Kuuawa kwa Veronica: Je kilikuwa ni kifo cha kujitakia……………? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kuuawa kwa Veronica: Je kilikuwa ni kifo cha kujitakia……………?

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, Jun 29, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  Jun 29, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  [​IMG] [​IMG][​IMG]
  Veronica Guerin
  [​IMG]
  Martin Cahil the General
  [​IMG]
  John Gilligan
  [​IMG]
  John Traynor the Coach


  Ilikuwa ni Juni 26, 1996 Veronica Guerin alikuwa ndani ya gari lake aina ya Opel nyekundu akikatiza mitaa ya nje ya jiji la Dublin nchini Ireland, wakati akirejea nyumbani kwake baada ya pilikapilika za mchana kutwa akitafuta habari. Huyu ni mwandishi wa habari za kiuchunguzi nchini Ireland ambaye alikuwa ni mwiba mchungu kwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya na wahalifu walioshindikana.

  Alipofika kwenye taa za kuongozea magari, Veronica alisimama, kisha akanyanyua simu yake ya mkononi na kumpigia rafiki yake mmoja ambaye ni Polisi. Hakupata majibu zaidi ya kujibiwa na sauti iliyorekodiwa kwenye simu ya mhusika ikimwelekeza aache ujumbe. Wakati anaanza kuongea ili kuacha ujumbe kwenye simu ya rafikiye, hakujua kwamba kulikuwa na pikipiki iliyokuwa na watu wawili ikimfuata kwa nyuma ambayo ilisimama mita chache kutoka pale aliposimama.

  Mtu yule akiwa amevaa kofia ya kuendeshea pikipiki alishuka kwenye pikipiki yake na kulisogelea gari la Veronica kisha akafyatua risasi tano kupitia dirisha la dereva ambapo zilimuua Veronica sawia. Ni muda mfupi Veronica alikuwa hai akiongea na kucheka kwenye simu na muda huohuo anauawa kwa kupigwa risasi. Ni tukio ambalo lilichukua sekunde chache sana. Mwendesha pikipiki yule alitoweka na pikipiki yake, akitokomea kwenye viunga vya Dublin baada ya kufanya mauaji yale.

  Kuuawa kwa Veronica kuliishtua jamii ya Wa-Irish ambayo pamoja na kushuhudia mauaji mbalimbali yanayoendeshwa na kundi la IRA, lakini mauaji ya watu ambao hawahusiki na masuala ya kisiasa yalikuwa ni adimu sana kutokea nchini humo. Ni jambo lisilokuwa na ubishi kabisa kwamba mauaji yale yalikuwa ni ya kupangwa na kufadhiliwa na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevywa na wahalifu wakubwa ambao Veronica alikuwa akiwachunguza na kuandika habari zao.

  Waziri mkuu wa wakati huo wa Ireland John Bruton aliahirisha kikao cha Bunge la nchi hiyo kwa ajili ya kuungana na familia ya Veronica Guerin katika msiba huo. Waziri mkuu huyo alisema katika taarifa yake, "mtu fulani, mahali fulani anaamua kutoa roho ya mama huyu kwa sababu ya kuzuia habari za kihalifu zisitolewe hadharani, huu ni unyama."


  Salaam za rambirambi ziliendelea kutolewa kutoka kila mahali, Aengus Fanning mhariri wa gazeti la Sunday Independent gazeti ambalo Veronica Guerin alikuwa akiliandikia, katika taarifa yake alisema, "Veronica Guerin alikuwa ni mwandishi mahiri na jasiri ambaye sijapata kukutana na mwandishi wa aina yake katika maisha yangu."
  Mhariri huyo ambaye ndiye aliyekuwa bosi wa Veronica alitangaza hadharani kwamba gazeti la Sunday Independent litatoa zawadi ya kitita cha dola 150,000 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwa muuaji.

  Mazishi ya Veronica Guerin yalifanyika June 29, 1996, katika kanisa la Our Lady Queen of Heaven, ikiwa ni siku tatu baada ya kuuawa. Mazishi hayo yaliongozwa na baba askofu wa Dublin yalihudhuriwa na waombolezaji wapatao 1,000 wakiwamo Rais wa Ireland, waziri mkuu pamoja na baadhi ya mawaziri na watu mashuhuri.
  Siku mbili baadae nchi ya Ireland ilifanya kumbukumbu kwa wananchi wote nchi nzima kusimama kwa dakika moja, na Rais wa nchi hiyo alimtangaza Veronica Guerin, kuwa shujaa wa nchi hiyo.

  Ili kujua sababu za Veronica kuuawa, na pia kujua muuaji aliyehusika na mauaji hayo, Polisi walianza kuchunguza taarifa alizokuwa akiziandika pamoja na wahusika, aliowahi kuwaandika.

