbali na kusoma maoni ya watu mbalimbali tunaweza kuona jinsi watu walivyogawanyika makundi tena makundi ya uhasama wa kibinafsi. Katika nchi zenye demokrasia makundi ya kisiasa yanafuata itikadi na sera za mtu na hayaachwi kufikia uhasama wa wazi na uadui usiokoma. Kwa watu wetu leo hii mtu akitofautiana na mwingine mara moja anaanza kuitwa majina na huku yeye naye anaita wengine majina na wote wakiwa na watu wanaowaunga mkono ambao nao huingia katika huu uhasama kumlinda mtu au watu wao.

NI siasa za uhasama; ni watu walioshindwa kufuata kanuni ya kukubaliana kutokukubaliana na badala yake waliposhindwa kupingana kwa hoja sasa wanapigana kwa vioja! Hili ni muhimu kuliangalia kwa sababu tutakapowaangalia hawa wanasiasa wetu watatu maarufu nina uhakika kabisa mwitikio wa baadhi ya watu utakuwa ni "Mwanakijiji ana chuki na mtu witu"; wengine hawatochelewa na kusema "Tunajua Mwanakijiji ni mtu wa nani". Leo hii watu wanapima hoja ya mtu siyo kutokana na ukweli na ushahidi wa hoja yenyewe bali wanapima kwa kuangalia nani kasema. Na mara moja wanaamua ukweli wa hoja kwa kuangalia aliyesemwa ni nani kwani kama kasemwa ‘fulani' basi aliyesema ni mtu wa ‘fulani'! Ni fikra muflisi kwani zinatokana na woga usio na sababu.

Mtu anapokosoa si lazima awe mtu wa fulani na kwa kweli ni udhaifu mkubwa kwa mtu mzima kujenga hoja kwa kufuata watu (personalities); kwamba Ni lazima watu wajifunze kutofautiana tena hata kwa mambo makubwa kabisa lakini bila ya kufika mahali pa kujenga uadui. Udhaifu mmoja wa wanasiasa wetu ndio huu; mtu ambaye anaamini ni maarufu anapokosolewa na labda kwa ukali mara moja huingia katika hali ya kujihami (defensive posture) na kuona kuwa ameshambuliwa na hivyo aliyemshambulia kawa kambi ya adui. Matokeo ya hili kama tutakavyoona punde ni kuwa wanasiasa wetu wamejitahidi kuhakikisha wanazungukwa na marafiki zao na watu wanaokubaliana nao kila kitu; akijitokeza kati yao akionesha tofauti tu basi mara moja anaanza kutengwa na hata kuanza kushukiwa. Hapa ndipo siasa zetu zilipofika.

Mwanasiasa anayezungukwa na watu anaokubaliana nao tu au ambao hawawezi kuhoji mawazo yake kwa sababu hawataki kumkwaza ni mwanasiasa ambaye hajitakii mema kwani anajinyima fikra mbadala na hoja za kikosoaji ambazo ni muhimu kuweza kulifikiria jambo kwa kina.

Kukubaliana na Demokrasia (compromise and democracy)


Jambo la pili ambalo ningependa kuliweka bayana ni kuwa si lazima hoja za mtu zikubaliwe ili iwepo demokrasia. Msemo mmoja niliouanzisha miaka kadhaa nyuma ni ‘hoja hujibiwa kwa hoja si vioja'. Msingi wa kauli hii ni kuwa hoja inapotolewa inatakiwa ijibiwe kwa hoja nyingine na wakati wowote watu wanaacha kujibu na kuanza kumshambulia mtoa hoja au kuleta mambo yasiyo husiana na hoja manake ni kuwa wameshindwa hoja na hawataki kukubali tu. Unapotoa hoja kwa mwanasiasa au hata kwa mtu mwingine yeyote yule si lazima hoja hiyo ikubaliwe ndio uamini kuwa na wewe (mtoa hoja) unakubalika.

