KUTOKA BUNGENI: Rais Magufuli kuhamia Dodoma rasmi mwaka 2020

RUCCI

JF-Expert Member
Oct 6, 2011
1,701
1,714
Leo Septemba 16, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha mkutano wa nne kwa Bunge la 11 uliodumu kwa muda wa wiki mbili, amesoma ratiba ya serikali kuhamia Dodoma.

“Ili kufanikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma, tayari imeandaliwa ratiba itakayowezesha Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu, kuanzia mwezi Septemba, 2016 hadi mwaka 2020, bila ya kuathiri bajeti yetu ya mwaka 2016/2017 kama ifuatavyo”–


1. Septemba 2016 – Februari 2017.

Waziri Mkuu na Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wote, Manaibu Makatibu Wakuu wote watahamia Dodoma katika Awamu ya Kwanza. Aidha, kila Wizara itatakiwa kuhamisha Watumishi wa Idara moja au mbili, na wakati huo huo kuendelea kuweka utaratibu wa kupeleka Watumishi wa Idara nyingine kuhamia Dodoma;

2. Machi 2017 – Agosti 2017.

Kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali kuweka katika Bajeti zao za mwaka 2017/2018 gharama za kuendelea kuhamisha watumishi wake kuja Dodoma.

3. Septemba 2017 – Februari 2018.

Katika awamu hii, Wizara zitaendelea na uhamishaji wa Watumishi wa Idara zilizo ndani ya Wizara.

4. Machi 2018 – Agosti 2018.

Katika kipindi hiki, Wizara zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.

5. Septemba 2018 – Februari 2020.

Katika kipindi hiki, Wizara zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.

6. Machi 2020 – Juni 2020.

Katika kipindi hiki, Ofisi ya Rais ikiongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watakuwa wanahamia Dodoma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitumia wasaa huu kuzishauri Wizara zote kuanzisha mifumo ya utunzaji kumbukumbu wa kielektroniki badala ya kuhama na mafaili kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma, tunataka Dodoma iwe ya kielektroniki, alisisitiza Waziri Mkuu.
==================================
HOTUBA YA WAZIRI MKUU BUNGENI LEO
UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutulinda na kutupa afya njema hadi kutufikisha siku ya leo tunapohitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge lako Tukufu tuliouanza tarehe 6 Septemba, 2016.

Nitumie fursa hii pia kukupa pole, Mheshimiwa Spika, kwa maradhi yaliyokusibu lakini kikubwa nielezee furaha yangu kwa uponyaji ambao Mwenyezi Mungu amekujaalia na hivi sasa tuko pamoja humu ndani. Tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu uendelee kupata nguvu na afya njema.

Mheshimiwa Spika, tangu tulipokutana mara ya mwisho, kumekuwepo majanga na matukio mbalimbali ya maradhi, ajali, ujambazi na matukio mengine ambayo yamesababisha vifo na majeruhi kwa Watanzania wenzetu, wakiwemo Waheshimiwa Wabunge. Hivyo, ninatoa pole kwa wafiwa wote na wale wote waliopatwa na majanga kutokana na matukio hayo. Tunawaombea afya njema wale waliopata majeraha na waliopo hospitali.

Mheshimiwa Spika, leo tunahitimisha mkutano huu tukiwa tumekamilisha shughuli zote zilizopangwa kwenye Mkutano huu. Naomba nitumie fursa hii ya awali kabisa kukupongeza sana Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kukamilisha kazi zote kwa ufanisi mkubwa. Kazi hizo zilijumuisha kujadili na hatimaye kupitisha Miswada mbalimbali ya Serikali. Napenda kukiri kwamba mijadala ya mkutano huu ilikuwa ya uwazi na hoja zilizotolewa zililenga kuiletea maendeleo nchi yetu. Kutokana na michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge na yenye tija, ilibidi mara kadhaa vikao vyetu kuendelea hadi usiku nje ya muda wa kikanuni.Nawapongeza sana!

TUKIO LA JANGA LA TETEMEKO LA ARDHI LILILOTOKEA MIKOA YA KANDA YA ZIWA

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka kuwa tarehe 13 Septemba, 2016 Serikali iliwasilisha hapa Bungeni taarifa ya masikitiko kuhusu maafa makubwa yaliyoikumba Nchi yetu tarehe 10 Septemba, 2016 kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Kagera, Geita, Mwanza na Mara. Tukio hilo ambalo liliathiri zaidi Mkoa wa Kagera lilitokea siku ya Jumamosi majira ya saa 9.27 alasiri, ambapo Mji wa Bukoba ulikumbwa na tetemeko la ardhi, lenye nguvu ya mtetemo wa kipimo cha 5.7, kwa kutumia skeli ya “Ritcher”. Tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu 17 na majeruhi253. Napenda nitumie nafasi hii kwa mara nyingine kuwapa pole wafiwa wote na wale waliopata majeraha mbalimbali. Tunaomba Mungu aziweke roho za Marehemu mahali pema peponi. Amina. Kwa wale waliopata majeraha, tunamuomba Mungu awaponye haraka.

Mheshimiwa Spika, tukio hilo limesababisha uharibifu mkubwa sana wa nyumba, vituo vya afya, shule pamoja na miundombinu ya barabara. Aidha, shule nne za Nyakato, Ihungo, Kashenge na Buhembe, zimeharibika ikiwemo vyoo, nyumba za walimu, kumbi za shule na mabweni. Nyumba 840 zimeteketea kabisa, na nyingine 1,264 kupata nyufa. Kwa sasa uongozi wa Mkoa wa Kagera pamoja na Kamati ya Maafa ya Mkoa na Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wataalamu wa masuala ya matetemeko, na wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya kina ya kiasi cha hasara iliyopatikana.