  Je Huyu Veronica Guerin ni nani, na kwa nini aliuawa?

  Veronica Guerin alizaliwa hapo mnamo mwaka 1958 katika eneo la Artane jijini Dublin na wazazi wake walikuwa ni Christopher na mkewe Bernadette. Veronica alipewa jina la utani la "Ronnie."
  Alisoma katika shule ya seminari ya Kikatoliki na alichukua masomo ya uhasibu. Baada ya kumaliza masomo yake aliajiriwa na baba yake katika kampuni yake na baada ya kifo cha baba yake miaka mitatu baadae, alibadilisha taaluma yake na kuanzisha kampuni yake ya mambo ya uhusiano (Public Relations) hapo mnamo mwaka 1983 kampuni ambayo aliiendesha kwa miaka saba.

  Kuanzia mwaka 1983 mpaka mwaka 1984 aliajiriwa katika kampuni moja ijukanayo kama Fianna Fail akiwa kama katibu muhtasi. Baadae alihamia katika kampuni nyingine iitwayo Charles Haughey na kufanya kazi kama msaidizi wa Mkurugenzi mkuu (Personal Assistant to CEO)Mnamo mwaka 1990 alibadilisha taaluma yake na kuwa mwandishi wa habari, wakati huo akiwa na umri wa miaka 30, na mama wa mtoto mmoja wa kiume aitwae Cathal aliyemzaa na mumewe aitwae Graha Turley.

  Alianzia katika gazeti la Sunday Business Post na baadae gazeti la Sunday Tribune.
  Akiwa na ujuzi wa biashara na taaluma ya uhasibu aliweza kuchanganya taaluma hizo na kwa umahiri mkubwa alimudu kufuatilia habari kwa kuanzia kwenye chanzo bila kujali usalama wake ili kupata habari yenye mashiko. Utendaji wake mzuri katika kufuatilia habari ulimjengea jina na kumuweka karibu na vyombo vya usalama (Polisi) vya nchi hiyo ambavyo vilikuwa vikinufaika na habari alizokuwa akiziandika juu ya uhalifu uliokuwa ukilitikisa jiji hilo la Dublin.

  Mnamo mwaka 1993 alipata bahati ambayo mwandishi yeyote angeota kuipata. Katika kipindi hicho kuliibuka kashfa ambayo ilimhusu padri wa kikatoliki wa kanisa la Galway aitwae Eamonn Casey, ilipokuja kugundulika kwamba alikuwa na mtoto wa kiume wa umri wa ubarubaru aliyemzaa nchini Marekani. Baada ya kashfa hiyo kuibuka, padri huyo alijiuzulu na kutoweka kusikojulikana, Veronica Guerin alichunguza na kugundua kwamba padri Eamonn Casey alikimbilia Amerika ya Kusini ambapo alimfuata na kufanya naye mahojiano yaliyokuja kutangazwa karibu dunia nzima yakiripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari. Mahojiano hayo yalimfanya Veronica kuwa maarufu kwa muda mfupi mno.

  Miezi michache baadae Veronica alianza kuwindwa na vyombo vikubwa vya habari, kila chombo kikimhitaji kwa ajili ya kukiandikia habari.
  Katika harakati hizo za kugombewa ni gazeti la Sunday Independent pekee ndilo lililofanikiwa kumnyakua mwanamama huyo.

  Veronica na habari za wahalifu wasioguswa………………

  Kuanzia mwaka 1994 alikuwa akiandika habari za kihalifu katika gazeti hilo la Sunday Independent, ambapo alikuwa kifuatilia habari za kihalifu na zile za kifisadi kwa kumulika zaidi ngome za wahalifu zilizokuwa zikiogopwa nchini humo. Baadae aligeukia ngome ya wauzaji wa madawa ya kulevya na wasafirishaji wa fedha haramu (Money Laundering) na alianza kuwachunguza magwiji wa biashara hiyo walioshindikana.

  Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Veronica kujijengea maadui ambao walimuona kama tishio kwa biashara zao.
  Mtu wa kwanza kuanza kufuatiliwa na Veronica alikuwa ni Martin Cahill, ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la utani kama The General. Huyu alikuwa ni mtu hatari aliyekuwa akiogopwa sana katika jiji la Dublin kutokana na kufadhili magenge ya kihalifu.Pia alikuwa ni mtu katili ambaye aliwahi kumpigilia misumari sakafuni askari kanzu mmoja aliyekuwa akimfuatilia na katika tukio lingine aliwahi kumchuna ngozi akiwa hai kibaraka mmoja wa polisi.