Mojawapo ya matatizo ambayo yatatusumbua sana ni kuwa watu wanapotoa hoja za aina fulani hata kama ni nzuri kiasi gani wanatarajia zikubaliwe na zinapokataliwa wao wenyewe wanafikiria ndio wamekataliwa. Ni muhimu basi kuelewa tofauti kati ya hoja na mtoa hoja. Mara nyingi ninaposoma kwenye mitandao mbalimbali jinsi watu wanavyojibiziana huwa naangalia kwa mshangao kwani hata baadhi ya watu ambao wanaonekana ni wasomi wanashindwa kutofautisha kiurahisi kabisa kati ya hivi viwili. Hoja ya mtu ni hoja tu inaweza kuwa nzuri inaweza kuwa mbaya; inaweza kuwa ina mchanganyiko wa yote n.k.

Jukumu la watu wanaoisikiliza hoja hiyo ni kuichambua na kuiona mambo yako mazuri (merits) na kuona matatizo yake na kuona kama inaweza kuboreshwa zaidi. Unapotoa hoja basi usitarajie ni lazima ikubaliwe jinsi ilivyo na kuwa kama ikikubaliwa na kufanyiwa marekebisho (madogo au makubwa haijalishi) basi huini tena kama ni hoja yako. Hii si sawasawa. Ni lazima wanasiasa wetu na hasa katika upinzani wajifunze Sanaa ya kukubaliana na wengine (compromise).

Nimesema hapo juu kuhusu kupinga kama alama mojawapo ya demokrasia alama nyingine (kati ya nyingi) ni ule uwezo wa watu kukubali kubadilisha mawazo na hata kubadili msimamo. Hapa sizungumzii kubadili kanuni za msingi za mtu bali nazungumzia kukubaliana kuchukua kidogo kuliko kikubwa ambacho mtu aliamini anastahili. Ni sawasawa na mtu anapoenda kununua kitu na anajadiliana na mchuuzi hadi wanafikia bei ambayo wote wawili wanaona inafaa; bei ambayo bado inampa faida mchuuzi lakini pia si mzigo mkubwa kwa mnunuzi. Ukiangalia siasa zetu leo hii hili ni mojawapo ya mambo ambayo hayatokei sana; zaidi utaona ni kuwa watu wanapeana misimamo mikali – ama iwe hivi au vile; kubali yote au kata yote (all or nothing). Hii siyo siasa ni sayansi tena ya hisabati ambapo 2 + 2 mara zote ni 4 haijalishi kama anayejumlisha yuko Ujerumani, Ileje au Tokyo!

Hili ni jambo muhimu sana kulielewa kama tunataka kweli kujenga demokrasia. Kwa upande wa CDM hili nalo ni jambo ambalo linawasumbua sana hasa pale ambapo mtu anaamini ana hoja nzuri na anaona hoja hiyo haikubaliki sana na wengine. Au pale ambapo watu wanapoona fulani katoa hoja basi hata kuiangalia hawaiangalii na kuona uzuri wake au namna ya kuiboresha badala yake wanaitupilia mbali. Mambo haya mawili ni muhimu sana kuyaelewa; wanasiasa wetu wajifunze kukubaliana kutokukubaliana, kupingana bila kupigana, na kukosoana bila kukosana. Kwamba ni katika tofauti ya mawazo ndipo mawazo bora zaidi yanapatikana; hakuna mtu mwenye ukiritimba wa mawazo (ukiondoa mimi); na hakuna mtu ambaye mawazo yake yanaweza kuangalia kila kitu.

Lakini pia ni muhimu tujifunze kupokea na kutoa, tujifunze diplomasia ya kukubali kuachilia na wakati mwingine kushikilia; mwanasiasa asiyejua kucompromise atafute fani nyingine; kwani wengine wanasema siasa ni sayansi ya kucompromise. Leo unashinda, kesho unashindwa n.k. Huu mtindo wa lazima nipate, au lazima nikubaliwe unasababisha migogoro na husda, na wakati mwingine huzuni.

