Kutoka Grand Coalition hadi Membe, Nini kitatokea kwa upinzani kuelekea Oktoba?

WOWOWO

JF-Expert Member
Aug 3, 2011
590
430
Kati ya tukio lililochukua headlines kwenye mchakato wa CCM kuwapata wagombea wake wa nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu ni kitendo cha Mwenyekiti wa muda wote na mmiliki wa chama cha UDP John Cheyo aka Bwana Mapesa kumwomba Mwenyekiti wa CCM Mbunge mmoja na madiwani watatu. Hili linafanana kabisa na TLP ya Bwana Augustine Mrema ambaye naye chama chake kimetangaza kumnadi rais Magufuli bila shaka kwa matarajio kwamba atapewa ubunge.

Msingi wa haya yote pamoja na kuwa umejengwa kwenye “kuunga mkono maendeleo ya JPM” lakini una kila dalili za uhusiano na vikao visivyo rasmi ambavyo Rais Magufuli alivifanya na vyama kadhaa vya upinzani Ikulu hususan vya ACT-Wazalendo (ukiiangaza Zanzibar zaidi), NCCR-Mageuzi (Upande wa Tanzania Bara), CUF, UDP na TLP. Katika vikao hivi chama kikuu cha Upinzani cha CHADEMA hakikualikwa kwa sababu ambazo nitajaribu kuzidadisi na kuziweka wazi.

Vyama pekee ambavyo vinaonekana kuweka wazi manuwio yao kutoka kwenye vikao au uhusiano na Ikulu ya Magogoni ni vya TLP na UDP. Hatusikii mengi yakisemwa kuhusu NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo iliyowakilishwa na Maalim Seif Sharif. Hata hivyo duru zinaripoti kwamba NCCR imepewa nguvu na ushirikiano ili kiwe chama kikuu cha upinzani Tanzania bara baada ya Oktoba, 2020. Lengo likiwa ni kukitokomeza CHADEMA kwa kile kinachoelezwa siasa za chama hiki kikuu cha upinzani haziungi mkono maendeleo bali kupinga na kufanya siasa zisizo za kistaarabu. Na hili ndilo sababu ya CHADEMA kutokushirikishwa katika kile kinachoitwa mazungumzo na Rais Ikulu. Mwenyekiti wake Freeman Mbowe wakati akihutubia wajumbe wa Baraza la Wanawake wa Chama hicho (BAWACHA) alinukuliwa akisema hawakualikwa na kwamba hata kama wangealikwa angetaka mazungumzo rasmi, ya kitaasisi na yenye kutanua ushiriki wa wadau wapana ili kujenga utengamano kuelekea uchaguzi mkuu. Alisisitiza haendi ikulu kutafuta uchumba.

Hata hivyo kitu pekee hakisemwi hapa ni ACT-Wazalendo na uwezekano wa ndoa Zanzibar na CCM. Ikumbukwe kwamba Katiba ya Zanzibar iliyopatikana kwa muafaka wa kisiasa inatambua Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Chama kishinde au kishindwe kina uhakika wa kuwemo kwenye serikali ya umoja wa kitaifa kama kitakidhi akidi hitajika ya kura. Udadisi wa mambo katika ushiriki wa Maalim Seif Sharif kwenye mazungumzo ya Ikulu unalalia kwenye ulali kwamba mazungumzo hayo yalilenga zaidi Siasa za Zanzibar kuliko bara. Na ni baada ya hapa ndipo viongozi wa ACT-Wazalendo wakiongozwa na watu wa aina ya ZZK, Jusa nk wamekuwa wakihubiri kile wanachokiita ‘The Grand Opposition Coalition’.

Duru na udadisi wa mambo unaonesha kwamba nyuma ya hiki kiitwacho the grand coalition ni mkakati wa ACT-Wazalendo kuziba ombwe la Tanzania Bara baada ya kuonekana kufunga mahesabu Zanzibar. Ingawa Chama hiki kinaonesha kutaja coalitions, lakini hakiamini katika hili maana tayari kinaonesha kuwa katika makubaliano yasiyo rasmi ya siasa za uchaguzi za Zanzibar. Yatosha kusema, ACT-Wazalendo tayari iko kwenye mkakati wa kuunda Serikali ya Umoja Zanzibar chini ya CCM. Hili linachagizwa zaidi na umri wa Maalim Sharif kusogea sana kiasi cha kuthubutu kusema hapa kwamba uchaguzi wa mwaka huu wa 2020 waweza kuwa wa mwisho kwake na hivyo kuhitaji kustaafu kwenye manufaa kwake. Hili la umri wa Maalim Seif linaathiri pia uhai wa harakati za upinzani imara ambazo zinazunguka zaidi jina lake kuliko wanasiasa wengine wa upinzani visiwani humo.