  Veronica alimfuatilia The General kwa muda wa mwezi mmoja, hadi akakubali kufanya naye mahojiano, lakini kwa masharti kwamba, asirekodiwe kwenye kifaa cha kurekodi mahojiano, yaani kinasa sauti.
  Katika mahojiano hayo The General alikanusha katukatu kushirikiana na magenge ya kihalifu. Miezi michache baada ya mahojiano yale, mnamo mwezi agosti, 1994 The General aliuawa na muuaji wa IRA na sababu ya kuuawa ilitokana na kushirikiana kwake na wapiganaji wa kiprotestant walioko magharibi mwa Ireland. IRA ni kikundi cha kupigania uhuru wa Ireland kutoka uingereza.

  Veronica aliliandika tukio la kuuawa kwa The General kama mpango maalum ulioandaliwa na IRA ili kuwazuia mabwana wakubwa hao kuhojiwa na vyombo vya habari, ingawa hakumtaja muuaji katika makala yake. Wiki chache baada ya habari ile kutoka gazetini, Veronica alivamiwa na mtu mmoja mwenye silaha ambaye alifyatua risasi kupitia dirishani katika chumba cha kupumzikia, muda mfupi baada ya Veronica na mwanae aliyekuwa na umri wa miaka minne kuondoka pale sebuleni.

  Tukio lile lilimtisha sana Veronica lakini alisema halitosababisha yeye kurudi nyuma. Mtu wa pili kufuatiliwa na Veronica alikuwa rafiki wa karibu wa The General, ambaye si mwingine bali alikuwa ni John Traynor ambaye pia alijulikana kwa jina la The Coach. Traynor alikuwa ni tapeli la kutupwa ambaye hata polisi waliamini kwamba ndiye aliyehusika na shambulio lililofanywa nyumbani kwa Veronica.

  Pamoja na kujua kwamba Traynor ni mtu wa kuogopwa, lakini Veronica alimfuatilia na kufanya naye mahojiano mara mbili mwaka 1994. Mnamo Januari 1995 Veronica aliandika makala iliyomwelezea Traynor kama mhalifu wa kuogopwa na ambaye amewahi kufadhili na kushiriki katika matukio ya kihalifu siku za nyuma.Polisi hawakutilia maanani makala ile na walipuuza na kusema haina ushahidi wa kina wa kumhusisha Traynor na uhalifu uliotokea siku za nyuma…….

  Kitendo cha kuwagusa wahalifu walioshindikana chamtumbukia nyongo.....................

  Wiki moja baada ya makala ile kutoka katika gazeti la Sunday Independent, Veronica alivamiwa na nyumbani kwake akiwa peke yake na mtu aliyeficha uso wake ili asitambulike. Mtu yule alimshurutisha Veronica apige magoti chini na alimuelekeza bastola kisogoni na kuashiria kuifyatua lakini alisita na kumpiga Veronica risasi ya mguuni halafu akatoweka.

  Veronica alifanikiwa kujiburuza na kuifikia simu na kuwapigia polisi kuwajulisha kuhusu uvamizi ule, Polisi walifika na kumkimbiza hospitalini. Veronica alitoka mwenyewe hospitalini bila kuruhusiwa na daktari, kwa kuwa alikuwa hajapona vizuri kiasi cha kushindwa kuendesha gari, mumewe Graham Turley alimchukua na kupita naye kwenye maeneo ya wahalifu aliowatuhumu kuhusika na tukio la kuvamia nyumbani kwake ili kuwaonesha kwamba amepona na atarejea kazini kwake kama kawaida.

  Ndani ya wiki moja tangu alipopigwa risasi, Veronica alirejea kwenye dawati lake la habari na kwenye toleo la gazeti la wiki iliyofuata aliandika kuhusu mkasa alioupata lakini aliwaonya maadui zake kwamba wasidhani ataacha kuandika habari zao.Kwa maneno yake mwenyewe aliandika, "nilisema na ninarudia tena, sidhani kama ninayo dhamira ya kuacha kuandika uozo wenu, ingawa bosi wangu amenipa chaguo la kubadilisha mwelekeo wa habari zangu, sitarajii kabisa kuacha na sitarajii kuanza kuandika habari za matamasha ya wanyange na ulimbwende au kuandika habari za namna ya kutengeneza na kutunza bustani za maua."

  Kutokana na tishio hili la kutaka kuuawa, bosi wake alimuwekea walinzi wa kumlinda wakati wote na pia Polisi wa nchi hiyo walimuwekea Polisi wa kuongozana naye katika mizunguko yake ya kutafuta habari, lakini katika hali ya kushangaza alikataa ulinzi huo kwa maelezo kwamba walinzi hao wanamzuia kufanya kazi yake kwa ufanisi..............

  Veronica aendelea kuyaweka maisha yake hatarini…………………..