Wanasiasa wetu watatu

Kama nilivyosema nitajaribu kuwaangalia wanasiasa wetu watatu ambao kwa kweli naamini wataamua hatima ya CDM. Niliahidi kuwaangalia wanasiasa wetu Freeman Mbowe, Dr. Wilbrod Slaa na Zitto Kabwe na jinsi gani hawa watatu wana nafasi ya pekee katika kumaliza migogoro ndani ya chama. Kama umenisoma vizuri hapo juu unaweza ukawa umeelewa jambo moja kwamba CDM ina makundi ambayo yamezunguka watu na hasa viongozi hawa watatu. Na inawezekana ikasemwa kwa haki kabisa makundi yenyewe hasa ni mawili; lipokundi ambalo liko nyuma ya Mbowe/Slaa na lipo kundi ambalo liko nyuma ya Zitto Kabwe.

Kati ya makundi haya mawili yapo makundi madogo madogo ambayo nayo yamefuata wanasiasa mbalimbali, wanasiasa ambao nao wamejipanga (align) na makundi haya mawili. Kwa mfano, wapo watu wanaomuunga mkono Mbunge wa Arusha Godbless Lema kwa kadiri ya kwamba Lema amejipanga upande wa kundi la Mbowe/Slaa. Tuliona kundi la vijana wa CDM ambao walionekana kujipanga nyuma ya Zitto Kabwe na pamoja nao baadhi ya makundi kuanzia makao makuu hadi mikoani. Yote haya ni matokeo ya watu kutokuelewa kanuni hizo hapo mbili; na kwa kadiri ya kwamba watu wataendelea kutokuzikubali kanuni hizi (ama kwa kutokujua au kwa kiburi) basi migongano baina ya wanasiasa wetu haitokoma.

Sifa Kuu za Wanasiasa Wetu Watatu

Kabla sijaangalia matatizo ya kila mmoja – kwa maoni yangu – naomba nioneshe tu kuwa wanasiasa wetu hawa watatu wote wana sifa ambazo zinalingana kwa kiasi fulani na pia kuna mambo ambayo yanaonekana kwa wote.

1. Wote ni wazungumzaji wazuri: Ninapozungumzia uzungumzaji nazungumzia ule uwezo wa mtu kusimama kwenye jukwaa mbele ya kadamnasi na kuwavuta wasikilizaji wake kwa namna anavyozungumza. Ni watu ambao ukiwasikiliza wanaweza kukufanya ulengwe na machozi kwani wanazungumza "kwa hisia kali". Naweza kusema ni miongoni mwa watu wenye vipaji vya kuzungumza.

2. Wote ni wajenga hoja wazuri: Watu wengi wanauwezo wa kuzungumza na kuvutia watu; utawakuta watu wa namna hiyo kwenye vilabu hata mtaani tu vijiweni. Lakini ni tofauti mtu kuweza kujenga hoja; yaani kupangilia mawazo vizuri kwa kufuata mantiki na kutoa hitimisho linaloonekana kukubalika (plausible argument). Mbowe, Slaa na Zitto ni wanasiasa ambao wanajua kujenga hoja toka mwanzo wake hadi mwisho wake. Hata kama wakati mwingine wanaweza kufanya makosa katika hoja (fallacious argument) bado hoja zao zinaweza kuvuta watu wengi na kwa vile watu wengi hawaangalii sana hoja zilivyo wanasiasa wetu hawa wanavuta watu wengi sana kila wanaposimama kuzungumza au kwa maandishi yao.

