Kusitishwa kwa Chakula Mnazi Mmoja hospitali Zanzibar sivyo asema Maalim Seif

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130
[h=1]
img_1852.jpg
[/h]Written by Stonetown (Kiongozi) // 27/11/2012 // Habari // 1 Comment


Na Khamis Haji, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameutaka uongozi wa Wizara ya Afya kuzingatia upya uamuzi wao wa kuondosha huduma ya chakula kwa wagonjwa wanaolazwa hospitali kuu ya Mnazimmoja, kwa vile uamuzi huo unaweza kusababishia hali ngumu kwa wagonjwa wanaotoka nje ya mji wa Zanzibar ambao hawana jamaa.
Maalim Seif aliyasema hayo jana katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), alipozungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Afya, baada ya kumaliza ziara ya kuzitembelea taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo Unguja na Pemba.
Alisema wagonjwa wanaolazwa katika hospitali hiyo sio kuwa wote wana jamaa katika mji wa Zanzibar, bali kuna wengine wanatoka vijiji vya mbali na hata Tanzania Bara, ambao hulazwa na kupatiwa huduma hapo, hivyo, kukosekana kwa chakula cha wagonjwa kama ilivyokuwa zamani itasababisha hali ngumu kwa wagonjwa kama hao.
Maalim Seif alitoa agizo hilo, baada ya kuelezwa katika mkutano huo kuwa huduma ya chakula kwa wagonjwa wa ndani imeondolewa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa kutokana na ufinyu wa bajeti ya Wizara ya Afya, hivyo wagonjwa wote huletewa chakula na jamaa zao.
“Pamoja na maelezo yote suala la kutokuwepo chakula sijaridhika nalo, kuna wagonjwa wengine wanatoka vijiji vya mbali kabisa wala hawana jamaa hapa si hawa watakuwa wanapata shida na usumbufu mkubwa wa chakula”, alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alihoji kwanini wagonjwa wanaolazwa katika hospitali ya Mnazimmoja wakose chakula wakati wenzao wa hospitali za Pemba wanapata milo miwili kwa siku, licha ya hali hiyo hiyo mbaya ya kibajeti iliyopo.
Alisema ipo haja viongozi wa Wizara hiyo wakae walijadili suala hilo kwa undani kabisa, na baadaye waone haja ya kujibana kwenye bajeti yao, lakini utaratibu wa wagonjwa waliolazwa kupatiwa chakula una umuhimu wake kwa wananchi wanyonge.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Mohammed Jidawi alisema viongozi wa Wizara watakaa kulizingatia shauri hilo, ili kuchukua hatua zinazofaa.
Aidha, Maalim Seif alisema Serikali itaendelea kuchukua juhudi kuhakikisha madaktari na wafanyakazi wote wa sekta ya afya wanafanyakazi katika mazingira mazuri, ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo.
Alieleza kuwa Serikali inafahamu kuwa wafanyakazi katika sekta hiyo wanakabiliwa na changamoto nyingi, lakini pamoja na hayo wameweza kuonesha moyo na ari ya hali ya juu kuwatumikia wananchi, hivyo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wanaendeleza kazi hizo kwa kasi zaidi na bila ya matatizo.
Nao wafanyakazi wa sekta ya afya walimueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa, miongoni mwa changamoto zinazowakabili Unguja na Pemba ni uhaba wa wataalamu na watendaji wengine katika hospitali na vituo vya Afya.
Mfanyakazi kutoka hospitali ya Mnazimmoja, Mwanakhamis Abdallah alisema miongoni mwa sababu zinazochangia kukosekana huduma za kuridhisha katika hospitali hiyo ni msongamano wa wagonjwa kutokana na wananchi kuongezeka, uhaba wa fedha, pamoja na maslahi duni kwa wafanyakazi.
Alitoa mfano katika hospitali hiyo kuna Wodi zenye idadi kubwa ya wagonjwa zinahudumia wagonjwa 34, wakati choo ni kimoja na kinatumiwa na wagonjwa wote na jamaa wanaowauguza.
Maalim Seif amesema tayari Serikali imeandaa mpango wa kulimaliza tatizo la uhaba wa wafanyakazi kwa kusomesha vijana katika fani tafauti ndani na nje ya nchi katika kukabiliana na uhaba huo.
Mapema, Waziri wa Afya, Juma Duni Haji alisema wizara hiyo imeandaa mpango wa masomo wa miaka mitano wenye lengo la kumaliza uhaba wa madaktari na wataalamu wa kada nyengine za afya.
Makamu wa Kwanza pia alihimiza kushughulikiwa matatizo yaliyopo katika hospitali ya Wazazi Mwembeladu ambayo yamesababisha kuzorota kwa huduma na akinamama wengi wanaotaka kujifungua kukimbilia Mnazimmoja na kusababisha msongamano mkubwa.
 
Back
Top Bottom