Kuuelewa Mgogoro wa CHADEMA - 5: Wanasiasa Wetu Watatu - Mbowe, Slaa na Zitto...

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,987
Ni mwendelezo kutoka Makala ya Kuuelewa Mgogoro wa CHADEMA. Kama hujasoma sehemu ya kwanza hadi ya 4 unaweza kupata shida kuona nimefikafikaje hapa. Nashauri upitie mada ile kwanza uweze kufuatana name katika mtiririko huu wa hoja.

1. Mwenyekiti wa CHADEMA Bw. Freeman A. Mbowe
Bila ya shaka Freeman Mbowe amesimamia mafanikio mengi ambayo yameipaisha CDM mbele ya umma wa Watanzania. Chini ya uongozi wake chama kimekuwa kwa kila kipimo na kimeendelea kuvutia maelfu ya watu kila kona ya nchi. Huwezi kuzungumzia mafanikio ya CDM bila kumtaja Mbowe; amejitolea mengi na amefanya mengi kuifikisha CDM ilipofika. Hata hivyo siyo kusudio langu kupeana mashada ya maua leo hii nitaacha hili kwa siku nyingine, inshallah.
Mojawapo ya mambo ambayo nilitaka kuyafanya wakati naanza kuandika makala hizi ni kuwaanglaia viongozi hawa kwa kupima yale wanayoyafanya kwa kuangalia majukumu yao ya Kikatiba. Hata hivyo, kama nilivyosema kwenye suala la muundo na mfumo wa chama CDM kwa sababu isiyoeleweka haijaanisha majukumu au kazi za kila kiongozi wa taifa ndani ya Katiba yake.* Katiba imeweka nafasi za “viongozi wa taifa” kwenye Ibara ya 7.7.3 ambapo wanaotajwa kuwa ni viongozi wa taifa ni:

Mwenyekiti wa Taifa
Makamu Mwenyekiti Bara
Makamu Mwenyekiti Zanzibar
Katibu Mkuu
Naibu Katibu Mkuu Bara
Naibu Katibu Mkuu Zanzibar


Hata hivyo Katiba haielezi majukumu ya kila mmoja kama ambavyo Katiba ya CCM inasema kuhusiana na viongozi wake kuanzia kwenye Ibara ya 117 ya Katiba yake. Inawezekana majukumu na kazi za viongozi hawa zimeanishwa katika nyaraka nyingine za chama; hata hivyo binafsi naamini kuwa kazi hizi zinapaswa kuwa kwenye Katiba ya chama na si nje yake.

Mbowe hajawajibika ipasavyo kama Kiongozi Mkuu wa Chama

Mbowe kama Mwenyekiti wa Chama amekuwa ndiyo sura ya chama vile vile mbele ya jamii na kimsingi ndio kiongozi mkuu wa chama. Ni yeye ndiye anawajibika kuonesha na kutoa uongozi katika chama. Na binafsi nambebesha yeye mzigo wa uwajibika wa matatizo ya kinidhamu na migongano ya viongozi wa kitaifa na viongozi wengine ndani ya chama.

Kama Mwenyekiti Mbowe anatarajiwa kuwa wa kwanza kuhakikisha kuwa viongozi wenzake wanaelewana ndani ya chama na pale ambapo kunakuwa na tofauti basi zinabakia kuwa ni tofauti za kiitikadi au maono lakini zisiwe tofauti hadi za kusababisha viongozi wanarushiana vijembe hadharani. Tumeona udhaifu mkubwa wa uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete kwa viongozi wenzake ambapo mawaziri wanapingana, wabunge wanarushiana vijembe na hata ambapo amejaribu kuwarudisha watu kwenye mstari imeonakana ameshindwa na mara kadhaa sasa badala ya kuwawajibisha wahusika amejikuta akifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Mbowe hawafuatilii inavyopasa viongozi walio chini yake

Mbowe anakabiliwa – kwa maoni yangu – na tatizo la kuwa na ufuatiliaji wa mbali wa viongozi wenzake. Sijui kama ni tatizo la Kikatiba (kwamba hajapewa majukumu yanayoeleweka na Katiba) au ni tatizo tu la kwake binafsi. Vyovyote vile ilivyo kama kiongozi Mbowe alitakiwa awe wa kwanza kufuatilia viongozi wanaopishana na kujaribu kupatanisha au kujaribu kuwaonesha njia – ndio maana ya kuwa kiongozi mkuu wa chama.

Siyo kwenye chama tu kwa ujumla hata Bungeni ambako yeye ndiye Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB). Mifano miwili inahitaji kuangaliwa. Wengi tunakumbuka hoja ya Zitto kutaka kumuondoa Waziri Mkuu pale alipoanzisha kutia sahihi kwa wabunge ili kuonesha kuwa kweli wamedhamiria kumuondoa Waziri Mkuu. Binafsi sikuunga mkono tukio lile kwa sababu hakukuwa na uwezekano wa kumuondoa Waziri Mkuu; na niliona kama ni mkakati mbaya. Hata hivyo kwa KUB kuruhusu hoja kama ile nzito namna ile ilikuwa ni makosa; na ilikuwa ni makosa kwa sababu haikuwa hoja ya chama na haikutoka kwenye Kamati Kuu (kama nilivyoonesha hapo nyuma juu ya kazi za KK). Hapa pia naweza kuutolea mfano wa hoja ya kukataa posho zote ambayo Zitto aliipigania Bungeni. Hii pia ni hoja nzito kwani nayo inahusiana na utaratibu na sheria Bungeni. Mbowe alitakiwa kama kiongozi (Mwenyekiti na KUB) kuhakikisha kuwa hoja ya Zitto inajadiliwa ndani ya chama na msimamo wa pamoja unachukuliwa; msimamo ambao unaweza kufuatiliwa vizuri. Badala yake hili nalo limekuwa likiwakosanisha watu kiasi kwamba wabunge wa CDM Godbless Lema na Zitto Kabwe wamegongana hadharani juu ya suala hili bila kusikia kauli ya Mwenyekiti au KUB.