Mheshimiwa Spika, kama Bunge lako Tukufu lilivyojulishwa, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali, imechukua hatua kadhaa kushughulikia athari za tetemeko hilo ikiwa ni pamoja na kufanya jitihada ya kurejesha hali ya utulivu, miundombinu iliyoharibika ili kuirejesha katika hali ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada mbalimbali zilizofanyika ikiwemo viongozi kutembelea maeneo yenye madhara, mpaka sasa Serikali imefanya mambo yafuatayo:-

(a) Kuhusu Chakula: Wananchi wenye mahitaji ya chakula wameendelea kupatiwa chakula kama vile, unga, mchele na maharage, sukari na chumvi pamoja na mafuta ya kula. Tathmini ya kubaini mahitaji halisi ya chakula inaendelea.

(b) Kuhusu Matibabu: Serikali imeimarisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kwa kupeleka dawa na vifaa tiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa. Aidha, Timu ya Wataalam na Madakta 12 wamepelekwa Bukoba kutoka Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Bugando. Napenda kuwashukuru pia wadau mbalimbali ambao wamechangia eneo hili wakiwemo Medecins Sans Frontiers, Ubalozi wa China, Jhpiego (USAID) na Chama cha Wafamasia.

(c) Makazi: Wananchi waliokosa kabisa hifadhi ya makazi wamepewa maturubai na mahema kwa ajili ya makazi ya muda. Aidha, waathirika ambao nyumba zao zimebomoka kabisa, kwa kuanzia kila mmoja ametengewa mabati 20, saruji mifuko mitano, blanketi na mikeka. Pia wapangaji waliokuwa katika nyumba hizo kila mmoja ametengewa kodi ya pango ya miezi sita ili apate mahali pa kujihifadhi.

(d) Kuhusu Shule zilizoathirika: Serikali inajenga miundombinu ya muda ya shule kama vile madarasa, mabweni na vyoo hususani katika shule za sekondari za Ihungo na Nyakato zilizofungwa kwa muda wa wiki mbili. Tathmini ya kitaalam ikikamilika, mpango wa ujenzi wa miundombinu ya kudumu itafanyika na maandalizi yanaendelea kupata rasilimali kwa ajili hiyo.

(e) Mazishi: Serikali imeshiriki katika kuwafariji wafiwa na pia kushiriki mazishi kwa kusaidia kutoa jeneza, sanda, usafiri na kutenga fedha Shilingi milioni 20 za rambirambi kwa wafiwa ambazo zitatolewa kwao muda wowote kuanzia sasa.

(f) Barabara: Tathmini ya uharibifu wa barabara imefanyika na barabara zilizoharibika zitarejeshwa katika hali ya kawaida ili wananchi waendelee kupata huduma za msingi. Vilevile, Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha miundombinu ya maji safi na maji taka inakarabatiwa na kuhakikisha usafi unaendelea kuwa katika viwango stahiki.

Kwa ujumla, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa taasisi za umma ikiwemo majeshi ya ulinzi na usalama na rasilimali zake vinatumika kutoa huduma zote muhimu kwa waathirika katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kitaalam kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Chuo cha Madini Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kubaini chanzo cha tukio, kiasi cha athari zilizotokea chini ya miamba na juu ya ardhi. Tathmini hii ya kitaalamu itatupa picha na mwelekeo wa kushughulikia urejeshaji wa miundombinu iliyoharibika.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kukushukuru sana wewe binafsi Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge kwa namna mlivyoshirikiana na Serikali katika kushughulikia janga hili la kitaifa la tetemeko la ardhi Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu ya hali na mali na kwa kututia moyo katika kushughulikia tukio hili kubwa lililoathiri maisha na shughuli za wananchi pale mkoani Kagera.

Mheshimiwa Spika, vilevile, kwa niaba ya Serikali, na kipekee, nitumie fursa hii kuishukuru Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Waheshimiwa Mabalozi, Wawakilishi wa Mashirika ya Umma na ya Kimataifa waliopo nchini, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla, ambao waliitikia wito wa Serikali wa kushiriki na kusaidia juhudi za Serikali za kuwasaidia waaathirika wa tetemeke la ardhi. Tunawashukuru sana wote waliotuunga mkono kwa fedha na vifaa mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo zinazofanywa, Serikali imeshatoa na inaendelea kukusanya michango kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali. Hivyo, kwa wananchi na wadau walio tayari kuchangia wanaweza kutumia Akaunti ya Maafa iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB yenye Namba.015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztzkwa kutuma fedha kwa njia ya kawaida au Mobile Banking. Vilevile, michango hiyo inaweza kutumwa kwenye Namba za simu za mkononi, 0768-196-669 (M-Pesa), au Namba 0682-950-009 (Airtel Money) au Namba 0718-069-616 (Tigo Pesa).

Nawaomba wananchi wote, Sekta Binafsi na Jumuiya ya Kimataifa tuonyeshe mshikamano kuungana na Serikali katika kusaidia wenzetu walioathirika na tetemeko hilo kwa kutoa michango ya hali na mali.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali itaendelea kuratibu michango yote itakayotolewa na kuifikisha kwa walengwa. Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kuimarisha uwezo wetu wa ndani wa kukabiliana na majanga ya aina hii na mengineyo.

SHUGHULI ZA BUNGE

Mheshimiwa Spika, tunahitimisha mkutano huu tukiwa tumepata fursa ya kujadili Miswada, Maazimio na Kauli mbalimbali za Mawaziri. Miswada iliyowasilishwa na Serikali na kusomwa kwa mara ya pili na pia kusomwa mara ya tatu ni kama ifuatavyo:-

Kwanza: Muswada wa Sheria ya upatikanaji wa Habari wa mwaka 2016; (The Access to Information Bill, 2016);

Pili: Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016; (The Valuation and Valuers Registration Bill, 2016);

Tatu: Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa mwaka 2016; (The Government Chemist Laboratory Authority Bill, 2016);

Nne: Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016; (The Chemist Professionals Bill, 2016);

Tano: Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo wa Mwaka 2016; (The Tanzania Agricultural Research Institute Bill, 2016);

Sita: Muswada wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi wa Mwaka 2016; (The Tanzania Fisheries Research Institute Bill, 2016).