  Kwa kipindi cha miezi tisa kilikuwa ni cha kuchapa kazi kama kawaida na katika kipindi hicho aliweza kufichua kashfa kadhaa za rushwa na uhalifu zilizotamalaki katika jiji la Dublin. Kutokana na kufichua uozo huo, Veronica alijitanabahisha kama adui namba moja aliyekuwa amejijengea maadui wengi miongoni mwa wahalifu wakubwa.

  Mnamo mwaka 1995 Septemba, Veronica aliona huo ndio wakati muafaka wa kulivaa gwiji la uhalifu liitwalo John Gilligan ili amhoji maswali kadhaa.
  Historia ilikuwa inamuonesha John Gilligan kama mhalifu mzoefu ambaye si chini ya miaka mitatu iliyopita ndio alikuwa ametoka jela, lakini kwa kipindi kifupi akawa amefungua mradi uliogharimu mamilioni ya dola.

  Veronica alitaka kujua amewezaje kufungua mradi mkubwa vile na kwa muda mfupi kiasi kile, tangu alipotoka jela?
  Alikwenda kwa Gilligan bila taarifa na kwa mujibu wa maelezo yake, alipofika nyumbani kwa Gilligan alikutana naye mlangoni akiwa na vazi la kuogea.Inasemekana Gilligan alikuwa mkali na alipomkaribia alimsukuma na kofi la uso na baadae la kifuani huku akimwambia, "kama ukiandika jambo lolote linalonihusu mimi, hakika nitakuua wewe, mumeo, mtoto wenu, familia yako na kila mtu anayekuhusu."

  Alipomaliza kusema hivyo alimsukumia kwenye gari alilokuja nalo kisha akamchania nguo zake ili kuangalia kama veronica alikuwa na mashine ya kunasia sauti ambayo hata hivyo hakuwa nayo. Baada ya kuhakikisha kama hakuwa na kinasa sauti alimuamuru aondoke pale haraka sana. Kwa vile lilikuwa ni shambulio la moja kwa moja, ukweli ni kwamba lilimtisha sana Veronica kushinda matukio mawili ya nyuma yaliyohusisha silaha.

  Baada ya kuripoti tukio lile kwa bosi wake, ilibidi washauriane na mwanasheria wa gazeti na hatimaye walifungua kesi ya shambulio dhidi ya Gilligan. Kutokana na shambulio lile Veronica alianza kufikiria kuacha kazi ile ya uandishi wa kiuchunguzi, hasa baada ya kuona familia yake nayo iko hatarini kwa sababu ya kazi anayoifanya. Siku ya jumanne ya tarehe 25, Juni 1996 John Gilligan alifikishwa katika mahakama ya Dublin akishitakiwa kwa kosa la shambulio la aibu dhidi ya Veronica Guerin.

  Gilligan alikanusha mashitaka na kuachiwa kwa dhamana akisubiri kesi kusikilizwa rasmi tarehe 9 Julai, 1996. Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Gilligan aliondoka mahakamani moja kwa moja na kuelekea uwanja wa ndege na kupanda ndege kuelekea Amsterdam, safari ambayo aliieleza kama ya kibiashara.Gilligana alijua dhahiri angehusishwa na mauaji ya Veronica, hivyo kuwepo kwake nje ya Ireland alijua kungemsaidia kutohusishwa na mauaji yale.

  Alipopigiwa simu na mwandishi wa gazeti la Daily Mail alijibu kwa mkato, "sijafanya jambo lolote baya na wala sina ushahidi wowote kuhusiana na mauaji hayo, na ninadhani mauaji hayo yamepangwa na kutekelezwa ikiwa ni mpango maalum ili nihusishwe."Wakati Gilligan akiwa ni mtuhumiwa katika mauaji ya Veronica, polisi wa Dublin waliingia katika operesheni maalum ya kuwasaka watuhumiwa wakubwa na waliokuwa kama miungu watu.

  Katika operesheni hiyo iliyohusisha wapelelezi maalum wapatao 50, walifanikiwa kuwahoji washukiwa zaidi ya 1,000, miongoni mwao watuhumiwa 60 walitiwa nguvuni lakini hakuna aliyeshitakiwa kwa kosa la mauaji ya Veronica Guerin.
  Hata hivyo polisi hao walifanikiwa kukamata fedha zenye thamani ya dola 200,000 na silaha zilizokuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria.Mnamo tarehe 8 October 1996 John Gilligan alikamatwa na askari wa ushuru kwenye uwanja wa Heathrow jijini London akiwa njiani kupanda ndege kuelekea Amsterdam, huku akiwa na kiasi kikubwa cha pesa kinachokadiriwa kufikia dola 500,000.