Mbowe si Bingwa wa Mikakati

Ushindi wa kisiasa mahali popote duniani hutegemea ujumbe, mjumbe na mikakati. Kati ya yote haya katika ulimwengu wa demokrasia mikakati ina nafasi ya pekee kabisa katika kushinda. NI sawasawa kabisa na jeshi linaloenda kupigana vitani; linaweza kuwa na watalaamu, vifaa na nia nzuri kabisa ya kushinda vita lakini ili liweze kushinda linahitaji mbinu na mikakati ambayo ikitekelezwa vizuri basi inatengeneza tofauti ya kushinda na kushindwa.

Mbowe kama kiongozi wa kitaifa si mtu wa mikakati iliyo bora. Mfano mzuri wa jinsi ambavyo Mbowe alishindwa kukiongoza chama kwenye mkakati mzuri wa kutafuta ushindi ni uchaguzi wa 2010. Leo tukiangalia nyuma tunaweza kusema pasi ya shaka kuwa jinsi ambavyo CDM ilienda kwenye uchaguzi mkuu wa 2010 ilikuwa haijajiandaa kushika dola na kampeni nzima haikuonesha kama kweli wanataka kushika dola. Hii ni kwa sababu – kama nilivyoonesha katika makala ya Pembetatu – uamuzi wa viongozi karibu wote wa kitaifa kugombea nafasi mbalimbali ulikifanya chama kikose uongozi wa karibu wa kina wakati wa kampeni. Na hata siku ya uchaguzi tuliona jinsi viongozi wote wa kitaifa wakiwa wamebanwa katika majimbo yao – kama nilivyotabiri kwenye Pembetatu – na kusababisha Mgombea wao wa Urais abaki mwenyewe kwa masaa mengi huku wagombea wengine ambao nao walibanwa katika majimbo yao huku wakihitaji msaada kutoka makao makuu wakijikuta hawana cha kufanya isipokuwa kusubiri tu wakati matokeo yanachakachuliwa. Nani atasahau yaliyomkuta Marehemu Regia Mtema kule Kilombero?

Japo watu wengi wanafikiri CDM ilifanya vizuri sana 2010 ukweli haikufanya vizuri kama ilivyopaswa kufanywa. CDM hata kwa kutokupata Urais ingeweza kupata wabunge wengi zaidi. Mkakati mzima wa kuelekea uchaguzi mkuu haukuwa sahihi na haukuangaliwa vizuri na mtu anayebeba lawama kwa matokeo yale – japo na uzuri wake wote – ni Mwenyekiti.

Baadhi yetu – waliokuwa nyumbani na walioko nje – tuliamini wakati ule baada ya uchaguzi mkuu Mbowe angejiuzulu Uenyekiti ili kumpisha mtu mwingine. Angejiuzulu si kwa sababu ameshindwa bali kwa sababu ya chama kutokufanya vizuri zaidi kulinganisha na matarajio ya wananchi wetu. Na hata baadhi ya mambo ambayo ameyafanya baadaye – suala la kuisifia serikali ya Kikwete (ili awe msema kweli, mpenzi wa Mungu) au kuhudhuria ile dhifa ya kitaifa ya Obama – yameacha maswali juu ya hekima na maono yake kama kiongozi.

Mbowe na Suala la Fedha
Mojawapo ya mambo ambayo yamekuwa yakisumbua sana CDM kwa miaka sasa ni masuala ya fedha. Hili nalo naweza kuliangalia kama mtu aliye nje. Mbowe ana ujiko mkubwa wa kisiasa ndani ya chama kwa sababu ya biashara na fedha zake. Siyo mwanasiasa wa kwanza katika Tanzania kutumia utajiri wake kusaidia chama chake; walifanya kina Abdulwahid Aziz, John Rupia na wengine. Na hili si la CDM peke yake hata ndani ya CCM wanasiasa wenye uwezo wa fedha wameweza kushika nafasi mbalimbali za uongozi na wengine kupewa nafasi mbalimbali – Rostam Aziz ni mfano mmoja tu kati ya mingi.

Hata hivyo kwa upande wa CDM nafasi ya Mbowe inaleta shida kubwa mbili. Kwanza, inatengeneza kile ambacho tayari tumeona kikisumbua CCM – wafanyabiashara wenye nguvu na wanasiasa. Chama cha Mapinduzi kilijikuta kimeingia kwenye ufisadi mkubwa na serikali kuwa katika mikono ya wenye nacho kwa sababu ya undue influence. Naamini CDM inapata shida hii vile vile; viongozi wenye fedha (Mbowe mmojawapo) wanaushawishi mkubwa zaidi kuliko ule wa vyeo vyao. La pili, Kutokana na hilo la kwanza ni vigumu kwa wanachama au viongozi wengine wenye hoja tofauti na viongozi wenye nguvu kuweza kutoa ushawishi ndani ya chama.

Hili linasababisha hoja ifuatayo: kwa kiongozi mwenye ukwasi na cheo kama Mbowe wengi wetu tulitarajia kuwa chama kingekuwa na mfumo mzuri zaidi wa masuala ya fedha kiasi kwamba yasingekuwepo maswali juu ya hili kabisa. Hata hivyo, maswali yamebakia kuhusiana na mapato na matumizi ya chama; kuhusiana na ukusanyaji wa fedha mbalimbali na kuhusu uwekezaji wa chama. Katiba ya CDM inadokeza kuwa chanzo kimojawapo cha mapato ya chama ni “mapato yanayotokana na hisa na miradi halali ya chama”. Swali mojawapo ambalo halijawahi kujibiwa vizuri ni kuwa chini ya uongozi wa Mbowe chama kimewekeza kwenye miradi gani “halali” na kina hisa kwenye taasisi au makampuni gani na kimeweza kujipatia mapato kiasi gani?

Nje ya swali hilo kuna swali zima la suala la uwazi juu ya mapato na matumizi hasa suala la nani anayepanga matumizi. Kama nilivyoonesha huko nyuma juu ya suala la udhaifu wa Katiba hata kwenye masuala ya fedha ni hivi hivi. CDM inahitaji kuangalia mfumo wake wa masuala ya fedha ili kuhakikisha kinawapatia Wanachama na Watanzania kwa ujumla uwazi ambao unastahili chama kinachotaka kuja kuwaongoza. Tayari tumeshaona usiri wa CCM na mambo yake, tumeshaona vya kutosha –kupitia Meremeta/Tangold – jinsi chama cha siasa kinavyoweza kuzama katika kutafuta mapato nje ya utaratibu wa kawaida na watu wasiwajibishwe. CDM inahitaji kujiangalia katika hili na nitaligusa hili wakati natoa mapendekezo yangu, inshaallah.