Miswada ya Sheria ya Serikali iliyosomwa kwa mara ya kwanza ni:-

(a) Muswada wa Sheria ya huduma za Hbari za Mwaka 2016 (The Media services Bill, 2016).

(b) Muswada wa Sheria ya marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2016 (The Written Laws Micellianeous Amendments) (No.3) Bill, 2016).

Mheshimiwa Spika, katika Bunge hili, Serikali ilitoa kauli zifuatazo:-

Kwanza: Kauli ya Serikali kuhusu hali ya chakula nchini na uzalishaji kwa msimu wa mazao kwa mwaka 2015/2016; na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017;

Pili: Kauli ya Serikali kuhusu tukio la tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 10 Septemba, 2016 Mkoani Kagera na Mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Spika, kipekee, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na Wataalam wake, kwa mchango wao mkubwa katika kuandaa miswada hiyo kwa umakini mkubwa na hivyo kuwawezesha Waheshimiwa Mawaziri kuiwasilisha Bungeni kwa weledi mkubwa. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri. Serikali itazingatia ushauri na maoni yenu wakati wa utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 110 ya msingi na mengine 222 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Vilevile, jumla ya maswali matano ya msingi na ya nyongeza ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu ya kila Alhamisi yaliulizwa na kupata majibu.

MWENENDO NA MWELEKEO WA HALI YA UCHUMI

Mheshimiwa Spika, katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na wasiwasi kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi, hususan mtiririko wa fedha kwenye uchumi wa Taifa. Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kuwa mwenendo wa uchumi ni wa kuridhisha na unaendelea kuimarika. Aidha, tathmini iliyofanyika kuhusu viashiria vya uimara wa sekta ya fedha, inaonesha kuwa Mabenki yetu bado yapo salama, na yana mitaji ya kutosha na mwenendo wa sekta ya fedha ni wa kuridhisha. Aidha, Wizara ya Fedha na Mipango, Benki Kuu ya Tanzania na Taasisi ya Taifa ya Takwimu zinafuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa Hali ya Uchumi Nchini. Mathalan, tarehe 14 Septemba, 2016 Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi nchini ambapo alilihakikishia Taifa na Jumuiya ya Kimataifa kwamba hali ya uchumi wetu ni shwari kabisa na si mbaya kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.

Mheshimiwa Spika, katika taarifa hiyo ya Benki Kuu pamoja na mambo mengine, imebainishwa kwamba katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji wa uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa wa kuridhisha. Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka 2015.Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, huduma za mawasiliano, utangazaji na huduma ya intaneti; kuongezeka kwa uchimbaji na madini. Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ya juu katika kipindi hicho ni sekta ya fedha kwa asilimia 13.5, mawasiliano asilimia 13.4 na utawala wa umma asilimia 10.2.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mwenendo huo mzuri wa viashiria vya shughuli za uchumi, ni dhahiri kwamba mwelekeo wa uchumi katika kipindi kijacho unatoa matumaini ya uchumi kuendelea kuimarika kama ilivyokadiriwa hapo awali na kufikiwa kwa lengo la ukuaji wa Pato la Taifa la asilimia 7.2 kwa mwaka 2016. Hii inachangiwa pia na ukweli kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri katika kuimarisha uchumi endelevu; usimamizi thabiti wa rasilimali za umma; na ujenzi wa miundombinu bora yenye kuimarisha lengo la kujenga uchumi wa viwanda chini ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

MWENENDO WA UKUSANYAJI WA MAPATO YA SERIKALI KWA MWEZI JULAI NA AGOSTI, 2016

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali. Katika mwaka 2016/17, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Aidha, Serikali imeendelea kudhibiti utoaji wa misamaha ya kodi ili kuleta tija kwa Taifa katika ukusanyaji mapato.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali imelenga kukusanyamapato ya ndani, ikijumuisha mapato ya Halmashauri, ya jumla ya shilingitrilioni 18.46, sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote ya shilingi trilioni 29.5.Takwimu za mwenendo wa ukusanyaji mapato zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Agosti, 2016, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yalikuwa shilingi trilioni 2.168 ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi trilioni 2.113, sawa na asilimia 103 ya lengo. Aina za kodi zilizochangia sana katika ongezeko hilo ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mashine za kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato. Mapato yasiyo ya kodi kwa kipindi hicho yalikuwa shilingi bilioni 271.1; sawa na asilimia 60 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 448.4. Aidha, mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri yalikuwa Shilingi bilioni 45.4; ikiwa ni asilimia 41 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 110.9. Napenda kutumia fursa hii kuzihimiza Wizara na Halmashauri kuongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua zifuatazo:-

Kwanza: Kuendelea kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya biashara, viwandani, migodi, bandarini, kwenye viwanja vya ndege na maeneo ya mipakani ili kuhakikisha kodi stahiki zinakusanywa;

Pili: Kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato;

Tatu: Kuendelea kupanua wigo wa walipa kodi, ikiwa ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iweze kuingia katika mfumo wa kodi;

Nne: Kuimarisha ufuatiliaji wa mapato yanayokusanywa na taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali na Halmashauri zote nchini; na

Tano: Kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.