Zitto Kabwe na ACT amebaki na kazi nzito Tanzania Bara kwa maana ya Uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Awali ZZK alianza harakati za kumshawishi Tundu Lisu kufanya kazi hiyo, kupitia kugombea urais wa JMT. Hili limekwama. Itakumbukwa katika moja ya safari zake Ubelgiji ZZK alijikuta katika msuguano mkubwa na CHADEMA kwa tuhuma kwamba anakichonganisha chama hicho na Mwanasheria na sasa Makamu Mwenyekiti wake Lisu.

Baada ya mkakati huu kupata utata, ZZK alirejea tena kuhubiri grand coalition. Hapa akilenga ushirika na CHADEMA. Lengo ni kurejea kulekule, kujijenga bara zaidi. Bahati mbaya CHADEMA haikuonesha nia ya wazi kuingia kwenye ushirika hadi pale Katibu Mkuu wake John John Mnyika alipotangaza kufungua milango kwa vyama vinavyotaka ushirika. Ingawa katika hatua hii ACT-Wazalendo kupitia Katibu Mkuu wake Ado Shaibu kilionesha kuguswa na tangazo la CHADEMA itoshe kusema, bado hakuna dalili za wazi za hili kutokea. Kilichokuja kuongeza ugumu wa hili, ni kauli ya Mwenyekiti wa CHADEMA Mbowe pale alipotembelewa na viongozi wa CHASO nyumbani kwake siku kadhaa zilizopita. Alinukuliwa akisema wazi kwamba chama hicho hakiko katika kundi la vyama vinavyosaka wabunge wawili-watatu, bali kinasaka dola. Hii ni ishara kwamba CHADEMA hakihitaji nguvu ya vyama alivyoviita ‘visaka wabunge”, hivyo kitaenda katika uchaguzi mkuu wa 2020 kikiwa peke yake.

Aidha, mchakato wa ndani wa kumpata mpeperusha bendera wa nafasi ya urais wa JMT na Zanzibar inadhihirisha wazi hili. Tayari michakato hii miwili ndani ya CHADEMA imeshika kasi zaidi na iko katika hatua za mwisho. Hili ni tofauti na ACT-Wazalendo, ambacho kwa Zanzibar tayari kinaonesha kuwa na mgombea defacto Maalim Seif huku upande wa Tanzania Bara (JMT) kikisuasua.

Kuonekana kwa viongozi wa juu kabisa wa ACT-Wazalendo wakiwa na Waziri wa Zamani wa Mambo ya Kigeni Bernald Membe ambaye ametemwa na CCM kunaleta hitimisho kwamba chama hiki kiko katika kumshawishi Membe abebe bendera ya urais. Ikiwa ina maana ACT-Wazalendo pamoja na viongozi wake kuonekana mara kadhaa wakililia ‘Grand Coalitition’ ya opposition parties bado pia wanaendelea kumsaka Membe kugombea nafasi ya Urais (JMT). Ikumbukwe kwamba Membe pia aliwahi kutajwa kuwa nyuma ya uanzishwaji na baadaye usajili wa chama cha ACT-Wazalendo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.

HII INA MAANA GANI KWA SIASA ZA UPINZANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU?

Ni wazi vyama vya upinzani vitaingia kimoja-kimoja katika uchaguzi mkuu wa 2020 pamoja na kuwepo wa baadhi ya viongozi wanaohubiri ushirikiano. Hili linatokana na mazingira niliyoyaeleza hapo juu. Kuonekana kwa Bernard Membe kuutaka urais kwa udi na uvumba huku akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa ACT-Wazalendo kunaongeza zaidi ugumu wa ushirikiano. Kwa CHADEMA hii inatokana na historia aliyoiacha Edward Lowasa. Kisiasa CHADEMA kimejeruhiwa sana na kupokea Wagombea kutoka CCM na ni wazi kauli za Mbowe zinaonesha wazi kwamba chama hicho kimejifunza somo gumu. Uwepo wa Membe katikati ya mchakato ya Urais haioneshi kuvuma kwa upepo mwanana ndani ya CHADEMA zaidi ya kuamini mchakato wake wa ndani.