3. Wote wana ujiko wa kipekee wa kisiasa: Mbowe kama kiongozi mkuu wa chama ana ujiko wa pekee hasa kwa jinsi alivyokipokea chama kutoka kwa waliomtangulia na kukifikisha kilipofika. Dr. Slaa kwa upande wake anasimama katika jukwaa la peke yake kwa umahiri wake wa kukiwakisha katika hoja ya ‘mafisadi' kuanzia Bungeni (sakata la Balali) hadi pale Mwembe Yanga alipoa ile orodha maarufu ya mafisadi na kwa hakika alipojitokeza kuacha ubunge na kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zitto naye ana ujiko wa aina yake akiwa mwanasiasa kijana zaidi aliyelitetemesha Bunge la Muungano na kuandika historia pale ambapo Wabunge wa CCM walipomuona tisho na kuamua kumfungia kufuatia sakata la Buzwagi. Na ameendelea kuibua hoja mbalimbali na kujijenga kwenye hoja mbalimbali (kama ya kujaribu kumwondoa Waziri Mkuu au suala la kukataa posho).

4. Wote wana makundi yanayowakubali kwa kiasi kikubwa hata kwa kiapo: Kama nilivyoonesha hapo juu wanasiasa wetu watatu wana makundi ya watu wanaowakubali, kuwafuata na kuwatii wakati mwingine hadi kupitiliza. Kwa miaka miwili sasa nimekuwa nikiwasoma watu mbalimbali wa makundi haya mawili wakijibishana na kubishana kwenye mitandao na tofauti kati yao ni kama mwanga na giza; makundi haya kwa kiasi kikubwa naamini yamechangia sana katika kukoleza tofauti baina ya kambi hizi mbili kubwa ndani ya CDM. Hata hivyo, kukubaliwa na makundi ya watu si jambo baya katika siasa ndio maana nimeliweka hili kama sehemu ya mambo ambayo wote wanayo. Hapa sijali sana usahihi wa kuwa na makundi au la; kwamba makundi yapo ndio hoja yangu.

5. Wote wanajionesha wanaipigania Tanzania na watu wake: Wanasiasa wetu hawa watatu bila ya shaka wamejipambanua kwa namna mbalimbali kuwa wanaipigania Tanzania. Wote hawa wamesimama kwenye majukwaa kutujulisha Watanzania kile ambacho utawala wa CCM umefanya au umeshindwa kufanya; tumewakubali kwa vile wameonesha ujasiri ambao hatukuwahi kuuona kwa wanasiasa wetu kabla. Tukiwahukumu kwa haya ambayo wameyafanya hakuna shaka kuwa wamejipambanua kama wanaharakati wa Tanzania Mpya Inayowezekana.

6. Wote wanajionesha kuwa wanaipenda CDM kweli kweli: Hapa siwezi kusema mengi kwani hili linajisema lenyewe. Hata hivyo, licha ya sifa hizo hapo juu kati ya nyingie nyingi wanasiasa wetu ukiwaangalia mmoja mmoja utaona sifa ambazo zimechangia kuanzisha na kuchochea migogoro. Sifa hizi zaweza kuwa ni kwa sababu ya nyadhifa zao ndani ya chama na ujiko wao wa kisiasa (political clout) ambayo wote wanayo kama nilivyoonesha hapo juu. Naomba niseme tu kuwa katika kuuelewa mgogoro huu na kuutafutia suluhisho la kudumu ni vizuri niwaangalie mmoja mmoja na nitoe maoni yangu juu ya uongozi wao, sifa zao za kiuongozi na maoni yangu kwa nini naamini sifa hizi zote (nzuri na mbaya) zimechangia mgogoro CDM. Nitaanza na Mwenyekiti Freeman Aikaeli Mbowe.

(Itaendelea Kesho In Shaa Allah)
 
Kazi nzuri MMKJ...

Ila nikukumbushe kuwa nchi yetu haina mfumo WOWOTE, either wa siri au wa wazi wa kulea na kukuza VIONGOZI. Tusitarajie kupata viongozi bora kama tumewalea hovyo hovyo.