Suala la fedha ni miongoni mwa masuala yanayosababisha utovu mkubwa wa nidhamu hasa pale ambapo wanachama au baadhi ya viongozi wanaona kama hakuna uwazi au uwajibikaji katika ngazi hii. Hoja hii inaweza pia kumhusu Katibu Mkuu wa CDM Dr. Wilbrod Slaa.

Na hapa kuna swali moja ambalo bado sijalipatia majibu – CDM inapata wapi madaraka ya kukopa fedha kama mojawapo ya vyanzo vya mapato yake? Hili swali ni muhimu kujibiwa hasa pale ambapo kuna taarifa za viongozi wakuu au wakubwa wa chama kukikopesha chama. Utaratibu huu unapatikana wapi katika Katiba ya CDM?
Hata hivyo, wajibu mkuu unamuangukia Mwenyekiti wa Chama kwani yeye ndiye kiongozi mkuu na ndiye anatakiwa (angalau kinadharia) kuonesha mwelekeo wa chama. Kwa kadiri ya kwamba hakuna uwazi katika suala zima la fedha, na kwa kadiri kwamba wapo baadhi ya watu wanaona kuna matumizi mabaya ya fedha na hakuna kuwajibika basi Mwenyekiti anapaswa kubeba lawama. Hivi ndivyo tunavyomfanyia Kikwete vilevile kama Rais wa nchi. Tunapoona udhaifu katika utendaji kazi na ufujaji wa fedha na watu wanaendelea kushikilai nafasi zao hatuna namna isipokuwa kumshukia Kikwete kwani yeye ndiye mtendaji mkuu wa serikali yetu.

Kushindwa kutoa mwelekeo wa kifikra na kiitikadi wa chama
Lakini la mwisho kuhusiana na Mbowe naweza kusema ni kuwa kama Mwenyekiti Mbowe ameshindwa kutoa ule mwongozo wa kifikra na kiitikadi wa chama (philosophical and ideological leadership). Kila kiongozi mkuu wa chama au wa taasisi fulani anapaswa kuangaliwa na watu waliochini yake kama kiongozi siyo wa kama msimamizi tu bali pia kuonesha anataka chama kielekee wapi. Mwenyekiti wa chama anapaswa kuwa ni kiongozi wa kifikra zaidi kuliko kitu kingine chochote; watu wajue anataka chama kiwe na mwelekeo gani, anataka serikali iende vipi na kama wao wakiingia madarakani nchi yetu itaenda upande gani. Haitoshi kuendelea kumwaga lawama na kuitaka serikali ifanye hivi au vile.

Binafsi naamini huu ni udhaifu mkubwa zaidi wa Mbowe kuliko hivyo vingine vyote kwani kiongozi asiyeshawishi fikra kwa ubora wa fikra zake anaongoza watu kwa kitu kingine basi au kwa ushawishi mwingine.

2. Dr. Wilbrod P. Slaa – Katibu Mkuu wa CDM

Hakuna mwanasiasa aliyejipatia jina na ambaye amekuwa na mvuto mkubwa nchini sasa hivi kama Dr. Slaa. Kama nilivyoonesha hapo nyuma Dr. Slaa kama walivyo Mbowe na Zitto ana ujiko wake mkubwa wa kisiasa lakini zaidi ya hawa wawili ni mwanasiasa aliyetikisa malango ya CCM na yakatikisika. Dr. Slaa aliwapa Watanzania matumaini kuwa akitokea mwanasiasa mwenye mvuto, hoja, na nia hasa ya kusimama dhidi ya CCM upinzani unaweza kweli kuchukua Ikulu.

Mwaka 2010 CDM ilimsimamisha kutokana sifa nyingi alizokuwa nazo. Kitu pekee ambacho naamini hata CDM hawakukitegemea ni mwitikio wa wananchi juu ya Dr. Slaa. Viongozi wa CDM walijua kuwa Dr. Slaa angeweza kuwapatia kura nyingi za wabunge; kitu pekee ambacho hawakuwa wamejiandaa nacho ni ukweli kuwa Watanzania walitaka kumfanya Rais –wengine wanaamini aliupata Urais ila akachakachuliwa. Niseme mapema kuwa Slaa ni miongoni mwa wanasiasa wanaonivutia sana na wanaonipa matumaini kuwa siku moja utawala ulioshindwa utakuja kusimama na kuwabishwa mbele ya umma. Nilimuunga mkono wakati ule na ninaamini bado ni mwanasiasa ambaye kukiwa na mkakati mzuri na mipango mizuri anaweza kabisa kuongoza kuing’oa CCM madarakani. Sijaona bado mwanasiasa mwingine upinzani aliye na mvuto wa aina hii.

Tatizo la Katiba
Hata hivyo Dr. Slaa kama ilivyo Mbowe anakabiliwa na matatizo yale yale ambayo nimeyaanisha hapo juu kumhusu Mbowe kwa kiasi kikubwa. Tatizo la kwanza na kubwa ni lile la Kikatiba; kwamba na yeye kama ilivyo kwa Mwenyekiti nafasi yake haijaelezwa kwa kirefu majukumu yake hasa nini – wigo wa utendaji kazi wake. Inawezekana majukumu hayo yameanishwa katika nyaraka nyingine (kama nilivyosema hapo juu) lakini kwa Katiba ya CDM kushindwa kuanisha majukumu na kazi za Katibu Mkuu wa chama ni udhaifu mkubwa wa Katiba.

Katiba ya CDM inadokeza tu katika sehemu ya kuelezea maana ya maneno mbalimbali (fasili) kuwa Katibu Mkuu “ni mtendaji mkuu makao mauu ya chama”. Maana hii kama ile ya Mwenyekiti haitoshi kuelezea upeo na uwezo wa majukumu yao. Katiba ya Chama ndio mamlaka makubwa ya uendeshaji wa chama kwani hata kanuni zinapopingana na Katiba ni Katiba inayofuatwa. Hata hivyo kutoanisha majukumu na kazi za watendaji hawa wakuu wa chama kumeacha mwanya mkubwa wa ama mtu kutumia madaraka vibaya au kutumia madaraka asiyokuwa nayo.