  Alishitakiwa kwa kifungu cha sheria ya usafirishaji wa dawa za kulevywa pamoja na kiasi kikubwa cha pesa. Gilligan aliwekwa kwenye gereza lanye ulinzi mkali la Belmarsh, ambapo alihojiwa na maofisa kadhaa wa polisi kuhusiana na tuhuma zinazomkabili ikiwemo ya mauaji ya Veronica Guerin, lakini alikanusha kuhusika na mauaji hayo.Siku kumi baada ya Gilligan kukamatwa, kijana mmoja aitwae Paul Ward, aliyekuwa na umri wa miaka 32 alikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la la kula njama na kutekeleza mauaji ya Veronica Guerin, pamoja na kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la utani kama Tosser ambaye ndiye aliyeaminika kuwa aliendesha pikipiki siku ya mauaji.

  Watu hao wawili walifikishwa mahakamani ingawa vielelezo kama vile pikipiki na silaha iliyotumika havikupatikana.
  Mnamo November 1998 Paul Ward alipatikana na hatia ya mauaji ya Veronica Guerin na kuhukumiwa kifungo cha maisha. Wakati akiendelea kutumikia adhabu yake ya kifungo cha maisha, mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la Brian Meehan naye alipatikana na kosa la kushiriki katika mauaji ya Veronica Guerin.Kama vile Paul Ward, naye alihukumiwa kifungo cha maisha.

  Kwa upande wa John Gilligan, kesi yake iliendelea kuunguruma nchini Uingereza na hatimaye alihukumiwa kifungo cha miaka 28 kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya, adhabu ambayo ilipunguzwa hadi miaka 20 baada ya kukata rufaa.
  Tukio la kuuawa kwa mwandishi huyu wa habari lilipelekea kutengenezwa kwa filamu mbili zilizojizolea umaarufu ambazo ni When the Sky Falls iliyotengenezwa mwaka 2000 na nyingine iliyopewa jina la mwandishi huyu, iitwayo Veronica Guerin iliyotengenezwa mwaka 2003.

  Hata hivyo yupo mwandishi mmoja wa habari nchini Ireland aitwae Emily O'Reilly ambaye ametunga kitabu kinachozungumzia maisha hadi kifo cha Veronica Guerin alichokitoa mwaka 1998 na kukipa jina la Life and Death of a Crime Reporter.

  Kitabu hicho kinaonekana kinamsimanga Veronica na waajiri wake, kwamba Veronica binafsi alikuwa mzembe na aliyejisababishia umauti wake mwenyewe, kimeshutumiwa na watu wengi, kiasi cha kumuita mama huyu aliyetunga kitabu kwamba ana roho mbaya na anatafuta umaarufu kupitia mgongo wa Veronica Guerin baada ya kifo chake, madai ambayo, Emily binafsi aliyakanusha wakati alipohojiwa na BBC.   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 2. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #2
  Jun 29, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Haya kama kawaida ni Ijumaa nyingine tena nimekuja na mkasa huu wa kuuawa mwandishi wa habari mahiri nchini Ireland Veronica Guerin.
  Leo sina mengi ya kusema kwani habari yenyewe imejitosheleza............................
   
 3. PetCash

  PetCash JF-Expert Member

  #3
  Jun 29, 2012
  Joined: Mar 20, 2012
  Messages: 1,679
  Likes Received: 170
  Trophy Points: 160
  kisa cha kusisimua hasa
   
 4. ram

  ram JF-Expert Member

  #4
  Jun 29, 2012
  Joined: Oct 5, 2007
  Messages: 6,203
  Likes Received: 905
  Trophy Points: 280
  Mtambuzi, hizi za wazungu zimetushosha, leta za wabongo, kesi ya Sara Simabaulanga wapi?
   
 5. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #5
  Jun 29, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Naomba muwe wavumilivu, hii nchi yetu kupata kesi kunahitaji subira, za wazungu zimejaa mtandaoni..............
   
 6. mbalu

  mbalu JF-Expert Member

  #6
  Jun 29, 2012
  Joined: May 18, 2012
  Messages: 553
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  Obhe'ja goku, ni kweli alijitakia kifo kwa ukaidi wake, ingawa kibinadamu napaswa kumhurumia na kumpongeza pia.
   
 7. JOYCE PAUL

  JOYCE PAUL JF-Expert Member

  #7
  Jun 29, 2012
  Joined: Jan 8, 2010
  Messages: 1,007
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 135
  unamaaanisha hii unailinganisha na ya dr ulimoka au?
   
 8. ndetichia

  ndetichia JF-Expert Member

  #8
  Jun 29, 2012
  Joined: Mar 18, 2011
  Messages: 27,641
  Likes Received: 236
  Trophy Points: 160
  na licha ya hivyo ukitoa tu wanaku ulimboka..
   
