Kutoka London:Maendeleo yanavyoua maadili katika nchi zinazoendelea

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,297
33,082
Na Freddy Macha
KILA siku ya Mungu nilivyompita mama mzee anayeishi mtaa wangu hapa London nilimsikia akiongea peke yake. Mara ya kwanza kumsikia nilidhani ananisemesha.


Nikamsabahi. Duu. Akanisonya.
Watu weusi waliohamia hapa zamani kutoka visiwa vya Karibian na Afrika Magharibi ni wasonyaji wakubwa. Ni moja ya tabia ambazo mzungu hanazo kabisa. Mzungu akikasirika anavunja vunja vikombe, sahani, chupa, chochote kilicho mbele yake ndiyo namna yake yakuonyesha hasira kuhasimu vitu na vyombo. Sana sana atakutukana au kukunyooshea kidole (cha kati) lakini si mila yao kukufyonzea ulimi.


Basi nikajifunza; sikumsabahi tena ajuza. Si ajabu mji huu ukamsabahi mtu asiyekujua akakushangaa ingawa wapo wengi wanaoipokea salamu lakini kuidhihaki salamu ya asiyemjua ni sehemu mahsusi ya mila za miji mikubwa ya nchi zilizoendelea maana desturi ni hii: “kama hunijui au sikujui, usinijue jue.”
Lakini.


Tumrudie ajuza niliyemsema.
Baada ya kunisonya nilijawa na dukuduku. Nikauliza ulizia na kugundua huyu ni nyanya wa watu si mwenda wazimu tena si mtu mbaya. Hata ukienda kanisa fulani la hapa mtaani utamkuta Jumapili kajikwatua yuko na familia. Ana watoto wenye tabia za kawaida na wajukuu wake hawajawahi kukamatwa wameiba au kubeba visu (moja ya hulka kuu za London).


Nikabakia na maono fulani. Huyu mwanamke ni kati ya wengi wanaoweweseka peke yao si kwa vile wenda wazimu ila kwa kuwa mazingira haya hayana mambo ya kusemeshana semeshana ovyo.


Kwa kuwa hakuna kusemeshana semeshana ovyo basi ataongea peke yake. Utawakuta mama wa makamo au wazee weusi waliohamia hapa (zamani miaka 40 kuendelea) wako vile.
Katika basi utamwona ajuza au mama wa makamo kama huyu akiimba nyimbo za dini kwa Kiingereza:
“Yesu anakupenda, Yesu asifiwe.”
Ukiwa maduka makubwa makubwa (‘supamaketi’) si ajabu kumwona mama aina hiyo akiongea peke yake au akiuliza tu kwa nguvu.


“Jamani siagi iko wapi? Mbona siioni?”
Kidesturi kwa kuwa mila ya hapa si ya kusemeshana semeshana ovyo hadharani hatajibiwa. Ila siku hii kakukuta Mswahili unayejali utamaduni wa mawasiliano.
“Siagi? Iko kulee.” Utamwonyesa.
Atakushukuru. Siku nyingine utakutana na mwingine. Huyu atalalamika.


“Siku ya leo ya ovyo sana. Kila kitu wamepandisha bei. Miye basi siangalii tena bidhaa nasoma kwanza bei.”
Utamkubalia : “Kweli kabisa. Hata miye hivyo hivyo.”


“Nafurahi nimekutana na mtu anayeongea. Kila mtu humu ndani kajinunia tu.”
“Ni hali ya hewa, mama. Huoni jua halijawaka majuma mangapi sasa?”
Na kweli mvua na ukungu huwakosesha wananchi furaha. Kifupi hali ya hewa na mazingira huwafanya binadamu wawe na tabia kulingana. Bongo tunalalamika jua kali na joto vumbi, uchovu, mbu na ukame majuu lalamiko ni ukosefu wa jua baridi, unyevunyevu, pepo kali (wikiendi iliyopita pepo zilisababisha hata vifo kwa waendesha magari kutokana na miti kuvunjika ovyo) na mvua.


Basi kutokana na hali ya hewa na hiyo mila ya kila mtu na lwake watu hawasemeshani ovyo labda mjuane , labda muwe mnafanya kazi pamoja.


Lazime kuwe na sababu; kila mtu na lwake, bahati ya aliye mbele; aliyebakia nyuma akumbwe na shetani wake. Hizi ndizo kauli za utamaduni wa biashara na uchumi wa mashindano na fedha. Mwalimu Nyerere alitupa nahau maarufu ; “Ubepari ni unyama.”