Naelewa kuna baadhi ya nafasi ambazo Katiba imempa madaraka ya kuteua watendaji wake ama yeye mwenyewe au kuwa mshauri wa Mwenyekiti katika teuzi zinazopaswa kufanywa na Mwenyekiti. Bila kuanisha katika Katiba kazi na wajibu wa Katibu Mkuu CDM imefungua mlango wa yeyote anayeshikilia kiti hicho ama kuamini ana madaraka makubwa kuliko aliyokuwa nayo au kutokutumia madaraka ambayo alipaswa kuwa nayo.

Chukulia kwa mfano, Katibu Mkuu wa CCM chini ya Ibara ya 120:7 ya katiba yao ana madaraka mengi lakini yafuatayo yameanishwa wazi kuwa anayo: (a) Kuratibu kazi zote za Chama Cha Mapinduzi. (b)Kusimamia kazi za Utawala na Uendeshaji katika Chama. (c ) Kufuatilia na kuratibu masuala ya Usalama na Maadili katika Chama. (d) Kusimamia Udhibiti wa Fedha na Mali za Chama. Kimsingi, matatizo ya Kimaadili ndani ya CCM mtu wa kuulizwa ni Katibu Mkuu. Katika CDM jukumu hili inaonekana limepewa Kamati Kuu nzima! Angalau kwa kuangalia Katiba.

Ukosefu wa Nidhamu Makao Makuu ya Chama

Mojawapo ya vitu ambavyo vinanisumbua sana na hili bila ya shaka inabidi limuangukie Katibu Mkuu kwani ndiye Mtendaji Mkuu Makao Makuu ya chama ni suala la nidhamu katika makao makuu. Kama ningeulizwa neno moja la Kiingereza kuelezea kinachoendelea makao makuu ya CDM ningesema “dysfunctional”. Hii maana yake ni kuwa haifanyi kazi inavyotakiwa kufanya. Ushahidi wa hili ni maelezo yaliyotolewa na Kamati Kuu kuhusiana na kuvuliwa vyeo kwa kina Zitto kuwa baadhi ya mambo yalihusisha maafisa wa Makao Makuu na tukaona jinsi ambavyo hadi Makamu Mwenyekiti Bara akijiuzulu.

Binafsi naweza kusema pasipo shaka kuwa kumekuwa na udhaifu mkubwa katika kusimamia makao makuu ya CDM kiasi kwamba kutoka hapo wanasiasa na watendaji wengine wa chama mikoani wamekuwa shaghalabaghala. Tumeshuhudikia Katibu Mkuu akienda na kuingilia utendaji kazi mikoani ili kuleta nidhamu; ukweli naamini sehemu ya kwanza ambayo ilihitaji nidhamu ni Makao Makuu kwani hapa ndipo wanachama na Watanzania wanaiounga mkono CDM wanataka kuona nidhamu inatawala, umoja na ushirikiano.

Bahati mbaya sana mgawanyiko mkubwa na mgogoro mkubwa umekuwepo ukihusisha watu wa makao makuu. Ni kwa kiasi gani Katibu Mkuu anaweza kuingilia kati pale wabunge wa chama chake wanapobishana na kurushiana madongo hadharani? Ni vipi Katibu Mkuu anapoona kuna ajenda imeenda Bungeni ambayo haikutoka kwenye chama lakini chama kinapaswa kuiunga mkono? Nimeonesha hapo juu jinsi ambavyo CCM imempa madaraka Katibu Mkuu kusimamia masuala ya fedha, kwa upande wa CDM ni kwa kiasi gani Katibu Mkuu anasimamia mapato na matumizi ya chama.

Tumeshuhudia wakati mwingine watu ambao wanaonekana kuwa wanamahusiano ya karibu na Makao Makuu au ni maafisa wa Makao Makuu wakitoa michango yao hadharani kwenye mitandao ya kijamii ambayo kwa kweli haiendani na uzito wa ofisi wanazoshikilia. Katibu Mkuu – yeye mwenyewe au wasaidizi wake – anapaswa kuhakikisha kuwa maafisa wa makao makuu wanatenda kama maafisa wa serikali inayokuja. Vinginevyo, ukiangalia unaweza usione tofauti kubwa kati ya utendaji wa watu walioko kwenye serikali ya sasa na wale wanaotaka kuunda serikali siku moja.

Na swali lile nililouliza kuhusiana na Mbowe lapaswa kuulizwa hapa tena. Kwa muda wote huu hadi hivi sasa CDM imeweza kuwekeza kwenye mradi gani au hisa gani ili kujiongezea mapato? Kama kwa muda wote huu CDM haina mradi wowote wa maana au hisa za maana kuongeza mapato yake je kwanini lawama zisiende kwa Mtendaji Mkuu wa chama?

CDM kutokuwa na Makao Makuu ya Kisasa

Mojawapo ya maswali ambayo binafsi nimebakia nayo kwa muda mrefu – na labda wengine vile vile – ni kwanini chama ambacho kinaonekana kupendwa na watu wengi, kikiwa kimekusanya wasomi wa kila namna na ambacho kweli kinataka kushika dola hakina ofisi za kisasa za makao makuu ya chama? Ofisi ambazo zinaendana na hadhi na njozi ya wanachama wake? Kwanini Makao Makuu ya CDM hayalingani na hadhi na jina la chama hiki?

Swali hili nitajaribu kulijibu mapema mwakani kwani naamini name naweza kutoa mchango wangu kidogo katika kuisaidia CDM kuwa na makao makuu ya kisasa yenye kujionesha kuwa ni chama kweli ambacho kinataka kushika dola.