MPANGO WA SERIKALI WA KUHAMIA DODOMA

Mheshimiwa Spika, tarehe 23 Julai, 2016 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi hapa Dodoma alieleza kuhusu dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukamilisha mchakato na ahadi ya Serikali ya kuhamia katika Mji wa Makao Makuu – Dodoma. Aidha, Mheshimiwa Rais alirejea kauli hiyo tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Nchini ambayo yalifanyika Kitaifa kwa mara ya kwanza katika Viwanja vya Mashujaa, mjini Dodoma. Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa anatarajia kwamba Serikali yake yote itakuwa imehamia Dodoma katika kipindi cha miaka minne na miezi minne, hadi kufikia mwisho wa mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika, napenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwamba Mpango wa sasa wa Serikali wa kuhamia Dodoma ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 iliyozingatia agizo lililotolewa tarehe 1 Oktoba, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa Chama cha TANU. Hivyo, hatua zinazochukuliwa sasa na Serikali ya Awamu ya Tano ni mwendelezo tu wa utekelezaji wa mipango ya awali iliyokuwa inatekelezwa mwaka hadi mwaka na Serikali za Awamu zilizopita, kuanzia Awamu ya Kwanza lilipotolewa tamko hilo mwaka 1973; chini yaUongozi wa Rais wa Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano, baada ya tamko la Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli la tarehe 23 Julai 2016, yafuatayo yamefanyika:

Kwanza: Tarehe 26 Julai, 2016 nilikutana na Viongozi wa Mkoa wa Dodoma (Viongozi wa Chama na Serikali wa Mkoa na Wilaya, Wazee maarufu, Viongozi wa Madhehebu ya Dini na Wadau mbalimbali) ili kuwajulisha kuhusu mkakati wa sasa wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Aidha, niliutaka Uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuwasilisha mapendekezo ya mpango kazi wa kutekeleza uamuzi wa Serikali wa kuhamia Dodoma;

Pili: Katika kipindi cha siku 14, Uongozi wa Mkoa wa Dodoma uliwasilisha kwangu Taarifa ya Serikali kuhamia Dodoma kama ilivyokusudiwa. Aidha, tarehe 15 Agosti, 2016 Mkoa uliwasilisha Mpango huo katika Kikao cha Baraza la Kazi la Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu na kupata ushauri na maoni yao ya kuuboresha;

Tatu: Serikali imeunda Kamati Ndogo chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa lengo la kufanya mapitio ya upatikanaji wa Ofisi na Makazi na miundombinu muhimu. Kamati hiyo inashirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali zilizopo Dodoma na Kitaifa, zikiwemo TBA, DUWASA, TANROADS, TEMESA, TANESCO, SUMATRA, TTCL, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji;

Nne: Aidha, Serikali imeunda Kamati ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu ambao wanaratibu zoezi zima na utaratibu wa Serikali kuhamia Dodoma;

Tano: Tarehe 1 Septemba, 2016, Serikali ilikutana na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Fedha, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Sekta Binafsi zinazohusika na ujenzi wa miundombinu nchini. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kupata mawazo ya Sekta Binafsi, Taasisi za Fedha na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuisaidia Serikali kuboresha mikakati ya kuhamia Dodoma kwa kuzingatia kuwa Serikali peke yake haiwezi kukamilisha jambo hili. Katika kikao hiki tumekubaliana kwamba kuanzia sasa kuwepo na vikao baina ya Makatibu Wakuu na Wadau wa Sekta Binafsi, angalau mara moja kwa mwezi chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Kamati hiyo akiwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Kikao hicho kitakuwa cha mashauriano na kupeana mrejesho wa utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhamia Dodoma kwa kuzingatia mchango wa sekta ya umma na sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi na kijamii, uwekezaji na uzalishaji biashara na huduma mbalimbali;

Sita: Serikali pia imeunda Kamati Maalum ya Wataalam Washauri itakayoshirikiana na CDA kufanya Mapitio ya Mpango Kamambe (Master Plan) wa Mji wa Dodoma ili kubaini mahitaji halisi ya sasa na siku zijazo katika upeo wa miaka 50 na zaidi. Zoezi hili litahitaji ushirikishwaji mkubwa wa jamii na sekta binafsi. Lengo la Serikali ni kuwa na mji uliopangwa vizuri na unaozingatia vigezo mbalimbali vya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inatambua jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali za awamu zilizopita zilizoongozwa na Chama cha Mapinduzi za kuweka miundombinu mbalimbali muhimu ya kufanikisha mpango wa Serikali kuhamia Dodoma. Tathmini iliyofanywa na OWM, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, pamoja na wadau mbalimbali, inaonyesha kuwa kwa ujumla miundombinu iliyopo Dodoma kwa sasa ina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu kuanzia mwezi huu wa Septemba, 2016 hadi mwaka 2020.

RATIBA YA SERIKALI KUHAMIA DODOMA

Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma, tayari imeandaliwa ratiba itakayowezesha Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu, kuanzia mwezi Septemba, 2016 hadi mwaka 2020, bila ya kuathiri bajeti yetu ya mwaka 2016/2017 kama ifuatavyo:

Kwanza: Awamu ya Kwanza itakuwa kati ya mwezi Septemba, 2016 na Februari, 2017. Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wote, Manaibu Makatibu Wakuu wote watahamia Dodoma katika Awamu ya Kwanza. Aidha, kila Wizara itatakiwa kuhamisha Watumishi wa Idara moja au mbili, na wakati huo huo kuendelea kuweka utaratibu wa kupeleka Watumishi wa Idara nyingine kuhamia Dodoma;

Pili: Awamu ya Pili itakuwa kati ya mwezi Machi 2017 na Agosti 2017. Kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali kuweka katika Bajeti zao za mwaka 2017/2018 gharama za kuendelea kuhamisha watumishi wake kuja Dodoma;

Tatu: Awamu ya Tatu itakuwa kati ya mwezi Septemba 2017 na Februari 2018; ambapo Wizara zitaendelea na uhamishaji wa Watumishi wa Idara zilizo ndani ya Wizara.