Hawa vijana wa sasa wenye tamaa ya hali ya juu ya madaraka hawana nidhamu ya uongozi, hawakulelewa kokote kule kuwa viongozi. Wengine walibatizwa kwa moto, kwa kupata ubunge wakati wakiwa hawajawahi hata kuajiriwa.

Kwa mfumo huu tutegemee nchi yenye viongozi duni zaidi miaka ijayo, hasa sisi vijana wa sasa...
 
Ni matumaini yangu, makala itasaidia kunielewesha juu ya tofauti kati ya Nidhamu ya uoga na nidhamu halisi.

Itaelezea kwa kina je kutokutii Amri haramu ni sehemu mojawapo ya nidhamu?.

Je nidhamu ya kijeshi ni Universal?, kwamba hiyo hiyo ndiyo inayotakiwa katika orgization za kisiasa, au hata bureaucratic institutions?.

Na pia Itasaidia kuelezea mchakato wa haki, ni utaratibu gani ambao ni mujarrab wa utoaji haki kwa mwanachama, ili isije ikawa kutofautiana na mwanachama fulani ikachukuliwa kuwa umetofautiana na Chama kizima.
 
Wakuu,

Hii hoja ameleta Mwanakijiji ni msingi saana, ni moja ya nakala ukisoma, ikasomwa na ile ya Duru ya Siasa inayo endelea pale Great Thinkers (https://www.jamiiforums.com/great-t...-kambi-ya-upinzani-chadema-3.html#post8060971)Chadema wanaweza kabisa ku reform for the better toka walipo hapa (pabaya) kuelekea kuimarika zaidi. 2015 Siyo mbali.

Kuna members ambae akijibu hoja kwa kuendeshwa na hisia ama ushabiki humshangai sababu hakuna mahala umewahi kuona akijenga hoja hivyo uwezo wake wa kuchambua na kutazama mambo unakua hujui, uchakulia uwezo wake wa kuwakilisha ni mdogo hivyo hashangawi.

Inapotokea hoja ya msingi na makala nzuri kama hii aliyoweka leo Mwanakijiji akaja mzoefu wa Jukwaa kama ZeMarcopolo ama Tuko ambao nawajua vema kwa uchambuzi makini wakiamua wakaweka hoja za ku divert mjadala, huwa nasikitika saana. Na zaidi nawasikitikia Watanzania wengi ambao wanahitaji ukombozi toka kwa wale wenye uwezo wa kuwakomboa lakini badala yake nafasi hiyo inatumika vibaya.

Tuache ushabiki na tubadilike. Tujadilini hoja, tujifunze, na kujifunza kunakuja hata kwa kufuatilia na kuwa msomaji si lazima kila mmoja aka post (hili ni kwa wale wanaojibu kila kitu kwa kuendeshwa na hisia).

DISCLAIMER: Kaka zangu sisemi kua hizi ni tabia zenu, nimegusia sababu hapa ndicho mlichokifanya; ikiwa nimewakwaza naomba in advance mnisamehe.

Mzee Mwanakijiji, this is a great written peace. Looking forward to itakavyoendelea.
 
Wakuu,

Hii hoja ameleta Mwanakijiji ni msingi saana, ni moja ya nakala ukisoma, ikasomwa na ile ya Duru ya Siasa inayo endelea pale Great Thinkers (https://www.jamiiforums.com/great-t...oro-kambi-ya-upinzani-chadema-new-post.html); Chadema wanaweza kabisa ku reform for the better toka walipo hapa (pabaya) kuelekea kuimarika zaidi. 2015 Siyo mbali.

Kuna members ambae akijibu hoja kwa kuendesha na hisia ama ushabiki humshangai sababu hakuna mahala umewahi kuona akujenga hoja hivyo uwezo wake wa kuchambua na kutazama mambo unakua hujui, uchakulia uwezo wake wa kuwakilisha ni mdogo hivyo hashangawi.

