Kushughulikia wanaochochea maandamano ni mwafaka

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
2,000
VYAMA vya siasa ni nguzo muhimu katika ujenzi wa demokrasia ya uwakilishi.

Vyama vina kazi nyingi kama vile kuelimisha, kushawishi watu kushiriki katika michakato ya kisiasa, kutafuta wanachama, kuandaa viongozi, kutunga sheria kupitia Bunge, na kushiriki katika chaguzi kubwa ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha nchi inakuwa na amani. Ili taifa lolote liweze kupiga hatua za maendeleo la muhimu zaidi ni taifa hilo kuwa na amani. Kila raia ana wajibu wa kuhakikisha amani inadumishwa kwa ajili ya ustawi wa taifa husika.

Ni kutokana na amani wananchi wanaweza kufanya shughuli za uzalishaji, watoto kusoma shule na hata waumini kwenda kwenye majumba ya ibada bila wasiwasi wowote. Vyama vya siasa ni wadau wakubwa katika kudumisha amani ya nchi. Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi Polisi limepiga marufuku mikutano yote ya hadhara, maandamano ya vyama vya siasa kuanzia Juni 7, mwaka huu hadi hapo hali ya usalama itakapotengemaa.

Jeshi hilo limewataka wanasiasa kuacha mara moja kuwashinikiza wananchi kutotii sheria za nchi, huku likitishia kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu au chama chochote cha siasa kitakachokaidi agizo hilo. Taarifa ya jeshi hilo ya hivi karibuni inasema kwamba limepokea taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa wakitaka kufanya mikutano na maandamano. Hata hivyo, kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya habari, jeshi hilo linasema limebaini mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.

Imekuwa kama kasumba, vyama vinapotaka kushinikiza jambo fulani kuhamasisha maandamano wakati mwingine kwa kichwa ngumu na kuwatumia vijana, katika vurugu hizo za kisiasa. Kama watu hawatafuata utamaduni wa kufuata sheria na kutii mamlaka zilizopo, hali hiyo inaweza kuchangia machafuko katika nchi na kuvuruga amani. Watu kama wanaona wanaonewa wanatakiwa kufuata taratibu zilizopo.

Kama taratibu hizo zinaonekana ni tatizo bado wanatakiwa kuwa na subira na kuondoa taratibu hizo zenye matatizo kwa kufuata taratibu zinazohusika.Mara nyingi tumeshuhudia watu, hususani vijana wakifuata matakwa ya wanasisa wanaohangaishwa na mihemko, kwa maana ya kutokuwa na hoja ya msingi ya kuandamana. Lakini maandamano haya yasiyoruhusiwa na vyombo vya dola yanapotokea na jeshi la polisi kutumia nguvu kuyazuia, mara nyingi ni vijana hawa, wengi wao wakiwa wale wasio na ajira, ndio wanaopata madhara makubwa ya kuumia hata kupoteza maisha.

Kwa upande mwingine wa shilingi, wahamasishaji wa maandamano hayo ambao ni viongozi wa kisiasa, wao huwa wanatoka salama salimini na huku familia zao zikiwa nyumbani zimetulia. Baadhi ya vijana hawa wanatumiwa kwa makusudi ya mara moja na kuachwa wakiwa na hali mbaya ya mahusiano katika jamii wanayoishi mara baada ya chama kutekeleza waliochotaka kufanya.

Tumeshuhudia hata uteuzi mbalimbali zinazofanywa ndani ya vyama hivi zina harufu ya nani anamjua nani na siyo ushiriki wao katika zinazoitwa harakati za kisiasa. Tulishuhudia vurugu zilizotokea Kenya baada ya ucha guzi mkuu wa nchi hiyo wa mwaka 2007 ambapo vijana walishiriki kufanya fujo kubwa na kusababisha maisha ya watu kupotea. Baada ya vurugu hizo, vijana hao hawakupata faida yoyote.

Waliendelea na maisha yao magumu yalizidishwa ugumu na vurugu hizo zilizodidimiza uchumi wa nchi hiyo. Viongozi wa vyama waliendelea kuneemeka, wao na familia zao na hakuna aliyewakumbuka vijana waliojitoa kupambana kwa jina la kutetea demokrasia. Katika hatua inayoonekana kutaka kuwanusuru vijana wanaojikuta katika mtego huu wa wanasiasa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema kuanzia sasa Serikali itawashughulikia viongozi wanaoongoza wananchi kufanya uchochezi, maandamano na uvunjifu wa amani nchini badala ya wanaochochewa.

Nchemba alitoa kauli hiyo bungeni wakati akijibu maswali ya nyongeza ya wabunge waliotaka kujua Serikali inatoa kauli gani kuhusu vyama vya upinzani kuleta vurugu katika maeneo mbalimbali yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani. Mwigulu alisema ikitoke uchochezi wa aina yoyote, serikali sasa itashughulika na kiongozi aliyewaongoza wananchi katika uchochezi. “Kila kiongozi anawajibu wa kuimiza amani ya taifa letu.

Ikitokea uchochezi wa aina yoyote na kiongozi yupo, utaratibu ambao tutautumia kuanzia sasa ni kwamba tutashughulika na kiongozi aliyewapeleka wananchi hapo. “Mara nyingi viongozi wamekuwa wakiwatanguliza watu wengine kupata madhara kwa sababu wao hawaguswi na madhara. Nitawaambia vijana wangu (vyombo vya usalama) kunapotokea na uchochezi hangaikeni na mzizi wa tatizo,” alisema.

Awali akijibu, Naibu waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni, alisema Jeshi la polisi limekuwa likitekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na kanunu na kusisitiza kuwa kila mtu atashughulikiwa kulingana na kosa alilofanya bila kuangaliwa wadhafa wake. “Iwe mbunge au kiongozi wa chama cha kisiasa atachukulia hatua kulingana na matendo aliyoyafanya, Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge inamlinda mbunge kwa kile anachokisema bungeni lakini si kwa matendo ya uhalifu atakayofanya nje,” alisema.

“Wale watakaoleta ukorofi watachukuliwa hatua kali bila ya kujali kama ni kiongozi wa aina gani na mahali gani anapotokea, lazima sheria ichukue mkondo wake,” alisema Masauni. Vijana wa Tanzania sasa wanatakiwa kufikiria mbele na kuitanguliza Tanzania yao, kutanguliza maslahi ya nchi ya nchi yao, maslahi ya familia zao na maslahi ya uhai wao.

Tatizo la ajira ambalo liko karibu kila nchi limekuwa likishughulikiwa na serikali iliyoko madarakani na tayari Rais John Magufuli ameweka wazi kwamba yeye ni rais wa maskini akimaanisha anatambua anajua tatizo la umaskini ambalo serikali yake inalishughulikia usiku na mchana.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom