Steve Dii
JF-Expert Member
- Jun 25, 2007
- 6,402
- 1,262
Inasikitisha, lakini ndiyo tena yametokea, baada ya kufumaniwa na mke wa mtu, jamaa katobolewa jicho na kukatwa masikio; tafadhali soma zaidi hapa chini:
Hoja:
--Je, wewe ukimfumania mpenzi wako, mke,mume au hawala akifanya mapenzi na mtu, unaweza kufanya yaliyotendeka kama hapo juu?!
--Kama sivyo, ni hatua zipi utachukua?
--Je, kama wewe ni mfumaniwa, ni bora kuuawa au kuachiwa kilema kama hicho?
Naomba mawazo yenu WanaJF. Ahsante.
SteveD.
Source link: IppMedia.Akatwa masikio, atobolewa macho baada ya kufumaniwa
2007-11-10 09:29:07
Na Nathan Mtega, PST, Songea
Joshua Ndunguru, 28, wengi wanamjua kama kijana mtanashati, aliyezaliwa akiwa hana kilema chochote.
Lakini sasa, kama Mungu atamnusuru na kifo na kutoka hospitalini salama, wengi watamsahau kwani atakuwa si yule Joshua wanayemjua.
Huyu wa sasa atakuwa na chongo huku akiwa hana masikio.
Hii imekuja baada ya kuadhibiwa kwa kukatwa masikio na kutobolewa jicho lake moja baada ya kufumaniwa akifanya ngono na mke wa ndugu yake.
Habari zinasema kwamba Ndunguru, mkazi wa kijiji cha Lakeshore, ufukweni mwa Ziwa Nyasa, wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma alikutwa kitandani na mke wa ndugu yake aitwaye Tele Mapanje.
Akisimulia tukio hilo, ndugu wa majeruhi huyo Bw. Andrew Ndunguru alisema mke wa Mapanje alishukiwa mapema kuwa na uhusiano usiofaa na shemejiye huyo.
Alidai kuwa mumewe alisikia madai hayo na kufuatilia nyendo za mkewe kwa muda mrefu na akafanikiwa kuwakamata Oktoba 7 mwaka huu, saa 7:30 usiku na ndipo akaamua kumwadhibu mgoni wake kwa hasira.
Aliongeza kuwa baada ya fumanizi hilo, mkewe alitoroka na kukimbia lakini mtuhumiwa alikamatwa na Mapanje pamoja na wapambe aliokuwa ameongozana nao na kumkata masikio na kisha kumtoboa jicho la kulia.
Baada ya tukio hilo, Andrew Ndunguru anasimulia kwamba majeruhi aliyekuwa akivuja damu kwa wingi alikimbizwa katika hospitali ya serikali ya Wilaya ya Mbinga na hali yake inaelezwa kuwa ni mbaya.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Falhum Mshana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa polisi inawashikilia watu watatu ambao ni mume wa mwanamke huyo Mapanje, Barnaba Kagoma na Lika Boy ambao alisema watafikishwa mahakamani mara tu baada ya uchunguzi kukamilika.
Hoja:
--Je, wewe ukimfumania mpenzi wako, mke,mume au hawala akifanya mapenzi na mtu, unaweza kufanya yaliyotendeka kama hapo juu?!
--Kama sivyo, ni hatua zipi utachukua?
--Je, kama wewe ni mfumaniwa, ni bora kuuawa au kuachiwa kilema kama hicho?
Naomba mawazo yenu WanaJF. Ahsante.
SteveD.