Kutoka London:Taswira na mandhari ya mabasi usiku jijini London – 2

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,122
Na Freddy Macha
YARABI, ni saa tisa usiku. Bado niko ndani ya kiberenge. Ndiyo tumeingia mtaa wa Finsbury Park. Kwa kawaida basi lisingepita njia hii ila barabara zimefungwa fungwa. Kutokana na matayarisho ya michezo ya Olimpiki mwakani, London imekuwa ikikarabati mitaro, mifereji na mabomba ya kupitishia maji, vinyesi na uchafu wa vifaa, magari, majumba na watu. Miezi kumi hivi tu imesalia hadi hala hala za mashindano hayo ya kimataifa. Ingawa viwanja vikubwa vikubwa vya tukio hili viko mashariki ya jiji; mji mzima unajipika na kujiremba.


Waingereza walianza kupigania uenyeji wa mashindano ya Olimpiki mwaka 2005. Punde tu waliposhinda kura wakiongozwa na mwanasoka maarufu David Beckham na mkimbiaji wa zamani Sebastin Coe ambaye kaongoza shughuli hizi, magaidi walipasua mabomu vituo kadhaa mjini na kuua watu 52.


Kati ya malengo yao ilikuwa kuonyesha kwamba, London si mji wa amani. Lakini wakazi wa mji huu walisimama dede wakidai London imezoea kiama cha mabomu. Kwamba wakati wa vita vikuu vya Pili vya dunia (1939-1945) mji uliteketezwa kwa mabomu ya Wajerumani. Angamizo hilo lililoitwa “Blitz” halikuiua ari ya Wana London, wanasema wenyeji.

Waliamka wakakarabati mji wakaendelea na maisha. Fundisho moja. Ugaidi hauzuii amani na maendeleo.
,
Hapa Finsbury Park pana msikiti maarufu uliofungwa na kuanza kuchunguzwa sana baada ya mabomu ya New York mwaka 2001. Inasemekana wahusika wengi walikuwa wakisali hapa. Mmoja wa mashehe maarufu, Sheikh Hamza mwenye mkono na jicho moja alihubiri hapa. Leo yuko jela la Belmarsh akitumikia kifungo cha maisha.


Mtaa mzima umetulia kimya, wanaopita pita ni Waislamu wachache waliovaa kofia za barghashia baada ya sala kadhaa wakisubiri daku. Nashuka ndani ya basi. Mtaa huu una hoteli nyingi za Waarabu (hasa toka Algeria)na Waturuki. Nakutana na Issa rafiki yangu toka Algeria. Ndiyo katoka msikitini. Issa analo duka si mbali na tuliposimama.
“Vipi wewe Freddy bado unazurura?”
Tunacheka.


Wakati tukiongea wanapita jamaa kibao (Wasomali, Waarabu, Wapakistani) wamevalia kanzu na barghashia. Mwezi Ramadhani. Asiyeonekana hapa ni Mzungu. Kalala fofofo saa hizi.


Tunaongozana hadi kajihoteli ka’ Mturuki.
Naagiza chai ya rangi kwa tangawizi; Issa anachukua kondoo wa kuoka kwa mkate wa boflo wa Kituruki.


“Hutakula kitu?” Ananiuliza.
Naagizia Baklava ambayo ni kama Kalimati. Sema hii ya Waturuki imejaza sukari inayochuruzika utadhani uji wa asali.
“Vipi mambo?” Namuuliza.
“Alhamdulilahi,” anajibu kwa lepe la ukiwa.
“Biashara ngumu siku hizi; watu hawana fedha. Kila kitu kigumu, lakini Inshallah mambo yatanyooka.”
Runinga mbele yetu inaonyesha vurugu za Libya.
“Karibu watamshika,” naanza.
“Nani Muammar Gaddafi?”
“Ndiyo. Watu kibao wanamwonea huruma kwamba atauawa, atakamatwa; atapelekwa mahakamani.”
Issa anaguna.

“Nani wanamwonea huruma? Ohooo! Watu wanasahau Muammar Gaddafi ni mwanajeshi. Alipoingia uwanjani mwaka 1968 alikuwa jemadari, kijana wa miaka 27. Kanali. Si ****; si kifa urongo. Mbabe yule. Toka enzi hizo kafanya nini? Kasaidia wapigania uhuru wa IRA, Wapalestina; kasaidia Waafrika...Nasikia alimsaidia hata Idi Amin wa Uganda. Nyinyi Watanzania si mlimnyuka Idi Amin? (ninaitikia kwa kichwa). Kila mtu aliyetaka Uhuru, amani, maendeleo duniani alisaidiwa na Muammar Gaddafi. Lakini alichosahau kimoja tu. Watu wake. Ya nini unasaidia wengine kwako unapaacha?”