Inapotokea hoja ya msingi na makala nzuri kama hii aliyoweka leo Mwanakijiji akaja mzoefu wa Jukwaa kama ZeMarcopolo ama Tuko ambao nawajua vema kwa uchambuzi makini wakiamua wakaweka hoja za ku divert mjadala, huwa nasikitika saana. Na zaidi nawasikitikia Watanzania wengi ambao wanahitaji ukombozi toka kwa wale wenye uwezo wa kuwakomboa lakini badala yake nafasi hiyo inatumika vibaya.

Tuache ushabiki na tubadilike. Tujadilini hoja, tujifunze, na kujifunza kunakuja hata kwa kufuatilia na kuwa msomaji si lazima kila mmoja aka post.

DISCLAIMER: Kaka zangu sisemi kua hizi ni tabia zenu, nimegusia sababu hapa ndicho mlichokifanya; ikiwa nimewakwaza naomba in advance mnisamehe.

Mzee Mwanakijiji, this is a great written peace. Looking forward to itakavyoendelea.

Sawasawa,

Tuendelee kuwa pamoja...
 
Well said Mwanakijiji, wasioamini waamini ya kwao CDM wasonge mbele, hatuwezi kufika kule ambako Waziri Mkuu anaamini watu wana nguvu kuliko serikali eti analiambia Bunge tukiwachukulia hatua mafisadi wa RICHMOND nchi itatikisika, kweli nchi itatikisika kwa kuwachukulia hatua waovu?

Reagan alikuwa mwanachama mzuri sana wa Democrtas lakini hakukidhi vigezo na wala hakusimamia misingi ya chama na pamoja na umaarufu wake democrats walimwambia atafute jukwa atakalosemea mambo yanayopingana na democrats' Values ndipo akaenda REPUBLICAN na hatimae kuwa RAIS WA US
 
nasubiri uchambuzi wa namna viongozi wakuu wa CDM wamekuwa chanzo au vichocheo vya mgogoro.

1. Je itahusu ziara ya slaa kigoma wakati huu ambao tunajua lazima ingeleta mnyukano?
2. Je, itahusu namna walivyotoa ile nyaraka ya kina mkumbo hadharani?
3. Je, itahusu ukweli kwamba mbowe kama mwenyekiti kwa muda mrefu sana, kwa maaelezo kwamba wanachama bado wanamkubali?
4. je, itakua kuhusu tetesi tunazosikia kwamba katiba imebadilishwa kidogo ili kuondoa ukomo wa uongozi? hasa wa juu?
 
nasubiri uchambuzi wa namna viongozi wakuu wa CDM wamekuwa chanzo au vichocheo vya mgogoro.

1. Je itahusu ziara ya slaa kigoma wakati huu ambao tunajua lazima ingeleta mnyukano?
2. Je, itahusu namna walivyotoa ile nyaraka ya kina mkumbo hadharani?
3. Je, itahusu ukweli kwamba mbowe kama mwenyekiti kwa muda mrefu sana, kwa maaelezo kwamba wanachama bado wanamkubali?
4. je, itakua kuhusu tetesi tunazosikia kwamba katiba imebadilishwa kidogo ili kuondoa ukomo wa uongozi? hasa wa juu?

Mtu ukishajua anasimamia upande gani hakupi shida.

This is politics. Kuna watu wanajifanya pundits lakini the truth of the matter ni kwamba wako kwenye "marketing".

Huwezi kufanya upembuzi yakinifu kabla hujafanya declaration of interest, ili wasomaji wawe aware wanasoma mawazo ya mrengo gani.

This analysis will not be neutral.
 