Kutowapa Wanachama na Mashabiki kitu cha kufanya

Mojawapo ya maswali ambayo pia yatahitaji majibu huku mbeleni ni jinsi gani Dr. Slaa na Mwenyekiti wake wamewapatia watu walioamshwa mambo ya kufanya kujiletea maendeleo. Tumeshuhudia kwa muda sasa mikutano mbalimbali, maandamano n.k Mamia ya watu wanakuja kusikiliza na wanatoka huku wamenyosha vidole kwa alama ya ushindi! Lakini zaidi ya hapo hawa maelfu ya watu waliohamasika wanafanya nini kubadilisha jamii zao, maisha yao na kujiletea maendeleo? Kwa muda sasa viongozi hawa wawili kitaifa – na wengine bila ya shaka – wamejitahidi kuwaamsha watu waamke waone kuwa maisha yao na hali zao mbaya zimetokana moja kwa moja na utawala ulioko madarakani. Hili limefanyika kwa kiasi kikubwa na pongezi zinawastahili wote waliowaamsha hivi Watanzania. Lakini, baada ya kuamka sasa kifuate nini? Binafsi naamini udhaifu mkubwa wa mwamko huu ambao umefanywa na Slaa na viongozi wengine (wa juu na ngazi za chini) ni kutokuwapa wananchi nafasi ya kuanza kujiletea maendeleo ama kwa kutumia nguvu kazi, michango (mali, ujuzi na hali).

Haitoshi kuendelea kuwaamsha watu waliokwisha amka; watu wakishaamka wape kitu cha kufanya! Vinginevyo mikutano itakuwa ni ya mambo yale yale ya kuwaambia wananchi vitu vile vile ambavyo tayari wanajua chanzo chake ni kile kile na hivyo wanaondoka (baada ya kusisimka sana) wakiwa na maisha yale yale hadi mkutano mwingine!
Pamoja na haya yote Dr. Slaa bado anaonekana ni tishio kubwa sana kwa CCM na ninaamini kutokutulia kwa hali ndani ya chama kunawapa nafasi ya kupumua wana CCM.

3.Zitto Zuberi Kabwe – Mbunge wa Kigoma Kaskazini
Matatizo niliyoyaonesha hapo nyuma kuhusiana na Katiba na nafasi za viongozi yanahusiana na Zitto kabla ya kuvuliwa Unaibu Mkuu. Katiba haijaanisha wazi majukumu yake hasa ni yepi na anatakiwa kufanya kazi vipi na Katibu wake (yeye na Naibu kutoka Zanzibar). Ieleweke kuwa Naibu ni tofauti na kuwa Kaimu Katibu Mkuu. Naibu ni cheo cha kudumu wakati Kaimu ni nafasi ya muda. Kaimu anaweza kuwa na madaraka yote ambayo Katibu Mkuu anayo wakati Naibu anapaswa kuwa na madaraka yale ambayo amepewa na Katiba tu. Hili halijafanyika na matokeo yake ni wakati mwingine kutokuelewa sana ulazima wa uwepo wa nafasi hizi mbili (kwanini kuna Manaibu Wawili au Makamu wawili sielewi).

Ni wazi bila ya shaka hakuna mwanasiasa kijana wa nyakati hizi zetu ambaye amekuwa na mvuto wa kipekee kama Zitto Kabwe. Amekuwa ni sababu na kichocheo cha vijana wengi kuingia katika siasa na uthubutu wake na moto wake umewapa vijana wengi hamu na matumaini kuwa hata kijana anaweza. Kwa kiasi kikubwa utendaji kazi wake uliwavutia vijana wengi sana kuingia kwenye siasa na wengine kujaribu kugombea nafasi za uongozi. Siyo tu kwa vile ni kijana lakini pia kwa vile ni msomi na ameonesha kutumia elimu yake kupigania nchi yake.

Hata hivyo mgogoro mkubwa ndani ya CDM kati ya viongozi na viongozi na hata kwa wanachama utakuta jina lake linatajwa. Kwa watu wanaofuatilia jina lake limetajwa kwenye chaguzi za BAVICHA, kwenye kugombea Uenyekiti na hata katika hili sakata ambalo walivuliwa uongozi yeye na Dr. Kitila na Samson Mwigamba.

Zitto na Uenyekiti wa CDM
Binafsi kwa kweli sijaona tatizo la Zitto kutaka kugombea Uenyekiti wa CDM. Iwe sasa au baadaye. Kama Zitto anaamini ana uwezo wa kuiunganisha CDM na kuweza kuipeleka ushindi anapaswa kupewa nafasi kama wagombea wengine wowote wale. Hii ndio maana ya demokrasia. Na itakuwa vizuri kweli kama nafasi ya kugombea uongozi wa CDM itakuwa wazi kwa mwanachama yeyote kugombea kama Katiba ilivyoainisha. Wanachama ndio wawe waamuzi nani wanamuamini na ijulikane ni wao pia watakuwa waamuzi kama wataona hawana Imani naye.

Swali kubwa ni vipi Zitto angeweza kukileta chama pamoja katika umoja? Inawezekana vipi mtu kuongoza watu asiokubaliana nao au watu ambao watakuwa wanamshuku? Lakini zaidi ni uwa hata yeye angekuwa kiongozi sidhani kama angeona vyema kuona kuna mtu au kikundi cha watu ambao wanaonekana kukosa nidhamu ndani ya chama.

Zitto na Tangazo la Kutaka Kugombea Urais

Mojawapo ya mambo ambayo yamemletea tatizo sana Zitto ni tangazo lake la nia hata matamanio ya kutaka kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano. Kauli hii ilimletea shida kwani mara kadhaa tamko hilo lilienda sambasamba na kuhusisha kuwa mgombea ajaye anapaswa kuwa “kijana”. Hakuwa peke yake kwenye msimamo huo kwani baadhi ya wanasiasa ndani ya chama tawala na nje nao wamekuwa wakipendekeza jambo hili. Kwa Zitto hata hivyo ilimletea matatizo kwa sababu kwanza Katiba isingeweza kumruhufu kufanya hivyo na hata alipojitokeza kutaka umri wa kugombea Urais ushushwe ilionekane zaidi kwa ajili ya kumfaa yeye.

Kauli yake hii ilianza au kuendeleza kugawa wanachama; binafsi naamini haikuwa kauli iliyopaswa kutolewa namna ile na kuwa kutolewa kwake kulipaswa kufikiria matokeo yake ni nini?

Zitto na Hoja Nzito Bungeni

Nimeonesha huko nyuma jinsi Katiba ya CDM ilivyoweka utaratibu wa kuanzisha hoja katika Kamati Kuu kabla ya kwenda Bungeni. Katika nchi kama ya kwetu ambayo inafuata mfumo wa kibunge (parliamentary system) wabunge wanapaswa kuangalia na kufuata kwa kadiri wanavyoweza uongozi wa chama kuhusiana na mambo ambayo wanaamua kuyasimamia Bungeni.

Kwa namna isiyoeleweka baadhi ya hoja za Zitto ambazo zina uzuri wake mwingi tu zimebakia kuwa ni hoja za Zitto na hili si jambo zuri katika utendaji wa chama. Hii ni kweli kwenye hoja ya posho kwa mfano na hata kwenye hoja ya kumuondoa Waziri Mkuu. Hili pia ni kweli kwenye suala la kufuatilia mabilioni yaliyofichwa Uswisi; kwanini hii isingekuwa hoja ya chama wakaipigania Bungeni nan je ya Bunge? Badala yake sasa inaonekana ni hoja ya Zitto na kina Werema wakijua matatizo ya CDM wamemrushia kamba ikiwa na fundo. Hili nimelidokeza hapo nyuma. Katika masuala mazito na yenye hisia kali kama haya chama kinatakiwa kutoa mwongozo ambao wabunge wake wanapaswa kuufuata na siyo kuwaacha wabunge wajiamulie tu.

Jinsi Zitto alivyokuwa Triangulated na CCM

Kwa wanaokumbuka sakata la Buzwagi lililompaisha Zitto kupita kiasi jambo moja lilikuwa wazi kabisa. Kwamba Zitto alijionesha kuwa tishio dhidi ya CCM. Kwa baadhi yetu tuliokuwa tunafuatilia kikao cha Bunge na hasa uamuzi wa kumfungia tuliona na tukaelewa ukweli mmoja ulio wazi – Zitto ni kijana ambaye ameitisha CCM na kama ataendelea hivyo basi CCM iko matatani. TUnakumbuka jinsi ambavyo watu walilia pale Jangwani wakati Zitto amepokelewa kama shujaa. Sidhani kama kuna mwanasiasa ambaye alifanya wananchi waumizwe moyoni kwa kuona dhulma ikitendeka.
Hata hivyo, wakati ule uamuzi ulichukuliwa mapema tu na watawala; kumvuta Zitto karibu na kupunguza (neutralize) nguvu yake. Mara moja watu ambao walisimama kumfungia na kumuita Muongo wakageuka mara moja kumuona rafiki. Hata leo hii tumeshuhudia ukigeugeu huu wa CCM ambapo Zitto ameonekana kupiganiwa na kuliliwa na wana CCM kana kwamba kweli wanaamini uwezo wake.

Hili bila ya shaka limejenga hisia ya yeye kutokuaminika na wakati mwingine yeye mwenyewe ameshindwa kujionesha mbele ya wenzake kuwa anastahili kuaminika. Ni sawasawa na watu ambao wako vitani mnapoona mmoja wa makamanda wenu yuko karibu sana na upande wa pili na upande wa pili wanapigania sana awe Jenerali wenu wa vita wapiganaji inabidi mjiulize kama Kamanda huyo ni wenu wenu au wenu wa kwao!?

Kuna msemo kuwa “waweke rafiki zako karibu, lakini adui zako karibu zaidi”. Baadhi yetu tulielewa zile sifa ambazo alimwagiwa na wana CCM na ukaribu ambao Mwenyekiti wa CCM amemuonesha na hata viongozi na vijana wengine ndani ya CCM zilikuwa ni sifa za kumkata makali. Na kwa kiasi kikubwa hili limefanikiwa na kwa upande fulani limechangia kwenye migogoro CDM. Hata hivyo, kama nilivyowahi kusema mahali pengine, binafsi siwalaumu CCM hata kidogo kwa migogoro upinzani. Nimewahi kusema kuwa CCM ilitakiwa ifanye nini? Sielewi watu wanaotarajia kuwa CCM itafanya mambo ili upinzani ukomae na uwe imara. Kwanini CCM iamue kutengeneza mafuta ya kujikaangia? CCM kama chama cha siasa kinachoshika madaraka na ambacho hakina nia ya kuyaachia hivi karibuni kitafanya yote kinayoweza kuhakikisha kuwa upinzani unakuwa dhaifu, unagawanyika na ikiwezekana unavunjika kabisa! Hili ni jukumu lao kama vile ni jukumu la upinzani kudhoofisha chama tawala ili kikataliwe na wananchi ili wao wakubaliwe!

Kama Zitto hakuiona hatari hii au aliiona na akaipuuzia hili ni swala jingine. Kwa baadhi ya mashabiki na wanachama wa chama chake wameona ukaribu huu way eye na CCM kuwa ni ukaribu wa kama swala na simba; ni urafiki wenye mashaka.

Hapa ni lazima tutofautishe urafiki wa kibinafsi ambao mtu anao na watu wa chama kingine. Itakuwa ni makosa kumhukumu Zitto kwa kuwa na marafiki CCM au watu wa CCM au hata serikalini kwani hii ni haki ya msingi ya kila mtu.

Jumla ya Wanasiasa Wetu Watatu

Ndugu zetu hawa wangeweza mapema sana kushughulikia matatizo ndani ya chama na baina yao na kuhakikisha kuwa chama hakifiki hapa kilipokifishwa. Wote kwa namna moja au nyingine wamechangia (kwa kujua au kutokujua) kuwepo kwa mgogoro, mgogoro ambao umezama hadi chini ambako nako kuna migogoro ya aina yake kwenye baadhi ya maeneo. Lakini chama hakiwezi kuishi na migogoro mikubwa hivi ni lazima migogoro imalizwe vizuri na kwa ustadi tena si kwa kuziba viraka tu bali hata kwa kutengeneza upya kilichobomoka.

Katika sehemu ya mwisho ya mfululizo huu nitaainishe baadhi ya mapendekezo ambayo naamini yakichukuliwa moja moja au kwa ujumla yatachangia kuisaidia CDM kutoka hapa ili hatimaye iwe na amani ya ndani wakati ikijiandaa kushinda Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2010. Naamini pigo kubwa kabisa kwa CCM litakuwa ni kurudia na kuimarika kwa umoja ndani ya CDM kabla ya chaguzi hizo.
(Itamalizika Kesho)

(*) Nimetumia Katiba ya CDM toleo la 2006 kama inavyopatikana kwenye mitandao mbalimbali. Inawezekana kuna mabadiliko ya Katiba ambayo yalianisha kazi na majukumu ya viongozi hawa. Hadi nimemaliza kuandika makala hii sikuwa nimepata mtu yeyote mwenye nakala iliyo tofauti na niliyotumia hususan kwenye suala la kazi na majukumu ya viongozi wa kitaifa. Nitakuwa tayari kusahihishwa.
 
ok.........umeeleweka,kwa jinsi ulivyomchambua mbowe na slaa upo uwezekano ukaitwa msaliti eti kwa sababu una mtazamo tofauti na wao lakini ukweli utabaki palepale ,kuhusu mbowe na slaa kuwa andiko lako lina sehemu ya "waraka wa ushindi 2013 by samson mwigamba" hayo matatizo uliyoyaanisha ni ya kweli kabisa na kwa mwanachama wa CDM mpenda demokrasia na sio mhafidhina akiwa mchambuzi wa kina na awe tayari kukubaliana na ukweli atakubaliana na wewe na hiyo yote ni kwa sababu ya mstakabali wenye afya wa chama,na falsafa zako hazina tofauti na hii picha hapa chini

attachment.php
 
sehemu ya sita itakua tamu zaidi, Asante MM

afu watu walewew Mzee Mwanakijiji ni MM hata kabla ya ile siri ya ushindi ya kina kitila
 
Nasubiri tu mwisho katika mapendekezo ya kumaliza uu mgogoro..katika kosa tutajutia daima dumu ni kumfukuza ZZK uanachama
 
Mzee Mwanakijiji unachokifanya ni sawa na kelele za mlango CC imeshaamua full stop jiandaeni kumpokea msaliti atakapofukuzwa rasmi.

Kosa kubwa mnalofanya ni kutumia utetezi ule ule na mipango ile ile kwa kutumia mbinu zile zile zilizoshindwa za akina TUNTEMEKE, Mwampamba & co. kuwadhalilisha viongozi wetu.

Labda nikukumbushe tu kuwa chama cha siasa siyo kampuni au shirika la umma kuwa lazima lishirikishe intellectuals waliobobea kwenye fani, siasa ni uungwaji mkono toka kwa wanachama na wananchi walio wengi, kwenye chama hata kama utakuja na mipango kabambe bila kuungwa mkono na walio wengi ni kazi bure. Mbowe hata kama haungwi mkono na intellectuals lakini anaungwa mkono na wanachama wengi.
 
Hongera Mzee MM kwa maoni yako mazuri. Naona dhahiri yametuingia vizuri ndio maana sioni comment nyingi mpaka mida hii. Hata wale wenye akili fupi wasiopenda viongozi wao/chama chao kukosolewa na kupelekea kutoa matusi wameshikwa na butwaa. Mojawapo ya nililonifurahisha ni nukuu hii hapa chini.

Ni mwendelezo kutoka Makala ya Kuuelewa Mgogoro wa CHADEMA........
Kutowapa Wanachama na Mashabiki kitu cha kufanya

Mojawapo ya maswali ambayo pia yatahitaji majibu huku mbeleni ni jinsi gani Dr. Slaa na Mwenyekiti wake wamewapatia watu walioamshwa mambo ya kufanya kujiletea maendeleo. Tumeshuhudia kwa muda sasa mikutano mbalimbali, maandamano n.k Mamia ya watu wanakuja kusikiliza na wanatoka huku wamenyosha vidole kwa alama ya ushindi! Lakini zaidi ya hapo hawa maelfu ya watu waliohamasika wanafanya nini kubadilisha jamii zao, maisha yao na kujiletea maendeleo? Kwa muda sasa viongozi hawa wawili kitaifa – na wengine bila ya shaka – wamejitahidi kuwaamsha watu waamke waone kuwa maisha yao na hali zao mbaya zimetokana moja kwa moja na utawala ulioko madarakani. Hili limefanyika kwa kiasi kikubwa na pongezi zinawastahili wote waliowaamsha hivi Watanzania. Lakini, baada ya kuamka sasa kifuate nini? Binafsi naamini udhaifu mkubwa wa mwamko huu ambao umefanywa na Slaa na viongozi wengine (wa juu na ngazi za chini) ni kutokuwapa wananchi nafasi ya kuanza kujiletea maendeleo ama kwa kutumia nguvu kazi, michango (mali, ujuzi na hali).

Haitoshi kuendelea kuwaamsha watu waliokwisha amka; watu wakishaamka wape kitu cha kufanya! Vinginevyo mikutano itakuwa ni ya mambo yale yale ya kuwaambia wananchi vitu vile vile ambavyo tayari wanajua chanzo chake ni kile kile na hivyo wanaondoka (baada ya kusisimka sana) wakiwa na maisha yale yale hadi mkutano mwingine!
Pamoja na haya yote Dr. Slaa bado anaonekana ni tishio kubwa sana kwa CCM na ninaamini kutokutulia kwa hali ndani ya chama kunawapa nafasi ya kupumua wana CCM.

........Nitakuwa tayari kusahihishwa.


wana CDM tuache kushinda kwenye mitandao we have to do something for our development while waiting for the ballot in 2015, let forget ndoto ya nguvu ya umma.
 
Makala bora sana,

Kiukweli sina la kuongeza hasa udhaifu wa viongozi wawili wa juu wa CDM lakini nadhani upande wa Zitto unaweza kuwa mpana zaidi.Kutokuaminika kwa Zitto kumechangiwa sana na kauli zake nyingi ambazo hazijengi chama chake na ni kauli za kujitenga yeye na udhaifu wa chama chake.

Pamoja na Zitto kuwa kijana mwenye uwezo mkubwa sana lakini kuna hulka ndani yake (ubinafsi) ambayo inakatisha tamaa kama anaweza kuishinda mwenyewe.Zitto ni kama anapenda yeye kuwa juu ya kila kitu na sidhani kama hata akiwa mwenyekiti ataweza kukubali fikra mbadala kama anavyodai sasa.