 9. ummu kulthum

  ummu kulthum JF-Expert Member

  #9
  Jun 29, 2012
  Joined: Feb 6, 2012
  Messages: 2,791
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  inaniogopesha hii.kalale pema peponi
   
 10. Kamkuki

  Kamkuki JF-Expert Member

  #10
  Jun 29, 2012
  Joined: Feb 1, 2011
  Messages: 1,067
  Likes Received: 94
  Trophy Points: 145
  Ni kisa cha kusisimua kweli kweli, Dunia gunia loh!!!!
   
 11. The Listener

  The Listener JF-Expert Member

  #11
  Jun 29, 2012
  Joined: Feb 5, 2012
  Messages: 977
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Kuna mambo mengi ambayo makundi mbalimbali yenye maslahi katika masuala yanayohusiana na uhalifu yanaweza kujifunza:

  • Umaarufu na ujasiri wa Veronica (Kazi ya uandishi wa kiuchunguzi): Alikuwa mwandishi maarufu na jasiri alipokuwa hai lakini umaarufu wake uliendelea na umeendelea kuwepo hata baada ya umauti kumkuta. Kazi yake ya kiuchunguzi ilimjengea maadui wengi lakini na marafiki wengi pia wengi wao wakiwa mapolisi ambao walifaidika sana na taarifa zake za kiuchunguzi.  • Uwepo wa makundi hatari/biashara haramu miongoni mwa wanajamii: Zimekuwepo kazi haramu na halali ambazo zote zimekuwa zikiwapa kipato wahusika lakini kwa upande mmoja kazi nyingi haramu zimekuwa zikitoa matunda mazuri ndani ya muda mfupi (Mfano mzuri ni kiasi cha dola 500,000 alizokamatwa nazo JoHN Gilligan kwa biashara zake haramu zilizohusisha na ukwepaji wa kodi). Malalamiko makubwa yamekuwepo hapa nchini kwetu juu ya ukwepaji mkubwa wa kodi kwa wafanyabiashara wakubwa. Huu pia ni uharamu/uhalifu. Biashara ya madawa ya kulevya imezidi kuota mizizi na wahusika wamekuwa hawashikiki kiurahisi.Wahusika wakuu wamekuwa na uwezo mkubwa wa kuchukua hatua yoyote mikononi mwao kufanya jambo lolote kwa yeyote anayejaribu kuingilia kati mafanikio ya biashara yao.  • Eneo la tukio: Hili ni eneo linalohitaji elimu pana na hasa kwa wale wote wanaopambana na masuala ya kiuhalifu (wanamipango miji, wanausalama, wananchi wa kawaida bila kudharau mchango wa wahalifu wazoefu ambao wameamua kwa hiari yaop kuachana na matukioa ya kiuhalifu). Ni muhimu kwa maeneo yote yenye msongamano mkubwa wa watu au magari yakawa na kamera - CCTV Camera - kwa lengo la kuhifadhi kumbukumbu za kiuhalifu kwa ajili ya ufuatiliaji. Ni sehemu ngapi hapa kwetu TZ zenye vifaa hivi na hasa katika miji mikubwa - Inanikumbusha katika miaka ya mwanzo ya 2000 ambapo kuna tukio kubwa la kiuhalifu la kibenki lilitokea makutano ya barabara ya ubungo na mandela maarufu kama ubungo mataa. Lilitokea bonge la sinema ambalo lilinaswa na wenye simu wachache na ambao walikuwa majasiri kupiga picha tukio lile. Ingekuwa kuna vifaa hivi basi nadhani watuhumiwa wote wangekuwa kunakostahili- sina uhakika kama walikamatwa au la.  • Kuguswa kwa Serikali na uimara au udhaifu wa Idara ya Polisi na vyombo vya usalama: Serikali ya Ireland iliguswa na tukio hili kwa kuwa ilikuwa na dhamira ya dhati ya kupambana na matukio ya kiuhalifu na hasa mapambano dhidi ya madawa ya kulevya. Kwa kuthibitisha hili iliweka mnara maalumu kumuenzi Bi Veronica na ilitenga dau kubwa la Dola 150,000 kwa yeyote ambaye angeweza kutoa habari ambazo zingefanikisha kukamatwa kwa watu waliohusika na kifo cha Bi Veronica. Nimewasikia baadhi ya wabunge wakimshambulia Dr Ulimboka kwamba anastahili kipigo alichokipata wakati asili ya mgomo wa madaktari ni kuisaidia Serikali kuboresha sekta ya Afya nchini (Sina uhakika kama kuna mguso wa dhati kwa hili - mi si mwanasiasa nisilaumiwe kwa maoni haya kwani ni mtazamo wangu tu). Kama zilivyo idara nyingi za kiusalama za nchi nyingi duniani, nyingi kati ya hizo zina hofu ya ama makusudi au kuzidiwa ujanja na wahalifu katika kuwafuatilia wahalifu wakubwa na wazoefu hadi yatokee maafa makubwa au ya watu maarufu kama yaliyomtokea Bi Veronica (Lengo kubwa hapa liwe ni kuzuia uhalifu usitokee na si kufanya uchunguzi baada ya matukio kutokea).  • Wahalifu wa kaliba ya Gilligan na mbinu zao ongofu kwa serikali: Gilligan alikuwa ni mhalifu mzoefu ambaye alikuwa na uwezo wa kutumia mbinu yoyote kuihadaa Serikali ili kufanikisha matakwa ya uhalifu wake.