Nne: Awamu ya Nne itakuwa kati ya mwezi Machi 2018 na Agosti, 2018; na Awamu ya Tano itakuwa kati ya Mwezi Septemba 2018 hadi Februari, 2020. Katika kipindi hiki cha Awamu ya Tatu na Nne; Wizara zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.

Tano: Awamu ya Sita, itakuwa kati ya mwezi Machi, 2020 na Juni, 2020ambapo Ofisi ya Rais ikiongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watakuwa wanahamia Dodoma.

Nazishauri Wizara zote kuanzisha mifumo ya utunzaji kumbukumbu wa kielektroniki badala ya kuhama na mafaili kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma, tunataka Dodoma iwe ya kielektroniki.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo wa ndani na nje kuwekeza Dodoma ili kuboresha zaidi miundombinu iliyopo na kuongeza majengo ya Ofisi na makazi ya Watumishi kuwekeza katika huduma za afya na elimu, huduma za kibiashara kama mabenki, maduka makubwa (Shopping Malls) na masoko, mahoteli na maghala. Aidha, napenda kurejea maelekezo niliyoyatoa kwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) na Mkoa wa Dodoma na Manispaa kuhakikisha kwamba Mji Mkuu wa Dodoma unaendelezwa kwa kasi ili kupokea watumishi wengi na familia zao pamoja na sekta binafsi watakaohamia Dodoma.

Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kuwa Mkoa wa Dodoma na CDA wahakikishe kuwa pamoja na kuandaa maeneo ya makazi na Ofisi, pia watengemaeneo maalumu ya huduma muhimu kama vile maeneo kwa ajili ya kituo kikuu cha biashara, bustani, bandari kavu na kuendelea kuongeza eneo la viwanda na huduma mbalimbali za kibiashara. Aidha, naagiza Mamlaka za Mipango Miji Mkoani Dodoma na hasa CDA wahakikishe wanaweka mfumo wa kielektroniki wa upatikanaji wa viwanja ambao utatambua mahitaji kwa utaratibu wa wazi, na bila urasimu usio wa lazima. Vilevile, nashauri Wakazi wa Mkoa wa Dodoma na Sekta binafsi kutumia fursa hii kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na mahoteli ili watumishi na wageni wanapokuja Dodoma wasipate taabu kutafuta mahali pazuri pa kuishi.

SEKTA YA KILIMO:

Hali ya Uzalishaji na Upatikanaji Chakula Nchini:

Mheshimiwa Spika, tathmini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2015/16 iliyofanyika mwezi Juni 2016 inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa utafikia tani 16,172,841. Aidha, Mikoa 11 kati ya 26 ilibainika kuwa na ziada ya chakula, mikoa 12 kuwa na utoshelevu wa chakula na miwili (2) uhaba wa chakula. Kutokana na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2016/2017 kuwa tani 13,159,326, nchi itakuwa na utoshelevu wa chakula kwa wa asilimia 123, sawa na ziada ya tani 3,013,515 kwa mazao yote ya chakula.

Mheshimiwa Spika, tathmini hii ilibaini pia kuwa chakula kingi aina ya nafaka kilikuwa tayari kimesafirishwa nje ya nchi kutokana na nchi jirani kutokuwa na mavuno mazuri bila kuzingatia kwanza haja ya utoshelevu wa ndani ya nchi.

Ili kuhakikisha kuwepo kwa hali ya usalama wa chakula Nchini na kuepuka baa la njaa hapo baadaye, Serikali imeamua kuwa kuanzia tarehe 10 Septemba 2016 sehemu ya ziada ya nafaka ya mahindi na mchele itasafirishwa nje ya nchi kwa vibali vitakavyotolewa kwa ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pekee. Serikali itasimamia ili kusiwe na upungufu wa chakula nchini.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa yote nchini kuwahamasisha wakulima na wafanyabiashara kuongeza thamani ya mazao ya kilimo hususan mahindi na mpunga kwa kuyasindika, kabla ya kusafirisha nje ya nchi ili yapate bei nzuri zaidi, na pia kuzalisha ajira kwa Watanzania.

Utaratibu wa kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo katika msimu wa 2016/2017

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2003/2004 hadi mwaka 2015/2016, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya chakula, na hususan mahindi, mpunga na mtama. Pia, ruzuku ya pembejeo hutolewa kwa mazao ya biashara ya korosho, pamba, chai, kahawa na alizeti. Ruzuku hiyo, imekuwa ikitolewa kwa kutumia mfumo wa vocha na vikundi vya wakulima kukopeshwa pembejeo hizo kupitia taasisi za fedha na makampuni ya pembejeo za kilimo. Pamoja na juhudi hizo, kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika kufikia lengo hilo.

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi, katika msimu wa 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 5 kwa ajili ya ruzuku ya viuatilifu vya mazao ya kilimo na shilingi bilioni 25 kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo nyingine za kilimo. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 20 ni za kununua tani 21,892 za mbolea kwa kaya 354,928. Aidha, Serikali italipia asilimia 30 ya bei ya mbolea kwenye soko, sawa na shilingi 20,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kupandia; na shilingi 12,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kukuzia.

Mheshimiwa Spika, ili mbolea hizo ziweze kuwafikia walengwa kwa wakati na kwa bei nafuu, Kampuni ya Mbolea Tanzania itasambaza mbolea katika vituo vyake 29 nchini na kuiuza kwa Mawakala wa Pembejeo za Kilimo kwa shilingi38,000 kwa mfuko wa kilo 50 kwa mbolea ya kupandia na shilingi 26,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kukuzia. Ninaziagiza Halmashauri zote kuhakikisha Mawakala wa Pembejeo wanauza mbolea kwa bei itakayopangwa. Ni imani yangu kuwa wakulima wengi watatumia fursa hii ya kupata mbolea ya ruzuku kuendeleza kilimo cha kisasa, chenye tija na cha kibiashara.