Binafsi siwezi kuwa mnafiki kwa kukataa ukweli juu ya uwezo wa Zitto lakini hajengi mazingira ya kumuamini kama kiongozi wa taasisi.Nadhani pengine Mbowe alikuwa na nia njema kwa hawa vijana akijua ndio wangekuja kuipeleka CDM ikulu lakini nidhamu na haraka zao kutaka madaraka zinaogopesha hasa kutokana na siasa za CCM ambazo kwa Afrika ni moja ya chama kikongwe na chenye kila mbinu kumaliza upinzani.

Nakubali tunahitaji msukumo mpya kuelekea 2015 lakini msukumo mpya unatoka kwa watu wanaoaminika na watii kwa chama.Siasa si uadui lakini pia siasa sio urafiki tu bali kuna mipaka ambayo itaweza kufanya wewe kama kiongozi uonekane unaweza kuchukua hatua kwa yeyote.

Mwisho wapiganaji walio mstari wa mbele muwe na msimamo na mtu anapokosea akosolewe pale pale bila kusikilizia upepo ili ujue useme nini.Kauli za wanasiasa hawa kama za kumuita kiongozi wako "kibabu" alafu mtu anajua wewe ndio umetamka hayo si kitu kizuri hata kidogo na ukosefu wa heshima kwa vijana hawa.Kijana kama Zitto anapokosea wazi kwa kauli zake mara nyingi wapiga kelele ni wachangiaji wa kawaida kabisa mitandaoni huku wale manguli wakiwa kimya!! Tunafanya yale yale tunayosema viongozi wa juu wanakosea.

Nitasema ukweli daima! Fitna kwangu ni mwiko! Tanzania kwanza!
 
ok.........umeeleweka,kwa jinsi ulivyomchambua mbowe na slaa upo uwezekano ukaitwa msaliti eti kwa sababu una mtazamo tofauti na wao lakini ukweli utabaki palepale ,kuhusu mbowe na slaa kuwa andiko lako lina sehemu ya "waraka wa ushindi 2013 by samson mwigamba" hayo matatizo uliyoyaanisha ni ya kweli kabisa na kwa mwanachama wa CDM mpenda demokrasia na sio mhafidhina akiwa mchambuzi wa kina na awe tayari kukubaliana na ukweli atakubaliana na wewe na hiyo yote ni kwa sababu ya mstakabali wenye afya wa chama

Duh!
Ila hilo lipo wazi na linajulikana kuwa Wananudhaifu huo, tatizo Je udhaifu huu unautibu vipi?
1. kwa Kuwapindua?
2. kwa kuwakashifu?
3. kwa kuwasliti/kukisaliti chama?
 
Hongera Mzee MM kwa maoni yako mazuri. Naona dhahiri yametuingia vizuri ndio maana sioni comment nyingi mpaka mida hii. Hata wale wenye akili fupi wasiopenda viongozi wao/chama chao kukosolewa na kupelekea kutoa matusi wameshikwa na butwaa. Mojawapo ya nililonifurahisha ni nukuu hii hapa chini.

[/COLOR]

wana CDM tuache kushinda kwenye mitandao we have to do something for our development while waiting for the ballot in 2015, let forget ndoto ya nguvu ya umma.


Hhahah,
wapewe mashamba wakalime?
wasomi hawataki kuajirwa tena , wansubiri udiwani na Ubunge huku wakiendelea kupika majungu na kujipendekeza ili wapate kula.
 
Imenena kweli MM Naamini hawa watu watatu kwa sasa ndo wataamua hatima vya hiki chama ikitokea hata leo wakajisahihisha utakuwa ni wakati mzuri wa kuipeleka CCM shimoni kinyume chake utakuwa ndo mwisho wa hiki chama hawa viongozi watatu wakiungana na kufanya kazi kama timu itasaidia sana kuiongeza mshikamano ndani ya chama
 
Huu ni uchambuzi mzuri, upo balanced, hujamwonea mtu. wana CDM wanapaswa kutambua ukweli kuwa viongozi hawa ni binadamu hivyo mapungufu wanayo pia, i hope wana CDM wataupokea positively kama changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi.

Nasubiri kuona mapendekezo yako, natumaini kuwaondoa wale ambao kwa makusudi wamekuwa wakikihujuma chama (ZZK na wenzake) litakuwa moja ya mapendekezo yako:smile-big:
 
Imenena kweli MM Naamini hawa watu watatu kwa sasa ndo wataamua hatima vya hiki chama ikitokea hata leo wakajisahihisha utakuwa ni wakati mzuri wa kuipeleka CCM shimoni kinyume chake utakuwa ndo mwisho wa hiki chama hawa viongozi watatu wakiungana na kufanya kazi kama timu itasaidia sana kuiongeza mshikamano ndani ya chama
Wataungana saa ngapi wakati mwingine yuko bize kuwapindua.
 
Huu ni uchambuzi mzuri, upo balanced, hujamwonea mtu. wana CDM wanapaswa kutambua ukweli kuwa viongozi hawa ni binadamu hivyo mapungufu wanayo pia, i hope wana CDM wataupokea positively kama changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi.

Nasubiri kuona mapendekezo yako, natumaini kuwaondoa wale ambao kwa makusudi wamekuwa wakikihujuma chama (ZZK na wenzake) litakuwa moja ya mapendekezo yako:smile-big:

kamanda acha ubaguzi, toa mapendekezo na kwa upande wa mwenyekt......
 
kamanda acha ubaguzi, toa mapendekezo na kwa upande wa mwenyekt......
Mkuu Mwenyekiti kwa mtazamo wangu mapungufu anayo, lakini hana nia ya MAKUSUDI ya kuihujumu CDM wakati ZZK yeye anaihujumu CDM kwa MAKUSUDI. Wakati mapungufu ya Mwenyekiti ni ya kibinadamu zaidi yanayoweza kutatuliwa kwa kuweka mifumo mizuri eg, kuainishwa kwa kazi za viongozi wakuu ndani ya katina nk, ZZK kosa lake ni la uhaini dhidi ya chama.

Ni ukweli tu mkuu, hakuna upendeleo kwa yeyote hapo.
 
Back
Top Bottom