Nnauimba wimbo maarufu wa Kiswahili wa zamani : “Masuti njiani kumbe nyumbani kunguni tele.”

Issa anacheka karibu akabwe na kipande cha ile nyama ya kondoo anayokula.
“Wallahi, wallahi...”

Taarifa ya habari inamwonyesha mganga mmoja mjini Tripoli akilalamika namna hospitali za Libya zinavyohitaji dawa na waganga.

Issa : “Ananikumbusha Mugabe wa Zimbabwe. Yule mtu alipokuwa kijana pia alipigania haki ya nchi yake.Baada ya Uhuru kachinja watu wake. Mkombozi gani huyo? Jana nilikuwa nabishana na Marasta fulani toka Jamaika hujaga pale dukani kwangu. Wanasema eti wakienda Zimbabwe

hawahitaji viza. Mugabe kawahakikishia wakija Zimbabwe ni nyumbani kwao. Marasta wanampenda sana Mugabe. Si eti Bob Marley aliimba Zimbabwe ilipopata uhuru, 1980? Unakumbuka? Sasa kama Mugabe ni mpenzi wa marasta vipi anaua watu wake? Siwaelewi akina Muammar Gaddafi na Mugabe...kupendwa nje huku unatesa watu wako. Faida yake nini? Nimependa sana huo wimbo wa masuti njiani nyumbani kunguni tele. Nani aliutunga?”


Gumzo limestawi na baada ya kumaliza malaji tunaagana. Nangojea basi jingine namba 253 linaloelekea Stamford Hill; kitongoji cha Wayahudi. Basi linawapita wanaume wa Kiyahudi waliovalia suti nyeusi na majoho. Kidesturi, Wayahudi huvinjari mitaa yao wakihakikisha hakuna wahuni. Asubuhi sana wanaume hudamkia mahekalu yao yaitwayo sinagogi. Mbele yangu yuko mtu mfupi mnene, kibarange, anakoroma kwa nguvu.

Kando kakaa mwanamke , mkubwa mweusi. Ananikonyeza akizuia kicheko, akiutazama ute ukivuja mdomoni mwa yule kibarange.
“Kazi nyingi...” nasema.
“Kweli. Kila mtu saizi kachoka.”

Huyu mwanamke ana Kiingereza chenye lafudhi ya Nigeria au Afrika Magharibi.

Ghafla basi limesimama.
Kuna kijana kaja na baiskeli mbele ya basi; hajali atagongwa. Dereva anachungulia dirishani akijibizana na ‘yanki mmoja’.

“Unataka kufa sio?”

Kijana anamnyoshea dereva kidole cha kati kama kumtukana.

Basi linapotaka kuondoka, wanatokea vijana wengine wanne ; wote wamevalia makoti yaliyofunika vichwa na nyuso zao. Wawili wanachangia baiskeli; mmoja anaendesha; mwenzake kadandia nyuma huku kasimama. Sasa baiskeli zinalifuata basi. Kituo kinachofuata baiskeli zinakuja mbele ya basi. Wanacheza mbele yetu wakitafuta uchokozi.

“Hii nchi inakwenda wapi?” anauliza Mama wa Kinigeria.

Dereva anapiga honi, wale vijana wanaendelea na utukutu wao.
“Ingekuwa kwetu Nigeria dereva angewagongelea mbali.”

Basi linashusha abiria;huku wengine wapya wakipanda kwa hamasa.

Miye nashuka. Nimechoka na mabasi.
Naamua kutembea kuelekea kwangu.

Ingawa itanichukua dakika 15; nimechoshwa na vituko.

Ninapoingia barabara yangu baa kadhaa bado wazi. Walevi wanapiga kelele wakiimba kwa ile ile “raghba ya mkanja”. Kifupi wanachangamkia maisha, baadhi wakisaka wanawake; wanawake nao wakizuzuana na kuzozana na jamaa.

Wavuta sigara wamepangana nje; maana nchi hii kuvuta ndani uhalifu.

Niko mlangoni. Nje kakaa mbweha anajisaidia. Anaponiona anakitoa. Ukimbiaji wake wa kuchechemea. Kaumia mguu. Ngozi yake ina mabaka mabaka meusi na vidonda.
London hii usiku vioja tu.


Barua pepe: kilimanjaro1967@hotmail.com
Tovuti: Freddy Macha
 
Kaka fredi kwani umehama east london,Beckton na sasa upo uswahilini?
 
Back
Top Bottom