Mambo mawili yatatokea. Membe likely atagombea urais kupitia ACT, maana ni ndoto yake, anaugua ugonjwa wa urais na haoneshi kuamini kwamba kuna mtu zaidi yake katika kupeperusha bendera. Kwa CHADEMA karata ziko nyingi, ingawa swali linabaki kwenye hatma ya jina la mwisho na usalama wa chama baada ya hapo. Aidha, kazi ngumu zaidi iko katika mchakato wa uteuzi wa Tume ya Uchaguzi. Historia ya kilichotokea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka jana 2019 bado ni Mwalimu Mkuu kwenye uchaguzi mkuu huu. Hapa patahitaji busara zaidi za kisiasa na uvumilivu wa vyama vya upinzani.

Katikati ya Bernard Membe kubeba bendera ya ACT-Wazalendo kwenye urais wa JMT huku Zanzibar chama hiki kikiwa wazi katika siasa zake na CHADEMA kuamini katika inward politics kutokana na historia, kuna mambo matatu yatatokea. Mosi, mchakato wa ndani wa vyama viwili vikubwa vya CCM na cha Upinzani CHADEMA katika kupata wagombea ubunge na madiwani waweza kukigeuza chama cha ACT kimbilio la ‘watakaokatwa’. Kwa ACT kupata faida hapa itategemea kama vyama vitashindwa kufanya michujo kwa umakini na kuzingatia popularity ya wagombea. Pili; kura za urais za ACT-Wazalendo zitategemea uimara na ushawishi wa Bernad Membe na kwa historia ya Lowassa uwezekano mkubwa kura zitakazopungua ni za Mgombea wa urais wa CCM kuliko wa CHADEMA. Hapa ina maana kwamba kama Bernard Membe ana ushawishi ndani ya CCM ataiathiri zaidi CCM kuliko CHADEMA. CHADEMA itabaki na mtaji wake wa ‘CHADEMA ni msingi’ kama kweli upo na kubaki na ushindani wa undecided voters. Tatu; NCCR-Mageuzi ambayo awali ilipewa nafasi kuchukua nafasi ya chama kikuu cha upinzani baada ya Oktoba 2020 itapoteza maana katikati ya Bernard Membe, CHADEMA na CCM.

Vyovyote vile mtanange wa Bernard Membe chini ya ACT Wazalendo, John Pombe Magufuli chini ya CCM na Mgombea wa CHADEMA (pengine Tundu Lissu) utaleta historia mpya ya Siasa za Tanzania. Kama uwanja ukiachwa kwa wanasiasa, waucheze kwa hoja, mikakati halali na mbinu za ushindi wa haki basi uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa kipekee na mchakamchaka kwa pande zote utakuwa si wa kitoto. Hata hivyo yote haya yatategemea busara za vyombo vya dola katika kusimama katikati na kutimiza wajibu wake wa kikatiba.
 
....mikakati halali na mbinu za ushindi wa haki basi uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa kipekee na mchakamchaka kwa pande zote utakuwa si wa kitoto.
Asante sana kwa mada yako juu ya uchaguzi wa mwaka huu, Mkuu.

Ninaomba utoe ufafanuzi zaidi juu ya maneno yako uliyoandika na mimi nikayanukuu hapo juu. Hasa vipengele vya ' mikakati halali na mbinu za ushindi wa haki'. Itakuwa vyema kama kwenye ufafanuzi wako utaweza kutoa na mifano ili mimi pamoja na baadhi ya wengine tuweze kuelewa kwa ufasaha ulichokuwa una maanisha kwenye mafungu hayo ya maneno niliyosisitiza.

Karibu.
 
Asante sana kwa mada yako juu ya uchaguzi wa mwaka huu, Mkuu.

Ninaomba utoe ufafanuzi zaidi juu ya maneno yako uliyoandika na mimi nikayanukuu hapo juu. Hasa vipengele vya ' mikakati halali na mbinu za ushindi wa haki'. Itakuwa vyema kama kwenye ufafanuzi wako utaweza kutoa na mifano ili mimi pamoja na baadhi ya wengine tuweze kuelewa kwa ufasaha ulichokuwa una maanisha kwenye mafungu hayo ya maneno niliyosisitiza.

Karibu.
Akikujibu niletee message. Khe khe khe kheeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee
 
11 Reactions
Reply
Back
Top Bottom