Mbu
JF-Expert Member
- Jan 11, 2007
- 12,745
- 7,771
Afungwa kwa kukiri kumuua mumewe
2007-11-11 10:11:45
Na Jumbe Ismailly, Singida
Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imemhukumu mjane Asha Ramadhani (43), kufungwa jela miaka mitano baada ya kukiri kosa la kumuua mumewe bila kukusudia.
Mfungwa huyo mkazi wa kijiji cha Irisya katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida alikiri kumuua mumewe Selemani Ntandu(70)kwa kumchoma na kijanga cha moto mwili mzima.
Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Mwanaisha Gwariko wa Mahakama Kuu,wakati wa vikao vya mahakama hiyo vinavyoendelea mjini Singida.
Mwendesha Mashtaka na Mwanasheria wa serikali Bi.Neema Mwanda alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba 2002.
Mwanasheria huyo alidai siku hiyo saa 2:00 usiku katika kijiji cha Irisya Asha alimuua Ntandu baada ya kumchoma sehemu mbalimbali mwilini kwa kijinga cha moto.
Alidai kuwa mshtakiwa ambaye sasa ni mfungwa siku hiyo alirudi nyumbani akitokea kwenye pombe ya kienyeji akiwa amelewa chakari.
...sawa, madhali amekiri, 'naweza' kubali hakukusudia, lakini,...
Kwa mujibu wa Mwanasheria huyo wakati wanandoa hao wakiwa chumbani, mumewe alimhoji mkewe Asha sababu za kuendelea kulewa pombe wakati alimkataza tabia hiyo.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo hakupendezwa na kukaripiwa badala yake aliamua kuchukua kijinga cha moto na kumchoma sehemu mbalimbali za mwili mumewe.
Mwanasheria huyo alidai muda mfupi baadaye Ntandu alifariki dunia na mshtakiwa huyo alimburuza hadi sebuleni na kumlaza chini.
Alichukua kamba ya kufungia ng`ombe na kuifunga kwenye paa la nyumba kisha kuiviringisha kwenye shingo ya marehemu mumewe.
Alidai kuwa baada ya kumtundika kwa lengo la kuharibu ushahidi alikwenda kwa majirani kuwapa taarifa kwamba mumewe alijinyonga hadi kufa.
Hata hivyo, ilisemekana kwamba majirani zake hawakukubaliana na maelezo hayo na walipofanya uchunguzi, waligundua kuwepo kwa damu kwenye kitanda cha wanandoa hao.
...hapo ndipo ninapoingiwa na mashaka iwapo ni kweli hakukusudia!
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, wakili wa kujitegemea Bwana Nyangarika, aliiomba mahakama hiyo impe adhabu nafuu mteja wake kwa kuzingatia kwamba amekaa mahabusu miaka mitano na kwamba alitenda kosa hilo akiwa amelewa pombe.
Alimtetea kuwa, kwa kuwa alikuwa amelewa ni dhahiri amejuta na pia ni mara ya kwanza kukosa.
Akitoa adhabu hiyo, Jaji Gwariko alisema Mahakama yake imetafakari maombi ya mshtakiwa yaliyotolewa kwa niaba yake na wakili wake Nyangarika.
Pia imebaini kuwa mshtakiwa pamoja na kuwepo kwa pengo kubwa la umri kati yao lakini alikuwa anampenda mumewe kwa sababu ameonyesha dhahiri kujutia kosa hilo.
``Kwa hivyo Mahakama hii imefikia uamuzi wa kumpa mshtakiwa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka mitano jela ``, alisema jaji Gwariko.
...mnh, hainiingii akilini wajameni, hii inaweza kutokea tena katika jamii, kisingizio ikawa 'alilewa pombe, aliua bila kukusudia, ingawa pia alichukua kamba ya kufungia ng`ombe na kuifunga kwenye paa la nyumba kisha kuiviringisha kwenye shingo ya marehemu mumewe na kumtundika kwa lengo la kuharibu ushahidi.
swali;
...Inaingia akilini hii kweli?