  FUNZO: Kuna haja ya kuwa na waandishi wa aina ya Bi Veronica kwa manufaa ya nchi yetu. Waandishi wetu leo wamekuwa ni wa kununuliwa kufuatana na upepo wa siasa zetu waendaje. Imenikumbusha mbali kidogo ile ishu ya Jerry Muro na Watawala wa nchi

  'Mwanzo wa ngoma mara zote huwa ni kigelegele - Tubadilike leo kwa manufaa ya nchi yetu'

  Asante sana Mtambuzi. This is one of the good stuffs to learn
   
 12. The Listener

  The Listener JF-Expert Member

  #12
  Jun 29, 2012
  Joined: Feb 5, 2012
  Messages: 977
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Kimsingi Bi Veronica hakufa kifo cha kujitakia bali alikuwa jasiri na shujaa kwa kazi yake na faida ya Taifa lake kwa ujumla. Kuna mambo mengi ambayo makundi mbalimbali yenye maslahi katika masuala yanayohusiana na uhalifu yanaweza kujifunza:

  • Umaarufu na ujasiri wa Veronica (Kazi ya uandishi wa kiuchunguzi): Alikuwa mwandishi maarufu na jasiri alipokuwa hai lakini umaarufu wake uliendelea na umeendelea kuwepo hata baada ya umauti kumkuta. Kazi yake ya kiuchunguzi ilimjengea maadui wengi lakini na marafiki wengi pia wengi wao wakiwa mapolisi ambao walifaidika sana na taarifa zake za kiuchunguzi.  • Uwepo wa makundi hatari/biashara haramu miongoni mwa wanajamii: Zimekuwepo kazi haramu na halali ambazo zote zimekuwa zikiwapa kipato wahusika lakini kwa upande mmoja kazi nyingi haramu zimekuwa zikitoa matunda mazuri ndani ya muda mfupi (Mfano mzuri ni kiasi cha dola 500,000 alizokamatwa nazo JoHN Gilligan kwa biashara zake haramu zilizohusisha na ukwepaji wa kodi). Malalamiko makubwa yamekuwepo hapa nchini kwetu juu ya ukwepaji mkubwa wa kodi kwa wafanyabiashara wakubwa. Huu pia ni uharamu/uhalifu. Biashara ya madawa ya kulevya imezidi kuota mizizi na wahusika wamekuwa hawashikiki kiurahisi.Wahusika wakuu wamekuwa na uwezo mkubwa wa kuchukua hatua yoyote mikononi mwao kufanya jambo lolote kwa yeyote anayejaribu kuingilia kati mafanikio ya biashara yao.  • Eneo la tukio: Hili ni eneo linalohitaji elimu pana na hasa kwa wale wote wanaopambana na masuala ya kiuhalifu (wanamipango miji, wanausalama, wananchi wa kawaida bila kudharau mchango wa wahalifu wazoefu ambao wameamua kwa hiari yaop kuachana na matukioa ya kiuhalifu). Ni muhimu kwa maeneo yote yenye msongamano mkubwa wa watu au magari yakawa na kamera - CCTV Camera - kwa lengo la kuhifadhi kumbukumbu za kiuhalifu kwa ajili ya ufuatiliaji. Ni sehemu ngapi hapa kwetu TZ zenye vifaa hivi na hasa katika miji mikubwa - Inanikumbusha katika miaka ya mwanzo ya 2000 ambapo kuna tukio kubwa la kiuhalifu la kibenki lilitokea makutano ya barabara ya ubungo na mandela maarufu kama ubungo mataa. Lilitokea bonge la sinema ambalo lilinaswa na wenye simu wachache na ambao walikuwa majasiri kupiga picha tukio lile. Ingekuwa kuna vifaa hivi basi nadhani watuhumiwa wote wangekuwa kunakostahili- sina uhakika kama walikamatwa au la.  • Kuguswa kwa Serikali na uimara au udhaifu wa Idara ya Polisi na vyombo vya usalama: Serikali ya Ireland iliguswa na tukio hili kwa kuwa ilikuwa na dhamira ya dhati ya kupambana na matukio ya kiuhalifu na hasa mapambano dhidi ya madawa ya kulevya. Kwa kuthibitisha hili iliweka mnara maalumu kumuenzi Bi Veronica na ilitenga dau kubwa la Dola 150,000 kwa yeyote ambaye angeweza kutoa habari ambazo zingefanikisha kukamatwa kwa watu waliohusika na kifo cha Bi Veronica. Nimewasikia baadhi ya wabunge wakimshambulia Dr Ulimboka kwamba anastahili kipigo alichokipata wakati asili ya mgomo wa madaktari ni kuisaidia Serikali kuboresha sekta ya Afya nchini (Sina uhakika kama kuna mguso wa dhati kwa hili - mi si mwanasiasa nisilaumiwe kwa maoni haya kwani ni mtazamo wangu tu). Kama zilivyo idara nyingi za kiusalama za nchi nyingi duniani, nyingi kati ya hizo zina hofu ya ama makusudi au kuzidiwa ujanja na wahalifu katika kuwafuatilia wahalifu wakubwa na wazoefu hadi yatokee maafa makubwa au ya watu maarufu kama yaliyomtokea Bi Veronica (Lengo kubwa hapa liwe ni kuzuia uhalifu usitokee na si kufanya uchunguzi baada ya matukio kutokea).  • Wahalifu wa kaliba ya Gilligan na mbinu zao ongofu kwa serikali: Gilligan alikuwa ni mhalifu mzoefu ambaye alikuwa na uwezo wa kutumia mbinu yoyote kuihadaa Serikali ili kufanikisha matakwa ya uhalifu wake.