SEKTA YA USHIRIKA

Maboresho katika tasnia ya Ushirika

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa ushirika, kama chombo cha kuwaunganisha, kuwapa nguvu na kuwatetea wanachama wao katika kilimo, ufugaji, uvuvi na tasnia nyingine, unakabiliwa na changamoto nyingi za usimamizi mbovu, ubadhirifu na ufujaji mali wa baadhi ya viongozi. Changamoto hizo zinawaumiza sana wakulima na kuwafanya wakate tamaa katika uzalishaji, masoko na uendeshaji wa shughuli zao za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na changamoto hizo, Serikali itafanya marekebisho makubwa ndani ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika; iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kuchukua hatua za kinidhamu kwa watakaobainika kuhusika na ubadhirifu wa mali za ushirika. Aidha, baadhi ya Maafisa Ushirika waliokaa katika kituo kimoja kwa muda mrefu watahamishiwa katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, Serikali itafanya marekebisho makubwa kwa Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) ambalo limeshindwa kufanya kazi zake kwa weledi.

Mheshimiwa Spika, katika kufufua ushirika, Serikali itahuisha Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002, na kuijengea Tume ya Maendeleo ya ushirika uwezo wa kuajiri/kuhamishia watendaji katika ofisi za Mikoa na Halmashauri zote ili kusimamia vyama vya ushirika; kufanya kaguzi za mara kwa mara, kuondoa tatizo la upotevu wa rasilimali za vyama; kusimamia upatikanaji wa viongozi wenye sifa na watendaji wenye weledi wenye kuongoza vyama kwa ufanisi; kupanua wigo wa shughuli za ushirika katika sekta nyingine za kiuchumi zaidi ya kilimo ili kuongeza idadi ya vyama vya ushirika nchini na hivyo kuchochea ukuaji wa kipato kwa wananchi wengi.

SEKTA YA ELIMU

Motisha kwa Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na usimamizi mzuri na wa karibu shuleni, Serikali imeanza kutoa posho ya madaraka kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata kila mwezi kuanzia mwezi Julai, 2016 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5.09 kimetolewa. Aidha, mpango mwingine uliopo ni kuwapatia Waratibu Elimu Kata pikipiki ili ziwawezeshe katika ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za kielimu katika kata zao nchi nzima. Kwa kuanzia, Waratibu Elimu Kata wa Mikoa 7 ambayo ilikuwa na ufaulu wa chini katika matokeo ya kuhitimu darasa la saba tayari wameshapatiwa jumla ya pikipiki 1,015. Mikoa iliyopatiwa pikipiki hizi pamoja na idadi ya pikipiki ni kama ifuatavyo: – Dodoma (192); Mara (99), Simiyu (122), Shinyanga (128), Tabora (200), Kigoma (135), Lindi (139). Mikoa iliyobakia itapatiwa pikipiki chini ya programu ya Kukuza Stadi za Kusoma na Kuandika ya LANES (Literacy and Numeracy Education Support Program) pamoja na UNICEF.

Upungufu wa Walimu na Miundombinu

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa upungufu wa walimu, Serikali imeamua walimu wapya watakaoajiriwa mwaka 2016 wapangwe shuleni moja kwa moja na kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa wa walimu.

Hali ya Madawati

Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa tarehe 16 Machi, 2016 Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 30 Juni, 2016 kusiwepo mwanafunzi anayekaa chini kwa kukosa dawati.

Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais, kufikia mwezi huu wa Septemba madawati 951,610 kwa shule za Msingi yalitengenezwa na hivyo kufikia madawati 3,084,781 sawa na asilimia 94.4. Kwa upande wa shule za sekondari, idadi ya madawati yaliyotengenezwa yamefikiamadawati 1,490,488 sawa na asilimia 99.4 na kufanya upungufu kuwa madawati 182,864 kwa shule za Msingi na 8,380 kwa Shule za Sekondari.

Madawati hayo yanaendelea kutengenezwa na Mikoa ambayo haijakamilisha inatakiwa iwe imekamilisha ifikapo tarehe 30 Septemba, 2016.

MAABARA KATIKA SHULE ZA SEKONDARI

Mheshimiwa Spika, mahitaji ya Maabara kwa shule za sekondari ni 10,803. Maabara zilizopo ni 5,756 sawa na asilimia 53.2 ya mahitaji. Upungufu uliopo ni maabara 5,047 ambazo zingine zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Katika mwaka wa fedha 2016/17, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri imetenga jumla ya shilingi bilioni 18.876 kwa ajili ya umaliziaji wa maabara2,135 katika shule za sekondari kwenye Halmashauri mbalimbali nchini. Serikali inaendelea na ujenzi wa jumla ya maabara 290 kupitia mpango wa MMES II katika shule za sekondari 528. Upungufu utakaokuwepo baada ya kukamilika kwa maabara hizi ni maabara 4,807. Serikali itaendelea kubuni mikakati mbalimbali ya kuondoa upungufu huo.

Mitihani ya Elimu ya Msingi

Mheshimiwa Spika, mtihani wa kumaliza darasa la saba ulifanyika tarehe 7 hadi 8 Septemba, 2016 nchini kote. Idadi ya watahiniwa 795,761 walisajiliwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2016. Aidha, taarifa za awali zinaonesha kuwa takriban watahiniwa 789,302 walifanya mtihani huo, sawa na asilimia 99.2 ya waliosajiliwa. Taarifa rasmi itatolewa baada ya Mikoa na Halmashauri kukamilisha kufanya mawasilisho ya taarifa kamili ya ufanyikaji wa Mtihani huo.