MZEE m/ k umewaza na kuwazua ndani ya cdm hakuna mgogoro babu 1. Ukabila 2. Tamaa ya madaraka 3. Kutawala hazina. Haya mambo matatu yameuuwa imani za watu wenye ufahamu mzuri. Sasa tafuteni wanasiasa wa kweli co vibaya kuanza moja. MF kuchukua posho na kufanya shopping za family yake mtu. Kunajimbo moja wanapokea posh halmashauri na Mbunge bungeni anatia ndani kisha kwenye majuuuu KWA hawaitii serikali sasa co wizi huo wa kimacho macho. Chama kinakufa kwa ujinga tu.
Co kila cku utamdanganya MTU mwenye akili timamu. Hila imegundulika mnajennga majumba na pesa za kodi kisha hamtendi haki mnaumbuka sasa
 
Mzee Mwanakijiji andiko lako ni zuri sana. Naomba nisubiri umalize nyaraka zote. Kwa sasa nauchukulia kama "waraka wa kwanza wa mwanakijiji wa wanachadema"

Nachaweza kusema nje ya nidhamu katika chama, hii race ya white people wanaendelea kwa sababu ya "nidhamu" wanaheshimu muda, kazi, promise, uongozi etc.

Nasuburi umalize nikujibu vizuri.
 
Last edited by a moderator:
Kinachonishangaza ni hiki pale wanachama/viongozi wa chama tawala wanapokwenda kinyume na nidhamu ya chama tunawapongeza na kuwaona mashujaa wa demokrasia lakini hali hiyo hiyo ikitokea upinzani tunawaona ni wasaliti.
 
Mzee umeanza vizuri. Nimependa ulivyochambua maana ya nidhamu na kuhusisha nidhamu na demokrasia. Umewasha moto wa kutaka kusoma zaidi. Tafadhali endelea na ujaribu kwa nguvu zote bila kushabikia yanayoendelea huko CDM na wala kuona na kusikia yanayorushwa dhidi ya CDM, ili mwishowe tupate kujifunza wapi tumejikwaa na jinsi ya kutoka hapo. Nasema haya sio kama mpenzi wa CDM (na wala sijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa!) bali kwa ajili ya kupanga jamvi nzuri kwa viongozi wetu wajao- maana kama alivyosema mmoja wetu hapo juu, tatizo taifa halijaandaa viongozi!

Wakati ule wa awamu ya kwanza kulikuwepo na mada nyingi sana zilizohusu uongozi (leadership) na mengi yalitokana na nadharia za kina Marx na Engels ambao walikuwa na upeo mkubwa kuona jinsi gani matabaka katika jamii yanavyoweza kujitokeza na kuharibu mifumo na jinsi gani yanavyoweza kutumika kurekebisha na kuboresha mfumo. Kwa bahati mbaya sana wafuasi wa Keynes wamefanikiwa kabisa kuonyesha fikra za hawa wakonge ambao waliwaita wakomunisti hazina matinki na leo hii hata humu ndani ukizungumzia nadharia hizi unaweza ukapewa majina.

Makongomano mengi ya vijana nchini yanazungumzia 'fursa' tu, ni 'fursa' au 'nafasi' za vijana katika taifa, tena zinaingiliwa na wasanii ambao taifa halijawaandaa ambao wao wamekuwa raisi kufikia jamii kwa sauti nzuri walizojaliwa na Muumba wao- lakini kwa kuwa hawajaandaliwa hupotosha hata ile maudhui ya fani yenyewe. Ni nadra sana hata kwenye makongomano ya vijana sio ya ujumla tu hata ya dini kuona wanazungumzia 'uongozi' kama mada muhimu (leadership and social responsibility)
 
Mtu ukishajua anasimamia upande gani hakupi shida.

This is politics. Kuna watu wanajifanya pundits lakini the truth of the matter ni kwamba wako kwenye "marketing".

Huwezi kufanya upembuzi yakinifu kabla hujafanya declaration of interest, ili wasomaji wawe aware wanasoma mawazo ya mrengo gani.

This analysis will not be neutral.

Nimesoma soma comments za Mzee Mwanakijiji baada ya hili sakata, alikua ali-like sana yale matamko ya habari maelezo, nasubiri sana analysis yake.
 
Back
Top Bottom