  FUNZO: Kuna haja ya kuwa na waandishi wa aina ya Bi Veronica kwa manufaa ya nchi yetu. Waandishi wetu leo wamekuwa ni wa kununuliwa kufuatana na upepo wa siasa zetu waendaje. Imenikumbusha mbali kidogo ile ishu ya Jerry Muro na Watawala wa nchi

  'Mwanzo wa ngoma mara zote huwa ni kigelegele - Tubadilike leo kwa manufaa ya nchi yetu'

  Asante sana Mtambuzi. This is one of the good stuffs to learn

  The Listener - Ex Detective
   
 13. nameless girl

  nameless girl JF-Expert Member

  #13
  Jun 29, 2012
  Joined: Apr 22, 2012
  Messages: 3,905
  Likes Received: 715
  Trophy Points: 280
  hakujitatakia, aliishi maisha ya kujiamini, tunapaswa kuiga mfano wake hasa waafrika
   
 14. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #14
  Jun 29, 2012
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 541
  Trophy Points: 280
  Asante sana ndugu mtambuzi kisa kinasisimua sana .
   
 15. Kayoka

  Kayoka JF-Expert Member

  #15
  Jun 29, 2012
  Joined: Jun 21, 2011
  Messages: 1,427
  Likes Received: 166
  Trophy Points: 160
  Mtambuzi kaka naomba kukumbushwa ile kesi ya yule bwana wa kitanzania aliyemuua mpwa wake na kukatakata mwili wake na kutupwa kando ya mto huko marekani, ulikuwa umeweka heading gani hapa jamvini?
  Ninaomba msaada wako
   
 16. Chris_Mambo

  Chris_Mambo JF-Expert Member

  #16
  Jun 29, 2012
  Joined: Aug 11, 2010
  Messages: 597
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Very interesting!!!
   
 17. Jodoki Kalimilo

  Jodoki Kalimilo JF-Expert Member

  #17
  Jun 29, 2012
  Joined: Feb 12, 2012
  Messages: 8,631
  Likes Received: 2,055
  Trophy Points: 280
  Hii ni kama ya Kubenea wa Mwanahalisi
   
 18. k

  kaeso JF-Expert Member

  #18
  Jun 29, 2012
  Joined: Mar 22, 2011
  Messages: 551
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Huyu mama hiki kifo alijitakia.
   
 19. p

  punainen-red JF-Expert Member

  #19
  Jun 30, 2012
  Joined: Nov 18, 2010
  Messages: 1,735
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Inaumiza sana jinsi wahalifu wasivyotaka kushindwa, uzuri wa wenzetu serikali zao angalau ziko imara, sisi hadi polisi wanasaidia kuwaua wapigania haki...
   
 20. paty

  paty JF-Expert Member

  #20
  Jun 30, 2012
  Joined: Oct 19, 2010
  Messages: 1,256
  Likes Received: 166
  Trophy Points: 160
  mkuu hiki kisa matata sana, nadhani hata kwenye jamii yetu tunaitaji watu majasiri kama bib Veronica
   
Loading...