Mheshimiwa Spika, tafsiri ya idadi ya kubwa ya wanafunzi waliofanya mitihani ya darasa la saba ni kwamba yapo matarajio kuwa idadi ya wanafunzi watakaoingia kidato cha kwanza katika mwaka 2017 itakuwa kubwa kuliko nafasi zitakazo kuwepo mwanzoni mwa mwaka 2017 katika shule za Sekondari ikiwa hali ya miundombinu itaendelea kuwa kama ilivyo sasa. Hivyo basi, natoa wito kwa Halmashauri zote nchini zijiandae kuwawezesha wanafunzi wote watakaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza kwa kuongeza vyumba vya madarasa, madawati, matundu ya vyoo na nyumba za Walimu.

UHAKIKI WA VYETI KWA WATUMISHI

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi ingawa limeendelea kuleta usumbufu kwa watumishi katika baadhi ya maeneo. Naagiza kwa Wakurugenzi waandae vituo maalum vilivyo jirani na vituo vyao vya kazi badala ya kuwakusanya kituo kimoja ili kuwapunguzia adha na gharama. Halmashauri zote zizingatie agizo hili ili maafisa utumishi waende kwenye vituo hivyo.

JITIHADA ZA SERIKALI KUIMARISHA USAFIRI WA ANGA

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuzungumzia kidogo kuhusu jitihada za Serikali za kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini kuanzia mwaka 2016/2017 Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea na mpango wake wa kuboresha usafiri wa anga hapa nchini. Hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kuendelea kuboresha viwanja vya ndege nchini. Lengo ni kuhakikisha kuwa kila Mkoa unakuwa na kiwanja cha ndege cha kisasa, chenye ubora unaofaa kutua ndege.

Mheshimiwa Spika, ili kwenda sambamba na azma ya Serikali kuhamia Dodoma muda mfupi ujao, kiwanja cha ndege cha Dodoma kimefanyiwa ukarabati mkubwa ili kuweza kuhudumia ndege zenye uwezo wa kubeba hadi abiria 90. Sambamba na hatua hizo, Serikali imedhamiria kuimarisha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege mpya kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa anga kupitia ATCL.

Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imenunua ndege mbili (2) aina ya Dash 8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zitakazotumika kutoa huduma za usafiri wa anga kwa soko la ndani na nchi jirani. Ndege hizo zinatarajia kuwasili nchini mwezi huu wa Septemba, 2016. Aidha, taratibu za kununua ndege nyingine mbili zenye ukubwa wa kati (medium haulage aircraft) zitakazokuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 110 zimeanza. Ndege hizo zitahudumia soko la kikanda.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hiyo Serikali imeanza kazi ya kuiunda upya ATCL. Jana tarehe 15 Septemba, 2016, Mheshimiwa Rais amefanya uteuzi wa Mtendaji Mkuu mpya wa ATCL. Aidha, mchakato wa uteuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo unakamilishwa. Vilevile, Serikali imegharamia mafunzo ya wataalam mbalimbali wakiwemo wahandisi watakaohudumia ndege mpya. Hatua hizo zitasaidia sana kuboresha shirika letu la ndege na usafiri wa aga hapa nchini katika kipindi kifupi kijacho.

HALI YA AMANI NA UTULIVU NCHINI

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vimeendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini kwa manufaa ya ustawi wa nchi yetu. Usalama wa raia na mali zao umeendelea kudumishwa kwa kutambua kuwa ni miongoni mwa misingi mikuu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Kwa namna ya pekee, napenda kutumia fursa hii kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi kwa weledi.

Mheshimiwa Spika, ili Jeshi la Polisi liendelee kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kubaini, kuzuia na kukabiliana na uhalifu Nchini, Serikali itaendelea kuwajengea uwezo Maafisa, Wakaguzi na Askari na pia kutekeleza mambo yafuatayo:-

Kwanza: Kutabiri mwelekeo wa uhalifu kwa kutumia takwimu za uhalifu, kumbukumbu za uhalifu pamoja na mabadiliko ya uhalifu ili kuweza kutambua maeneo korofi, wahalifu wanaohusika, mahali walipo na namna ya kukabiliana na uhalifu huo.

Pili: Kuyatambua maeneo nyeti (hotspots) yenye vivutio vya uhalifu, na kuyapangia ulinzi, misako na doria imara.

Tatu: Kutoa elimu kwa jamii kuhusu mbinu mbalimbali za kuzuia na kupambana na uhalifu kwa kutumia vyombo vya habari, mihadhara, mikutano, maonesho na usambazaji wa machapisho na vipeperushi.

Nne: Kufanya misako na doria mara kwa mara ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali nchini.

Tano: Kushirikiana na wadau wote wa ulinzi na usalama kubadilishana taarifa za kiintelijensia pamoja na uzoefu katika kuzuia uhalifu kwa kuibua mifumo mipya na kuboresha ya zamani.

Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kuwa suala la amani, na usalama na utulivu nchini halina mbadala. Nawaomba tudumishe hali ya amani na usalama ili tufanikishe lengo letu la kukuza uchumi na kuondoa umaskini.