Kwa upande mmoja ubepari ni maendeleo ya juu sana ya sayansi, elimu na zana; upande mwingine maendeleo hayo hujenga ubinafsi, uchoyo na kauli ya kutomjali mwenzio hata kama yuko katika hali mbaya.
Na huu ndiyo msingi wa kisa kilichompata msichana mmoja miezi michache iliyopita jiji la Nottingham Kaskazini ya London. Yaliandikwa na kuongelewa sana katika vyombo vya habari.


Dada wa kitishi (miaka 22) katoka zake klabu na wenzake. Saa tisa usiku. Keshauchapa vizuri lakini si mtoto wa kihuni bado anasoma anaishi na wazazi na hajalewa kiasi cha kujisahau. Kunywa pombe si dhambi wala makosa yategemea mtu na mtu. Mamake alikuwa akimsubiri ampokee kwa gari akishashuka kituo cha basi. Sasa alipopanda basi (tunaambiwa) hakuwa na pesa ya kutosha. Nauli ilikuwa pauni tano (kama shilingi elfu kumi na mbili).




Mabasi ya majuu huwa hayana kondakta; ukipanda mlangoni unampa dereva pesa ndiyo anakuruhusu kuingia. Dereva kakaa nyuma ya geti lenye kizuizi cha hali ya juu. Mna kamera zinazopiga picha kila linaloendelea ndani ya basi.


Dogodogo sasa yuko mlangoni anabishana na dereva.
“Nauli haitoshi.” (Dereva huyo).
Dada kabembeleza: “Nimepungukiwa pensi 20 tu( kama shilingi 500). Naomba nipande tukifika mbele ya safari mama yangu ananisubiri tutakupa hizo senti kidogo sana zilizobakia.”
Dereva: “Ah wapi. Huna nauli hili basi husipandi.”


Dada kamtolea jamaa pesa yote kasoro hizo pensi (senti) ishirini kamwonyesha dereva kamwomba, kamlilia, kamwomba. Dereva kamkatilia. Huku wakijadiliana, huku abiria wengine (kibao), wanasukumana kuingia, wengine chakari, wengine wamechoka, wanampita dada, kila mmoja analipa nauli, anaelekea zake kukaa. Kimya.


Magazeti yakaandika: “Hakuna hata abiria aliyejitolea kumsaidia msichana yule zile senti chache.”
Msichana akatolewa nje. Akaamua kutembea hadi amkute mamake anamsubiri maana mamake alimpigia simu anakuja kumfuata na gari.
Baada ya dakika chache si kakutana na mshashi (kijana wa miaka 19)? Mshashi keshazichapa, keshapakia bangi zake (bangi huvutwa miji hii ya Ulaya utadhani chai) akambaka na zaidi ya kumvunjia heshima hiyo akampiga sana msichana wa watu. “Alimtwanga kiasi ambacho hata mamake mzazi hakumtambua,” gazeti kubwa la nchi Daily Mail likaandika.


Baadaye lakini mbakaji alishikwa, akahukumiwa jela. Lakini tunaelezwa na mmoja na askari waliokichunguza kisa kwamba dereva hakuvunja sheria.
La muhimu kujiuliza ni suala la ustaarabu na ubinadamu wa nchi zilizoendelea na dunia inayoitwa ya kisasa. Je ubinadamu uko wapi?
Askari akasema :“Kila abiria aliyekuwa katika lile basi usiku ule, lazima ajiulize swali. Ajiulize moyoni mwake mna nini?”


Tabia ya wanadamu kujali nafsi zao tu na kutosaidia wenzao imeenea sana nchi tajiri. Katika nchi maskini mara nyingine hueleweka hohehahe wanapoparamia mabasi kwa woga wa kuyakosa lakini tujiulize moja. Je watu hawa hawa wakipewa utajiri watakuwaje? Je roho zao zitabadilika? Je binadamu wa leo kweli tuna ustaarabu kiasi gani?



Barua pepe: kilimanjaro1967@hotmail.com
Tovuti: Freddy Macha
 
Hichi kisa kinasikitisha sana lakini ndio faida ya kujifanya mmendelea sana mpaka UTU unakosa nafasi yake.
 
Kaka umenikumbusha mbali kidogo niliishi hapo bila family siku hazisogei,ubinafsi wa kila mtu kuweka headphones masikioni na novel mkononi ulikuwa mgumu sana kwangu,iwe kwenye transport iwe pub,au park ni hivyo tu!but kuna tofauti kati ya nchi waamerika wako interactive zaidi.
 
Back
Top Bottom