MICHEZO

Nchi yetu imeendelea kuwika kimichezo hasa katika soka. Nitumie fursa hii kuwapongeza vijana wetu wa Serengeti Boys kwa ushindi wao. Hivi sasa timu yetu inajipanga kupambana na timu ya Congo (DRC) hapo Septemba 18.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, wakati tunahitimisha mkutano huu leo, napenda nitumie nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia vizuri na kwa weledi mkubwa vikao vyote vya mkutano huu. Niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu. Ninashukuru pia Watendaji wa Serikali kwa kuwasaidia Mawaziri na Naibu Mawaziri katika kujibu maswali na hoja mbalimbali za Wabunge. Niwashukuru madereva wote kwa kuwaendesha Mawaziri, Wabunge na Watendaji wote kwa usalama kabisa. Thanx to wanahabari kwa kuihabarisha jamii juu ya mkutano wetu. Kipekee, nimshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah na timu yake kwa kutuwezesha kukamilisha shughuli zote za mkutano huu kwa mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Spika, wakati tunahitimisha mkutano huu leo na kuelekea katika Majimbo yetu, sote tunatambua kuwa msimu wa mvua za vuli na masika unakaribia. Hivyo, napenda kutumia fursa hii kuziagiza Wizara zinazohusika na usambazaji wa pembejeo kuhakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati na kwa bei iliyopangwa. Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe kwamba wanasimamia kikamilifu shughuli za kilimo katika maeneo yao ili kila familia na kaya ianze maandalizi ya kilimo mapema.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kurejea katika kusisitiza kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya kukuza uchumi katika Taifa letu. Hivyo, nichukue fursa hii kuwahakikishia wafanyabiashara na wenye viwanda na wawekezaji kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwapa ushirikiano wa dhati ili kuendeleza shughuli zao kama ambavyo wamejipanga. Wafanye shughuli zao bila woga au tashishi yoyote.

Mheshimiwa Spika, mwisho, lakini si kwa umuhimu, nitumie muda huu kumwomba Mwenyezi Mungu awalinde na awaongoze Waheshimiwa Wabunge wote katika safari ya kurejea majumbani kwenu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 1 Novemba, 2016, siku ya Jumanne, Saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
 
Kiuhalisia ilikuwa ngumu sana kuhama kwa haraka, hapa ndo mmeanza kuona wengine walichokuwa wan akisema. Hili jambo linahitaji bajeti na si kusema kuanzia mwezi Tisa ofisi ya Waziri Mkuu itakuwa imehama Dar na kwenda Dodoma, tena na kusema Waziri Mkuu atatambulishwa rasmi. Huu mchezo wa kuhamia Dodoma HAUHITAJI hasira, unataka upembuzi yakinifu hasa kwenye swala la Bajeti na Miundombinu imara.
 
Leo Septemba 16, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha mkutano wa nne kwa Bunge la 11 uliodumu kwa muda wa wiki mbili, amesoma ratiba ya serikali kuhamia Dodoma.

“Ili kufanikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma, tayari imeandaliwa ratiba itakayowezesha Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu, kuanzia mwezi Septemba, 2016 hadi mwaka 2020, bila ya kuathiri bajeti yetu ya mwaka 2016/2017 kama ifuatavyo”–


1. Septemba 2016 – Februari 2017.

Waziri Mkuu na Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wote, Manaibu Makatibu Wakuu wote watahamia Dodoma katika Awamu ya Kwanza. Aidha, kila Wizara itatakiwa kuhamisha Watumishi wa Idara moja au mbili, na wakati huo huo kuendelea kuweka utaratibu wa kupeleka Watumishi wa Idara nyingine kuhamia Dodoma;

2. Machi 2017 – Agosti 2017.

Kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali kuweka katika Bajeti zao za mwaka 2017/2018 gharama za kuendelea kuhamisha watumishi wake kuja Dodoma.

3. Septemba 2017 – Februari 2018.

Katika awamu hii, Wizara zitaendelea na uhamishaji wa Watumishi wa Idara zilizo ndani ya Wizara.

4. Machi 2018 – Agosti 2018.

Katika kipindi hiki, Wizara zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.

5. Septemba 2018 – Februari 2020.

Katika kipindi hiki, Wizara zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.

6. Machi 2020 – Juni 2020.

Katika kipindi hiki, Ofisi ya Rais ikiongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watakuwa wanahamia Dodoma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitumia wasaa huu kuzishauri Wizara zote kuanzisha mifumo ya utunzaji kumbukumbu wa kielektroniki badala ya kuhama na mafaili kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma, tunataka Dodoma iwe ya kielektroniki, alisisitiza Waziri Mkuu.

Chanzo: Swahili Times
Inaitaji uwe na mwanasheria wako ili uweze kuchungia Uzi huu.napita tuu
 
Wakija na mipango kama hiyo tutawaunga mkono maana ni realistic. Sio mizuka kama pale awali. Mbona Waziri mkuu anawahi sana kuhamia wakati rais bado atakuwa dar kwa miaka takriban 3 na ikumbukwe rais anafanya kazi kwa karibu na waziri mkuu?
 
Kama waziri mkuu, mawaziri na hao makatibu wakuu wa wizara watakuwa Dodoma, halafu Rais na makamu wako Dar hivi mikutano ya baraza la mawaziri itafanyikaje? Yaani kila siku ama Rais na makamu wake wasafiri kwenda Dodoma au Waziri mkuu, mawaziri, n.k wasafiri kwenda Dar. Hapo ndio kubana matumizi kwa serikali yetu pendwa na inayokubalika bila chenga. Hapa kazi Tu!
 
Hapo sawa, mpango umekaa sawa kiasi chake ukilinganisha na zimamoto iliyotarajiwa kwa kila Waziri/Afisi kuja na tamko la kuelekea Idodomya.
Kila la kheri Awamu ya Tano
 
Ukihama mapema wananchi wa Tz watasahau, Hama karibu na uchaguzi ili uwaambie kuwa mmeona.
Lakini ilipaswa hii road map ipangwe kabla ya kutoa matamko. Kuna watu wameshaathirika kisaikolojia kutokana na hili. ofisi nyeti zimeshatikisika sana kwa matamko ya mtu kuamka na kuanza kuagiza hadharani.

kiukweli Utawala unakosa "misingi muhimu ya kiutawala". Hakuan "Team work".
 
Back
Top Bottom